BREAKING NEWS:- TUNDU LISSU ASHINDA KESI YA KUPINGA UBUNGE WAKE

  • Hoja zote za upande wa mlalamikaji zatupwa.
  • Maofisa Jeshi pamoja na kikosi maalum waudhulia maakamani.

Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu, ameshinda kesi iliyofunguliwa dhidi yake mjini Singida kupinga ushindi uliomweka madarakani

Hukumu imetolewa na Jaji Moses Mzuna anayetoka mahakama kuu kanda ya Kilimanjaro, iliyofunguliwa na makada wawili wa CCM, Shabani Itambu na Pascal Hallu.

Kesi hiyo imekuwa kivutio sana kwa wananchi wengi wa mkoa Singida na nchini kwa ujumla, kutokana na umaarufu wa mbunge huyo machachari.

Leo mahakamani wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa, wananchi wa Singida, na waandishi wa habari walijitokeza kwa wingi sana katika eneo la mahakama.

Idadi ya Polisi pia ilikuwa kubwa, ndani na nje ya mahakama.Kilicho kuwa cha ajabu kidogo leo getini maofisa wote wakubwa wa jeshi la polisi walikuwepo pale na kikosi maalumu kwa ajili ya kukagua kila anayeingia mahakamani,  kila mtu aliyekuwa anaingia mahakamani alipekuliwa hadi wabunge waliokuja kusikiliza kesi hiyo.

Akisoma hukumu Jaji Moses Mzuna alisema “HOJA YA TISA, Kama Mgombea wa walalamikaji (CCM) alikataa kusaini matokeo. Hoja hii haipaswi kunipotezea muda sana. Njau hakuhudhuria, aliwakilishwa na mlalamikaji wa kwanza ambaye alikataa kusaini matokeo.

Wakili wa serikali alisema, kukataa pekee kusaini matokeo hakusaidii kutengua matokeo. Hivyo hata hoja ya tisa naitupilia mbali. Haikuwa sahihi.

Hoja ilitolewa hapa, kuwa mawakala walikula kiapo kwa hakimu. Walalamikaji walisema kuwa walipaswa kula kiapo kwa msimamizi wa uchaguzi. Je kuapishwa na hakimu kunabatilisha matokeo?

Hoja zilizotolewa na mawakili wa serikali walisema Hakimu ana mamlaka ya kutoa viapo. Binafsi nasema kuwa waliotunga sheria hawakumaanisha kuwa Mahakimu hawaruhusiwi kuapisha mawakala, vinginevyo kungekuwepo fomu ya hakimu tu. Lakini fomu zinaonyesha hakimu, Msimamizi wa uchaguzi na Msimamizi msaidizi, fomu inatambulika kisheria, kwa sheria ya Uchaguzi. Hii haihusiani na zoezi la uchaguzi.

Katika kesi ya Prince bagenda Vs Wilson masilingi, katika kesi hii
mawakala walifanya kazi bila kuapishwa, na ilichukuliwa kuwa sehemu ya kutengua uchaguzi, angalia pg 240.

Kwa lugha yake jaji alisema hawakuwa na mamlaka halali, lawful mandate, lakini ilisaidia kutengua, na mwanasheria wa serikali alihusika katika hili.

Maelezo hayo yanatofautiana na kesi iliyo mbele yangu, jimbo la Singida mashariki mawakala walikula kiapo, na walikuwa na mamlaka halali. Hivyo hoja hii naitupilia mbali

HIVYO, UCHAGUZI ULIKUWA WA HAKI, NA TUNDU LISSU NI MBUNGE HALALI NA UCHAGUZI ULIKUWA HURU NA WA WA HAKI, HIVYO SIWEZI KUTENGUA.

Walalamikaji wa kesi hiyo, iliyofunguliwa mahakama kuu kanda ya Dodoma, walikuwa wanatetewa na wakili Godfrey Wasonga, kutoka mkoani Dodoma, huku Lissu akijisimamia mwenyewe.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Machi 12, 2012, kufuatia makada wawili wa CCM, kupinga ushindi wa Lissu kwa madai kuwa uchaguzi huo uligubikwa na dosari nyingi.

Awali Katika mahojiano na Lissu, alisema vyovyote mahakama itakavyo hukumu, anajivunia kuimarisha demokrasia na kuwa mbunge wa kwanza kutoka upinzani, kwenye historia ya mikoa ya kanda ya kati.

Advertisements

HATIMA YA SUDAN KUSINI KUJIUNGA NA EAC KESHO.

  • Kuangaliwa kama imetimiza masharti
  • Nchi nyingine 3 zatajwa kuomba kujiunga na Jumuia hiyo.

MKUTANO wa kumi wa marais wa Jumuia ya Afrika Mashariki unatarajiwa kufanyika Jumamos Aprili 28,2012, i mjini Arusha utajadili pia uwezekano wa Sudan Kusini kujiunga na jumuia hiyo.

