KUVUANA GAMBA NA KUFUKUZANA UANACHAMA BILA KUTATHMINI GHARAMA

Taarifa za kufukuzwa uanachama au kuvuana gamba si jambo geni katika nchi hii; au ulimwengu wa sasa. Pindi mtu anapokwenda kinyume na utaratibu na kuonekana hawezi kurekebishika kwenye jamii au chama basi kunakuwa hakuna budi iwe ni kwa chama ama kwa mtu binafsi kumuomba awapishe kwa kuwa wanachokuwa wanakipigania, wanachokitarajia au kukiamini sio kimoja tena.

Lengo letu hapa si kupinga au kuingilia maamuzi ya jamii au vyama ambavyo vimechukua maamuzi magumu ya kuwaondoa wanachama wenzao. Lengo letu kubwa ni kiasi gani wananchi wa kawaida wanaumia kutokana na maamuzi hayo.

Ni gharama kiasi gani zinatumika au kuelekezwa katika uandaaji wa chaguzi ndogo, na je, fedha hizo kwa busara ya kawaida zisingeweza kutumika kwa kuelekezwa katika mambo muhimu ya kuwakomboa wananchi wa kawaida katika dimbwi la umaskini?

Kwa mfano taarifa zinasema kuwa katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Igunga mkoani Tabora, chama cha mapinduzi kilitumia takribani shilingi billion 3 na huku mmoja wa wanachama wake akiwapa ufadhili wa helikopta. Nacho  chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinasadikiwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 400.  Na fedha hizo ni za vyama viwili tu vilivyoshiriki mbali na serikali na vyama vingine. Taarifa zinasema serikali hutumia takribani shilingi milioni 400 katika uchaguzi mdogo wa kila jimbo. Hebu tujiulize hizo fedha kama zingeelekezwa kwenye miradi ingewakomboa wangapi?

Kwanini katiba isionyeshe kwa uwazi au kutamka njia ya kufuata pindi tatizo Kama hilo litakapo jitokeza? Njia itakayoliokoa taifa katika janga la kutumia mabilioni ya shilingi kila baada ya miaka miwili katika uchaguzi? Au busara na uzalendo zitumike kwa viongozi wa vyama pendwa ili kufikia maamuzi ambayo hayataleta mzigo mkubwa kwa jamii husika.

Mathalan chama kingeweza kuchukua hatua kali za kumfungia mkosaji kwa kutojihusisha na kazi za chama kwa muda wote wa maisha yake. Hii ikiwa na maana atabaki kuwa mbunge au diwani lakini pindi muda wake utakapokwisha hataweza tena kugombea nafasi yoyote kupitia chama hicho.

Tunajua kila chama kinahitaji uwakilishi katika vyombo husika, na hivyo basi pamoja na kumpa adhabu ya kutoshiriki siasa za chama wamlazimishe muhusika kuendana na sera na ilani ya chama kilichomuweka madarakani. Hilo kwa muhusika nafikiri ataweza kulitekeleza pamoja na utovu wake wa nidhamu.

“Sisi tunaona katika siku za usoni migogoro inakaribia kuwa ni moja ya maisha yetu ya kawaida, na ndicho kinachotufanya sisi kutetemeka kwa ajili ya majaliwa ya nchi yetu. Bila busara kutumia au kubadilisha katiba tunapoelekea ni kubaya sana”. Alisema mmoja wa wadau wa masuala ya kisiasa nchini Bw. Richard Medutieki.

Hayo ya NCCR-Mageuzi siyo ya kwanza kutokea, tuliona yaliyomkuta mbunge wa wakati huo ambaye alikuwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Mh. Augustin Lyatonga Mrema, kabla ya kuamua kuhamia TLP. Tumeshuhudia ya Rostam Aziz wa Igunga ambaye alijivua ubunge pamoja na ujumbe wa NEC na sasa mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila wa NCCR-Mageuzi. Orodha hii ndefu haiwezi kuacha kuwazungumzia madiwani wa CHADEMA mkoani Arusha ambao nao walikumbwa na kizaa zaa hicho, na wala msifikirie hilo litaishia hapo ila kwa sasa tunajiweka tayari kusubiria linaloweza kutokea CUF huko Wawi.

