NINI SABABU YA MWANAUME KUTENDA UKATILI KWA WAPENZI WAO.

Image

Kila mara watu wanaposikia ukatili baina ya wapenzi wawili, haraka haraka hufikiria makosa ya jinai, bila kufikiria kuwa kuna njia nyingi za ukatili unaweza kutendeka katika mahusiano.

Hata hivyo hisia za wengi wetu hugubikwa na lawama na hasira juu ya wanaume na tabia zao za kupenda kutumia mabavu, japokuwa siyo kweli kuwa wanaume wote ni watu wa vurugu.

Katika maisha yetu ya kawaida majumbani na katika jamii inayotuzunguka kuna mifano mingi ya maovu wanayofanyiwa wanawake na watoto wa kike kwa visingizio mbalimbali ambavyo watu hawaoni sababu ya kuchukua hatua ati kwa sababu ndiyo taratibu ambazo wanawake wanapaswa kupitia katika maisha au ndio mfumo wa maisha uliorithiwa toka kwa wahenga wetu.

Wanawake pia wamekuwa wakijikuta kukubali hali hii na kutoitolea taarifa kwa kudhani kuwa ndio maisha ya kawaida yanavyopaswa kuwa.

Ingawa tunasema hakuna sababu au utetezi unao paswa kutolewa ili kuhalalisha ukatili wa aina yoyote dhidi ya Mwanamke, lakini ni wangapi kati yetu walijaribu kufuatilia kwa undani na kutaka kujua chanzo kinacho sababisha mwanaume ampige au amuue mkewe ambaye alimtolea mahari na kuahidi kumpenda na kumlinda mpaka kufa?

M2S kwa kushilikiana na kampeni ya “TUNAWEZA” ya ukanda wa kaskazini iliwahoji zaidi ya wanaume 21 kuhusu hili la kumpiga mke, kwa ujumla wote walionyesha kutokupendezwa kwa jambo hili, wengi walitabanaisha kuwa endapo hali nyumbani ikizorota na kuchochewa zaidi ya kipimo cha uvumilivu suluhisho ni bora utoke na kwenda matembezini na ukirudi anaweza kuanza majadiliano upya.

Kwa hiyo nini humfanya manaume mwenye akili zake timamu na busara akurupuke na hasira na kumshambulia kwa kumpiga na hata kuua mke wake, mwanamke huyo huyo aliyekuwa anampenda na kumtambulisha kama mwandani wake?

Niliwauliza tena wanaume wale wale, katika orodha ya majibu yao jambo lililoongoza lilikuwa ni kumfumania mwandani wako akiwa kitandani na mwanaume mwingine.

Jambo la pili lililo chukuwa nafasi katika orodha yao ni kutokutendewa haki kwa watoto. Wanaume hujivunia sana uwepo na majaliwa ya watoto wao. Hatua yoyote isiyokuwa ya uwajibikaji huchukuliwa kama hatua ya kutaka kuangamiza kizazi chake, hii ni pamoja na mateso, kutelekezwa, uzembe na kupuuzwa kabisa kwa ustawi wa mtoto.

Sababu nyingine zilizoelezwa ni pamoja na kushambuliwa kwa manaume na mkewe na kusabisha mwanume ajitetee; hasira za muda mrefu ambazo hazikupatiwa ufumbuzi; kushindwa kujizuia wakati wa mabishano hususan pale mwanamke anapogoma kumpa mme wake muda wa kumsikiliza na kusababisha kuvunjika kwa mawasiliano baina ya pande hizo mbili.

Wanaume hao walieleza vilevile pale mke anapoamua kuleta changamoto kwa kudhoofisha mamlaka ya mume wake kama kichwa cha nyumba na hivyo kumfanya naye ahisi haja ya kudai na kurudisha uongozi wake; mke kuonyesha utovu wa nidhamu uliokithiri katika jamii; kumdharaulisha au kumpa aibu mume wake mbele ya umma wa wanajamii; kufanya nyumba isikalike au kufanya mazingira ya kuishi kuwa magumu kwa mume wake.

Sababu nyingine ni ushawishi wa nje kama vile uwepo wa nyumba ndogo. Hii inaweza kuwa sababu ya mwanaume kumfanyia ukatili mke wake ili tu aondoke na kumfanya huru aweze kuoa tena.

Vilevile ni pamoja na nyakati ngumu za kiuchumi, (pombe na madawa ya kulevya), ushawishi hasi kutoka kwa marafiki, na kuingiliwa kwa jamaa (ndugu)

Ufumbuzi wa migogoro hii kama ilivypendekezwa na mmoja wa wanaharakati nilio muhoji alishauri kuwa ni vyema kujadili tofauti kabla mambo hayajawa mabaya au kufika wakati ambao ni vigumu kupat suruhu.

“Nitapata hasira na kusononeka sana kama nitagundua kuwa nilimkwaza mke wangu lakini yeye hakuniambia kwa kipindi kirefu, yaani alikuwa anaishi kwa mashaka na anapata ujasiri wa kusema pale anapozidiwa au linapoibuka jambo jingine,” alisema

Sisi tulishajiwekea njia ya kufuata ili kunusuru ndoa yetu na migogoro. Endapo kutatokea kukwaruzana au kutokuelewana haraka huweka kila kitu wazi mezani kupata muda wa kukijadili kwa kina na kupanga namna ya kukitatua. Pia walikubaliana na kuwa wazi juu ya suala la fedha na kipato kwasababu wanajua kwamba hii ni moja ya sababu kubwa ya migogoro baina ya wanandoa.

“Kuna wakati hali ya maelewano inakuwa tete sana ndani ya nyumba, pale majadiliano yanapoonekana yanakwenda ambako siko mimi huepusha shari kwa kutoka na hurudi baada ya muda mambo yakitulia” aliongeza.

Mmoja wa wanaume hao aliniambia kuwa baadhi ya wanawake pia wanafanya ukatili mkubwa dhidi ya wanaume, ukatili wao siyo wa nguvu. Mbinu yao si ile ya mfumo wa makofi au ngumi. Lakini katika hali ya mapambano ya kihisia na kisaikolojia huwabana sana wanaume zao, silaha yao kubwa ni tendo la ndoa. Na ni mara chache sana hunyooshewa vidole na kukemewa.


Advertisements