RIPOTI YA CAG YAONYESHA MAPUNGUFU MAKUBWA KATIKA MATUMIZI YA FEDHA ZA SERIKALI


Image

  • Deni la taifa laongezeka na kufikia Sh. 14.4 trilioni mwaka jana.
  • Serikali yatumia Sh 544 bilioni bila idhini ya bunge
  • Sh. 3 bilioni zatumika kuwalipa watumishi hewa
  • Sh. 2.6 zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za mfuko wa jimbo zayeyuka
  • Sh. 6.5 zashindwa kukusanywa na TRA kutokana na misamaha ya kodi.

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh tarehe 12/04/2012 aliwasilisha ripoti yake bungeni inayoonyesha mapungufu katika matumizi ya fedha serikalini huku deni la taifa likiongezeka kutoka Sh10.5 trilioni mwaka juzi na kufikia Sh14.4 trilioni mwaka jana.

CAG alisema Serikali imetumia Sh 544 bilioni bila kuidhinishwa na Bunge, Sh bilioni moja azijulikani zilipo ila inakisiwa kuwa zimelipwa kama mishahara kwa watumishi hewa na Sh 3bilioni zimetumika katika Balozi za Tanzania nje ya nchi ambazo ziko nje ya bajeti iliyoidhinishwa na bunge.

Utouh akitoa utetezi wake juu ya ongezeko la deni la taifa alisema “Kuna ongezeko kubwa la deni la taifa, lakini hoja hapa si kuongezeka kwa deni la taifa bali ni kwamba deni hili limeletwa kwa mikopo yenye manufaa kwa taifa na yenye kukuza uchumi wa nchi? Hii ndio hoja ya msingi ya kuangalia,”

Akizungumzia mapungufu katika balozi zote 32 zilizokaguliwa Utouh, alisema ukaguzi uliofanywa katika ofisi hizo umebaini kuwapo matumizi yasiyoridhisha na kuwapo kwa Sh3 bilioni ambazo zimetumika nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge la Jamhuri.  Kuhusu Mfuko wa Jimbo (CDCF) ulioanzishwa kwa Sheria ya Bunge, ripoti hiyo inaonyesha kuwa Sh 2.6 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za mfuko huo hazikutumika katika Halmashauri 51 zilizokaguliwa.

Kwa upande wa mashirika ya umma, alisema baadhi yake hayana bodi za wakurugenzi, vikao vya bodi haviitishwi kwa wakati na baadhi ya mashirika hayo huchelewa kukamilisha hesabu zao za mwaka kwa wakati.

Kuhusu misamaha ya kodi, CAG alisema pamoja na wananchi, wabunge na asasi za kiraia kupigia kelele misamaha ya kodi, ukaguzi umeonyesha kuwapo kwa misamaha ya kodi inayofikia Sh1.02 trilioni.

Alifafanua kuwa taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zilionyesha kuwa misamaha ilitolewa kwa taasisi mbalimbali yenye thamani ya Sh1,016,320,300,000 ambazo ni sawa na asilimia 18 ya makusanyo yote nchini.

Kwa mujibu wa Utouh, kama kiasi hicho kisingesamehewa, TRA ingekusanya Sh6.5 trilioni ikiwa ni sawa na Sh717.4 bilioni zaidi ya kiasi kilichokadiriwa kukusanywa ambacho ni Sh6,566,525,544,378.

“Siku zote tumekuwa tukipiga kelele kuhusu misamaha ya kodi ingawa tunasema misamaha ya kodi haiepukiki, lakini lazima isimamiwe na iwe ni lazima kutolewa. kwa kweli eneo la misamaha ya kodi ni la kutazamwa,”alisema.

Alikosoa mfumo mzima wa mchakato wa kupitisha bajeti akisema, mjadala wa bajeti huanza Juni hadi Agosti kila mwaka wakati sheria ya matumizi ya fedha zinazopitishwa hutakiwa kuanza Julai mosi.

Alifafanua kwamba mjadala wa bajeti huanza kwa kujadili bajeti ya taifa ambayo pia hupitishwa kabla ya kuanza kujadili fungu moja moja la bajeti na hivyo, kufanya mchakato mzima wa kupitisha bajeti uonekane ni kugonga tu mhuri.

“Utaratibu huu unafanya mchakato mzima wa bajeti uonekane kama ni zoezi la rubber stamp (kugonga mhuri) kwani wabunge tayari walishapitisha bajeti ya taifa ambayo kimsingi inatokana na bajeti za fungu moja moja,” alisema.

CAG alipendekeza Serikali ijadiliane na Bunge kuhusu uwezekano wa kubadili mzunguko wa bajeti ya taifa ili kuruhusu mabadiliko ya tarehe za majadiliano kukamilika, kabla ya au ifikapo Juni 30 ya kila mwaka.

Katika mapendekezo hayo, CAG alisema mjadala wa wabunge kuhusu bajeti uanze kwa kujadili bajeti za fungu moja moja na bajeti ya taifa iwe ya mwisho kujadiliwa ili kuondoa ile dhana ya kuwa na bajeti isiyo na uhalisia.

Hali katika halmashauri Alisema kuwa ukaguzi maalumu uliofanywa katika halmashauri za wilaya za Sengerema, Ludewa, Kishapu, Kilindi, Moshi, Monduli, Longido na Manispaa ya Ilala umebaini kuwapo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma. CAG pia aliagiza kufanywa ukaguzi maalumu katika Halmashauri za Arusha, Songea, Morogoro, Kilindi na Misungwi kutokana na kutoridhishwa na taarifa za Halmashauri hizo kuhusu matumizi ya fedha za umma.

Advertisements