WANAHARAKATI WAPENDEKEZA RIPOTI YA CAG ITUMIKE KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WATUHUMIWA, WANASHERIA WAPINGA.

 • Diana Mwiru; “kila kitu kiko wazi tunachunguza nini tena”
 • Amina Uddy asema “Uwajibikaji wa viongozi umepungua, pia hawawajibiki katika kulinda rasilimali za nchi”.
 • Wanasheria wasema ripoti ya CAG haitoshi kuwafikisha wahusika mahakamani Uchunguzi wa TAKUKURU na DCI hauepukiki.

WANAHARAKATI nchini wamepinga   mpango wa Ikulu wa kutaka kuwapo na uchunguzi wa watendaji katika wizara na taasisi nyingine za umma wanaotuhumiwa kuhusika na ubadhilifu wa fedha za umma kwa kigezo kwamba ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inatosha kuwafikisha mahakamani.

Kauli hiyo imekuja baada ya Alhamisi Mei 10, 2012 Ikulu kuagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kuwachunguza watendaji hao kwa kile walichoeleza ni hatua za awali kabla ya kufungua kesi mahakamani.

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Jinsia katika mtandao wa Maendeleo na Jinsia (GDSS), Diana Mwiru alisema kwa sasa hakuna haja ya kufanya uchunguzi kwa kuwa ripoti ya CAG na zile za kamati tatu za bunge zinaonyesha wazi namna wahusika walivyohusika katika tuhuma hizo.

“Tuhuma zinazowahusu mawaziri zinatokana na wao kushindwa kuwajibika na kulisababishia hasara taifa, … ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za serikali (CAG) na ripoti za kamati tatu za bunge zote  ziko wazi na wote tumeona hasara iliyotokea ,hoja yangu ni kwamba tunachunguza nini tena? alihoji Mwiru na kuongeza:

“Kinachotakiwa kwa sasa ni wahusika kufikisha mahakamani kujibu tuhuma, unafanyika uchunguzi mwingine wa nini, hawa wanatufanya sisi hatujui kitu, kazi ya Takukuru ni kuchunguza rushwa swali ni je tuhuma hizo ni za rushwa? alihoji Mwiru.

Mwiru alisisitiza kuwa chunguzi zilizofanywa zinatosha na sasa watanzania wanataka kuona watuhumiwa wakifikishwa kwenye muhimili mwingine unao tafsiri sheria (Mahakama) ili kuona haki inatendeka.

Mawaziri waliondolewa katika nafasi zao walitajwa katika ripoti ya CAG, na pia ripoti za kamati za kudumu za bunge zilizowasilishwa kwenye vikao vya bunge lilifanyika hivi karibuni mkoani Dodoma.

Kamati hizo ni ile ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma (POAC) ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira  Mwenyekiti wake , James Lembeli zilionyesha namna mawaziri walivyoshindwa kuwajibika na kusababishia taifa hasara kubwa.

Ripoti za kamati hizo Bungeni ziliibua tuhuma za upotevu wa fedha huku zikiwataja baadhi ya mawaziri kushindwa kuwajibika hali iliyomsukuma Bunge wa Kigoma kaskazini, Zitto Kabwe kuitisha hoja ya kukusanya saini za kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Amina Uddy mwanaharakati toka ForDIA alisema, hali ya uwajibikaji nchini imeshuka kwa kiwango kikubwa hali inayowafanya viongozi washindwe kujali na kusimamia rasilimali za umma.

Alisema ripoti zimebainisha matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma kwenye  Mashirika ya Umma,  serikali za mitaa na serikali kuu ambapo kuna upotevu mkubwa wa mali za umma ikiwamo suala la ulipaji mishahara hewa.

“Uwajibikaji wa viongozi umepungua, maadili yameporomoka na hii inathibitika wanapotaja mali wakati wa kuingia kwenye nyazifa zao lakini wanapotoka hawataji mali zao, pia hawawajibiki katika kulinda rasilimali za nchi” alisema Uddi.

Uddi alitaja sababu zinazochangia hilo kuwa ni pamoja na vitendo vya kuporomoka kwa maadili ya viongozi na mhimili wa Dola kuingilia mamlaka ya utendaji wa  mihili mingine ya mahakama na bunge.

