WANAHARAKATI WAPENDEKEZA RIPOTI YA CAG ITUMIKE KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WATUHUMIWA, WANASHERIA WAPINGA.

  • Diana Mwiru; “kila kitu kiko wazi tunachunguza nini tena”
  • Amina Uddy asema “Uwajibikaji wa viongozi umepungua, pia hawawajibiki katika kulinda rasilimali za nchi”.
  • Wanasheria wasema ripoti ya CAG haitoshi kuwafikisha wahusika mahakamani Uchunguzi wa TAKUKURU na DCI hauepukiki.

WANAHARAKATI nchini wamepinga   mpango wa Ikulu wa kutaka kuwapo na uchunguzi wa watendaji katika wizara na taasisi nyingine za umma wanaotuhumiwa kuhusika na ubadhilifu wa fedha za umma kwa kigezo kwamba ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inatosha kuwafikisha mahakamani.

Kauli hiyo imekuja baada ya Alhamisi Mei 10, 2012 Ikulu kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwachunguza watendaji hao kwa kile walichoeleza ni hatua za awali kabla ya kufungua kesi mahakamani.

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia katika mtandao wa Maendeleo na Jinsia (GDSS), Diana Mwiru alisema kwa sasa hakuna haja ya kufanya uchunguzi kwa kuwa ripoti ya CAG na zile za kamati tatu za bunge zinaonyesha wazi namna wahusika walivyohusika katika tuhuma hizo.

“Tuhuma zinazowahusu mawaziri zinatokana na wao kushindwa kuwajibika na kulisababishia hasara taifa, … ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za serikali (CAG) na ripoti za kamati tatu za bunge zote  ziko wazi na wote tumeona hasara iliyotokea ,hoja yangu ni kwamba tunachunguza nini tena? alihoji Mwiru na kuongeza:

“Kinachotakiwa kwa sasa ni wahusika kufikisha mahakamani kujibu tuhuma, unafanyika uchunguzi mwingine wa nini, hawa wanatufanya sisi hatujui kitu, kazi ya Takukuru ni kuchunguza rushwa swali ni je tuhuma hizo ni za rushwa? alihoji Mwiru.

Mwiru alisisitiza kuwa chunguzi zilizofanywa zinatosha na sasa watanzania wanataka kuona watuhumiwa wakifikishwa kwenye muhimili mwingine unao tafsiri sheria (Mahakama) ili kuona haki inatendeka.

Mawaziri waliondolewa katika nafasi zao walitajwa katika ripoti ya CAG, na pia ripoti za kamati za kudumu za bunge zilizowasilishwa kwenye vikao vya bunge lilifanyika hivi karibuni mkoani Dodoma.

Kamati hizo ni ile ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (POAC) ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira  Mwenyekiti wake , James Lembeli zilionyesha namna mawaziri walivyoshindwa kuwajibika na kusababishia taifa hasara kubwa.

Ripoti za kamati hizo Bungeni ziliibua tuhuma za upotevu wa fedha huku zikiwataja baadhi ya mawaziri kushindwa kuwajibika hali iliyomsukuma Bunge wa Kigoma kaskazini, Zitto Kabwe kuitisha hoja ya kukusanya saini za kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Amina Uddy mwanaharakati toka ForDIA alisema, hali ya uwajibikaji nchini imeshuka kwa kiwango kikubwa hali inayowafanya viongozi washindwe kujali na kusimamia rasilimali za umma.

Alisema ripoti zimebainisha matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma kwenye  Mashirika ya Umma,  serikali za mitaa na serikali kuu ambapo kuna upotevu mkubwa wa mali za umma ikiwamo suala la ulipaji mishahara hewa.

“Uwajibikaji wa viongozi umepungua, maadili yameporomoka na hii inathibitika wanapotaja mali wakati wa kuingia kwenye nyazifa zao lakini wanapotoka hawataji mali zao, pia hawawajibiki katika kulinda rasilimali za nchi” alisema Uddi.

Uddi alitaja sababu zinazochangia hilo kuwa ni pamoja na vitendo vya kuporomoka kwa maadili ya viongozi na mhimili wa Dola kuingilia mamlaka ya utendaji wa  mihili mingine ya mahakama na bunge.

Baadhi ya wanasheria walio ongea na M2S wamesema Kimsingi TAKUKURU (au vyombo vingine vinavyohusika na maswala ya uchunguzi wa jinai  kwa  mfano polisi au mwendesha mashtaka mkuu wa serikali) wanao uwezo wa kufanyia kazi taarifa hizi kwa maana ya kuanza uchunguzi. 

Hilo halina shaka. Sababu ni kuwa vyombo hivi havibanwi na sheria eti kusubiri “taarifa maalumu” ndipo waanze uchunguzi wa makosa. Wanaweza kufanyia kazi hata tetesi, au hata mere “suspicion” tu. 

Na ndio maana hata kazi zake ni pamoja na “kuzuia” rushwa na makosa ya jinai-yaani kuchukua tahadhari kabla hayajatokea. 

Kwa mfano kifungu cha 7 cha sheria ya takukuru ambayo inasema wazi kuwa kazi ya takukuru ni “investigate any alleged or suspected offence under this Act”.

