PROFESA SHIVJI; AKOSOA MFUMO WA KUPATA KATIBA MPYA

  • Aushanga ushiriki mkubwa wa wanasiasa wastaafu
  • Ahoji kuendelea kuwapo kwa ibara ya 18 na 21
  • Asema bila ushiriki wa kutosha wa vyombo vya habari hakuna Katiba

MWENYEKITI wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, amesema kuwa Katiba Mpya inayotarajiwa kuundwa inaweza ikawa mbovu kutokana na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuruhusu wanasiasa wengi kuuteka mchakato wa uundwaji wake.

Akizungumza katika mkutano wa wandishi wa habari uliandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) Jumatatu Aprili 30, 2012 jijini Dar es Salaam, Prof. Shivji, alisema hatua hiyo inaweza kuunda Katiba mbovu yenye kulinda maslahi ya kundi moja hasa la wanasiasa.
“Inashangaza mchakato huu wa kutafuta Katiba mpya wameingizwa wanasiasa wastaafu, hawa waliingia baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenda Ikulu na vikafuata vyama vingine ambapo vyote vilipeleka hoja ya kushiriki,” alisema.
Kwa mujibu wa mhadhiri mstaafu huyo wa Chuo Kikuu ch Dar es Salaam, hata kitendo cha kuwapo kwa vifungu kadhaa kama vya ibara ya 18 na 21 vyenye kutoa adhabu ya kifungo jela na faini, vinaweza kuwa kikwazo cha umma wa Watanzania kutoa maoni yao.
Aliongeza kuwa vyombo vya habari havijionyeshi kushiriki katika mchakato huo kwani vimekosa uhuru na haki zao zimewekwa kwapani na serikali, wafanyabiashara, watoa matangazo na wamiliki wake.
Alisisitiza kuwa kama vyombo vya habari havitashiriki au kushirikishwa kikamilifu na kuhamasisha wananchi hakuna Katiba itakayopatikana badala yake tume itajikalia chumbani na kuamua wanachokiona kinawafaa.
Awali Meneja wa Maadili na Usuluhishi kutoka MCT, Alan Lawa, aliwahimiza waandishi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupata Katiba mpya licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo maslahi yao kuwa madogo.

Advertisements