Baadhi ya wanasheria walio ongea na M2S wamesema Kimsingi TAKUKURU (au vyombo vingine vinavyohusika na maswala ya uchunguzi wa jinai  kwa  mfano polisi au mwendesha mashtaka mkuu wa serikali) wanao uwezo wa kufanyia kazi taarifa hizi kwa maana ya kuanza uchunguzi. 

Hilo halina shaka. Sababu ni kuwa vyombo hivi havibanwi na sheria eti kusubiri “taarifa maalumu” ndipo waanze uchunguzi wa makosa. Wanaweza kufanyia kazi hata tetesi, au hata mere “suspicion” tu. 

Na ndio maana hata kazi zake ni pamoja na “kuzuia” rushwa na makosa ya jinai-yaani kuchukua tahadhari kabla hayajatokea. 

Kwa mfano kifungu cha 7 cha sheria ya takukuru ambayo inasema wazi kuwa kazi ya takukuru ni “investigate any alleged or suspected offence under this Act”.

Kama kuzuia walishidwa, basi wanapokua na shaka “suspicion” kwa kosa ambalo tayari limeshatendeka wanalo bado jukumu la kuchunguza mazingira yake ili kujiridhisha kwamba ni kweli au la.

Kwa hiyo, hizo taarifa za bunge na CAG ni sababu tosha ya vyombo hivyo kuanza huo uchunguzi (trigger of investigation). 

Sio lazima wachunguze mawaziri tu bali kila mtu anayehusishwa na kutenda hayo makosa ya rushwa, awe waziri au wafanyakazi wa chini yake, wanapaswa kuchunguzwa, na kama kuna ukweli katika hizo tuhuma wapelekwa mahakamani.

Cha msingi ni watanzania wajue kuwa hizo report pekee haziwezi kutosha kushinda kesi. Hizo ni, kama nilivyosema, triggers tu za uchunguzi. Kisheria zinaweza hata kuwa pungufu ya asilimia 50 ya ushaidi unaotakiwa. 

Ila zinaweza kutoa mwanga wa nani wachunguzwe, tuhuma gani, wapi wachunguze na watumie mbinu gani. 

Kama unakumbuka swala la Richmond na Rada watu walipiga sana kelele kwamba kwanini kesi hazikupelekwa mahakamani. 

Kunaweza kuwa siasa kweli zilitumika kuzima, lakini pia ikawa sio kweli. Mahakama zinafuata sheria na sio siasa.

Mamlaka yenye uwezo wa kufungua kesi za jinai dhidi ya watuhumiwa wa makosa hayo mahakamani ni mkurugenzi wa makosa ya jinai (DPP), ama mamlaka nyingine ambayo kisheria imepewa hiyo haadhi na DPP, au na sheria. Hii inaweza kuwa kwa mfano takukuru, polis n.k.

Tuchukue mfano wa takukuru. Takukuru yenyewe (on its own) haina mamlaka ya kufungua kesi mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika hadi iruhusiwe na DPP. 

Baada uchunguzi inapeleka kabrasha la uchunguzi huo kwa DPP ambaye akijiridhisha kwamba kweli kuna kesi inayoweza kufikia viwango vya kisheria kupelekwa mahakamani na ushindi ukapatikana (na sisitiza: viwango vya kisheria, sio kelele za kisiasa) basi anaruhusu kesi ifunguliwe.

Hili ni tatizo kwa sheria yetu ya rushwa hapa Tanzania. Nchi nyingine zimetoa mamlaka kwa taasisi zao za kupambana na rushwa kuweza kufungua kesi moja kwa moja bila kusubiri ruhusa ya DPP. Yaani, PCCB na DPP wangetakiwa wawe mamlaka mbili huru, zisizo tegemeana kwa namna yoyote. 

Bahati mbaya sisi bado tuko nyuma sana. Na katika hili tuko nyuma kiutendaji ukilinganisha na ule Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa dhidi ya Rushwa ambao unahitaji vyombo kama takukuru kuwa independent kwa kila Nyanja.

Advertisements

5 thoughts on “WANAHARAKATI WAPENDEKEZA RIPOTI YA CAG ITUMIKE KUWAFIKISHA MAHAKAMANI WATUHUMIWA, WANASHERIA WAPINGA.

