RIPOTI YA UCHUNGUZI WA UDA IMEKWISHAKABIDHIWA KWA WAZIRI MKUU

Image

  • Hatua zaidi kusubiri maamudhi ya Waziri  Mkuu

  • Watuhumiwa wote waojiwa na CAG

RIPOTI ya ukaguzi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), tayari imekamilika na amekwishaikabidhi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda tangu Aprili 6 mwaka huu kwa ajili ya hatua zaidi. Hayo yalisemwa Aprili 12 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh

Agosti 13 mwaka jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, George Mkuchika alimkabidhi CAG kazi ya ukaguzi wa hesabu za UDA na mchakato mzima wa uuzwaji wa hisa zake ambao unahusisha vigogo mbalimbali akiwemo, Idd Simba.

“Kwa sasa mimi nimeshamaliza kazi yangu ya ukaguzi wa UDA, ambapo Aprili 6 mwaka huu siku ya Ijumaa kuu, ndipo nilipo ikabidhi kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda,” alisema Utouh na kuongeza;

“Kitu ambacho kinatakiwa sasa ni kusubiri ripoti hiyo ipitiwe na Waziri Mkuu ndipo taarifa rasmi nini kilichokaguliwa na kilicho patikana katika ripoti hiyo kitawekwa wazi,” alisema.

Hatua hiyo ilitokana na tuhuma za uuzwaji holela wa hisa milioni 7.8 sawa na asilimia 52.535 za kampuni ya UDA dhidi ya Kampuni ya Simon Group, inayomilikiwa na Robert Kisena uliyoripotiwa na wabunge wa Dar es Salaam Agosti mwaka jana.

Baadhi ya vigogo wanaodaiwa kuhusishwa na kashfa hiyo, ni pamoja na Meya wa Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi, Idd Simba, na Meneja Mkuu wa UDA, Victor Milanzi.

UDA ilikuwa inamilikiwa kwa pamoja na Halmashauri zote za Jiji la Dar es Salaam na Serikali Kuu kupitia Hazina, wakiwa na jumla ya hisa milioni 15, kila hisa moja ikiwa na thamani ya Sh100.

Kutokana na mchanganuo huo, Halmashauri ya Dar es Salaam ilikuwa inamiliki asilimia 51 ya hisa hizo, huku Hazina ikimiliki asilimia 49.

Advertisements