Kama kuzuia walishidwa, basi wanapokua na shaka “suspicion” kwa kosa ambalo tayari limeshatendeka wanalo bado jukumu la kuchunguza mazingira yake ili kujiridhisha kwamba ni kweli au la.

Kwa hiyo, hizo taarifa za bunge na CAG ni sababu tosha ya vyombo hivyo kuanza huo uchunguzi (trigger of investigation). 

Sio lazima wachunguze mawaziri tu bali kila mtu anayehusishwa na kutenda hayo makosa ya rushwa, awe waziri au wafanyakazi wa chini yake, wanapaswa kuchunguzwa, na kama kuna ukweli katika hizo tuhuma wapelekwa mahakamani.

Cha msingi ni watanzania wajue kuwa hizo report pekee haziwezi kutosha kushinda kesi. Hizo ni, kama nilivyosema, triggers tu za uchunguzi. Kisheria zinaweza hata kuwa pungufu ya asilimia 50 ya ushaidi unaotakiwa. 

Ila zinaweza kutoa mwanga wa nani wachunguzwe, tuhuma gani, wapi wachunguze na watumie mbinu gani. 

Kama unakumbuka swala la Richmond na Rada watu walipiga sana kelele kwamba kwanini kesi hazikupelekwa mahakamani. 

Kunaweza kuwa siasa kweli zilitumika kuzima, lakini pia ikawa sio kweli. Mahakama zinafuata sheria na sio siasa.

Mamlaka yenye uwezo wa kufungua kesi za jinai dhidi ya watuhumiwa wa makosa hayo mahakamani ni mkurugenzi wa makosa ya jinai (DPP), ama mamlaka nyingine ambayo kisheria imepewa hiyo haadhi na DPP, au na sheria. Hii inaweza kuwa kwa mfano takukuru, polis n.k.

Tuchukue mfano wa takukuru. Takukuru yenyewe (on its own) haina mamlaka ya kufungua kesi mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika hadi iruhusiwe na DPP. 

Baada uchunguzi inapeleka kabrasha la uchunguzi huo kwa DPP ambaye akijiridhisha kwamba kweli kuna kesi inayoweza kufikia viwango vya kisheria kupelekwa mahakamani na ushindi ukapatikana (na sisitiza: viwango vya kisheria, sio kelele za kisiasa) basi anaruhusu kesi ifunguliwe.

Hili ni tatizo kwa sheria yetu ya rushwa hapa Tanzania. Nchi nyingine zimetoa mamlaka kwa taasisi zao za kupambana na rushwa kuweza kufungua kesi moja kwa moja bila kusubiri ruhusa ya DPP. Yaani, PCCB na DPP wangetakiwa wawe mamlaka mbili huru, zisizo tegemeana kwa namna yoyote. 

Bahati mbaya sisi bado tuko nyuma sana. Na katika hili tuko nyuma kiutendaji ukilinganisha na ule Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa dhidi ya Rushwa ambao unahitaji vyombo kama takukuru kuwa independent kwa kila Nyanja.

Advertisements

OFISI YA SENSA YATUMIA ZAIDI YA MILIONI 350 NJE YA BAJETI KUWALIPA WABUNGE

  • Katibu wa Bunge akiri fedha hizo zilipitia katika ofisi yake.

  • Zitto asema kuwa yeye amezirejesha kwa Katibu wa Bunge.

  • Hamad Rashid hana taarifa zozote, “NBS walifanya semina ambayo hata hivyo haikuwa na posho”.

Habari za kuaminika kutoka vyazo vyetu. Zimebainisha kuwa Ofisi ya Taifa ya Sensa, imewalipa wabunge mamilioni ya shilingi kwa ajili ya kufanya uhamasishaji kwenye majimbo hayo nje ya bajeti hiliyotengwa kwa kazi hiyo.

Inadaiwa ofisi ya sensa kutumia zaidi ya shilingi 350 milioni kuwalipa wabunge ambao idadi yao kwa sasa inafikia 350 kwa ajili ya kazi hiyo.

Malipo ya fedha hizo pia yanatia shaka kwani katika bajeti ya uhamasishaji wa sensa hakuna kipengele kinachoonyesha kwamba wabunge wanapaswa kupewa malipo hayo.

Fedha hizo zililipwa kupitia Ofisi ya Bunge baada ya kumalizika Kikao cha Bunge kilichopita, ambacho pamoja na mambo mengine, kilijadili Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), mjadala ambao ulizaa mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri.

Kutokana na bajeti ya sense ya aliyekuwa Waziri wa fedha Mustafa Mkulo ilionyesha Serikali ilipanga kukabiliana na nakisi ya Sh27.1 bilioni kwa kupunguza baadhi ya matumizi katika eneo la posho za vikao vya kamati za sensa kuanzia ngazi ya taifa na wilaya.

Hatua nyingine alizotaja ni kupunguza baadhi ya vifaa vya uhamasishaji kama vile khanga na vitenge na kutumia malori ya Serikali badala ya kukodi kwa ajili ya kusafirishia vifaa.

