VODACOM YAPUNGUZA GHARAMA ZA MAWASILIANO YA SIMU TANZANIA.

Ofisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Vodacom Tanzania Mwamvita Makamba.

•    Ujumbe mfupi (SMS) umepunguzwa kwa asilimia 45.
•    SMS zinazo sambazwa na tovuti ya Facebook na Twitter ni bure kabisa.


KAMPUNI ya simu za mikononi ya Vodacom, imepunguza kiwango chake cha gharama za upigaji simu, utumaji wa ujumbe mfupi na huduma za mtandao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, alisema wamezindua kampeni mpya itakayokuwa na punguzo hilo kwa nia ya kukidhi mahitaji ya walio wengi katika soko la mawasiliano la simu za mkononi, hususan vijana na itawawezesha kupata taarifa nzito za kila wakati na kuwasiliana kwa simu za sauti, ujumbe mfupi na intaneti kwa bei nafuu.

Katika kampeni mpya iitwayo Wajanja, wateja wa Vodacom wa malipo ya kabla watatozwa kiwango cha chini kabisa cha robo shilingi kwa simu za Vodacom kwenda Vodacom kuanzia saa 4 usiku hadi saa 1 asubuhi.

Ofa hii mpya vile vile itawatoza bei ya chini kabisa ya ujumbe mfupi ya sh 25 kwenda mtandao wowote Tanzania, pamoja na kusambaza tovuti ya Facebook na Twitter bure.

Alisema kampuni hiyo imepunguza bei ya ujumbe mfupi kwa asilimia 45. Hakika si vijana tu watakaofurahia ofa hii mpya bali wateja wote wa Vodacom wa huduma ya kulipia kabla watafaidika na huduma pamoja na viwango hivi vipya vya chini.

Vodacom Tanzania ni kampuni tanzu ya Vodacom Group (Pty) Limited, ya Afrika Kusini ambayo nayo ni kampuni tanzu ya Vodafone Group UK.

Vodacom Group (Pty) inamiliki asilimia 65 ya hisa zote huku nyingine 35 zikimilikiwa na mwanahisa wa Kitanzania na kampuni ya One Mirambo Ltd.

Advertisements