BAADA YA KUNYAMAZISHA JOSHUA NASSARI, SHERIA KANDAMIZI ZA KIKOLONI KUENDELEA KUWABANA WANAHABARI.

Joshua Nassari (MB)

  • Sina hakika kama bila sheria hii, Joshua Nassari angekana kauli yake na kulazimika kufanya kile kinacho tafsiriwa kujutia hotuba yake.
  • Makaramba, Sheria hii ni mbaya kwa ustawi wa waandishi wa habari pamoja na vyombo vyao.
  • Viongozi wakielezwa makosa hukubali na hujisahihisha, lakini watawala hununa ndiyo maana mara huita wanahabari wetu ‘uchwara’ mara ‘makanjanja’ na mara nyingine hukanusha hata “kauli” zao wenyewe.
  • “Tunapenda kuweka wazi kwamba, uvumilivu kwa mwenendo na hotuba hasidi katika jamii ni moja ya gharama inayopaswa kulipwa na jamii huru na iliyo wazi”, hiyo ndiyo gharama ya demokrasia.
Kwa tahadhali kubwa nimeamua kulizungumzia hili huku nikijuwa nitashambuliwa kwa nguvu zote na watetezi wa sheria hii kandamizi, uenda hata kuitwa kuhojiwa na vyombo vya sheria kwa kosa la kusema ninacho fikilia.

Maandishi yoyote au kauli, yawe kupitia vitabu vya fasihi au kwenye magazeti, Redio na TV au tovuti yanayotoa elimu ya uraia kwa umma au yanayo amsha akili na kuhamasisha watu wajitambue huchukiwa na watawala.

Wakosoaji wangu wakubwa watakuwa ni vyombo vya dola na wale walio madarakani, na kwa bahati mbaya kalamu yangu haiko kwa ajili ya kuwapendeza watu fulani fulani hivyo niko radhi nitengeneze uadui kwa kusema ukweli ili kuinusuru nchi hii na unafiki usiyo vumilika kama ilivyo kuwa kwenye simulizi za Shaban Robert na nchi ya kusadikika.

Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliwasakama, tena baadhi ya waandishi nguli, na kuwaita “waandishi uchwara”.

Lakini katika harakati za kuelekea ikulu, Jakaya Kikwete aliwaweka kwenye mtandao wake “waandishi uchwara wa Mkapa” wakaandika makala zilizoua hadhi ya baadhi ya wagombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama pinzani, na aliposhinda akawapa ulajiri ikulu, ofisi ya waziri mkuu na Wakuu wa Wilaya.

Rais Kikwete, amebadili msamiati, hawaiti waandishi uchwara ila makanjanja. Wakati Mkapa alikuwa anaruka kwa ndege hadi Ulaya kuteta na waandishi aliodai kuwa makini, Kikwete anabagua waandishi na vyombo vya habari anavyoona ni “kanjanja”.

Lengo si kumyooshea kidole mtu mmoja mmoja, au wakosoaji wangu watakavyo iweka kuwa najaribu kumsafisha Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari.

Hebu tujikumbushe Mwaka 1996 ulipofanyika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Temeke, Rais Benjamin Mkapa aliwaambia wakazi wa Temeke kwamba wasipompatia Cisco Mtiro wa CCM nafasi ya ubunge hatampa ushirikiano mshindi yeyote nje ya huyo Cisco. 

Kwa kauli hiyo Mkapa alitaka wananchi wasimchague Augustine Mrema aliyekuwa wa NCCR-Mageuzi.

Magazeti yakaandika ujumbe huo wa Mkapa na Tv za wakati huo zikamwonyesha akitoa ujumbe huo. 

Lakini siku iliyofuata, Mkapa aling’aka eti hakusema hivyo na akashutumu vyombo vya habari.

Hayo hayakuishia mwaka huo yameendelea mpaka leo hii, Tunamshutumu Joshua Nassari kwa kauli yake, je kauli kama hizi za Mkapa alizo kuwa anapambana nazo zikizungumzwa wazi wazi wakati wa Kampeni za Ubunge Arumeru Mashariki hakuna hata mmoja anaye zisema kuwa zilikuwa zinahatarisha ustawi wetu kama Taifa. 

Maandishi huhifadhi elimu, na mtu anayejua maandishi atakuwa amepata elimu, na mtu mwenye elimu atakuwa amepata silaha ya kupambana na maisha, kujitambua na kudai haki.

Hii ndiyo siri kwa nini watawala hawataki wananchi wasome maandishi yanayo zindua akili zao. Hawapendi kuona wananchi wanawafuatilia kwa karibu; hawataki tawala zao kuchunguzwa wala kudodoshwa.

Waandishi au watu wanaoweka wazi makosa ya watawala na serikali zao, hushutumiwa wao na vyombo vyao,  kuwa vinafanya uchochezi. Hutangazwa kuwa wanahatarisha amani ya nchi.

“Sheria hii ya uchochezi ilitungwa wakati wa ukoloni kwa ajili ya kuwalinda watawala wa wakati huo dhidi ya mtu yoyote au kundi la watu aliyetaka kutetea haki yaje ya msingi, lakini bahati mbaya mpaka sasa bado ipo na ni pana hivyo ikitumiwa vibaya inaweza kuwanasa wengi wakiwemo waandishi, wanaharakati hata wanasiasa wa upinzani” alisema Jaji wa Mahakma Kuu ya Tanzania Robert Makaramba

Ningependa tuungane pamoja katika utafiti tuliofanya kutoka katika matukio anuai ya kuaminika ndani ya nchi yetu na kujadiri hili bila unafiki wowote.

Wakati wa enzi za Wafalme, adhabu kali ilitolewa kwa wale waliojaribu kuhoji vitendo au mamlaka ya Mfalme. Leo hii ni hivyo hivyo kwa wale wanao hoji umoja wa kitaifa au muungano wetu. 

