MAWAZIRI WAPYA WAAPISHWA; WASEMA YALIYO MOYONI MWAO

Rais Jakaya Kikwete, Makamu wake Dkt. Mohammed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Katibu Mkuu Kiongozi, wakiwa katika picha ya pamoja na Mawaziri wateule baada ya kuapishwa rasmi Ikulu Dar es Salaam

•    Wahaidi kukabiliana na changamoto.
•    Makamba asema kazi yake ya kwanza ni kupitia upya garama za simu hapa nchini.
•    Dk. Mgimwa asema hakuna kitakacho shindikana, yeye kujikita zaidi na mfumko wa bei.

Rais Jakaya Kikwete amewaapisha mawaziri wapya pamoja na manaibu wake wakuu Jumatatu Mei 07, 2012 ikulu jijini Dar es Salaam.

Awali rais alifanya uteuzi huo kwa kufanya mabadiliko makubwa ya Baraza lake kwa kuingiza sura 13 mpya huku mawaziri na naibu mawaziri nane wakitupwa nje ya baraza hilo.

Katika mabadiliko hayo, amewapandisha naibu mawaziri wanne kuwa mawaziri kamili na kuwahamisha mawaziri nane na naibu mawaziri sita, huku mawaziri na naibu mawaziri 22 wakibaki katika wizara zao za awali.

Mawaziri wapya watio apishwa na Wizara zao kwenye mabano ni Mbunge wa Handeni,  Dk Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara), Mbunge wa Kalenga, Dk William Mgimwa (Fedha) na Mbunge wa Kuteuliwa, Profesa  Sospeter Muhongo (Nishati na Madini).

Manaibu Mawaziri wapya ni Mbunge wa Rufiji, Dk Seif Suleiman Rashid (Afya na Ustawi wa Jamii), Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene (Nishati na Madini-  Nishati), Mbunge wa Bumbuli, January Makamba (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia), Mbunge wa Buchosa, Dk Charles Tizeba (Uchukuzi) na Mbunge wa Mvomero, Amos Makala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo).
Wengine ni Mbunge wa Makete, Dk Binilith Mahenge (Maji), Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Maselle (Nishati na Madini ), Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki (Katiba na Sheria) na wabunge wa kuteuliwa, Janet Mbene na Saada Mkuya Salum ambao wote wamekuwa Manaibu Waziri wa Fedha.

Naibu Mawaziri waliopandishwa na kuwa mawaziri kamili ni Christopher Chiza (Kilimo, Chakula na Ushirika), Dk Harrison Mwakyembe (Uchukuzi), Dk Fenella Mukangala (Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo) na Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).

Baada ya kuapishwa baadhi ya mawaziri walinukuliwa wakisema malengo yao pamoja na vipaumbele vyao katika nafasi zao hizo mpya.

Dk Mgimwa
Waziri mpya wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa, alinukuliwa akisema kuapishwa kwake ni jambo la heshima hivyo ni lazima kujituma na kufanya kazi kwa maslahi ya Watanzania.

Alipoulizwa jinsi atakavyo kabiliana na changamoto ndani ya wizara hiyo ikiwa ni pamoja na tuhuma zilizomng ‘oa aliyekuwa waziri wa wizara hiyo Mustapha Mkulo, Dk Mgimwa ambaye ni Mbunge wa Kalenga alisema kabla ya kufanya lolote ni lazima kujiridhisha.

“Bungeni tulikuwa tunazungumza mengi kuhusu wizara hii lakini niseme kwamba ni lazima ufanye tathmini na ukishajua hali halisi ya tatizo ndio unaweza kuzungumza suluhisho la tatizo husika ni nini, hakuna kisichowezekana,” alinukuliwa Dk Mgimwa

Makamba
Kwa upande wake Naibu mpya wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli, alisema moja ya mambo ya kufanya katika wizara hiyo ni kutazama upya gharama za mitandao ya simu.

“Wizara hii inagusa maisha ya kila siku ya Mtanzania hivyo kuna ulazima wa kutizama gharama za mitandao ya simu ili iendane na maisha halisi ya mtanzania” alisema Makamba.

Akizungumzia masuala ya sayansi, Makamba alisema kuwa kuna ulazima wa kutizama upya msingi wa elimu ya sayansi kuanzia shule ya msingi kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi, lengo likiwa ni kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma somo hilo.

Pia, aligusia mikakati iliyowekwa awali ya asilimia moja ya pato la taifa kuingizwa katika ufanyaji wa tafiti mbalimbali na kwamba umefikia wakati wa suala hilo kuanza kutekelezwa kikamilifu.

“Tunatakiwa kuondoa urasimu wa matumizi ya teknolojia, hakuna haja ya watumishi wa Serikali na wananchi kupanga foleni kwa ajili ya kuchukua fomu, huu ni wakati wa fomu kujazwa katika mitandao tu,” alisema Makamba.

Hata hivyo, Makamba alisema kuwa mambo mengi anayoyaona na kuyazungumza hata bungeni yameshaanza kufanyiwa kazi na wizara hiyo.

Rashid

Naibu Waziri mpya wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Suleiman Rashid alisema kuwa kipaumbele katika wizara hiyo ni kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi, tena kwa ubora mkubwa.


“Huduma ya afya inatakiwa kuwafikia watu wote nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mgonjwa anasafirishwa eneo moja mpaka jingine kwa usalama” alisema Dk Rashid.


Rashid ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji alisema kuwa wizara inatakiwa kushughulikia sera na kutengeneza mipango mizuri ili watumishi wake wafanye kazi katika mazingira bora kwa faida yao na Watanzania wote.


Tizeba
Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ambaye ni Mbunge wa Buchosa alisema kwa kuwa ni msaidizi wa waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe, atahakikisha kila jambo analofanya bosi wake linakwenda sawa.


“Namshuruku sana Rais Kikwete, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais kwa kuwa wao ndio waliopendekeza mimi kuteuliwa kuwa waziri, nitatumia elimu yangu na uzoefu katika Serikali katika utendaji wangu wa kazi” alisema Dk Tizeba.


Mahenge
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara ya Maji, Dk Binilith Mahenge ambaye ni Mbunge wa Makete, alisema kuwa atazungumza zaidi mara baada ya kuapishwa.

 

Masele
Akizungumzia kuapishwa kwake Masele alisema kwanza atapambana kudhibiti mali ya umma, kuhakikisha udhibiti wa madini na kupata thamani halisi ya kile kinachozalishwa.


Pia alisema atashughulikia matatizo ya wachimbaji wadogo ambao wamekuwa wakinyonywa ili waweze kupata haki zao stahiki na kuinua uchumi wao.


“Niwahakikishie Watanzania kwamba nimepewa nafasi kubwa na nitafanya kazi kwa uadilifu, “alisema Masele.


Aliongeza kuwa; “Tutahakikisha tunazipitia sheria na kuhakikisha wamiliki wa migodi wanawasaidia wananchi na kila sehemu ulipo mgodi tutashughulikia ili wananchi na serikali vyote vinufaike.”

Alisema kuna watu wanapotosha kuhusu elimu yake, lakini ana Shahada ya Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) ambako alihitimu mwaka 2004.

Pia amewahi kufanya kazi katika benki kabla ya kupata nafasi ya kuwa Meneja Kanda ya Ziwa wa Kampuni ya Simu ya Mkononi ya Tigo.

Advertisements