 1. Ripoti ya CAG pekeyake haitoshi..ni ya kiauditor zaidi pia haina nguvu mahakamani..kwasababu ni tuhuma 2. Hebu tuwaachie TAKUKURU n’ DCI wafanye uchunguzi na hatimaye kukabidhi taarifa hiyo pamoja na ripoti ya CAG kwa DPP ili ajue kama watuhumiwa wana kesi ya kujibu mahakamani au la? T’s quite a process lads, ishu ni kwamba mchakato uwe wa wazi na tarehe za kumaliza kila chunguzi uwekwe wazi kwasababu ili jambo linahusu kuliwa kwa fedha/mali za watanzania maskini wa kutuptwa…

 2. kama Ripoti ya CAG haitoshi kuwafikisha mahakamani mbona wamewajibika kwa ripoti hiyo hiyo hizi ndo sanaa zinazowakera Watanzania,ila mwisho upo tutakapo pata katiba itakayo tuepusha na habari ya teua teua.

 3. Henry! lets me share also u re frustration…. ni kweli ila mapungufu yapo kwenye sheria zetu. kama ulivyosema ni jambo la heri kama tukipigania katiba yetu mpya iondoe hii mianya ya watu kula fedha za umma na kutokuchukuliwa hatua.

 4. Mimi sioni upungufu kwenye sheria kwa sababu tu report ya CAG haiwezi kutumika moja kwa moja mahakamani. Unajua ile report haijakaa kisheria imekaa kiukaguzi wa mahesabu. Na katika ukaguzi wa mahesabu hata kama hela inasemekana “imetumika vibaya” haina maana imeibwa. Kwa mfano, ile ya Tanesco kwamba wametumia hela nyingi zaidi kwenye manunuzi kuliko walivyoruhusiwa haitoshi tu kuanzisha kosa la jinai. Iinaweza kumaanisha kuwa kweli vitu vimenunuliwa ila tu wameexceed kiasi ambacho kilikuwa authorized. Hapa utakubaliana nami kuwa haina maana moja kwa moja kuwa hizo hela ziliingia mfukoni mwa mtu (wizi). Tatizo hapa ni usimamizi wa taratibu za manunuzi kitu ambacho ni kosa la kiutendaji, na wala haitoshi kuwa kosa la kuisababaishia hasara serikali.

  Kwa hiyo tuache wanasheria wafanye uchambuzi wa hiyo ripoti ndio wajue wapi kweli kuna kosa la jinai, wapi hamna. Makosa ya kiutendaji au kiutumishi ambayo sio ya jinai yatashughulikiwa kiutumishi. Hatuwezi tu kuwapeleka mahakamani on the basis of that report tu. Utashangaa wote wanaachiwa na tutaanza kusema oh “mahakama zinachukua rushwa”. Na tujue kuwa standard of proof hapa katika kosa la jinai ni “beyond any reasonable doubt”. Hapo ndio hakuna mwanasheria atakubali kuumbuka mahakamani kwa kupeleka kesi ya hisia tu. Sheria haiwezi kwenda kwa hisia ndugu zangu.

  Kuhusu kuachia ngazi hao mawaziri ni “political responsibility” tu. Katika sheria za utawala (administrative law) kuna kitu kinachoitwa “collective and individual responsibility”. Hii ya hapa ni individual responsibility imefanyika kuwaondoa hao. Kwa kifupi kama scandal inatokana na watendaji ambao kiutawala wako chini yako, mtu unatakiwa uachie ngazi: si kwa sababu wewe ndie uliyetenda hilo kosa bali kwa sababu hao waliotenda walikuwa your “extended arms” (alter egos). Kwa hiyo si lazima iwe kwamba hao mawaziri waliiba wao. Sasa kama walishiriki kuiba etc hayo yote sasa ndio yatamalizwa kwa uchunguzi wa kisheria na hiyo report ya CAG itakuwa ni sehemu muhimu ya kuanzia.

  Mimi nakubaliana kabisa na ndugu Kikoko kuwa hata iweje hii report haitoshi. Lazima uchunguzi huru wa kisheria ufanyike. Hakuna mwanasheria yeyote ambaye anaweza kuichukua na kusema sasa nina ushahidi wa kutosha (yaani hiyo ripoti tu kama ilivyo). Sheria sio rahisi hivyo ndugu zangu.

  Na hata katiba mpya haiwezi kubadilisha hili. Sijui ni kwa namna gani katiba mpya inaonekana itabadili utaratibu huu. Labda ndugu wa M2S wafafanue zaidi nini hasa wanatarajia katiba iseme ili hali ya sasa ibadilike.

  Asante

Comments are closed.