Taarifa zilizopatikana mjini Arusha zinaeleza kuwa mawaziri wa Afrika Mashariki kutoka nchi wanachama wa jumuia hiyo Jumatano Aprili 25, 2012. walipitisha kamati maalum ya kuhakiki na kuthibitisha kama nchi hiyo ambayo iliundwa rasmi Julai 9 mwaka jana kutoka iliyokuwa Sudan kama imetimiza vigezo vilivyowekwa.

Waziri wa Afrika Mashariki wa Rwanda, Monique Mukaruliza alinukuliwa na gazeti la  The New Times  akieleza kuwa endapo nchi hiyo itatimiza vigezo, timu maalum ya majadiliano itakutana kuzungumzia namna nchi hiyo itakavyojiunga na jumuia hiyo yenye wanachama watano.

Hatua hiyo inaoneka kuwa siyo ngumu sana kutokana na duru za kisiasa kueleza ushirika wake na nchi wanachama.

Tayari, Sudan Kusini imekuwa ikialikwa katika mikutano ya EAC kama mtazamaji.

Mkataba wa EAC unaweka masharti ya nchi zaidi kuwa wanachama yakiwamo ya kuheshimu kanuni za utawala bora, demokrasia, kuheshimu utawala wa sheria, kutimiza haki za binadamu.

Pia, masharti mengine ni kuitaka nchi inayotaka uanachama kuwa tayari kuchangia katika harakati za kuleta umoja, ukaribu wa kijiografia na faida za kiutawala na uchumi ambazo nchi wanachama zinao kwa mwanachama huyo mpya.

Mchumi maarufu wa Rwanda, Profesa Celestin Nyirishema, kutoka Chuo Kikuu cha Kigali (ULK) anaeleza kuwa Sudan Kusini inapaswa kupewa uanachama, kutokana na rasilimali na nafasi ilizo nazo za kusaidia kukuza uchumi kwa eneo hilo.

Nchi nyingine ambazo zimekuwa zikionyesha nia ya kujiunga na EAC ni pamoja na Sudan, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hata hivyo, katika mkutano wa karibuni wa viongozi hao mjini Bujumbura, Burundi, walikataa maombi ya Serikali ya Sudan kwa madai ya kutokidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa mkataba wa kuanzishwa kwa jumuia hiyo.

Pia, wakuu hao wa nchi watakuwa na kazi ya kuthibitisha uteuzi na Naibu Katibu Mkuu wa EAC (Siasa na  Muungano) kutoka Uganda anayeziba nafasi ya Beatrice Kiraso aliyemaliza mkataba wake na pia kuendelea kazini kwa Jean Claude Nsengiyumva kutoka Burundi anayeshughulikia Huduma za Jamii.

Viongozi hao pia watazungumzia mapendekezo ya mawaziri kuhusu umoja wa forodha wa nchi wanachama wa EAC.

KIKAO CHA KAMATI KUU YA CCM KUTOA SULUHISHO LA TUHUMA ZA MAWAZIRI LEO?

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete

  • Nape hagoma kusema ajenda za kikao
  • Mawaziri wanao tuhumiwa nao wanena

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete ameitisha kikao cha ghafla cha Kamati Kuu ya chama hicho kujadili pamoja na mambo mengine, hali ya siasa nchini.

Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, amethibitisha habari hii na kueleza kuwa kikao hicho kitafanyika Aprili 27, 2012 Ikulu Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi.

Ingawa Nape alisema hawezi kutaja ajenda za kikao hicho kwa kuwa ni siri, habari kutoka baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, zilisema kwavyovyote vile ajenda ya shinikizo la mawaziri hao kujiuzulu ni moja wapo.

Nape alishindwa kuthibitisha au kukanusha taarifa kwamba kikao hicho kitajadili hatima ya mawaziri hao wanaotakiwa kujiuzulu badala yake akasema, “Ni kweli kesho tuna Kamati Kuu Dar es Salaam, lakini agenda za kikao hicho haziwezi kuwekwa ‘public’ ujue hivyo tu inatosha,” alisema Nape.

Mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu ni Kepteni George Mkuchika (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Profesa Jumanne Maghembe (Kilimo, Chakula  na Ushirika), Mhandisi Omar Nundu (Uchukuzi) pamoja na  Mkulo na Nyalandu.

Shinikizo la kutaka mawaziri nane wajiuzulu liliibuka katika Mkutano wa Saba wa Bunge uliomalizika mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki hii, baada ya ripoti hiyo ya CAG kuonyesha tuhuma nzito za ufisadi katika wizara hizo huku baadhi ya mawaziri wakionekana kuhusika moja kwa moja na maamuzi waliyofanya.

Mkulo ambaye alikuwa waziri wa kwanza kutakiwa na wabunge ajiuzulu, kutokana na kashfa ya kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha tuhuma zake ikiwemo uuzaji wa kiwanja Na.10 kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL),  alisema  hawezi kuzungumzia suala la kujiuzulu kwa sababu hajui kosa lake wala madai ya wabunge dhidi yake.

Alipoulizwa kama yuko tayari kujiuzulu kuhusiana na kashfa zinazoikabili wizara yake, Mkulo alijibu, ‘ hapa, no comment,” akiwa na maana kwamba hana cha kuzungumza.

