UPATIKANAJ​I HAKI KWA DAMU NI CHANGAMOTO KUBWA

UHURU na Amani ni kitu cha muhimu sana katika maisha ya kila siku ya kila mwanadamu. Na katika dunia hii wapo wengi waliosaidia kuhakikisha kuwa uhuru huo unapatikana bila kujua kuwa unapatikana kwa njia gani ya amani ama ya kumwaga damu? Mmoja kati ya wapigania uhuru ni Malcom X ambae alianza harakati zake za kushawishi wa Amerika watumie nguvu kudai haki zao katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 9 November 1963.

“Angalia katika Mapinduzi ya Marekani ya mwaka 1776, mapinduzi hayo yalikuwa ya nini?  Kwa ukweli walitaka kukomboa ardhi yao, Kwanini walitaka ardhi?  Pia unaweza kusema kuwa wa amerika hao walitaka uhuru. Je, yalifanyika vipi? Kwa njia ya umwagaji damu kwasababu ardhi ilikuwa ni msingi wa nchi pamoja na misingi ya uhuru. Na njia pekee ya kupata ilikuwa kwa  njia ya umwagaji wa damu”. Alisema Malcom X Aliendelea kuzungumzia mapinduzi ya Ufaransa na kuonyesha kuwa mapinduzi hayo yalikuwa ni baina ya wenye ardhi na wasio na ardhi kwa hivyo mapinduzi hayo pia yalikuwa ni ya ardhi. Je, walipataje? Walipata kwa njia ya umwagaji wa damu. Je, hakukuwa na wapendwa waliopotea, je, kulikuwa hakuna maelewano wala  majadiliano? Mimi ninachoona ni kwamba  wengi wetu  hatujui uhuru maana yake ni nini? Lakini siku tukijua  tutakubaliana na msemo huu kuwa hakuna mapinduzi ya ukweli ambayo hayakuhusisha umwagaji wa damu.

Hiyo ndiyo tafsiri ya sehemu ya hotuba ya Malcom X ambaye jina lake halisi ni Malcolm Little ambaye vile vile alijulikana kama El-Hajj Malik El-Shabazz. Alikuwa ni Mmarekani mweusi na mpigania haki za binadamu, kwa mashabiki wake alijulikana kama kiongozi jasiri wa kutetea haki za watu weusi. Aliweza kuwashutumu wa Marekani weupe kwa kutumia lugha kali dhidi ya watu weusi na zaidi wakati walipokuwa wakiwadhulumu.Wapinzani wake walikuwa wakimtuhumu kwa kuhubiri ubaguzi wa rangi, na vurugu. Lakini wote wanakiri kuwa alikuwa Mmarekani mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika historia ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.

Nimeyakumbuka hayo leo kutokana na migogoro isiyoisha na ambayo kwa sasa inapelekea umwagaji wa damu, wakati huohuo nafikiria je, Tanzania tunamuhitaji Malcom X wetu ili atupe njia mbadala wa kutatua migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ni kero. Na je, ni kwamba njia ambazo Baba wa taifa Mwl. Julius K. Nyerere alizipigania na kuzifundisha zimeshindwa?

Nikiwa bado natafakari hayo ya Malcom X, nakwenda mbali kujaribu kuangalia mali ni kitu gani? Kwa tafsiri ya haraka haraka mali ni kitu chochote ambacho kinaweza kushikika ambacho humilikiwa na mtu mmoja au kundi la watu. Kulingana na asili yake, mmiliki wa mali ana haki ya kutumia, kwa kula, kuuza, kukodisha, kutumia kupata kipato, mikopo, kubadilishana au kuharibu mali hiyo, na kuwazuia  wengine kufanya mambo hayo.

Ibara ya 17 ya Azimio la Haki za Binadamu ( Universal Declaration of Human Rights (UDHR) inasomeka “kila mmoja ana haki ya kuwa na mali yake binafsi au kwa kushirikiana na wengine na hakuna mtu au kundi la watu watakaochukua  kiholela mali yao. Aidha ibara ya 24 ya katiba yetu ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasomeka kwamba kila mtu ana haki ya kumiliki mali na ana haki ya ulinzi wa mali yake kwa mujibu wa sheria.

