PAMOJA NA ZENGWE HOJA YA ZITO YA KUTOKUWA NA IMANI NA PINDA KUWASILISHWA JUMATATU

  • Mweshimiwa Zito Zuberi Kabwe

    Wabunge 75 wasaini wakiwemo 5 wa CCM

  • Juhudi za Spika kuhuzima kwa kutumia kanuni za gonga mwamba.
  • Mawaziri 8 washauliwa kuandika barua za kujiuzuru kumnusuru Waziri Mkuu
  • Wanazuoni waunga mkono kuiwajibisha serikali.

MKAKATI wa kukusanya majina 70 ya wabunge kama sehemu ya kukamilisha utaratibu wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ulioshirikisha wanaharakati mbalimbali kwa kutumia mitandao ya kijamii kwa kuwapigia simu au kuwatumia ujumbe wa maneno hili kuunga mkono hoja ya Zitto umefanikiwa kwa kiasi kikubwa hadi kufikia jana jioni, wabunge 75 walikuwa wameunga mkono hatua hiyo, watano kati yao, wakitokea chama tawala CCM.

Wabunge wa CCM waliotia saini hoja hiyo na kufanya idadi hiyo kufikia 75 ni Deo Philikunjombe wa Ludewa, Ally Keissy Mohamed wa Nkasi Kaskazini, Alphaxard Kange Lugola wa Jimbo la Bunda, Murtaza Ally Mangungu na mbunge mmoja wa Viti Maalumu kutoka Kanda ya Ziwa ambaye hakutaka atajwe kwa sasa.

Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, alisema zoezi hilo si la chama chochote cha siasa bali wabunge wote wanaoitakia mema Tanzania na watu wake.

Aliongeza, “Kuna wengine wamesema;  ooh! Waziri Mkuu hana makosa! Tunamuonea lakini tunataka tuwaambie ujumbe mmoja kuwa tunamheshimu sana Waziri Mkuu, tunampenda sana Waziri Mkuu lakini tunaiheshimu zaidi nchi yetu.”

Endapo mambo yatakwenda kama yalivyo sasa, Pinda atakuwa ameingia katika historia ya kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na Bunge, tangu Tanzania ipate uhuru wake Desemba 9, 1961.

Pamoja juhudi za Spika wa Bunge, Anne Makinda 20/04/2010 jioni kujaribu kudhohofisha mkakati huu kwa kueleza kuwa mchakato huo ni batili zoezi liliendelea mpaka idadi ya majina pamoja na sahini kukamilika.

Akinukuu vifungu vya Kanuni za Bunge na Katiba, Spika Makinda alisema mkakati huo ni batili kwa kuwa kanuni zinaeleza bayana kuwa ulipaswa kufanyika siku 14 kabla ya kuwasilisha hoja hiyo kwa Spika.

“Spika hajasema kitu, wamejipanga tu hawa. Sisi hatujampelekea hoja yetu. Tunampelekea Jumatatu kisha ataamua. Ili mradi iwe siku 14 kabla ya siku ya kutoa hoja. Wanaweweseka tu,” alidai Zitto.

Alifafanua; “Kanuni inasema siku 14 kabla, sisi tunakusanya saini ili tutimize sharti la kanuni. Spika anajaribu kulindaa Serikali ya chama chake kwa kupindisha kanuni.”

Habari zaidi zilidai kuwa Serikali kupitia kwa baadhi ya wabunge, maswahiba na mawaziri, jana walikuwa na kazi ya ziada kuwashawishi wabunge wa CCM wasisaini.

Nje ya viwanja vya Bunge, mawaziri na baadhi ya wabunge watiifu kwa Waziri Mkuu, walionekana wakihaha kila kona kujaribu kushawishi wabunge wasiikubali kusaini.

Baba Askofu Msaidizi Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba Methodius Kilani akizungumzia hatua hii alisema ni wakati mwafaka kwa viongozi na watendaji wanaotuhumiwa kuwajibika wenyewe bila kusubiri shinikizo.

“Bunge linatekeleza wajibu wake kwa niaba ya wananchi. Hii ni sehemu muhimu ya kazi zake. Pia kuna njia mbalimbali za Bunge kutumia katika kuiwajibisha Serikali. Hii ni moja wapo lakini siyo njia bora zaidi katika kuleta mabadiliko,” alisema Kilaini.

Alifafanua kuwa njia sahihi ni ile ya wahusika wenyewe kulazimika kujiuzulu pasipo kulazimishwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Deus Kibamba, alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuhimiza uwajibikaji ikiwa inafuata taratibu walizojiwekea.

“zipo kanuni zinazotoa mamlaka kwa bunge kuchukua hatua dhidi ya viongozi serikalini ambao uwajibikaji wao unazidi kushuka. Hii ni hatua muhimu katika kuhimiza utendaji serikalini na itachochea uwajibikaji,” alisema Kibamba.

Kwa upande wake, profesa Idris Kikula wa Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM) alisema ni vema watanzania wakasubiri kwanza na kuona kitakachofanyika, ili waweze kujadili.

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) Dk Rodrick Kabangila aliunga mkono hatua hiyo akisema itaamsha ari ya uwajibikaji serikalini, hususani kwa mawaziri watakaoteuliwa kushika nyadhifa hizo baada ya Baraza la sasa kuvunjwa.

Katika kujaribu kupunguza makali ya wabunge hao, wabunge wa CCM walikutana kwa faragha Ukumbi wa Pius Msekwa lakini mambo yalizidi kuharibika na kutaka mawaziri hao wajiuzulu.

Wabunge hao walishikilia msimamo kuwa kama mawaziri hao hawatajiuzulu, wangepiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa vile kikatiba, hawana mamlaka ya kuwawajibisha mawaziri hao isipokuwa Waziri Mkuu.

Advertisements

One thought on “PAMOJA NA ZENGWE HOJA YA ZITO YA KUTOKUWA NA IMANI NA PINDA KUWASILISHWA JUMATATU

Comments are closed.