WANAO TAKA URAIS WAJITANGAZE TUPATE MUDA WA KUWAPIMA

Image

Ni mara chache sana kukubaliana na kiongozi wa siasa asiyependa kuongea. Kwa maana uongozi ni pamoja na kuwaeleza unaowaongoza wapi unawapeleka na kwanini unawapeleka huko na siyo kwingine.

Mara nyingi kiongozi mpole na mkimya ni yule asiyependa kufanya makosa. Kwa upande mmoja hilo ni zuri. Lakini kiukweli ni baya sana kwasababu ni kiongozi asiyekuwa na maamuzi.

Kiongozi wa namna hii ni kiongozi ambaye anaogopa kuchukuwa upande kwasababu asingependa kuwaudhi waliomuweka madarakani na hivyo ni mtu wa kuwapendeza wakubwa zake siku zote.

Ni lazima daima kuchukuwa upande katika kila hatua. Kutokuegemea upande wowote ni unafiki na wala haujengi taswira ya mtu kama mtu mwenye utashi na matamanio.

Kiongozi mzuri ni yule anayefanya maamuzi na kukosea na kukubali kukosolewa. Lakini yule anayeogopa kufanya maamuzi kwa kuogopa kukosea ni hatari sana.

Pamoja na ukimya wake, Pamoja na kutokumsikia mara kwa mara Katibu Mkuu wa CCM Taifa Wilson Mukama, naungana nae pale alipotoa kauli ambayo hata hivyo ilitofautiana na baadhi ya viongozi wenzake. Alisema ni ruksa kwa wanaotaka urais kufanya hivyo lakini chama hakitambui kampeni zao.

Tokea mwanzo wa mwaka 2012 wanachama hususani wa chama tawala CCM wameanza kuzionyesha wazi mbio zao za kuwania nafasi hii ya juu kabisa katika nchi hii.

Kama alivyotabanaisha Bw. Mukama wanaowania kukalia kiti hicho wanatimua mbio; wanapita kwenye nyumba za ibada, wanatoa misaada, wanazindua miradi, nyimbo za kwaya, wanatoa ushauri na kupinga ufisadi ilihali waonekane machoni mwa wananchi.

Kuzuia mbio hizi ni sawa na kuzuia mvua kwa wavu. Maji ya mkondo hayazuiwi kwa ukuta. Busara ni kuyajengea njia ya kupita.

Kauli ya Mukama inapingana na ya Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho, Philip Mangula, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye na Mjumbe wa Halmashauri wa CCM, Abdulharam Kinana. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wassira  na waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,

Mukama kwa upande wake, anasisitiza CCM haiwezi kuwazuia watu kunuia kuwania urais lakini, yenyewe haitambui kampeni zao zinazoendeshwa kwa njia mbalimbali.

“Hili la watu kujitokeza kuwania urais lipo na wala siyo vibaya.  Hata Julius Caesar wa Roma aliwahi kusema ‘kuwa na ambition (nia) si vibaya’. Sisi tunajua kuwa tutapata mgombea mpya na mzuri,” alisema Mukama.

Kama anavyojiandaa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, na siye wananchi hatuna budi kujianda ili tusiachwe nyuma. Inabidi tuwafahamu mapema viongozi hao ili mwisho wasiku tuwe na maamuzi sahihi.

CCM iko makini katika kutafuta mgombea wake lakini, hakiwezi kuacha mambo mengine na kukalia kujadili wagombea urais wa mwaka 2015. “Msimamo wa chama ni kutojiingiza kwenye mambo hayo haraka, lakini  hakikatazi mtu binafsi kuanza kujiandaa,” alisema Mukama.

Ni vema sasa wananchi wote tuwajengee njia salama na mwafaka ya kupitia wanasiasa wote tena wa vyama vyote pendwa wanao tamani nafasi hiyo ya juu kabisa katika taifa hili; tuwaambie tena bila kumung’unya maneno kwamba tunataka rais ajaye awe chaguo la watu. Hatumtaki asiye na miiko wala maadili, huyo hatufai!

