Joshua Nassari (MB)
  • Sina hakika kama bila sheria hii, Joshua Nassari angekana kauli yake na kulazimika kufanya kile kinacho tafsiriwa kujutia hotuba yake.
  • Makaramba, Sheria hii ni mbaya kwa ustawi wa waandishi wa habari pamoja na vyombo vyao.
  • Viongozi wakielezwa makosa hukubali na hujisahihisha, lakini watawala hununa ndiyo maana mara huita wanahabari wetu ‘uchwara’ mara ‘makanjanja’ na mara nyingine hukanusha hata “kauli” zao wenyewe.
  • “Tunapenda kuweka wazi kwamba, uvumilivu kwa mwenendo na hotuba hasidi katika jamii ni moja ya gharama inayopaswa kulipwa na jamii huru na iliyo wazi”, hiyo ndiyo gharama ya demokrasia.
Kwa tahadhali kubwa nimeamua kulizungumzia hili huku nikijuwa nitashambuliwa kwa nguvu zote na watetezi wa sheria hii kandamizi, uenda hata kuitwa kuhojiwa na vyombo vya sheria kwa kosa la kusema ninacho fikilia.

Maandishi yoyote au kauli, yawe kupitia vitabu vya fasihi au kwenye magazeti, Redio na TV au tovuti yanayotoa elimu ya uraia kwa umma au yanayo amsha akili na kuhamasisha watu wajitambue huchukiwa na watawala.

Wakosoaji wangu wakubwa watakuwa ni vyombo vya dola na wale walio madarakani, na kwa bahati mbaya kalamu yangu haiko kwa ajili ya kuwapendeza watu fulani fulani hivyo niko radhi nitengeneze uadui kwa kusema ukweli ili kuinusuru nchi hii na unafiki usiyo vumilika kama ilivyo kuwa kwenye simulizi za Shaban Robert na nchi ya kusadikika.

Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa aliwasakama, tena baadhi ya waandishi nguli, na kuwaita “waandishi uchwara”.

Lakini katika harakati za kuelekea ikulu, Jakaya Kikwete aliwaweka kwenye mtandao wake “waandishi uchwara wa Mkapa” wakaandika makala zilizoua hadhi ya baadhi ya wagombea kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama pinzani, na aliposhinda akawapa ulajiri ikulu, ofisi ya waziri mkuu na Wakuu wa Wilaya.

Rais Kikwete, amebadili msamiati, hawaiti waandishi uchwara ila makanjanja. Wakati Mkapa alikuwa anaruka kwa ndege hadi Ulaya kuteta na waandishi aliodai kuwa makini, Kikwete anabagua waandishi na vyombo vya habari anavyoona ni “kanjanja”.

Lengo si kumyooshea kidole mtu mmoja mmoja, au wakosoaji wangu watakavyo iweka kuwa najaribu kumsafisha Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari.

Hebu tujikumbushe Mwaka 1996 ulipofanyika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Temeke, Rais Benjamin Mkapa aliwaambia wakazi wa Temeke kwamba wasipompatia Cisco Mtiro wa CCM nafasi ya ubunge hatampa ushirikiano mshindi yeyote nje ya huyo Cisco. 

Kwa kauli hiyo Mkapa alitaka wananchi wasimchague Augustine Mrema aliyekuwa wa NCCR-Mageuzi.

Magazeti yakaandika ujumbe huo wa Mkapa na Tv za wakati huo zikamwonyesha akitoa ujumbe huo. 

Lakini siku iliyofuata, Mkapa aling’aka eti hakusema hivyo na akashutumu vyombo vya habari.

Hayo hayakuishia mwaka huo yameendelea mpaka leo hii, Tunamshutumu Joshua Nassari kwa kauli yake, je kauli kama hizi za Mkapa alizo kuwa anapambana nazo zikizungumzwa wazi wazi wakati wa Kampeni za Ubunge Arumeru Mashariki hakuna hata mmoja anaye zisema kuwa zilikuwa zinahatarisha ustawi wetu kama Taifa. 

Maandishi huhifadhi elimu, na mtu anayejua maandishi atakuwa amepata elimu, na mtu mwenye elimu atakuwa amepata silaha ya kupambana na maisha, kujitambua na kudai haki.

