MARAIS WA EAC WAWAAGIZA MAWAZIRI WA JUMUIYA HIYO KUANZA UHAKIKI WA MAOMBI YA SUDAN KUSINI.

MARAIS wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wameliagiza Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo kuanza uhakiki wa maombi ya Sudan ya Kusini ambayo imeomba kujiunga na jumuiya hiyo.

Katika mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Ngurdoto jijini Arusha, Marais hao, Jakaya Kikwete ambaye alikuwa mwenyeji wa mkutano, Mwai Kibaki wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda na Makamu wa kwanza wa Rais wa Burundi, Therence Sinunguruza wameeleza kusikitishwa kwao na mgogoro wa nchi za Sudan.

Wametaka taarifa iwafikie katika mkutano ujao utakafanyika Novemba mwaka huu.

Mkutano huo pia umeshuhudia itifaki ya masuala ya ushirikiano wa ulinzi miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki ambapo hivi sasa nchi moja ikivamiwa nchi zote za jumuiya zitashirikiana katika vita hiyo.

Hivi sasa itifaki hiyo itatakiwa kuridhiwa na mabunge ya nchi wanachama ifikapo Novemba 30, mwaka huu na baada ya hapo utakuwa mkataba utakaozilazimu nchi hizo kushirikiana katika masuala hayo ya ulinzi.

Katika hatua nyingine marais hao wametaka vita kati ya nchi za Sudan na Sudan Kusini kukomeshwa na nchi hizo zirejee katika meza ya mazungumzo.

“Tunawaasa viongozi wa nchi hizo mbili warudi katika meza ya mazungumzo na kutafuta njia ya amani ya kumaliza masuala yaliyobaki katika mkataba wa amani,” wakuu hao wa nchi walisema katika taarifa ya pamoja ambayo pia imesema wataendelea na wajibu wa kutafuta 

amani katika nchi hizo mbili na zingine zinazopakana na nchi za jumuiya hiyo.

Advertisements