JOHN MYIKA; TAARIFA YA CCM INADHIHIRISHA MAMBO KADHAA YA MSINGI

MOSI, kwamba chama legelege huzaa serikali legelege.

Ulegelege wa serikali katika kushughulikia masuala ya mauji ya raia ni matokeo ya CCM kushindwa kuonyesha kwa vitendo inavyothamini utu na uhai wa binadamu.

CCM isingekuwa legelege ingeiwezesha serikali inayoongozwa na wanachama wake kufanya uchunguzi wa vifo vyenye utata (inquest) kupitia mahakama maalum (coronary court).

Pili, kwamba CCM imekosa uhalali wa kimaadili wa kukumea vitendo hivyo na kuchukua hatua zinazostahili kwa kuwa wanazungumza maneno matupu ya amani na utulivu huku viongozi na wanachama wake wanafanya matendo ya vurugu na umwahaji damu.

Nape anasema hakuna ushahidi wa kimazingira, wakati anajua kwamba mpaka sasa kuna majalada yamefunguliwa dhidi ya viongozi wa CCM Kiteto, Busanda, Biharamulo kwa vitendo vya umwagaji damu kwenye kampeni za chaguzi ndogo.

CCM inajua pia kifo cha kiongozi wa CHADEMA Arumeru mpaka sasa kuna viongozi wake wamekamatwa na kuhojiwa na polisi.

CCM inajua kuwa makada wake wametajwa kwa majina kwenye tukio la kukatwa mapanga kwa wabunge wa CHADEMA Mwanza tukio ambalo mashahidi wameeleza kuwa hata Askari polisi wameshuhudia na kuachia litokee.

CCM inajua kilichomo mpaka sasa kwenye jalada la uchunguzi la mauji ya Mbwana Masudi kule Igunga.

Orodha ni ndefu ya watu na matukio, hivyo taarifa ya CCM ya kutoa kanusho la ujumla ni ishara ya kuficha ukweli na kugeuza mjadala suala ambalo halitafanikiwa, tamko hili la Nape ni kama Al Sahaf kule Iraq, CCM ikae vikao vyake vya kikatiba itoe maamuzi ya chama hicho kuhusu suala hili la umwagaji damu na mauaji ambayo yanatuhumiwa kufanywa na viongozi wa chama hicho pamoja na vyombo vya dola sio kwa wanaCHADEMA tu bali hata kwa wananchi wa kawaida.

Inapaswa kuwa kutoka kauli ya amiri jeshi mkuu na kiongozi wa serikali Rais Jakaya Kikwete. Tunachohitaji kusikia ni hatua kuchukuliwa kwa wahusika kama kweli hawajatumwa na CCM na serikali na sio propaganda.

Tatu, imekuwa ni kawaida ya CCM kuanza kwa kuukana ukweli unapotolewa lakini hatimaye hukiri sehemu ya ukweli huo kama zilivyokuwa kauli za CCM mara baada ya kutolewa hadharani kwa Orodha ya Mafisadi.

Walianza kwa kanusho lakini hatimaye wakakubali kuna ufisadi ila wakadai mafisadi ni baadhi ya wanachama na sio chama, lakini mpaka leo wameshindwa kujivua gamba kama walivyodai.

Hata hili, wameanza kwa kukukana baadaye wanatesema ni la wanachama wachache waliotenda jinai bila kutumwa na chama, lakini ukweli utabaki kwamba haiwezekani matendo yote haya yakajirudiarudia bila vyombo vya ulinzi na usalama kufahamu.

Na tunazo taarifa juu ya mikakati ya CCM ya vurugu na vikundi wanavyotumia kufanya uharamia, na yapo majalada ambayo yamefunguliwa polisi. CCM inahitaji ushahidi gani zaidi toka kwa CHADEMA na umma?

Advertisements