Swala la kuwafahamu na kuanza kuwapima viongozi wetu ni jambo ambalo ni wajibu wetu sisi kama watanzania. Hivyo nakubaliana na kauli ya Sitta, alivyonukuliwa akisema baadhi ya wanasiasa wana upeo wa muda mfupi katika kupanga mipango ya kuwa madarakani  badala ya kufahamu kuwa wananchi wanahitaji kiongozi mwenye uwezo wa kutatua kero zao zikiwemo za umaskini na ujinga.

Uanasiasa sasa inaonekana kuwa ni kazi sawa na kazi nyingine. Mtu anayeingia katika taaluma ya uandishi na hajiwekei lengo kuwa siku moja awe Mhariri, huyo ana matatizo ya akili na kwa hakika hafai na wala hawezi kuwa mwandishi mzuri.

Kinana ambaye ni Mlezi wa CCM katika Mkoa wa Dar es Salaam, , alikemea makada walioanza mbio za urais wa 2015 akisema wanamdhoofisha Rais Jakaya Kikwete na serikali yake.

Aliwaelezea vigogo hao kuwa ni wabinafsi, wanaovuruga nchi na hawana lolote wanalolifanya kwa maslahi ya chama hicho tawala.

“Sasa hivi Rais Kikwete ana miaka mingine mitatu mbele kabla ya kumaliza uongozi wake na CCM ina kero nyingi za kushughulikia ili kutekeleza ilani yake, halafu wengine wanazungumzia urais sasa,” alishangazwa  Kinana.

Ningependa kumkumbusha Bw. Kinana kuwa mwanasiasa ambaye hana lengo la kushika cheo cha juu cha kisiasa kama urais wa nchi huyo ni mnafiki na siyo mkweli kwa watanzania na kwake mwenyewe, anayewaza leo, kuwa siku moja awe rais, huyo ni mwanasiasa halisi.

Vile vile napenda kutofautiana na kamanda mwenye dhamana ya propaganda ya chama hicho mpiganaji kijana Nape Nnauye kutokana na msimamo wake juu ya swala hili.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Januari 15, mwaka huu, Nape  alisema CCM haiko tayari kuendelea kuwavumilia wanachama wanaounda makundi ndani ya chama hicho kwa lengo la kutafuta urais 2015.

Nape alisema kitendo cha kuanza kampeni hizo sasa, kitazaa makundi ambayo yatasababisha kuvunjika kwa umoja na mshikamano ndani ya CCM.

Alisema wanaojiingiza kwenye mbio hizo wanatumia fedha nyingi katika kujipanga ili kufikia malengo na  akawashauri wasipoteze muda kwa maelezo kuwa siku ikifika chama hakitawapa nafasi.

Tungependa kutoa angalizo kuwa umaskini usiwe kigezo cha kumpa au kumnyima mtu fursa ya kuwania rais. Lakini mgombea maskini kwa ajili ya uvivu au upumbavu wake hatufai.

Vivyo hivyo utajiri wa mtu usiwe kigezo cha kumnyima au kumpa mtu fursa ya kuwania rais. Aliyetajirika kwa kudhulumu wengine au ufisadi, hatufai. Aliyetajirika kwa juhudi na kujihangaisha mwenyewe awekwe mezani ajadiliwe.

Kauli nyingine tofauti na ya Mukama ni ya Katibu mkuu mstaafu wa CCM Philip Mangula, aliyesema kitendo cha mwanachama kutangaza sasa nia ya kuwania urais mwaka 2015 kwa tiketi ya CCM ni makosa makubwa.

Mangula alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumzia mwenendo wa chama hicho kwa miaka 35 tangu kilipozaliwa, katika kipindi cha Asubuhi kinachorushwa na Kituo cha TV moja ya jijini Mwanza.

Alisema kuwa kitendo hicho kinamchanganya rais aliyeko madarakani kwakuwa yeye ndiye anayesimamia ilani ya uchaguzi ya CCM.

“Kujitangaza sasa kuwa unatarajia kugombea urais ni makosa makubwa. Kwa sababu chama kimejiwekea ilani kisha kikampa rais aisimamie. Lakini yule anayejitangaza anakuwa na mambo yake mwenyewe,” alisema Mangula.

Lakini Katibu mkuu huyu mstaafu wa CCM hakutuambia, je mgombea huyu tutapata wapi muda wa kutosha kumpima kama asipojitokeza sasa.