Ni jambo la kawaida kusikia vyombo vya habari kufungiwa, Wahariri na “wanaharakati” kushitakiwa kwa makosa ya jinai kwa sababu ya kuchapisha au kutamka maneno au maoni ya kawaida, lakini yanaweza kugeuzwa kwa ufundi wa kisiasa kuwa “uchochezi”, kwa sababu tu ya kutowafurahisha baadhi ya wenye madaraka.

Udhibiti huu wa habari na mawazo ya mtu binafsi mara nyingi unakwenda kinyume cha ibara ya 18 ya Katiba yetu inayosema:  “Kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari, anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake”.

Kinachokera ni kwamba, tumetoa uhuru (demokrasia) kubwa kupindukia katika sekta ya uchumi na biashara (ubinafsishaji, uwekezaji usiojali na uporaji rasilimali bila kudhibitiwa), lakini tumebana demokrasia ya mawazo na demokrasia ya kisiasa (Katiba isiyokidhi matakwa ya wengi, sheria 40 kandamizi, sheria mbovu ya uchaguzi), na kujenga taifa la kitabaka kati ya walio nacho kiuchumi na kisiasa na tabaka la wasio na chochote kiuchumi na kisiasa.

Uhuru wa kujieleza maana yake ni biashara ya mawazo, yenye soko kamili kama ilivyo kwa bidhaa nyingine katika soko.

Kwa uhuru huu, jamii hunufaika kwa njia ya kubadilishana mawazo kwani hakuna mtu mmoja aliye na jibu kamili juu ya mwelekeo sahihi na kwa matatizo yanayoweza kuikabili jamii.

Kwa sababu hii, si jukumu la Serikali wala la mtu mmoja kuamua ni mawazo yapi au habari ipi ni ya kweli na ipi ni ya uongo; ni soko pekee la mawazo linaloweza kuamua yote hayo. 

Kwa hiyo, ili jamii iweze kunufaika na mawazo pamoja na vipaji vya watu wake, haina budi kuruhusu ushindani wa kimawazo miongoni mwa watu wake. Kutofanya hivyo ni kuigeuza jamii kuwa ya mataahira.

Soko ndilo litakalokuwa muamuzi ambapo mawazo hafifu na dhaifu yatashindwa uwanjani kwa nguvu na ubora wa mawazo sahihi na ya kweli, wala si kwa shuruti au nguvu za Serikali.

Jamii lazima ifike mahali iruhusu mtu mmoja kutangaza kwamba “mfalme yuko uchi”, hata kama msemaji wa ukweli huo ataonekana “mwongo” kwa kuwa kile kinachoitwa uongo leo kinaweza kugeuka kuwa ukweli kesho, kama atapewa nafasi ya kusikilizwa. 

Tutazame kwa ufupi tu historia ya dhana ya uhuru wa kujieleza katika mazingira ya nchi zinazoongoza kwa demokrasia, tuone kama uhuru wa kujieleza kama sehemu ya demokrasia, unafanya kazi ipasavyo hapa kwetu.

Kwa mfano, mnamo karne ya tisa, Mfalme Alfred wa Uingereza aliagiza kuwa kila aliyejaribu kuihoji Serikali akatwe ulimi kwa kuwa ulimi ndio uliokuwa nyenzo pekee ya mawasiliano na njia ya kujieleza.

Hivi leo ulimi huo ni vyombo vya habari vinavyoweza “kukatwa” ulimi kwa njia ya kufungiwa au kushitakiwa kwa makosa ya “uchochezi”.

Ingawa mwaka 1620, uhuru wa kujieleza uliungwa mkono mno kutoka kwa Mfalme James wa Kwanza, lakini hata hivyo, Mfalme huyo naye hakuweza kutoa uhuru kamili alipoonya kwamba “masuala ya Serikali si mambo ya kuzungumzia mitaani; mtu hapashwi kusema au kumkosoa mtawala na utawala wake”.

Kuibuka kwa uchapishaji wa habari kulitoa tishio jipya kwa watawala kwa vile maandishi ni kitu cha kudumu na uwezekano wake wa kuwafikia watu wengi zaidi ni mkubwa.

Ili kukabiliana na hali hiyo, dola ilitoa amri magazeti yote yaandikishwe na kudhibitiwa, na yale yasiyofanya hivyo yafungiwe au kufutwa kabisa.

Ilikuwa mwaka 1689, Malkia Mary (na mumewe William) alipochukua madaraka kwamba Uingereza ilianzisha sheria ya haki za binadamu (Bill of Rights) na kulipa Bunge ukuu (Parliamentary Sovereignty) na uhuru wa kujieleza.

Kwa hatua hiyo, haki za raia zilitambuliwa, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa mawazo moja kwa moja au kupitia vyombo vya habari.

Huko Marekani uhasama kati ya Serikali na vyombo vya habari, ulisababisha uhuru wa kujieleza kutoweka kufuatia kesi ya uchochezi iliyomhusu mchapishaji John Peter Zenger, mwaka 1735, pale Mahakama ilipotoa uhuru na haki kwa raia wa kujieleza au kupinga na hata kuikosoa dola ilipobidi.

Kuanzia hapo, Sheria ya Uchochezi ilibakia kwa jina tu hadi mwaka 1801 ilipofutwa na Rais Thomas Jefferson alipoingia madarakani.

Uingereza kwa upande wake ilifuta makosa yote yanayohusu “habari za uongo” (False News Offences) mwaka 1887. Kinyume chake leo, miaka 50 ya uhuru, sisi tunaelekea kule wenzetu walikotoka miaka 110 iliyopita huku tunajitapa kujenga demokrasia kwa mfumo wa nchi hizo.

Uhuru wa kujieleza kama ilivyo demokrasia, lazima uzingatie vigezo na viwango vya kimataifa.