Haki ya kumiliki mali Tanzania imeendelea kukiukwa kutokana na baadhi ya mambo kubwa likiwa ni ukosefu wa uongozi bora, viongozi wala rushwa, uwekezaji, kuongezwa kwa hifadhi, uporaji holela wa ardhi na kukosekana kwa sera za kiuchumi na kijamii za kutosha kulinda maslahi ya jamii dhidi ya shinikizo la mali.

Ardhi ni moja ya mali nitakazo zizungumzia leo, sheria zinazosimamia umiliki wa ardhi msingi ni Sheria ya Ardhi namba 4 ya mwaka 1999 na ile ya Vijiji namba 5 ya mwaka 1999. Chini ya sheria ya ardhi kuna vifungu kadha vinavyo igawa ardhi ikiwa ni pamoja na ardhi inayosimamiwa na vijiji  katika ngazi ya chini ambayo inaruhusu kijiji kutoa cheti cha umiliki au hati ya umilikaji kwa mtu au taasisi yeyote.

Kwa upande mwingine, katika sheria ya Tanzania ya Ardhi ya 1967 inatoa ruhusa kuchukuliwa kwa ardhi kwa matumizi au madhumuni ya umma katika uhusiano na mipango ya makazi.  Sheria hii inahatarisha haki  binafsi kwa ajili ya maslahi ya umma na hivyo kukinzana na haki binafsi ya kumiliki mali kama zinavyoainishwa na Katiba ya Tanzania.

Makundi ya Watanzania wasio na hatia wamekuwa wakiondolewa kinyume cha sheria kutoka katika maeneo yao ambayo waliishi kwa miaka mingi. Katika maeneo ya vijijini na mijini, kufukuzwa kwao kunafanyika bila ya kufuata michakato yoyote ya kisheria.

Kuna idadi ya migogoro inayoendelea kuhusiana na umiliki wa mali Tanzania  ikiwa ni pamoja na uvunjaji wa nyumba Kipawa, migogoro ya ardhi Hanang, kufukuzwa kwa watu katika hifadhi ya Ngorongoro, mgogoro wa ardhi Kilosa, migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika bonde la Ruipa katika Wilaya ya Kilombero na mgogorojuu ya utengaji wa ardhi katika eneo la pori tengefu la Loliondo (LGCA).

Mwaka 1997  serikali ya Tanzania ilitaka kupanua uwanja wa ndege wa Julius Nyerere International Airport. upanuzi wa uwanja wa ndege ulitakiwa kuchukuwa eneo kubwa la kata ya Kipawa. Ili kuwezesha upanuzi, wakazi wa Kipawa walibidi waondolewe. Serikali  kupitia mamlaka ya Uwanja wa Ndege, alionyesha nia yake ya kulipa fidia kwa wakazi wa Kipawa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi ya Upataji, 1967 na wakati huo sheria mpya ya ardhi ilikuwa bado kupitishwa.

Serikali ilifanya tathmini ya mali ya wakazi wa Kipawa mwaka 1997 kwa kutumia Sheria ya Ardhi ya Upataji wa 1967. Serikali ilifikia uamuzi wa kuwalipa wakazi wa Kipawa mwaka 2009 kwa kutegemea tathmini iliyofanywa mapema mwaka 1997 yaani miaka kumi na miwili iliyopita.

Wengi wa wakazi wa Kipawa  hawakuridhika na hoja kuwa sheria husika iliyopaswa kutumika kuwalipia ni hile ya mwaka 1967. Baadhi ya wakazi walikubaliana na hilo na kupokea fidia iliyotolewa chini ya sheria ya ardhi ya upatikanaji ya mwaka 1967, wakati wengine, chini ya msaada wa kisheria kutoka kitengo cha haki za binadamu cha LHRC, waliamua kuchukua hatua za kisheria kuhoji uhalali wa matumizi ya sheria ya Ardhi ya mwaka 1967. wakazi waliohojiwa walidai kunyimwa haki yao ya

kutosha ya fidia, kwa sababu takwimu na tathimini iliyotumika ilikuwa ya mwaka 1997 chini ya kifungu 14 (a) na 15 (1) cha Sheria ya manunuzi ya ardhi.