“Kwanza sifahamu tuhuma zilizotolewa na wabunge kwa sababu sikuwepo, mimi nilikuwa safari,” alisema.

Kwa upande wake Nyalandu alisema kuwa, mpaka sasa haelewi kwanini ameingizwa kwenye kashfa hiyo kwa sababu katika ripoti ya CAG, hakutajwa na wenyeviti wa kamati mbalimbali za kudumu za Bunge.

“Sielewi kwanini nimeingizwa kwenye kashfa hii kwa sababu katika ripoti ya CAG sikuwemo. Ripoti ya Mwenyekiti wa Kamati ya POAC na PAC simo pia, lakini nilishangaa nilipoanza kusikia jina langu,” alifafanua Nyalandu.

Tayari Nyalandu alitoa waraka unaonyesha msimamo tofauti na wa bosi wake, Dk Chami kuhusu kashfa zinazowakabili ambazo ni tuhuma alizonazo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwango (TBS), Charles Ekelege anayedaiwa kuanzisha kampuni hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi hususani, Hong Kong na Singapore.

Wakati Nyalandu akishauri Ekelege asimamishwe kazi ili apishe uchunguzi wa CAG na endapo hatakuwa na tuhuma za kujibu arudishwe kazini, waziri wake (Chami) alisema kuwa Ekelege ni mteule wa rais, hivyo hawezi kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete kumtaka amwondoe wakati hakuna taarifa yoyote inayoonyesha tuhuma zake.

Kwa upande wake,  Dk Mponda anayekabiliwa na kashfa ya Bohari ya Dawa (MSD)pamoja na upotefu wa pesa za wizara hiyo amesema leo atatoa ufafanuzi wa kitugani kilitokea.

Waziri  Maige juzi aliamua kueleza baadhi ya tuhuma zinazomkabili ikiwamo umiliki wa nyumba aliyodaiwa kuinunua kwa Dola 700,000 za Marekani, akisema nyumba hiyo aliinunua kwa dola 410,000 na siyo dola 700,000 kama ilivyoelezwa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Mazingira, James Lembeli alipinga kauli hiyo akisema taarifa alizonazo zinaonyesha Maige alinunua nyumba hiyo kwa fedha taslimu dola 700,000.

Kashfa nyingine inayomkabili Maige ni ile iliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira huku ikitaka awajibishwe kwa kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa kampuni ambazo hazina sifa na kusafitishwa nje kwa wanyama wakiwamo twiga na tembo kinyume cha sheria.

Hata hivyo, Maige alisema  hivi sasa kuna mapambano ya kisiasa baina ya viongozi mbalimbali na kwamba habari mbaya dhidi yake zinalenga kumchafua kutokana na kuwa mkali katika utendaji wake wa kazi na kuongeza, kuna chuki kutokana na kwamba aliwahi kuwafukuza kazi baadhi ya watendaji wizarani kwake  jambo ambalo limewaudhi baadhi yao.

TUNAPASWA KUULINDA MUUNGANO KWA NGUVU ZOTE.

April 26, 2012 Tanzania iliadhimisha miaka 48 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mwaka 1964 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Shehe Abeid Amaan Karume, walisaini makubaliano ya kuungana.

Kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar kulizingatia zaidi masuala ya historia ya pande hizo mbili, lakini pia usalama wa Tanganyika na visiwa vya Zanzibar, hivyo hatua hiyo ilidhihirisha udugu wa kihistoria uliokuwapo tangu zamani.

Miaka 48 ni umri wa mtu mzima na hivyo Watanzania wanapaswa kujivunia hatua hii ambayo inaashiria wazi kukomaa kwa Muungano japo muungano huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimesababisha malalamiko kutoka pande zote za Muungano.


Na kwa kulitambua hilo, viongozi wa Tanzania kwa pamoja walikaa na kuunda Kamati maalumu ya kuangalia kero hizo na kuzitafutia ufumbuzi kwa maslahi ya Watanzania wote. 

Zimekuwapo kauli zikitolewa na baadhi ya watu hususan wanasiasa, zikitaka kuvunjwa kwa Muungano huu, kwa madai kuwa hauna manufaa kwa wananchi, jambo ambalo linatolewa bila kufikiria mustakabali wa nchi hii.


Kwa kuzingatia usemi wa ‘Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu’, Watanzania wameendelea kuwa wamoja chini ya Muungano huo na wakisaidiana kwa mambo mbalimbali yakiwamo ya raha na karaha.

Hivi sasa mchakato wa kuandika Katiba mpya ya nchi umeanza ambapo hata Rais Jakaya Kikwete katika hadidu zake za rejea kwa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba hiyo kwa wananchi, alitahadharisha dhidi ya michago inayoegemea katika kutaka kuvunja Muungano.

Sisi tunasema na kuwaasa wananchi kutoa maoni ambayo yanalenga katika kuimarisha Muungano wetu, kwasababu hatua ya kuuvunja tayari tumeisha ipita. Kwa nguvu zote tunapaswa kuhuenzi na kuudumisha Muungano kwa manufaa ya leo na kesho.