Hivyo, kama kweli tumekubali kufuata mifumo ya demokrasia, uhuru, na haki za binadamu ya nchi za Magharibi – kama vile demokrasia na utawala bora, soko, siasa na uchumi huria; iweje leo tuendeleze udhibiti kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari ambao mataifa hayo yalipiga marufuku karne mbili zilizopita, kama njia ya kuimarisha demokrasia?

Tunahofu nini? Au tunaogopa kuambiwa “mfalme yuko uchi” inapokuwa kweli kwamba Mfalme huyo hana nguo?

Jamii makini haiwezi kukubali kulazimishwa kushangilia au kusifia Mfalme asiye na nguo eti kwa sababu “suti” aliyovaa inaonekana kwa wasio na dhambi tu, wakati ukweli yuko uchi; na kwa vitisho eti kwamba “wasioiona” suti hiyo ni wadhambi, na hivyo watobolewe macho yote kama adhabu kwa “dhambi” zao. 

Hata iweje, wapo watoto “Kina Joshoa Nassari” watakaosema ukweli kwamba “Mfalme yu uchi”, kwa sababu watoto hawajui kujipendekeza, wala kwa kusema ukweli huo hawana cha kunufaika wala kupoteza; wanachojali ni ukweli mtupu.

Uhuru wa kujieleza nchini umedhibitiwa kwa sheria mbili ambapo unapofikia kiwango fulani huitwa “uchochezi” (sedition). Kwa kuanzia, “uchochezi” ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code) kifungu cha 50 na 55; pili “uchochezi” ni kosa chini ya kifungu 55 cha Sheria ya Magazeti, Namba 3 ya mwaka 1976.

Wakati sheria hizi mbili zinadhibiti uhuru wa kujieleza, kinyume cha sheria hizo, Katiba ya nchi inatoa uhuru huo bila kikomo, chini ya Ibara ya 18, kama nilivyoinukuu mwanzo.

Kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, je, si kweli kwamba yale yanayoitwa “makosa ya uchochezi” si uchochezi bali ndio uhuru wenyewe wa kujieleza na wa kutoa maoni yoyote? Je, huko si kuingilia uhuru wa mawasiliano wa mtu?

Ni nani mwenye haki ya kuamua uhalali wa maoni (yoyote) na aina ya uhuru wa mawazo ya mtu katika kutekeleza haki hiyo ya kikatiba?

Je, ni halali kwa mtu kushitakiwa chini ya sheria za makosa ya jinai? Ni kiwango gani cha uhuru kinachovumilika ili usiitwe “uchochezi”?

Maswali haya yananifanya nirejee kesi ya miaka ya karibuni nchini Uganda, ya Charles Onyango-Obo na mwenzake dhidi ya Serikali.

Oktoba 24, 1997 Charles Onyango-Obo, Mhariri wa gazeti la “The Monitor”, na mwenzake, Andrew Mujuni Mwenda, Mwandishi Mwandamizi, walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa kosa la kuchapisha habari za “uchochezi” zenye kichwa cha habari:  “Kabila aliilipa Uganda kwa dhahabu”, na kudai kuwa malipo hayo yalifanywa kuishukuru Uganda kwa kumsaidia (Kabila) kwenye vita nchini Zaire vya kumng’oa madarakani dikteta Mobutu Sese Seko wa nchi hiyo. Mahakama iliwaachia huru Obo na Mujuni kwa kuwaona hawakuwa na hatia.

Baada ya hapo, waandishi hao waandamizi walifungua kesi Mahakama ya Katiba kuiomba itoe ufafanuzi, kama Serikali ilikuwa na uwezo na haki ya kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari chini ya Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code) kwa kudai kulinda “maslahi ya umma”. 

Mahakama ya Katiba ilisema; “Serikali ilikuwa na haki na uwezo huo” na kutupilia mbali maombi yao.

Obo na Mujuni hawakuridhika; walikata rufaa Mahakama ya Rufaa (Supreme Court) dhidi ya uamuzi huo wa Mahakama ya Katiba.

Tunapotoa mfano huu, ikumbukwe kwamba Ibara ya 29 (1) ya Katiba ya Uganda ya 1995, inafanana na Ibara ya 18 ya Katiba yetu ya 1977 inayotumika hadi sasa.

Vivyo hivyo, kosa la “uchochezi” lililopo chini ya kifungu cha 50 cha Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code Act) ya Uganda ndilo hilo hilo lililopo chini ya vifungu namba 50 na 55 vya Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code), na kifungu 55 cha Sheria ya Magazeti ya Tanzania, Namba 3 ya 1976.

Suala katika kesi hii lilikuwa kuhusu kama kifungu cha 50 cha Sheria ya Makosa ya Jinai hakipingani na Ibara ya 29 ya Katiba ya nchi hiyo inayotoa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari bila ya kuingiliwa na mtu au chombo chochote.

Katika hukumu yake, Mahakama hiyo ya Rufaa ilibaini kuwa, kifungu cha 50 (kwa Tanzania, ni kifungu cha 50 na 55) cha Sheria ya Makosa ya Jinai kimedumu kabla na baada ya Uganda kuridhia Sheria ya Haki za Binadamu (Bill of Rights), kama ilivyo pia kwa Tanzania iliyoridhia haki hizo kwa Sheria ya 1984 na kuanza kutumika mwaka 1987.

Mahakama ilisema, kifungu hicho cha Sheria ya Makosa ya Jinai ni moja ya sheria za kikoloni zenye chimbuko lake la miaka ya 1200 nchini Uingereza.

Mahakama ilifafanua kuwa, “maslahi ya umma” yanakubalika na kulindwa na sheria yenye misingi ya uhuru na demokrasia, isiyoruhusu unyanyasaji wa kisiasa, kuweka watu kizuizini na udhalilishaji wa kibinadamu.