Hii ndiyo siri kwa nini watawala hawataki wananchi wasome maandishi yanayo zindua akili zao. Hawapendi kuona wananchi wanawafuatilia kwa karibu; hawataki tawala zao kuchunguzwa wala kudodoshwa.

Waandishi au watu wanaoweka wazi makosa ya watawala na serikali zao, hushutumiwa wao na vyombo vyao,  kuwa vinafanya uchochezi. Hutangazwa kuwa wanahatarisha amani ya nchi.

“Sheria hii ya uchochezi ilitungwa wakati wa ukoloni kwa ajili ya kuwalinda watawala wa wakati huo dhidi ya mtu yoyote au kundi la watu aliyetaka kutetea haki yaje ya msingi, lakini bahati mbaya mpaka sasa bado ipo na ni pana hivyo ikitumiwa vibaya inaweza kuwanasa wengi wakiwemo waandishi, wanaharakati hata wanasiasa wa upinzani” alisema Jaji wa Mahakma Kuu ya Tanzania Robert Makaramba

Ningependa tuungane pamoja katika utafiti tuliofanya kutoka katika matukio anuai ya kuaminika ndani ya nchi yetu na kujadiri hili bila unafiki wowote.

Wakati wa enzi za Wafalme, adhabu kali ilitolewa kwa wale waliojaribu kuhoji vitendo au mamlaka ya Mfalme. Leo hii ni hivyo hivyo kwa wale wanao hoji umoja wa kitaifa au muungano wetu. 

Ni jambo la kawaida kusikia vyombo vya habari kufungiwa, Wahariri na “wanaharakati” kushitakiwa kwa makosa ya jinai kwa sababu ya kuchapisha au kutamka maneno au maoni ya kawaida, lakini yanaweza kugeuzwa kwa ufundi wa kisiasa kuwa “uchochezi”, kwa sababu tu ya kutowafurahisha baadhi ya wenye madaraka.

Udhibiti huu wa habari na mawazo ya mtu binafsi mara nyingi unakwenda kinyume cha ibara ya 18 ya Katiba yetu inayosema:  “Kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari, anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake”.

Kinachokera ni kwamba, tumetoa uhuru (demokrasia) kubwa kupindukia katika sekta ya uchumi na biashara (ubinafsishaji, uwekezaji usiojali na uporaji rasilimali bila kudhibitiwa), lakini tumebana demokrasia ya mawazo na demokrasia ya kisiasa (Katiba isiyokidhi matakwa ya wengi, sheria 40 kandamizi, sheria mbovu ya uchaguzi), na kujenga taifa la kitabaka kati ya walio nacho kiuchumi na kisiasa na tabaka la wasio na chochote kiuchumi na kisiasa.

Uhuru wa kujieleza maana yake ni biashara ya mawazo, yenye soko kamili kama ilivyo kwa bidhaa nyingine katika soko.

Kwa uhuru huu, jamii hunufaika kwa njia ya kubadilishana mawazo kwani hakuna mtu mmoja aliye na jibu kamili juu ya mwelekeo sahihi na kwa matatizo yanayoweza kuikabili jamii.

Kwa sababu hii, si jukumu la Serikali wala la mtu mmoja kuamua ni mawazo yapi au habari ipi ni ya kweli na ipi ni ya uongo; ni soko pekee la mawazo linaloweza kuamua yote hayo. 

Kwa hiyo, ili jamii iweze kunufaika na mawazo pamoja na vipaji vya watu wake, haina budi kuruhusu ushindani wa kimawazo miongoni mwa watu wake. Kutofanya hivyo ni kuigeuza jamii kuwa ya mataahira.

Soko ndilo litakalokuwa muamuzi ambapo mawazo hafifu na dhaifu yatashindwa uwanjani kwa nguvu na ubora wa mawazo sahihi na ya kweli, wala si kwa shuruti au nguvu za Serikali.

Jamii lazima ifike mahali iruhusu mtu mmoja kutangaza kwamba “mfalme yuko uchi”, hata kama msemaji wa ukweli huo ataonekana “mwongo” kwa kuwa kile kinachoitwa uongo leo kinaweza kugeuka kuwa ukweli kesho, kama atapewa nafasi ya kusikilizwa. 