Chakushangaza  mwezi wa pili tarehe 5, 2010 wananchi waliokuwa wanaishi Kipawa waliamishwa ghafla na kwa ukatili, wakazi wengi walipoteza mali zao na kubakia hawana makazi. Majengo yapatayo 333 yalibomolewa ndani ya siku 2. Kulingana na ripoti ya LHRC ilisema kuwa kutokana na uamuzi huo wa kuwahamisha watu ghafla kulipelekea madhara makubwa kwa familia husika ambazo zilikuwa na haki ya kubaki katika maeneo yao ya makazi.

Wakazi wengi wa Kipawa walishindwa kutumia ardhi zilizotengwa kwa ajili yao kutokana na ukweli kuwa serikali haikuwalipa wananchi wengi waliokuwa wanamiliki ardhi hiyo awali. Wakati wa uchunguzi uliyofanywa na LHRC mara baada ya uvunjaji wa nyumba za wakazi wa Kipawa, shirika hilo liliweza kusajili malalamiko kutoka kwa baadhi ya waathirika.

“Naishi kwenye mwembe na wenyeji wangu hapa Chanika tuliko hamishiwa wananiambia nikijenga utakiona cha moto, naomba mungu mvua isinyeshe awali nilikuwa na vyumba 14 kule Kipawa sasa nalala nje pia watoto hawaendi shule tena hatuna viwanja na fedha hizo chache tunakula. Vitu vimeteketea huko kipawa na nimelipia Kiwanja hapa Chanika mpaka leo kiwanja nilichopewa No. 853 kina mgogoro na kesi zipo mahakamani”. Haya ni sehemu ya malalamiko yaliyo sajiliwa

Kwa ujumla  mchakato mzima wa watu kuhamishwa kutoka Kipawa ulikuwa na tatizo kwasababu Serikali haikuzingatia haki za watu kama zinavyoelekezwa kwenye sheria ya nchi. Sehemu ya 3 (1) g, ya Sheria ya Ardhi  ya 1999 inaeleza kwa  ukamilifu, fidia ya haki na kamilifu italipwa kwa mtu yeyote ambaye ana haki ya kumiliki ardhi, au kutambuliwa kuwa hayo ni makazi yake kwa muda mrefu, au matumizi ya ardhi ya kimila yakibadilika au kuingiliwa na serikali na hivyo kusababisha hasara kwa mmiliki.

Kuhamishwa kwa wakazi wa Kipawa na serikali bila ya kufuata mchakato wa sheria zake zenyewe, kwa ujumla wake ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Kwahiyo zoezi la uharibifu lililofanywa ilikuwa ni kinyume cha sheria. Serikali imeshindwa kuzingatia misingi ya utawala bora na haki za binadamu wakati wa zoezi zima la kuwahamisha wakazi wa Kipawa.

Mwishoni mwa mwaka jana, asasi isiyo ya kiselikali ya muungano wa wafugaji wa asili (PINGOs Forum) waligundua kwamba wakulima, wafugaji na wawindaji wenye asili ya Barbaig hasa kutoka katika kijiji cha Endagula katika wilaya ya Mbulu, waliondolewa kwa nguvu kutoka kwenye mkazi yao.

Uchunguzi uliyofanywa na PINGOs Forum uligundua kwamba wafugaji walizuiwa na serikali ya wilaya kutumia rasilimali kama vile maji na ardhi ya malisho katika msitu tengefu katika kijiji cha Endagula.

DC wa Wilaya ya Mbulu Bw. Anthony Choya, alikiri kuwa kulikuwa na tatizo katika kijiji cha Endagula, ila tatizo lilimalizika. Bw. Choya alisisitiza kuwa kufukuzwa kwa nguvu kwa wakazi hao kulifanywa bila kukiuka maadili ya sheria na haki yoyote ya jamii hizo za asili. Alisisitiza kuwa tatizo kubwa lilikuwa ni kukosekana kwa mpaka wa wazi kati ya kijiji na msitu huo tengefu.