Mahakama ilibaini kuwa Uganda, kama moja ya jamii za kidemokrasia, inapaswa kuzingatia misingi ya demokrasia kwa viwango vya kimataifa; na kwamba chini ya viwango hivyo, si halali kuugeuza uchapishaji wa habari za uongo kuwa kosa la jinai, wakati Katiba ya nchi na zile za kimataifa kuhusu haki za binadamu (Bill of Rights) zinapingana na dhana hiyo.

Wakifafanua matakwa ya Ibara ya 29 (Tanzania ni ibara ya 18) ya Katiba, Majaji wa Mahakama hiyo walisema, Katiba inatoa na kulinda uhuru wa hotuba, uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari:

“Tunapenda kuweka wazi kwamba, uvumilivu kwa mwenendo na hotuba hasidi katika jamii ni moja ya gharama inayopaswa kulipwa na jamii huru na iliyo wazi”, Mahakama ilisema na kuongeza kuwa, hiyo ndiyo gharama ya demokrasia.

Ni aina gani ya mawazo yanayoweza kuvumilika? 

Majaji wa Mahakama hiyo walichukua ibara ya 9 ya Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamu (The African Charter on Human and Peoples’ Rights) kama kielelezo na ambayo inafanana na ibara ya 29 ya Katiba ya Uganda (Tanzania ibara 18 (2), kwamba:

“Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali duniani kote” na kwamba, “kila mtu ana haki ya kutoa na kusambaza au kueneza mawazo yake”.

Walisema, “ni kutokana na ukweli huu kwamba, haki ya uhuru wa kujieleza haijumuishi haki pekee ya kuhifadhi, kupokea na kutoa aina zote za mawazo kama vile maoni sahihi, mawazo mazuri au taarifa za kweli; bali inajumuisha pia haki ya kuhifadhi, kupokea na kutoa mawazo, maoni na taarifa ambazo si lazima zionekane kuwa za kweli”.

Kwa maana nyingine ni kwamba, ushindani katika soko la habari utafanya ubora na ukweli wa mawazo kujichuja badala ya kuchujwa na Serikali, kwani katika jamii yenye demokrasia kamili, si kazi ya Serikali kuchuja mawazo na maoni ya wananchi wake.

Ni uamuzi wa jopo la Majaji hao saba juu ya kifungu cha 50 (Tanzania, kifungu cha 50 na 55 cha Penal Code na 55 cha Sheria ya Magazeti) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya Uganda (PC) kwamba, kitendo chochote cha kubana uhuru wa mawazo, kufungia chombo cha habari, kukamata na kuwafikisha mahakamani watu kwa kutoa mawazo yao kwa uhuru kwa madai ya uchochezi, ni batili na ni kinyume cha Katiba na haki za binadamu zinazotambuliwa kimataifa.

Uamuzi huu unatufunza nini, na una maana gani kwa Tanzania kuhusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari?

Ni kwamba, Mahakama ya Rufaa ya Uganda (Supreme Court) na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania zina hadhi sawa katika nchi husika, ambapo hukumu zake (precedents) zina ushawishi (persuasiveness) mkubwa katika kufikia uamuzi wa kesi zinazofanana kwa Mahakama ya kila nchi.

Na kwa kuzingatia pia kwamba Uganda na Tanzania (pamoja na Kenya) zina mfumo mmoja wa Mahakama, mfumo mmoja wa Sheria (Common law system), na kwamba hivi karibuni zimeanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo wazo la kuunda Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki huenda likatekelezwa, hukumu ya kesi ya Onyango-Obo ni sauti ya “Masiya” ajaye kwa ukombozi wa uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza uliomo kifungoni.  Hukumu hii si ya kupuuza katika ujenzi wa demokrasia ya kweli nchini.

Makala hii imeandikwa kwa msaada wa makala ya Joseph Mihangwa

Advertisements

MYUKANO NDANI YA CCM DHAIFU WAZIDI KUIBOMOA KWA KUTUMIA VYOMBO VYA HABARI BADALA YA VIKAO.

 Vita vya msituni sasa vya piganwa waziwazi.

 Uitaji uchunguzi kupambanua tofauti zao, hoja ya kundi moja inapingwa hata kama imetolewa kwa nia njema

 Yadaiwa tofauti zao ndiyo sababu ya matatizo ya wananchi kushamiri siku hadi siku. 

Hali bado siyo shwari katika kambi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya baadhi ya wabunge na makada wake kukisulubu chama hicho na serikali yake kwa madai ya kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Vikao vya CCM vya CC na NEC vikiwa bado vinaendelea mjini Dodoma ndivyo vinavyo tarajiwa kutoa ahueni ya kuimarika au kudumaa kwa chama hicho ambacho katika siku za hivi karibuni kimekumbwa na balaa la kuondokewa na makada wake wanaohamia vyama vingine.

Wajumbe wa vikao hivyo wameweka wazi kuwa CCM kinapoteza muda mwingi kushughulikia minyukano ya makundi ilhali matatizo ya wananchi yakizidi kushamiri siku hadi siku.

Hata hivyo makada hao wanakiuka agizo la CCM linalo wakataza kutoa kauli za kuwashambulia viongozi na chama chao hadharani bali wafanye hivyo kwenye vikao husika.

Kwasasa ni vigumu kujuwa nani ni msemaji wa chama hicho kikongwe hapa nchini, au kutofautisha kauli ipi ni ya chama au ya mtu binafsi hivyo kupelekea mpasuko mkubwa juu ya kuwadhibiti baadhi ya viongozi wanaoonekana kutoa kauli zinazohatarisha uhai wa CCM.

Miongoni mwa kauli za hivi karibuni silizo leta sitofaham ni ile iliyotolewa Ijumaa Mei 11, 2012 na Waziri Mkuu Mstahafu Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kuwa chama chake, kina tatizo la uongozi na utendaji ndiyo maana wananchi wamepoteza imani nacho, lakini yeye ataendelea kuwa mwanachama wa CCM.