Tutazame kwa ufupi tu historia ya dhana ya uhuru wa kujieleza katika mazingira ya nchi zinazoongoza kwa demokrasia, tuone kama uhuru wa kujieleza kama sehemu ya demokrasia, unafanya kazi ipasavyo hapa kwetu.

Kwa mfano, mnamo karne ya tisa, Mfalme Alfred wa Uingereza aliagiza kuwa kila aliyejaribu kuihoji Serikali akatwe ulimi kwa kuwa ulimi ndio uliokuwa nyenzo pekee ya mawasiliano na njia ya kujieleza.

Hivi leo ulimi huo ni vyombo vya habari vinavyoweza “kukatwa” ulimi kwa njia ya kufungiwa au kushitakiwa kwa makosa ya “uchochezi”.

Ingawa mwaka 1620, uhuru wa kujieleza uliungwa mkono mno kutoka kwa Mfalme James wa Kwanza, lakini hata hivyo, Mfalme huyo naye hakuweza kutoa uhuru kamili alipoonya kwamba “masuala ya Serikali si mambo ya kuzungumzia mitaani; mtu hapashwi kusema au kumkosoa mtawala na utawala wake”.

Kuibuka kwa uchapishaji wa habari kulitoa tishio jipya kwa watawala kwa vile maandishi ni kitu cha kudumu na uwezekano wake wa kuwafikia watu wengi zaidi ni mkubwa.

Ili kukabiliana na hali hiyo, dola ilitoa amri magazeti yote yaandikishwe na kudhibitiwa, na yale yasiyofanya hivyo yafungiwe au kufutwa kabisa.

Ilikuwa mwaka 1689, Malkia Mary (na mumewe William) alipochukua madaraka kwamba Uingereza ilianzisha sheria ya haki za binadamu (Bill of Rights) na kulipa Bunge ukuu (Parliamentary Sovereignty) na uhuru wa kujieleza.

Kwa hatua hiyo, haki za raia zilitambuliwa, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza na uhuru wa kutoa mawazo moja kwa moja au kupitia vyombo vya habari.

Huko Marekani uhasama kati ya Serikali na vyombo vya habari, ulisababisha uhuru wa kujieleza kutoweka kufuatia kesi ya uchochezi iliyomhusu mchapishaji John Peter Zenger, mwaka 1735, pale Mahakama ilipotoa uhuru na haki kwa raia wa kujieleza au kupinga na hata kuikosoa dola ilipobidi.

Kuanzia hapo, Sheria ya Uchochezi ilibakia kwa jina tu hadi mwaka 1801 ilipofutwa na Rais Thomas Jefferson alipoingia madarakani.

Uingereza kwa upande wake ilifuta makosa yote yanayohusu “habari za uongo” (False News Offences) mwaka 1887. Kinyume chake leo, miaka 50 ya uhuru, sisi tunaelekea kule wenzetu walikotoka miaka 110 iliyopita huku tunajitapa kujenga demokrasia kwa mfumo wa nchi hizo.

Uhuru wa kujieleza kama ilivyo demokrasia, lazima uzingatie vigezo na viwango vya kimataifa.

Hivyo, kama kweli tumekubali kufuata mifumo ya demokrasia, uhuru, na haki za binadamu ya nchi za Magharibi – kama vile demokrasia na utawala bora, soko, siasa na uchumi huria; iweje leo tuendeleze udhibiti kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari ambao mataifa hayo yalipiga marufuku karne mbili zilizopita, kama njia ya kuimarisha demokrasia?

Tunahofu nini? Au tunaogopa kuambiwa “mfalme yuko uchi” inapokuwa kweli kwamba Mfalme huyo hana nguo?

Jamii makini haiwezi kukubali kulazimishwa kushangilia au kusifia Mfalme asiye na nguo eti kwa sababu “suti” aliyovaa inaonekana kwa wasio na dhambi tu, wakati ukweli yuko uchi; na kwa vitisho eti kwamba “wasioiona” suti hiyo ni wadhambi, na hivyo watobolewe macho yote kama adhabu kwa “dhambi” zao. 

Hata iweje, wapo watoto “Kina Joshoa Nassari” watakaosema ukweli kwamba “Mfalme yu uchi”, kwa sababu watoto hawajui kujipendekeza, wala kwa kusema ukweli huo hawana cha kunufaika wala kupoteza; wanachojali ni ukweli mtupu.