Sote tunakumbuka sakata la Loliondo, kuhusu kufukuzwa kwa wananchi kutoka katika pori tengefu ambalo iliibua mjadala mkali wakati wa mijadala ya bunge 2009, na pia katika taifa na majukwaa ya kimataifa. Hii ilitokea baada ya wananchi kuamishwa kwa nguvu kutoka katika Wilaya ya Ngorongoro Loliondo-Julai mwaka 2009 na vikosi vya polisi kwa kushirikiana na kampuni ya uwindaji wa Kiarabu inayojulikana kama Ortelo Bussiness Coperation (OBC), inayofanya shuguli zake Loliondo.

Swala hili baadaye lilifikishwa Bungeni na majadiliano makali yalizuka. Na kupelekea kuundwa kwa tume ya  kamati ya bunge kuchunguza jambo hilo. Akihutubia bungeni, mmoja wa wabunge alitoa maneno makali akishutumu serikali kuwaunga mkono wawekezaji wa kigeni kwa gharama ya watu wake.

“Mbona Mwalimu Nyerere alikuwa anawakatalia hata Wazungu mambo mengi tu! Lakini siku hizi sisi tunawakumbatia sana wawekezaji, tunaacha kuwasikiliza wananchi.” Chanzo: – Hansard ya Bunge ya 9 (2009) ya 16 ya Bunge kikao-27, ukurasa wa 96.

Bila ya sababu yoyote ya msingi, ripoti ya Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza kufukuzwa kwa wakazi wa Loliondo haikuwahi kutolewa Bungeni. kushindwa kwa kamati hiyo ya bunge kuwasilisha ripoti ya wazi ilikuwa na maana ya bunge kushindwa kuiwajibisha serikali.

Uchunguzi uliofanywa ulibaini kuwa kushindwa kuwasilisha ripoti ilikuwa ni kwa makusudi kwa sababu viongozi wa serikali na makundi mengine ya watu waliohusika ikiwa ni pamoja na maafisa wa kampuni hiyo ya OBC kulaumiwa katika ripoti kwa ukiukwaji wa haki za binadamu.

Wakati serikali, Bunge na wanaharakati wengine wa haki za binadamu wamekuwa wakisita kukabiliana na unyama huo uliofanyika mwaka 2009. Baadhi ya asasi na mashirika yasiyo ya kiserikali ya kupigania haki, ya jijini Arusha yamefungua kesi kuhakikisha kuwa haki inatendeka.

Kama mchakato wa kuondoa wafugaji wenyeji wa loliondo utafanikiwa basi karibu 75% ya eneo la Ngorongoro itagawiwa kwa ajili tu ya matumizi ya wanyamapori na utalii na kuwafukuza wafugaji bila rasilimali muhimu kama ardhi ya malisho na maji kwa ajili ya kuendesha maisha yao.

Hili lilisisitizwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Ezekiel Maige ambaye alitembelea Loliondo mwishoni mwa mwaka jana katika jitihada za kukabiliana na tuhuma mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya magazeti yakidai kwamba pori tengefu la  Loliondo linakufa.

“Mimi sasa naondoka Loliondo, hata hivyo  lazima wote tuelewe kwamba ziara yangu siyo kwa ajili ya utenganifu wa ardhi ya kijiji lakini badala yake nilikuja kuthibitisha uvumi wa baadhi ya vyombo vya habari kwamba Wamasai wa Loliondo kwa msaada wa mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za kidini wameharibu maeneo ya asili ya Loliondo. Chakushangaza, nimeona kinyume na baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti. Hivyo nauambia umma kuwa  unapaswa kufahamu kwamba utekelezaji wa mpango wa kutengeneza mshorobo bado utaendelea, lakini hii haitakuwa mapumziko yetu ya mwisho baada ya jaribio la hatua nyingine ” alisema Waziri Maige

Utengefu wa ardhi ya kijiji halikuwa suala kuu wakati wa ziara ya Mh. Ezekiel Maige lakini madiwani wa Loliondo na wanakijiji walikiri kuwa Waziri aliwaeleza mpango wa kugeuza ardhi ya Loliondo kuwa Mshorobo uko pale pale.

Mshorobo ina maana ya eneo la hifadhi ambalo Waziri anaweza, kwa kutoa taarifa katika Gazeti la Serikali kutangaza kutenga eneo hilo, na kulifanya  kutumika kwa ajili ya utalii na wanyamapori peke. Hatua hiyo inampa waziri uwezo wa kuitoa ardhi hiyo kutoka katika maeneo ya vijiji.

