MADIWANI WA TARIME WAMKATAA MTEULE WA JK KUWA MKUU WA WILAYA.

  • Wadai yeye ndiyo chanzo cha kuzorota mahusiano kati ya mgodi wa Barrick na wananchi.

    Wagoma kufanya vikao vyovyote katika halmashauri ikiwa Rais Kikwete hatamwondoa.

  • TAMISEMI wasema hawana mamlaka ya kinidhamu ya kumuwajibisha mkuu wa wilaya.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara, Alhamisi Mei 10, 2012 kwa kauli moja waligoma kuendelea na mkutano wa Baraza la Madiwani wakipinga hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuteua tena John Henjewele kuwa mkuu wa wilaya hiyo.

Henjewele ni miongoni mwa wakuu wa wilaya 63 waliobaki katika uteuzi mpya wa wakuu wa wilaya. Kati ya wakuu 70 wapya, saba ni wana habari.

Madiwani hao ambao walikutana katika kikao cha kawaida kilichoitishwa kujadili mbali na mambo mengine taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), walisema hawako tayari kuendelea na vikao vyovyote katika halmashauri ikiwa Rais Kikwete hatamwondoa mkuu huyo wa wilaya kwa madai kwamba amekuwa akiendesha utawala wake kwa ubabe.

Bila kujali itikadi za vyama vyao, madiwani hao 41 walisema watachukua hatua ya haraka kuwasilisha malalamiko yao kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara John Tuppa kumtaka awasilishe ujumbe wake kwa Rais Kikwete wakiomba kuondolewa haraka wilayani hapo kwa Henjewele.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Amos Sagara aliwaambia waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuvunjika kikao hicho kuwa alilalizimika kuahirisha kikao hicho kutokana na jazba za wazi zilizoonyeshwa na wawakilishi hao wa wananchi dhidi ya mkuu wa wilaya.

“Sasa katika mazingira kama hayo wameniomba nimuite mkuu wa mkoa ambaye walisema wanataka kuongea naye kabla ya kuendelea na kikao chochote nami sikuwa na pingamizi kwa kuwa walidai hawamtaki mkuu wa wilaya,” alisema.

Alisema kwa kuzingatia uzito wa suala hilo atachukua hatua za haraka kuwasiliana na mkuu wa mkoa ili kumkutanisha na madiwani kwa kuwa kisheria hawana mamlaka ya kumuwajibisha DC kutokana na kuwa mteule wa Rais.

Miongoni mwa tuhuma zilizoainishwa na madiwani hao baada ya kugomea kikao hicho ni pamoja na kuingilia utendaji wa kazi ngazi za serikali ya vijiji wakidai amekuwa akiwaondoa wenyeviti wa serikali ya vijiji na kukaimisha watu wake bila kufanyika uchaguzi.

Diwani wa Kata ya Turwa, Charles Ndesi, alidai mkuu huyo wa wilaya amekuwa chanzo cha kuzorota mahusiano kati ya wamiliki wa mgodi wa Barrick na wakazi wanaozunguka viunga vyake katika mji wa Nyamongo huku wananchi wakizidi kuwa maskini na uvamizi wa mara kwa mara katika mgodi huo.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Fidelis Lumato alisema wao kama taasisi ya Wizara ya TAMISEMI hawana mamlaka ya kinidhamu ya kumuwajibisha mkuu wa wilaya bali aliye na uwezo huo ni rais peke yake.

Advertisements

One thought on “MADIWANI WA TARIME WAMKATAA MTEULE WA JK KUWA MKUU WA WILAYA.

Comments are closed.