Uhuru wa kujieleza nchini umedhibitiwa kwa sheria mbili ambapo unapofikia kiwango fulani huitwa “uchochezi” (sedition). Kwa kuanzia, “uchochezi” ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code) kifungu cha 50 na 55; pili “uchochezi” ni kosa chini ya kifungu 55 cha Sheria ya Magazeti, Namba 3 ya mwaka 1976.

Wakati sheria hizi mbili zinadhibiti uhuru wa kujieleza, kinyume cha sheria hizo, Katiba ya nchi inatoa uhuru huo bila kikomo, chini ya Ibara ya 18, kama nilivyoinukuu mwanzo.

Kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, je, si kweli kwamba yale yanayoitwa “makosa ya uchochezi” si uchochezi bali ndio uhuru wenyewe wa kujieleza na wa kutoa maoni yoyote? Je, huko si kuingilia uhuru wa mawasiliano wa mtu?

Ni nani mwenye haki ya kuamua uhalali wa maoni (yoyote) na aina ya uhuru wa mawazo ya mtu katika kutekeleza haki hiyo ya kikatiba?

Je, ni halali kwa mtu kushitakiwa chini ya sheria za makosa ya jinai? Ni kiwango gani cha uhuru kinachovumilika ili usiitwe “uchochezi”?

Maswali haya yananifanya nirejee kesi ya miaka ya karibuni nchini Uganda, ya Charles Onyango-Obo na mwenzake dhidi ya Serikali.

Oktoba 24, 1997 Charles Onyango-Obo, Mhariri wa gazeti la “The Monitor”, na mwenzake, Andrew Mujuni Mwenda, Mwandishi Mwandamizi, walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa kosa la kuchapisha habari za “uchochezi” zenye kichwa cha habari:  “Kabila aliilipa Uganda kwa dhahabu”, na kudai kuwa malipo hayo yalifanywa kuishukuru Uganda kwa kumsaidia (Kabila) kwenye vita nchini Zaire vya kumng’oa madarakani dikteta Mobutu Sese Seko wa nchi hiyo. Mahakama iliwaachia huru Obo na Mujuni kwa kuwaona hawakuwa na hatia.

Baada ya hapo, waandishi hao waandamizi walifungua kesi Mahakama ya Katiba kuiomba itoe ufafanuzi, kama Serikali ilikuwa na uwezo na haki ya kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari chini ya Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code) kwa kudai kulinda “maslahi ya umma”. 

Mahakama ya Katiba ilisema; “Serikali ilikuwa na haki na uwezo huo” na kutupilia mbali maombi yao.

Obo na Mujuni hawakuridhika; walikata rufaa Mahakama ya Rufaa (Supreme Court) dhidi ya uamuzi huo wa Mahakama ya Katiba.

Tunapotoa mfano huu, ikumbukwe kwamba Ibara ya 29 (1) ya Katiba ya Uganda ya 1995, inafanana na Ibara ya 18 ya Katiba yetu ya 1977 inayotumika hadi sasa.

Vivyo hivyo, kosa la “uchochezi” lililopo chini ya kifungu cha 50 cha Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code Act) ya Uganda ndilo hilo hilo lililopo chini ya vifungu namba 50 na 55 vya Sheria ya Makosa ya Jinai (Penal Code), na kifungu 55 cha Sheria ya Magazeti ya Tanzania, Namba 3 ya 1976.

Suala katika kesi hii lilikuwa kuhusu kama kifungu cha 50 cha Sheria ya Makosa ya Jinai hakipingani na Ibara ya 29 ya Katiba ya nchi hiyo inayotoa uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari bila ya kuingiliwa na mtu au chombo chochote.

Katika hukumu yake, Mahakama hiyo ya Rufaa ilibaini kuwa, kifungu cha 50 (kwa Tanzania, ni kifungu cha 50 na 55) cha Sheria ya Makosa ya Jinai kimedumu kabla na baada ya Uganda kuridhia Sheria ya Haki za Binadamu (Bill of Rights), kama ilivyo pia kwa Tanzania iliyoridhia haki hizo kwa Sheria ya 1984 na kuanza kutumika mwaka 1987.