Katibu wa Itikadi na Unezi wa CCM, Nape Nauye, alisema yeye anamsubiri kiongozi huyo kwenye vikao vya chama ambako ndiko atapata fursa ya kuchambua kwa kina hicho kilichosemwa.

“Mimi nimesoma kwenye vyombo vya habari kuhusu Lowassa, siwezi kuzungumza jambo lolote kwa sasa, tuna vikao vyetu, huko ndiko uwanja wetu,” alisema.

Wakati Nape akionekana kukwepa kuzungumzia kauli ya Lowassa, taarifa nyingine zinadai kuwa baadhi ya wajumbe wa Kikao cha Kamati Kuu, (CC) kilichoketi Jumamosi Mei 12, 2012 usiku mkoani Dodoma walitaka hatua za kumziba mdomo kiongozi huyo zichukuliwe.

Katika hali ambayo inaonyesha kukosa Ustahimilifu na kuzidi kuchochea mpasuko, Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, alishindwa kusubiri vikao husika na kuzungumza na moja ya gazeti la kila siku akisema si sahihi kwa Lowassa kutoa kauli hiyo kwenye mikutano ya hadhara wakati anajua bayana taratibu za chama hicho.
Alisema Lowassa alipaswa kuzungumzia matatizo ya jimbo lake yakiwemo migogoro ya ardhi, wawekezaji na wananchi, wakulima na wafugaji, maji na kero nyingine mbalimbali na si kuishambulia CCM.

“Tunamshangaa Lowassa kukaa kwenye mikutano ya hadhara na kuanza kukiponda chama, amejidhalilisha mwenyewe, kwa sababu aliwahi kuwa kiongozi mkubwa ndani ya chama na serikalini, lakini ameshindwa kutatua kero mbalimbali zinazoikabili nchi na jimbo lake pia, leo anakaa na kujadili matatizo ya chama kiutendaji wakati bado ni mwanachama na kwamba ana mamlaka ya kukikosoa kwenye vikao halali,”alisema Mukama.

Aliongeza kuwa mpaka sasa jimbo lake linakabiliwa na kero mbalimbali hivyo alipaswa kuwaambia wapigakura wake, ni kwa kiasi gani amezishughulikia tangu aanze kuliongoza.

Alisema Lowassa mpaka sasa bado ni mwanachama wa CCM, na kwamba ni miongoni mwa viongozi wanaohudhuria vikao mbalimbali vya chama,  hivyo alipaswa kutumia vikao hivyo na si kupanda majukwaani,  kujisafisha mbele ya wananchi ili aonekane mtetezi wa rasilimali za  umma.

Alisema hatua hiyo ya Lowassa ni kukurupuka kwani kama moja ya viongozi wa chama hicho, ana wajibu na jukumu la kutatua migogoro iliyopo ndani ya chama na hata kuishauri Serikali.

“Yeye ni miongoni mwa watu wanaopaswa kutatua matatizo iwe ya kichama au kuishauri Serikali iliyopo madarakani ambayo ni ya chama chake, hawezi kukurupuka, anapaswa kuwa na hekima na kukaa na wenzake kwa ajili ya kujadili matatizo yaliyopo ili yaweze kutatuliwa, si kama alivyofanya,” alisisitiza Mukama.

Alisema mbali na hilo, alipaswa kuweka wazi matatizo ya uongozi aliyokuwa akiyazungumzia kuwa yapo katika ngazi ipi ya kata, wilaya, mkoa au taifa, badala ya kuishia kusema kuna matatizo ya kiutendaji na uongozi ndani ya chama.

Lowassa alikaririwa akisema CCM itakapoacha misingi yake ya awali ikiwemo kutetea wanyonge, hatakuwa mmoja wa wanachama wake.

“Pamoja na uzuri wake, muundo wa chama chetu ni mzuri sana, imani ya chama chetu ni nzuri sana ,misingi inayoongoza chama chetu ni mizuri sana , lakini tuna tatizo la utendaji  na uongozi ndani ya chama chetu” alisema Lowassa na kuongeza;

“…ama katika kufanya uamuzi ama uamuzi usio sahihi au kutochukua hatua kwa matatizo yanayowakabili wananchi kwa wakati muafaka”.

Lowassa alisema matatizo hayo ndiyo yanayowafanya watu wakichukie chama hicho na kukiona kuwa ni kero na kuanza kutafuta mbadala wake.

“Tukionekana hatujali shida za wananchi wetu, watatafuta mbadala, lakini kero hizi zishughulikiwe kwenye vikao,” alisema.

Hoja ya kumwadabisha Lowassa inadaiwa kuwagawa wajumbe wa CC na huvyo kupata upinzani kabla hata ya kikao kuanza, kwa madai kuwa kama chama kinataka kuchukua hatua hiyo isimuache Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye mara kwa mara amekuwa akitoa kauli za kuiweka pabaya serikali aliyomo.

Wajumbe wa CC walibainisha kuwa ukimya wa viongozi wa ngazi za juu katika kushughulikia mipasuko na makundi yanayokinzana ndani ya chama hicho ndiyo yanayokiumiza na kukifanya kikimbiwe na makada wengi.

Wajumbe wa CC walikuwa wakisisitiza kuzibwa mdomo kwa Lowassa, hasa kwakuwa kiongozi huyo ni miongoni mwa watuhumiwa wa ufisadi wanaotakiwa kuvuliwa gamba.

Walijenga hoja kuwa Lowassa amekuwa akiichonganisha CCM, serikali yake na wananchi hasa kwa kutumia kete ya uhaba wa ajira kwa vijana, ambao umetokana na kutovaliwa njuga kikamilifu na utawala.