Kupitia Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hakuna mtu yoyote anayekatazwa kuzungumzia suala hilo wala kwenye katiba ya chama cha CCM hakuna kifungu kinacho mzuia mtu kuweka nia yake hadharani ili watu wamjue na kuanza kumpima.

Kwa vyovyote vile muda wa urais wa sasa tukiujadili au kwa kutoujadili baada ya miaka mitatu utakwisha. Je si vyema kuanza kujadili kifo sasa wakati tukiwa na nguvu tena wazima badala ya kungojea tukizidiwa kitandani na kwa vile tunajua lazima siku moja kitatokea?

Mangula anataka kutuaminisha kuwa kwa kukaa kimya kwetu au kwa kutojiandaa sasa ndiyo kutaongeza tija kwa serikali ya sasa? Najuwa kwa upande wake anaogopa kukosolewa kwa serikali ya sasa na viongozi walio ndani ya serikali hiyo.

Viongozi wetu lazima watambue kuwa wananchi wamezingirwa na kero nyingi. Kero kubwa ni uongozi wenyewe ambao hauonekani kuwa na uwezo wa kutatua kero za wananchi.

Je, hawa wanaoutaka urais sasa wanajua kuwa wananchi wanauona uongozi uliopo kuwa ni kero? Kati yao yupo wa kutufaa?

Siasa toka awali ilikuwa ni sanaa ya yawezekanayo. Leo hii imekuwa ni sanaa ya kinachowezekana – kucheza na akili za watu na mara nyingi bila maono yoyote makubwa wala hisia za matumaini na mawazo.

Ushabiki ni upumbavu. Kumchagua mtu kwasababu tu ni wa chama chako ni ujinga sawasawa na kumchagua mtu kwasababu tu ni wa dini yako.

Imedhihirika kuwa uongozi bila miiko ni uhuni. Maadili ya viongozi katika nchi yetu yalitupwa pamoja na Azimio la Arusha. Anayetaka urais atuambie bayana atairudishaje heshima ya viongozi waliyopoteza kwa kutupa miiko ya uongozi? Muumini wa Azimio la Arusha na awe wa kwanza kujadiliwa.

Kama yupo? Natangaza hadharani kujipa kazi tena bila malipo yoyote kwa kuzunguka nchi nzima kusaidiana naye aweze kuingia ikulu 2015.

Advertisements

NINI SABABU YA MWANAUME KUTENDA UKATILI KWA WAPENZI WAO.

Image

Kila mara watu wanaposikia ukatili baina ya wapenzi wawili, haraka haraka hufikiria makosa ya jinai, bila kufikiria kuwa kuna njia nyingi za ukatili unaweza kutendeka katika mahusiano.

Hata hivyo hisia za wengi wetu hugubikwa na lawama na hasira juu ya wanaume na tabia zao za kupenda kutumia mabavu, japokuwa siyo kweli kuwa wanaume wote ni watu wa vurugu.

Katika maisha yetu ya kawaida majumbani na katika jamii inayotuzunguka kuna mifano mingi ya maovu wanayofanyiwa wanawake na watoto wa kike kwa visingizio mbalimbali ambavyo watu hawaoni sababu ya kuchukua hatua ati kwa sababu ndiyo taratibu ambazo wanawake wanapaswa kupitia katika maisha au ndio mfumo wa maisha uliorithiwa toka kwa wahenga wetu.

Wanawake pia wamekuwa wakijikuta kukubali hali hii na kutoitolea taarifa kwa kudhani kuwa ndio maisha ya kawaida yanavyopaswa kuwa.

Ingawa tunasema hakuna sababu au utetezi unao paswa kutolewa ili kuhalalisha ukatili wa aina yoyote dhidi ya Mwanamke, lakini ni wangapi kati yetu walijaribu kufuatilia kwa undani na kutaka kujua chanzo kinacho sababisha mwanaume ampige au amuue mkewe ambaye alimtolea mahari na kuahidi kumpenda na kumlinda mpaka kufa?

M2S kwa kushilikiana na kampeni ya “TUNAWEZA” ya ukanda wa kaskazini iliwahoji zaidi ya wanaume 21 kuhusu hili la kumpiga mke, kwa ujumla wote walionyesha kutokupendezwa kwa jambo hili, wengi walitabanaisha kuwa endapo hali nyumbani ikizorota na kuchochewa zaidi ya kipimo cha uvumilivu suluhisho ni bora utoke na kwenda matembezini na ukirudi anaweza kuanza majadiliano upya.