Mahakama ilisema, kifungu hicho cha Sheria ya Makosa ya Jinai ni moja ya sheria za kikoloni zenye chimbuko lake la miaka ya 1200 nchini Uingereza.

Mahakama ilifafanua kuwa, “maslahi ya umma” yanakubalika na kulindwa na sheria yenye misingi ya uhuru na demokrasia, isiyoruhusu unyanyasaji wa kisiasa, kuweka watu kizuizini na udhalilishaji wa kibinadamu.

Mahakama ilibaini kuwa Uganda, kama moja ya jamii za kidemokrasia, inapaswa kuzingatia misingi ya demokrasia kwa viwango vya kimataifa; na kwamba chini ya viwango hivyo, si halali kuugeuza uchapishaji wa habari za uongo kuwa kosa la jinai, wakati Katiba ya nchi na zile za kimataifa kuhusu haki za binadamu (Bill of Rights) zinapingana na dhana hiyo.

Wakifafanua matakwa ya Ibara ya 29 (Tanzania ni ibara ya 18) ya Katiba, Majaji wa Mahakama hiyo walisema, Katiba inatoa na kulinda uhuru wa hotuba, uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari:

“Tunapenda kuweka wazi kwamba, uvumilivu kwa mwenendo na hotuba hasidi katika jamii ni moja ya gharama inayopaswa kulipwa na jamii huru na iliyo wazi”, Mahakama ilisema na kuongeza kuwa, hiyo ndiyo gharama ya demokrasia.

Ni aina gani ya mawazo yanayoweza kuvumilika? 

Majaji wa Mahakama hiyo walichukua ibara ya 9 ya Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamu (The African Charter on Human and Peoples’ Rights) kama kielelezo na ambayo inafanana na ibara ya 29 ya Katiba ya Uganda (Tanzania ibara 18 (2), kwamba:

“Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali duniani kote” na kwamba, “kila mtu ana haki ya kutoa na kusambaza au kueneza mawazo yake”.

Walisema, “ni kutokana na ukweli huu kwamba, haki ya uhuru wa kujieleza haijumuishi haki pekee ya kuhifadhi, kupokea na kutoa aina zote za mawazo kama vile maoni sahihi, mawazo mazuri au taarifa za kweli; bali inajumuisha pia haki ya kuhifadhi, kupokea na kutoa mawazo, maoni na taarifa ambazo si lazima zionekane kuwa za kweli”.

Kwa maana nyingine ni kwamba, ushindani katika soko la habari utafanya ubora na ukweli wa mawazo kujichuja badala ya kuchujwa na Serikali, kwani katika jamii yenye demokrasia kamili, si kazi ya Serikali kuchuja mawazo na maoni ya wananchi wake.

Ni uamuzi wa jopo la Majaji hao saba juu ya kifungu cha 50 (Tanzania, kifungu cha 50 na 55 cha Penal Code na 55 cha Sheria ya Magazeti) cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya Uganda (PC) kwamba, kitendo chochote cha kubana uhuru wa mawazo, kufungia chombo cha habari, kukamata na kuwafikisha mahakamani watu kwa kutoa mawazo yao kwa uhuru kwa madai ya uchochezi, ni batili na ni kinyume cha Katiba na haki za binadamu zinazotambuliwa kimataifa.

Uamuzi huu unatufunza nini, na una maana gani kwa Tanzania kuhusu uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari?

Ni kwamba, Mahakama ya Rufaa ya Uganda (Supreme Court) na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania zina hadhi sawa katika nchi husika, ambapo hukumu zake (precedents) zina ushawishi (persuasiveness) mkubwa katika kufikia uamuzi wa kesi zinazofanana kwa Mahakama ya kila nchi.

Na kwa kuzingatia pia kwamba Uganda na Tanzania (pamoja na Kenya) zina mfumo mmoja wa Mahakama, mfumo mmoja wa Sheria (Common law system), na kwamba hivi karibuni zimeanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo wazo la kuunda Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki huenda likatekelezwa, hukumu ya kesi ya Onyango-Obo ni sauti ya “Masiya” ajaye kwa ukombozi wa uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza uliomo kifungoni.  Hukumu hii si ya kupuuza katika ujenzi wa demokrasia ya kweli nchini.

Makala hii imeandikwa kwa msaada wa makala ya Joseph Mihangwa

Advertisements