Image

Advertisements

KUVUANA GAMBA NA KUFUKUZANA UANACHAMA BILA KUTATHMINI GHARAMA

Taarifa za kufukuzwa uanachama au kuvuana gamba si jambo geni katika nchi hii; au ulimwengu wa sasa. Pindi mtu anapokwenda kinyume na utaratibu na kuonekana hawezi kurekebishika kwenye jamii au chama basi kunakuwa hakuna budi iwe ni kwa chama ama kwa mtu binafsi kumuomba awapishe kwa kuwa wanachokuwa wanakipigania, wanachokitarajia au kukiamini sio kimoja tena.

Lengo letu hapa si kupinga au kuingilia maamuzi ya jamii au vyama ambavyo vimechukua maamuzi magumu ya kuwaondoa wanachama wenzao. Lengo letu kubwa ni kiasi gani wananchi wa kawaida wanaumia kutokana na maamuzi hayo.

Ni gharama kiasi gani zinatumika au kuelekezwa katika uandaaji wa chaguzi ndogo, na je, fedha hizo kwa busara ya kawaida zisingeweza kutumika kwa kuelekezwa katika mambo muhimu ya kuwakomboa wananchi wa kawaida katika dimbwi la umaskini?

Kwa mfano taarifa zinasema kuwa katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkoani Tabora, chama cha mapinduzi kilitumia takribani shilingi billion 3 na huku mmoja wa wanachama wake akiwapa ufadhili wa helikopta. Nacho  chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinasadikiwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 400.  Na fedha hizo ni za vyama viwili tu vilivyoshiriki mbali na serikali na vyama vingine. Taarifa zinasema serikali hutumia takribani shilingi milioni 400 katika uchaguzi mdogo wa kila jimbo. Hebu tujiulize hizo fedha kama zingeelekezwa kwenye miradi ingewakomboa wangapi?

Kwanini katiba isionyeshe kwa uwazi au kutamka njia ya kufuata pindi tatizo Kama hilo litakapo jitokeza? Njia itakayoliokoa taifa katika janga la kutumia mabilioni ya shilingi kila baada ya miaka miwili katika uchaguzi? Au busara na uzalendo zitumike kwa viongozi wa vyama pendwa ili kufikia maamuzi ambayo hayataleta mzigo mkubwa kwa jamii husika.

Mathalan chama kingeweza kuchukua hatua kali za kumfungia mkosaji kwa kutojihusisha na kazi za chama kwa muda wote wa maisha yake. Hii ikiwa na maana atabaki kuwa mbunge au diwani lakini pindi muda wake utakapokwisha hataweza tena kugombea nafasi yoyote kupitia chama hicho.

Tunajua kila chama kinahitaji uwakilishi katika vyombo husika, na hivyo basi pamoja na kumpa adhabu ya kutoshiriki siasa za chama wamlazimishe muhusika kuendana na sera na ilani ya chama kilichomuweka madarakani. Hilo kwa muhusika nafikiri ataweza kulitekeleza pamoja na utovu wake wa nidhamu.

“Sisi tunaona katika siku za usoni migogoro inakaribia kuwa ni moja ya maisha yetu ya kawaida, na ndicho kinachotufanya sisi kutetemeka kwa ajili ya majaliwa ya nchi yetu. Bila busara kutumia au kubadilisha katiba tunapoelekea ni kubaya sana”. Alisema mmoja wa wadau wa masuala ya kisiasa nchini Bw. Richard Medutieki.

Hayo ya NCCR-Mageuzi siyo ya kwanza kutokea, tuliona yaliyomkuta mbunge wa wakati huo ambaye alikuwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mh. Augustin Lyatonga Mrema, kabla ya kuamua kuhamia TLP. Tumeshuhudia ya Rostam Aziz wa Igunga ambaye alijivua ubunge pamoja na ujumbe wa NEC na sasa mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila wa NCCR-Mageuzi. Orodha hii ndefu haiwezi kuacha kuwazungumzia madiwani wa CHADEMA mkoani Arusha ambao nao walikumbwa na kizaa zaa hicho, na wala msifikirie hilo litaishia hapo ila kwa sasa tunajiweka tayari kusubiria linaloweza kutokea CUF huko Wawi.