Kwa hiyo nini humfanya manaume mwenye akili zake timamu na busara akurupuke na hasira na kumshambulia kwa kumpiga na hata kuua mke wake, mwanamke huyo huyo aliyekuwa anampenda na kumtambulisha kama mwandani wake?

Niliwauliza tena wanaume wale wale, katika orodha ya majibu yao jambo lililoongoza lilikuwa ni kumfumania mwandani wako akiwa kitandani na mwanaume mwingine.

Jambo la pili lililo chukuwa nafasi katika orodha yao ni kutokutendewa haki kwa watoto. Wanaume hujivunia sana uwepo na majaliwa ya watoto wao. Hatua yoyote isiyokuwa ya uwajibikaji huchukuliwa kama hatua ya kutaka kuangamiza kizazi chake, hii ni pamoja na mateso, kutelekezwa, uzembe na kupuuzwa kabisa kwa ustawi wa mtoto.

Sababu nyingine zilizoelezwa ni pamoja na kushambuliwa kwa manaume na mkewe na kusabisha mwanume ajitetee; hasira za muda mrefu ambazo hazikupatiwa ufumbuzi; kushindwa kujizuia wakati wa mabishano hususan pale mwanamke anapogoma kumpa mme wake muda wa kumsikiliza na kusababisha kuvunjika kwa mawasiliano baina ya pande hizo mbili.

Wanaume hao walieleza vilevile pale mke anapoamua kuleta changamoto kwa kudhoofisha mamlaka ya mume wake kama kichwa cha nyumba na hivyo kumfanya naye ahisi haja ya kudai na kurudisha uongozi wake; mke kuonyesha utovu wa nidhamu uliokithiri katika jamii; kumdharaulisha au kumpa aibu mume wake mbele ya umma wa wanajamii; kufanya nyumba isikalike au kufanya mazingira ya kuishi kuwa magumu kwa mume wake.

Sababu nyingine ni ushawishi wa nje kama vile uwepo wa nyumba ndogo. Hii inaweza kuwa sababu ya mwanaume kumfanyia ukatili mke wake ili tu aondoke na kumfanya huru aweze kuoa tena.

Vilevile ni pamoja na nyakati ngumu za kiuchumi, (pombe na madawa ya kulevya), ushawishi hasi kutoka kwa marafiki, na kuingiliwa kwa jamaa (ndugu)

Ufumbuzi wa migogoro hii kama ilivypendekezwa na mmoja wa wanaharakati nilio muhoji alishauri kuwa ni vyema kujadili tofauti kabla mambo hayajawa mabaya au kufika wakati ambao ni vigumu kupat suruhu.

“Nitapata hasira na kusononeka sana kama nitagundua kuwa nilimkwaza mke wangu lakini yeye hakuniambia kwa kipindi kirefu, yaani alikuwa anaishi kwa mashaka na anapata ujasiri wa kusema pale anapozidiwa au linapoibuka jambo jingine,” alisema

Sisi tulishajiwekea njia ya kufuata ili kunusuru ndoa yetu na migogoro. Endapo kutatokea kukwaruzana au kutokuelewana haraka huweka kila kitu wazi mezani kupata muda wa kukijadili kwa kina na kupanga namna ya kukitatua. Pia walikubaliana na kuwa wazi juu ya suala la fedha na kipato kwasababu wanajua kwamba hii ni moja ya sababu kubwa ya migogoro baina ya wanandoa.

“Kuna wakati hali ya maelewano inakuwa tete sana ndani ya nyumba, pale majadiliano yanapoonekana yanakwenda ambako siko mimi huepusha shari kwa kutoka na hurudi baada ya muda mambo yakitulia” aliongeza.

Mmoja wa wanaume hao aliniambia kuwa baadhi ya wanawake pia wanafanya ukatili mkubwa dhidi ya wanaume, ukatili wao siyo wa nguvu. Mbinu yao si ile ya mfumo wa makofi au ngumi. Lakini katika hali ya mapambano ya kihisia na kisaikolojia huwabana sana wanaume zao, silaha yao kubwa ni tendo la ndoa. Na ni mara chache sana hunyooshewa vidole na kukemewa.