TUNAPASWA KUULINDA MUUNGANO KWA NGUVU ZOTE.

April 26, 2012 Tanzania iliadhimisha miaka 48 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mwaka 1964 Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Shehe Abeid Amaan Karume, walisaini makubaliano ya kuungana.

Kuungana kwa Tanganyika na Zanzibar kulizingatia zaidi masuala ya historia ya pande hizo mbili, lakini pia usalama wa Tanganyika na visiwa vya Zanzibar, hivyo hatua hiyo ilidhihirisha udugu wa kihistoria uliokuwapo tangu zamani.

Miaka 48 ni umri wa mtu mzima na hivyo Watanzania wanapaswa kujivunia hatua hii ambayo inaashiria wazi kukomaa kwa Muungano japo muungano huo unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimesababisha malalamiko kutoka pande zote za Muungano.


Na kwa kulitambua hilo, viongozi wa Tanzania kwa pamoja walikaa na kuunda Kamati maalumu ya kuangalia kero hizo na kuzitafutia ufumbuzi kwa maslahi ya Watanzania wote. 

Zimekuwapo kauli zikitolewa na baadhi ya watu hususan wanasiasa, zikitaka kuvunjwa kwa Muungano huu, kwa madai kuwa hauna manufaa kwa wananchi, jambo ambalo linatolewa bila kufikiria mustakabali wa nchi hii.


Kwa kuzingatia usemi wa ‘Umoja ni Nguvu na Utengano ni Udhaifu’, Watanzania wameendelea kuwa wamoja chini ya Muungano huo na wakisaidiana kwa mambo mbalimbali yakiwamo ya raha na karaha.

Hivi sasa mchakato wa kuandika Katiba mpya ya nchi umeanza ambapo hata Rais Jakaya Kikwete katika hadidu zake za rejea kwa Tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Katiba hiyo kwa wananchi, alitahadharisha dhidi ya michago inayoegemea katika kutaka kuvunja Muungano.

Sisi tunasema na kuwaasa wananchi kutoa maoni ambayo yanalenga katika kuimarisha Muungano wetu, kwasababu hatua ya kuuvunja tayari tumeisha ipita. Kwa nguvu zote tunapaswa kuhuenzi na kuudumisha Muungano kwa manufaa ya leo na kesho.

Advertisements