Kitu kingine kinachotukera sisi ni kazi wanazobebeshwa wawakilishi wa wananchi wa kulazimika kukubalina na viongozi wao hata kama hoja zao zinakuwa hazina maslahi kwa wananchi walio wachagua wawakilishi hao, na wasipo fanya hivyo basi wajuwe watafukuzwa na kupoteza nafasi ya uwakilishi wao.

Tukijiuliza kwa makini na kufanya uchunguzi ni viongozi wangapi wamechaguliwa kutokana na sifa ya chama tu unaweza kushangaa. Ukweli ni kwamba sifa ya chama na umaarufu wake ni muhimu lakini bila kuwa na mtu makini ni vigumu kwa wananchi kumchagua au kumpatia nafasi ya uongozi mtu kwa sifa ya chama chake tu.

Tukijaribu kuangalia tatizo la NCCR utagundua ni mgawanyiko wa wazi wa wajumbe ulijikita zaidi kwenye mpasuko unaotokana na tofauti za kimsimamo kati ya Mwenyekiti wa chama hicho Bw. James Mbatia na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila. Na siku ya maamuzi hayo ilipangwa kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti wa chama hicho.

Taarifa zilieleza kwamba, mvutano mkubwa uliokuwapo ndani ni wa kupinga kura za kutokuwa na imani na Bw. Mbatia, inadaiwa kuwa Bw. Mbatia aliibuka mshindi kwa kura 40 za kuwa na imani naye dhidi ya nane zilizomkataa na mbili kuharibika. Kikao hicho kilikuwa na wajumbe 59, wakiwapo wabunge watatu wa chama hicho.

Je, ugomvi huu una maslahi na watu wa Kigoma Kusini? Ni kwa faida ya nani tunathubutu kuliingiza taifa kwenye uchaguzi mdogo utakaoligharimu taifa letu mamilioni ya shilingi. Je, tukiitwa wasaliti na wananchi ambao ndio wanaotuweka madarakani kwa kuelekeza fedha nyingi katika sehemu zisizokuwa na tija na kuwaacha wao wakiwa hata hawajui kuwa mlo wa siku hiyo utakuwa nini ama watashinda na kulala njaa watakuwa wamekosea?

Wakati huohuo je, fedha hizo zisingeweza kuwasaidia wakinamama wengi ambao ni wajawazito na wanaishi mbali na vituo vya afya na huku kipato chao kikiwa ni kidogo katika kujifungua salama bila ya kupatwa na madhara yoyote ikiwa ni pamoja na ya kupoteza mtoto ama mama kufariki?.

Hata ukijaribu kuangalia faida ambazo chama hicho kilichoamua kuchukua maamuzi hayo kinapata je, ni kubwa kuliko hasara ambazo watapata? Na hata wajumbe wa mkutano huo ambao walisikiliza hoja na kuamua kupitisha maamuzi hayo ya kumfukuza  uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, walitakiwa kuwa makini ili wasije wakakirejesha chama hicho kwenye vyama visivyo na wabunge.

Kauli hiyo ilisisitizwa na Dk Sengodo Mvungi ambaye alisema NCCR imetoka katika mazingira mabaya kisiasa kwa kutokuwa na mbunge hata mmoja, hivyo chokochoko za kumfukuza Kafulila, zinarudisha nyuma maendeleo ya chama.

Naye Bw. Kafulila aliwataka wajumbe wawe watulivu na kuongeza kuwa pamoja na kuwa yupo  kwenye mgogoro na Bw. Mbatia, wazee wa chama ndiyo wanaoweza kutumia busara kuwasuluhisha. Bila kutafakari mambo yafuatayo yatatuangamiza: siasa bila ya kanuni; radhi bila ya dhamiri, na mali bila kazi; elimu bila ya tabia, biashara bila maadili, sayansi bila ya ubinadamu, na ibada bila sadaka.

Kama hali itaendelea kuwa ni hii ya kila kukicha kunakuwa na habari ya tofauti na ya siku iliyopita juu ya matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi kweli kauli ya “Kuondoa ama kupunguza umasikini Tanzania hadi ifikapo 2015 na ajira kwa kila mtanzania itawezekana kweli?”