Alisema hatua hizo zingewezesha kukoa kiasi cha Sh3.7 bilioni hivyo kubaki nakisi ya Sh23.3bilioni ambazo zingetafutwa kwa njia mbalimbali.

Kamishna wa Sensa, Hajat Amina Said Mrisho alikiri kufanyika kwa malipo hayo kwa kile alichodai kuwa ni kuwawezesha wabunge kushiriki kazi ya kuhamasisha watu ili kufanikisha kazi hiyo.

“Ndiyo ni kweli kwamba tulitoa fedha kwa wabunge ijapokuwa siwezi kujua ni kiasi gani lakini kila mbunge alipewa shilingi milioni moja kwa ajili hiyo, tunafanya hivyo kwa lengo la kuwawezesha kuwahamasisha wananchi,” alisema Hajat Mrisho.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema fedha hizo zilipitia katika ofisi yake tu kwa ajili ya kuwafikia wabunge kama Ofisi ya Sensa ilivyoomba.

“Kama fedha hizo zingekuwa ni za Bunge ningekuwa na maelezo zaidi, lakini kusema kweli zimepitia tu kwa hiyo siwezi kuzisemea zaidi.” alisema Dk Kashililah

Hata hivyo baadhi ya wabunge waliohojiwa walionyesha kushangazwa na taarifa hizo huku wengi wakisema kuwa hawafahamu kama kuna fedha hizo na hawajapewa taarifa yoyote kuhusu suala hilo.

Hajat Mrisho alipoulizwa kama kutoa fedha kwa wabunge ni kuongeza mzigo kwenye bajeti alijibu: “Uhamasishaji ni moja ya mambo muhimu katika sensa.”

Aliongeza: “Fedha hazitolewi kwa wabunge tu, hata kwenye mikoa. Kwa mfano, tulipokuwa Tabora tuliupa mkoa Sh20 milioni kwa ajili ya kuuwezesha kufanikisha shughuli husika, tutaendelea kutoa fedha kwa ajili ya shughuli hizi zitakavyokuwa zikiendelea.”

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe alikiri Ofisi ya Sensa kuwaingizia kwenye akaunti za wabunge kiasi hicho cha fedha lakini akasema kuwa yeye amezirejesha kwa Katibu wa Bunge.

“Hii ni hongo, ni rushwa ya wazi kwa nini wabunge wapewe fedha hizi sasa? Mimi kweli niliwekewa lakini kwa kufahamu kwamba si sahihi nimezirejesha kwa Katibu wa Bunge, akitaka awarudishie wahusika,” alisema Zitto.

Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Stella Manyanya, alisema wabunge walipewa semina na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na kisha kuwataka wakirudi kwenye majimbo yao watoe elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa sensa na kuwahamasisha kushiriki kwa hali na mali.

“Nakumbuka baada ya semina hiyo wabunge waliwataka NBS kuwawezesha ili wawafikie wananchi kutoka na maeneo yao kuwa makubwa na wao NBS walisema wataangalia angalau namna ya kuchangia mafuta, lakini kwa kweli sijui kama kuna fedha ambazo zimeshatolewa,” alisema Manyanya na kuongeza:

“Kama wameshatoa nitawashukuru kwa kuwa watakuwa wamefanya vyema kwani kweli elimu kwa wananchi ni muhimu na maeneo ya wabunge ni makubwa.”

Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR Mageuzi), David Kafulila alisema hana taarifa zozote juu ya jambo hilo zaidi ya kujua kuwa, mbunge ni mjumbe wa kamati ya sensa ya wilaya.

Mbunge Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed alisema hana taarifa zozote juu ya suala hilo, zaidi ya kujua kuwa NBS walifanya semina ambayo hata hivyo haikuwa na posho.

“Walifanya semina bungeni na siku hizi hata posho huwa hawatoi na hizo fedha unazosema mimi sijaziona kabisa,” anasema Mohamed.

Hata hivyo, katika bajeti ya uhamasishaji wa shughuli za sensa ambayo ni Sh4.42 bilioni, hakuna kipengele cha malipo kwa wabunge kwa ajili ya kufanya uhamasishaji.

Badala yake, bajeti hiyo ya uhamasishaji imetenga fedha kwa ajili ya vifaa vya uhamasishaji (Sh3.95 bilioni), uimarishaji wa kitengo cha habari na mawasiliano kwa umma (Sh1.97 milioni) na matangazo kwenye vyombo vya habari (Sh74.8 milioni).

Gharama nyingine za uhamasishaji ni mikutano ya kuwaelimisha viongozi wa dini (Sh20.76 milioni), vipindi vya radio na televisheni (Sh57 milioni), kukodi magari na vifaa vya matangazo (Sh90 milioni) na gharama za mikutano ya uhamasishaji wilayani na mikoani (Sh117.3 milioni).

Fedha za sensa zinatolewa na Serikali ambayo imechangia asilimia 77 ya fedha zote na wadau wa maendeleo ambao ni Shirika la Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na Idadi ya Watu (UNFPA), Serikali ya Uingereza kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa (DFID) na Serikali ya Japan wametoa asilimia 23 ya bajeti nzima.