Kitu kingine kinachotukera sisi ni kazi wanazobebeshwa wawakilishi wa wananchi wa kulazimika kukubalina na viongozi wao hata kama hoja zao zinakuwa hazina maslahi kwa wananchi walio wachagua wawakilishi hao, na wasipo fanya hivyo basi wajuwe watafukuzwa na kupoteza nafasi ya uwakilishi wao.

Tukijiuliza kwa makini na kufanya uchunguzi ni viongozi wangapi wamechaguliwa kutokana na sifa ya chama tu unaweza kushangaa. Ukweli ni kwamba sifa ya chama na umaarufu wake ni muhimu lakini bila kuwa na mtu makini ni vigumu kwa wananchi kumchagua au kumpatia nafasi ya uongozi mtu kwa sifa ya chama chake tu.

Tukijaribu kuangalia tatizo la NCCR utagundua ni mgawanyiko wa wazi wa wajumbe ulijikita zaidi kwenye mpasuko unaotokana na tofauti za kimsimamo kati ya Mwenyekiti wa chama hicho Bw. James Mbatia na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila. Na siku ya maamuzi hayo ilipangwa kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti wa chama hicho.

Taarifa zilieleza kwamba, mvutano mkubwa uliokuwapo ndani ni wa kupinga kura za kutokuwa na imani na Bw. Mbatia, inadaiwa kuwa Bw. Mbatia aliibuka mshindi kwa kura 40 za kuwa na imani naye dhidi ya nane zilizomkataa na mbili kuharibika. Kikao hicho kilikuwa na wajumbe 59, wakiwapo wabunge watatu wa chama hicho.

Je, ugomvi huu una maslahi na watu wa Kigoma Kusini? Ni kwa faida ya nani tunathubutu kuliingiza taifa kwenye uchaguzi mdogo utakaoligharimu taifa letu mamilioni ya shilingi. Je, tukiitwa wasaliti na wananchi ambao ndio wanaotuweka madarakani kwa kuelekeza fedha nyingi katika sehemu zisizokuwa na tija na kuwaacha wao wakiwa hata hawajui kuwa mlo wa siku hiyo utakuwa nini ama watashinda na kulala njaa watakuwa wamekosea?

Wakati huohuo je, fedha hizo zisingeweza kuwasaidia wakinamama wengi ambao ni wajawazito na wanaishi mbali na vituo vya afya na huku kipato chao kikiwa ni kidogo katika kujifungua salama bila ya kupatwa na madhara yoyote ikiwa ni pamoja na ya kupoteza mtoto ama mama kufariki?.

Hata ukijaribu kuangalia faida ambazo chama hicho kilichoamua kuchukua maamuzi hayo kinapata je, ni kubwa kuliko hasara ambazo watapata? Na hata wajumbe wa mkutano huo ambao walisikiliza hoja na kuamua kupitisha maamuzi hayo ya kumfukuza  uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, walitakiwa kuwa makini ili wasije wakakirejesha chama hicho kwenye vyama visivyo na wabunge.

Kauli hiyo ilisisitizwa na Dk Sengodo Mvungi ambaye alisema NCCR imetoka katika mazingira mabaya kisiasa kwa kutokuwa na mbunge hata mmoja, hivyo chokochoko za kumfukuza Kafulila, zinarudisha nyuma maendeleo ya chama.

Naye Bw. Kafulila aliwataka wajumbe wawe watulivu na kuongeza kuwa pamoja na kuwa yupo  kwenye mgogoro na Bw. Mbatia, wazee wa chama ndiyo wanaoweza kutumia busara kuwasuluhisha. Bila kutafakari mambo yafuatayo yatatuangamiza: siasa bila ya kanuni; radhi bila ya dhamiri, na mali bila kazi; elimu bila ya tabia, biashara bila maadili, sayansi bila ya ubinadamu, na ibada bila sadaka.

Kama hali itaendelea kuwa ni hii ya kila kukicha kunakuwa na habari ya tofauti na ya siku iliyopita juu ya matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi kweli kauli ya “Kuondoa ama kupunguza umasikini Tanzania hadi ifikapo 2015 na ajira kwa kila mtanzania itawezekana kweli?”

Image

Advertisements