Image

UFAULU DARASA LA SABA KUONGEZEKA SAMBAMBA NA UCHAKACHUAJI, NANI ALAUMIWE?

Hivi karibuni yalitangazwa matokeo ya darasa la saba ambapo inaonekana kuwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi mwaka huu kimeongezeka kwa asilimia 4.76 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo ongezeko hilo limekwenda sambamba na ongezeko la asilimia 1.0 ya udanganyifu na hivyo wizara kuwafutia matokeo wanafunzi 9,736

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema wanafunzi 567,567 kati ya 983,545 waliofanya mtihani wamefaulu ambayo ni sawa na asilimia 58.28, ambapo mwaka jana, wanafunzi waliofaulu walikuwa asilimia 53.52.

“Pamoja na takwimu kuonesha kiwango cha ufaulu kinaongezeka, inasikitisha kuona kiwango cha udanganyifu mwaka huu kimeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana na tayari changamoto hii imeanza kufanyiwa kazi, ili kuwabaini wadanganyifu waliopita kwa njia mbalimbali, Serikali imeamua kuwa wale watakaojiunga na elimu ya sekondari mwakani, watafanya mtihani wa majaribio kupima stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu kabla ya kuanza masomo rasmi.” alisema Bw. Mulugo.

Hapo ndipo tunashindwa kukubaliana na maamuzi hayo ya serikali. Kwanza tunavyo fahamu sisi na bila shaka hata enzi za Mheshimiwa huyo hatua ya kujua kusoma, kuandika na kuhesabu ni ya darasa la pili, hivyo mwanafunzi dhabiti anayepaswa kuitwa mawanafunzi akifika darasa la pili anapaswa kujua kusoma na kuandika.

Kama mwanafunzi huyo hajuhi kusoma wala kuandika angefaulu vipi mtiani wa darasa la nne? Au udanganyifu umeanzia huko? Kama Bw. Mulugo ameweza kubaini kuwa kulikuwa na udanganyifu wa aina nne na uchunguzi wake kuweza kuwausisha hadi wataalamu wa miandiko anashindwa nini kutunga mtihani mwingine wenye vigezo vinavyo kubalika hili kuwabaini wanafunzi waliodanganya? Je katika mika 50 hii ndiyo Tanzania tunayoitaka? Isiyokuwa na uwajibishwaji, kwa kupeleka mambo kiolela olela tu.

Suala la gharama siyo tija, na wala haliingi akilini kabisa. Nakumbuka nilipokuwa nataka kuingia darasa la kwanza nilijaribiwa kwa kusoma kuhesabu na kuandika. Je inamaana kwa sasa hicho ndicho kipimo cha kujiunga na sekondari? Tunategemea wanafunzi kama hao waje wawe wataalamu kweli? Hivi tunaipeleka wapi nchi yetu?

Kutokana na Taarifa ya wizara husika Manyara imeongoza kwa uchakachuzi, ambapo wanafunzi 1,573 walihusika, ikifuatiwa na Arusha 1,012. Hii inaonyesha kuwa wizara inajua shule, wasimamizi na waalimu waliohusika kwenye udanganyifu huu. Lakini tofauti na wanafunzi kupewa adhabu hiyo hatujasikia shule, walimu au wasimamizi walio chukuliwa hatua? hii inamaanisha nini?

Wanafunzi wa shule za msingi ni wadogo sana kuweza kutengeneza mbinu na kufaulu katika udanganyifu kama huu bila msahada. Watoto wa umri huo awana uwezo wa kununua au kulipia udanganyifu kama huo. Lazima walipata msaada mkubwa kutoka kwa wazazi na waalimu husika.

Na hata kama mitiani hiyo ikirudiwa huko sekondari, je tuna uhakika gani kuwa mkono mrefu wa hao wachakachuaji hautatumika tena huko? Kama mitiani waliofanikiwa kuichakachua ilikuwa ikilindwa na vyombo husika vya usalama na bado hilo likafanyika je tuna uhakika gani hilo halitatokea tena uko sekondari?