Lowassa pia amekuwa akisisitiza kuwa chama na serikali vinashindwa kuchukua maamuzi magumu kwenye mambo ya msingi ndiyo maana nchi inasuasua kufikia maendeleo iliyoyakusudia.

Mara kadhaa viongozi wa serikali wakiwamo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, wamejitokeza kujibu kauli zilizotolewa na Lowassa.

Inadaiwa wajumbe wa CC walikuwa wakitaka maamuzi magumu yaanzie kwa Lowassa hata kama kiongozi huyo ataamua kuhamia vyama vya upinzani kama walivyofanya wafuasi wanaomuunga mkono hivi karibuni.

Kwa upande mwingine wakati hayao yakiendelea Katika mkutano wa hadhara ulihudhuriwa na idadi kubwa ya watu Jumamosi Mei 12, 2012 jimboni kwake Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), aliwashambulia baadhi ya viongozi wa chama na serikali ambao wameamua kutumia madaraka yao kwa masilahi binafsi, huku wananchi wakizama kwenye lindi la umaskini.

Alisema ni bahati mbaya sana ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baadhi ya wale waliopewa  dhamana wamewatelekeza wananchi, wanafuja mali za umma kwa manufaa yao binafsi na kusahau mambo ya msingi ambayo mtu mwenye akili timamu anapaswa kuyazingatia.

Mbunge huyo  ni miongoni mwa wabunge wachache wa CCM walioungana na wale wa  kambi ya  upinzani kuwashinikiza mawaziri wanane  waliotajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi  Mkuu wa Hesabu za Serikali  (CAG) na zile  za kamati za kudumu za Bunge waachie nyadhifa zao.

Filikunjombe ambaye hotuba yake ilikuwa ikikatizwa mara kwa mara na wananchi waliokuwa wakimshangilia, alisema kuwa yuko tayari kufa ili mradi anasimamia na kutetea wanyonge, akiamini kwamba akifa yeye atatokea mwingine kama yeye.

Mwanasiasa huyo kijana alimshambulia wazi wazi aliyekuwa waziri wa fedha, Mustafa Mkulo, kuwa alilazimika kumtaja hadharani bungeni kutokana na kuchangia kukwamishwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni kwake na hata katika majimbo mengine.

“Wakati nachangia nilikuwa nakumbuka jinsi ambavyo kuna miezi mingine serikali yetu haileti hata senti tano Ludewa, huku Waziri wa Fedha akitumia sh 1.3 trilioni kwa matumizi yake binafsi, bila idhini ya Bunge.

Matatizo yetu Ludewa yalinipa nguvu za kuikemea serikali yetu. Nikapiga moyo konde, nikasema, na nitasema ukweli,” alisema.

‘’Kabla ya kusaini waraka wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), kwa kutaka Bunge lipige kura kwa kutokuwa na imani na waziri mkuu,niliitwa na viongozi akiwemo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alinitaka nisitie saini lakini nikawakumbuka Wana Ludewa tabu wanazozipata, hasa katika kata zao, umaskini walionao, machozi yakaanza kunitoka, ndipo nikaona ngoja kwanza nisaini ndiyo nikamsikilize,” alisema Filikunjombe.

Chama Cha Mapinduzi kimekuwa kama Jogoo ambalo hudhani kila siku Jua huchomoza ili lisikilize linavyowika. Kwa mantiki hiyo kama CCM wanataka kujifunza, basi wajifunze kwamba siasa za makundi, mtandao na maslahi yasiyo ya kitaifa hayawezi kukiacha kikiwa kimesimama.

NCHEMBA AJIPA KAZI YA AFISA HABARI WA BOT NA KUMJIBU ZITTO KATIKA KILE KILICHODAIWA “BENKI KUU HAZINA YA TAIFA IMEKAUKA”.

Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nimesikitishwa na kushangazwa na taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari hivi leo na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Zuberi Kabwe.

Mimi nilikuwa ni Mchumi Daraja la Kwanza katika Benki Kuu ya Tanzania na nilikuwa nafanya kazi kwenye Kurugenzi ya Utafiti wa Uchumi na Sera. Hivyo, nafahamu jinsi Benki Kuu inavyofanya kazi.

Na nasikitika kwamba wanasiasa sasa, katika kujitafutia umaarufu, tunaingia kwenye kushambulia taasisi muhimu inayoendeshwa kwa weledi na uadilifu mkubwa.

Baada ya Mhe. Zitto Kabwe kukosa taarifa muhimu mtandaoni, ningetegemea Mbunge kama Zitto, ambaye Kamati yake inakagua mahesabu ya BOT, kuwasiliana na Benki na kuuliza kulikoni, badala ya kusambaza taarifa katika vyombo vya habari kulaani Benki Kuu na kusambaza tetesi kuhusu hali ya Hazina ya Taifa.

Lakini vilevile, ningetegemea kwamba, kama ameamua kusambaza taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, basi taarifa hiyo ingejumuisha yale aliyoyabaini baada ya kuzungumza na Benki Kuu.

Yeye kama kiongozi, kama anaamua kuwasiliana na umma kwa kusambaza taarifa kwa vyombo vya habari, basi walau aonyeshe umma jitihada nyingine alizofanya za kupata ripoti hizo zaidi ya kwenda tu mtandaoni, kwasababu sote tunajua kwamba hata namba ya Gavana wa Benki Kuu anayo.

Pili, kutokuwepo kwa ripoti mtandaoni hakumaanishi kwamba ripoti hizo aidha zimefichwa au hazipo.

Ni muhimu sana viongozi wakawa wa kweli na wakaacha mtindo wa kungoja siku ambayo haina habari (Jumapili) na kuamua kutengeneza habari kwa ajili ya vichwa vya habari vya Jumatatu.

Naomba kutoa ufafanuzi wa jinsi ukweli ulivyo, kwasababu hata sisi katika Chama tumekuwa tunafuatilia taarifa hizi za Uchumi kutoka Benki Kuu.