Kwa kawaida mtihani mpaka ufike kwenye chumba cha mtihani kuna hatua mbalimbali unapitia ukiwa chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya usalama. Tunaambiwa kuna maeneo mengine mitihani ilipelekwa kwa baiskeli huko Vijijini hivyo ni wazi kwamba mazingira yalikuwa yameandaliwa kwa makusudi ili mtihani uvuje.

Kwanini Wizara isifanye uchunguzi wa kina kujua nani mhusika wa uvujaji wa mtihani ili kama anayo kesi ya kujibu  ajibu? Bila kujali matatizo ya walimu na mfumo mzima wenye matatizo kinachotuuma sisi ni mzigo mzima kubebeshwa wanafunzi ambao ni wadogo na ambao wanachwa bila kujua hatima yao kimaisha majumbani mwao.

Naungana na wadau wa Elimu wanaosema kuwa watu wa kulaumiwa sio wanafunzi ila ni wasimamizi wa wanafunzi hao. Wadau hao kwa pamoja walilalamikia mfumo wa elimu nchini kuwa umejaa utabaka na kuwa haufai kwa sababu umetawaliwa na kasoro nyingi ikiwemo rushwa, mfumo mbovu wa ufundishaji na usimamizi wa mitihani usiokuwa thabiti.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Bashiru Ally alinukuliwa akisema “Matokeo haya yanaonyesha picha kamili ya jamii tuliyopo sasa na hii inaonyesha ni kutokana na mfumo uliopo sasa kwa kuwa na elimu iliyojaa utabaka kwa walio nacho na wasio nacho,”.

Mfumo wa sasa unasababisha utitiri wa shule za binanfsi na ambazo wamiliki wake wanachojali ni maslahi yao kwa kutafuta mbinu ambazo si halali, kwani hakuna mmiliki wa shule anayependa kuona shule yake inafanya vibaya na hapo ndipo mbinu mbadala hutafutwa kwa ajili ya kufaulisha wanafunzi hao ili shule yake izidi kupata jina na kufanikiwa kibiashara.

Serikali inapaswa kufanya uchunguzi kutafuta ni akina nani wanamiliki shule hizo zilizoshiriki katika uchakachuaji kisha hatua stahiki kuchukuliwa pasipo kujali zinamilikiwa na nani.

Maoni kama hayo yalitolewa pia na Mhadhiri mingine  wa Chuo, Dk Tillya Mkumbo ambaye alisema wa kuadhibiwa sio wanafunzi bali ni waliowapatia majibu au kuwasaidia wanafunzi hao katika mitihani ambao wanafahamika.

Tungeomba busara itumike badala ya kuwaadhibu  watoto hao ambao ushahidi unaonyesha wazi kuwa walirubuniwa kwa kuwapa nafasi ya kurudia tena mitiani yao. Tena wasisubiri mpaka mwakani jambo hilo lifanyike haraka hili wajiunge na wenzao.

Na hata baba Askofu mkuu wa Kanisa katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadnali Pengo alipokuwa anatoa salama za krismas alilizugumzia suala hili kwa kusema kuwa suala la elimu linaonyesha hali ya kutoridhisha kwa taifa. Pengo alisema tatizo la elimu liko katika pande zote na kusisitiza zinahitajika nguvu za pamoja katika kushughulikia suala hilo.

Inatupasa hata sisi kukumbuka kuwa sio sawa kuchukulia elimu tuliyopata kama mali yetu au juhudi zetu binafsi, kwasababu kama ilivyo demokrasia na uhuru, upatikanaji wake umehusisha watu wengi na ni vigumu kujuwa walijitoa  kiasi gani kufanikisha upatikanaji wa hayo tuliyo nayo leo, hivyo hivyo serikali yetu tunaiomba ijitoe ili kuwafanikishia hao watoto wa wakulima na wafanyakazi waweza kupata elimu.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi pia kuzungumzia suala la Elimu, na kusema kuwa mtu anayeipata aitumie kama nyenzo ya ukombozi wake mwenyewe na jamii yake, na si ili kujisifu kuwa amesoma, huku elimu hiyo haimsaidii chochote yeye mwenyewe wala jamii yake. Hivyo tunashauri serikali iangalie kwa makini uchakachuaji huu ulipoanzia na kuchukua hatua, pamoja na wasomi nchini kuitumia elimu kwa manufaa na si kujisifu.