Kwanza, katika taarifa yake Zitto anaomba taarifa za mwezi Januari, Februari, Machi na Aprili zitolewe.

Hili limenishangaza kwasababu nilitegemea kwamba mtu kama Zitto, ambaye ni mchumi na ambaye kamati yake hupitia hesabu za BOT, angefahamu kwamba ripoti ya mwezi husika inaanza kuandaliwa tarehe 15 ya mwezi unaofuatia – kwa maana kwamba report ya mwezi Machi ilianza kuandaliwa tarehe 15 Aprili, report ya mwezi Aprili, itaanza kuandaliwa tarehe 15 Mei, na report ya mwezi Mei itaanza kuandaliwa tarehe 15 Juni.

Huu ni utaratibu wa kimataifa, ambapo inategemewa kwamba katika kipindi hicho cha wiki mbili baada ya mwezi kuisha, takwimu muhimu kutoka sehemu mbalimbali zitakuwa zimekusanywa na kuhakikiwa.

Pili, ningetegemea pia Mhe. Zitto awe anafahamu kwamba kabla ya taarifa hizi za Benki Kuu kuchapishwa ni lazima zipitishwe na Kamati ya Sera za Fedha ya Bodi ya Benki Kuu (Monetary Policy Committee of the Board).

Huko nyuma, Kamati hii ilikuwa inakutana kila mwezi, lakini kutokana na maagizo ya Kamati ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mhe. Zitto kwamba vikao katika Benki Kuu vipunguzwe.

Hivyo, ikaamuliwa kwamba Kamati hii inayopitisha taarifa hizi muhimu iwe inakaa mara moja kila baada ya miezi miwili. Matokeo yake ni kuchelewa kupitia na kupitisha taarifa hizi muhimu.

Mara ya mwisho kikao kilikaa mwezi Machi kupitia taarifa ya mwezi Januari, ambayo imekwishasambazwa.

Tatu, si kweli kwamba Hazina ya Fedha za Kigeni Taifa imekauka.

Ambacho angeweza kufanya Zitto na ana mamlaka hayo na uwezo anao ni kumpigia simu Gavana au wasaidizi wake na kuwauliza ni kiasi gani cha Hazina kilichopo.

Mimi ndicho nilichofanya, na taarifa rasmi, ni kwamba hazina iliyopo ni kiasi cha dola za kimarekani bilioni 3.6, ambazo zinawezesha kuagiza mahitaji yetu yote ya bidhaa kwa kipindi cha miezi minne, na wala sio mwezi mmoja kama alivyodai Mhe ZITTO.

Na akiba ya watanzania iliyoko kwenye benki zetu nchini ni takribani dola za kimarekani 1.8 bilioni na taarifa hii pia IMF wanayo, (taarifa hii ni kwa kipindi kinachoishia tarehe 11 May 2012).

Binafsi nimesikitika sana kwamba kiongozi anaweza kuwa irresponsible kiasi hiki cha kusambaza taarifa za uvumi wakati anao uwezo wa kupata taarifa sahihi za maandishi na kuujulisha umma ukweli.

Mwisho, napenda kumsihi Mbunge mwenzangu kwamba ni muhimu kuwa makini na kutokurupuka katika mambo muhimu kama haya na ni muhimu kufanya utafiti kidogo kabla ya kuwasiliana na umma kwani sisi viongozi tunasikilizwa na kuaminiwa na watu na tunategemewa kuwa sahihi na wakweli wakati wote.

Imetolewa na:

Mwigulu Lameck Nchemba (MB)

Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa

Dodoma 13 Mei 2012

MWEZI ULIOBAKI KABLA YA BAJETI YA MWAKA 2012/13 UNATOSHA KULINUSURU BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI?

KAMA mawaziri wa baraza hili jipya wanafahamu sababu za kupewa nyadhifa hizo teule na kuwa miongoni mwa viongozi wetu wa kitaifa hiyo itakuwa nafuu kwao.

Kama wanafahamu kuwa waliowatangulia walituhumiwa kwa kutowajibika ipasavyo ikiwemo kuhusishwa na ufujaji wa fedha za umma na kutumia vibaya madaraka, hiyo ni bahati nyingine kubwa kwao.

Ikumbukwe, Viti ambavyo wameanza kuvikalia baada ya kula kiapo, ni vya moto; havikaliki havishikiki kirahisi.

Tunazungumzia lundo la changamoto zilizo mbele ya mawaziri wapya. Kwamba yale yaliyo changia kutokomeza wale waliowatangulia, yangali mabichi.

Je, wamejifunza? Wamejiandaa kwenda mwendo mzuri wa kujenga matumaini au wanafurahia kukalia viti kwa sababu watachuma?

Misimamo yao ndiyo itawadhihirisha waliyo ya dhamiria wanaposhika uongozi wa wizara.

Kama kuchuma watachuma maana watakuta machungu ya uongozi mbaya; 

vitendo vya ufisadi, rushwa, upendeleo na uzembe ndivyo vinavyosonga mbele badala ya tija.

Matatizo yaliyobainishwa kuwagusa mawaziri waliotemwa yamepunguza uwezo wa serikali kukusanya mapato na hivyo kusababisha ishindwe kuhudumia wananchi.

Yamezidisha malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa barabara, ukosefu wa maji safi na salama, umeme, walimu, vitabu na mikopo kwa wanaoingia vyuoni, pembejeo za kilimo na ununuzi wa mazao ya kilimo.

Wizara ya Fedha na Uchumi, kwa mfano, imekuwa dhaifu katika kutekeleza jukumu lake la kulinda raslimali za nchi kama vile majengo, viwanja na hisa katika mashirika na kampuni zilizobinafsishwa.

Watendaji wa wizara hii wamekuwa legevu katika kusimamia uchumi wa nchi kiasi cha kusababisha kuongezeka kwa deni la taifa.

Mbaya zaidi, viongozi waandamizi serikalini wamekataa kubadili mwenendo mbaya wa matumizi ya fedha za serikali.

Eneo hili limeleta madhara makubwa. Mara kadhaa serikali imelazimika kukopa benki za biashara ili kukidhi mahitaji yake ya kuendesha shughuli zake.

Mtindo huu unajenga taswira mbaya kwa wananchi na hata kwa wafadhili au washirika wa maendeleo; ambao wamekuwa wakiishutumu serikali kwa matatizo hayahaya tunayoyaelezea.

Mwezi mmoja uliobaki wa maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/13 hautawasaidia. Baasi, wajiandae kukabili vishindo vya wabunge walioamua kutumikia umma badala ya nafsi zao kwanza utakapoanza mkutano wa bunge la bajeti katikati ya mwezi ujao.

ZITTO KABWE; BENKI KUU, HAZINA YA TAIFA IMEKAUKA?

Mweshimiwa Zito Zuberi Kabwe

Benki Kuu ya Taifa lolote ndio taasisi pekee yenye takwimu zote nyeti na za uhakika zinazohusu uchumi wa Taifa hilo.

Katika tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania eneo la Machapisho kuna Taarifa nyeti sana mbili, Mapitio ya Uchumi ya Mwezi (Monthly Economic Review) inayotoka kila Mwezi katika Mwaka na Mapitio ya Uchumi ya Robo Mwaka (Quarterly Economic Bulletin).

Taarifa hizi hutoa taarifa kuhusu masuala yote muhimu yanayohusu Uchumi wa Jamhuri ya Muungano na Uchumi wa Zanzibar ikiwemo taarifa za Mfumuko wa Bei, Mapato na Matumizi ya Serikali, Mwenendo wa Biashara ya Kimataifa na Deni la Taifa.

Ukienda kwenye tovuti ya Benki Kuu Jumapili Mei 13, 2012 utakuta Taarifa hizi.

Lakini Taarifa hizi zimeishia Desemba mwaka 2011 zikitaarifu masuala ya Uchumi ya Mwezi Novemba na robo ya mwaka inayoishia Desemba.

Ukitaka kujua Bajeti ya Serikali na mwenendo wake hutapata taarifa za sasa bali za Mwezi Novemba mwaka 2011, miezi sita nyuma.

Huu sio utendaji uliotukuka. Hii ni kuficha taarifa kwa wananchi. Taarifa zinafichwa ili iwe nini? Nani anafaidika na kufichwa kwa taarifa muhimu kama hizi?

Kuna tetesi kwamba Hazina ya Taifa (Hifadhi ya Fedha za kigeni – foreign reserve) inakauka, kwamba tuna hifadhi ya kuagiza bidhaa nje kwa mwezi mmoja tu.

Niliposikia tetesi hizi sikuamini. Nilipoenda katika tovuti ya Benki Kuu ili kuweza kuwa na habari rasmi (authoritative) nimekuta takwimu za Novemba 2011.

Takwimu ya Mfumuko wa Bei iliyoko kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania ni ya mwezi Novemba mwaka 2011!

Ukitaka kujua mwenendo wa Bajeti ya Serikali kama makusanyo ya Kodi na Matumizi utapata Taarifa ya Mwezi Novemba mwaka 2011.

Ukitaka kujua manunuzi ya Mafuta (fuel imports) kwa miezi 3 ya mwanzo ya mwaka 2012 ili kuweza kuona namna Umeme wa dharura umeathiri urari wetu wa Biashara ya Nje hupati taarifa hiyo katika tovuti ya Benki Kuu.

Taarifa zinafichwa.

Ndio. Zinafichwa tena makusudi maana taarifa hizi zipo Benki Kuu.

Huu ni uzembe maana Nchi inawalipa wafanyakazi wa Benki Kuu mishahara minono ili wafanye kazi hizi.

Benki Kuu pia imetoa zabuni kwa Kampuni Binafsi kuchapisha Taarifa hizi. Kama Taarifa hazitoki kwa wakati ni wizi. Wizi ambao haupaswi kufumbiwa macho.


Benki Kuu ya Tanzania ipo miezi Sita nyuma. Aibu kubwa sana.

Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano akihakikishia mataifa duniani kuhusu uwazi Serikalini (#OGP), Taasisi kubwa kama Benki Kuu inaficha Taarifa ambazo ni nyeti kwa wananchi na muhimu kwa wafuatiliaji wa sera za Serikali.

Rais wa nchi anaongea Buluu, Gavana wa Benki Kuu anasimamia Kijani!

Inaudhi na kukera sana kwenda kwenye tovuti ya Benki Kuu na kukuta taarifa za miezi Sita iliyopita.

Benki Kuu hamstahili kuitwa Benki Kuu, labda benki kuu kuu.

Rekebisheni jambo hili haraka sana maana kuficha taarifa kwa Umma ni ufisadi.

Haki ya kupata taarifa ni haki ya msingi katika Katiba yetu. 


Hatutaki kushtukizwa na kuambiwa Hazina ya Taifa imekauka.

Prof. Ndulu hakikisha Taarifa ya Mapitio ya Uchumi wa kila Mwezi imewekwa kwenye tovuti kwa muda mwafaka.

Ifikapo mwisho wa Wiki inayoanzia Jumatatu Mei 14, tovuti ya Benki Kuu iwe na Taarifa za miezi yote (Desemba, Januari, Februari, Machi na Aprili).

Taarifa hizi ni muhimu ili nasi tutekeleze majukumu yetu ya Kikatiba kama Wabunge, Mawaziri vivuli na Wananchi wa Tanzania.


Imetolewa na:

Zitto Zuberi Kabwe (MB)

Waziri wa fedha Kivuri, Mwenyekiti Kamati ya bunge ya Mashirika ya Umma

13 Mei 2012