MWEZI ULIOBAKI KABLA YA BAJETI YA MWAKA 2012/13 UNATOSHA KULINUSURU BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI?

KAMA mawaziri wa baraza hili jipya wanafahamu sababu za kupewa nyadhifa hizo teule na kuwa miongoni mwa viongozi wetu wa kitaifa hiyo itakuwa nafuu kwao.

Kama wanafahamu kuwa waliowatangulia walituhumiwa kwa kutowajibika ipasavyo ikiwemo kuhusishwa na ufujaji wa fedha za umma na kutumia vibaya madaraka, hiyo ni bahati nyingine kubwa kwao.

Ikumbukwe, Viti ambavyo wameanza kuvikalia baada ya kula kiapo, ni vya moto; havikaliki havishikiki kirahisi.

Tunazungumzia lundo la changamoto zilizo mbele ya mawaziri wapya. Kwamba yale yaliyo changia kutokomeza wale waliowatangulia, yangali mabichi.

Je, wamejifunza? Wamejiandaa kwenda mwendo mzuri wa kujenga matumaini au wanafurahia kukalia viti kwa sababu watachuma?

Misimamo yao ndiyo itawadhihirisha waliyo ya dhamiria wanaposhika uongozi wa wizara.

Kama kuchuma watachuma maana watakuta machungu ya uongozi mbaya; 

vitendo vya ufisadi, rushwa, upendeleo na uzembe ndivyo vinavyosonga mbele badala ya tija.

Matatizo yaliyobainishwa kuwagusa mawaziri waliotemwa yamepunguza uwezo wa serikali kukusanya mapato na hivyo kusababisha ishindwe kuhudumia wananchi.

Yamezidisha malalamiko ya wananchi kuhusu ubovu wa barabara, ukosefu wa maji safi na salama, umeme, walimu, vitabu na mikopo kwa wanaoingia vyuoni, pembejeo za kilimo na ununuzi wa mazao ya kilimo.

Wizara ya Fedha na Uchumi, kwa mfano, imekuwa dhaifu katika kutekeleza jukumu lake la kulinda raslimali za nchi kama vile majengo, viwanja na hisa katika mashirika na kampuni zilizobinafsishwa.

Watendaji wa wizara hii wamekuwa legevu katika kusimamia uchumi wa nchi kiasi cha kusababisha kuongezeka kwa deni la taifa.

Mbaya zaidi, viongozi waandamizi serikalini wamekataa kubadili mwenendo mbaya wa matumizi ya fedha za serikali.

Eneo hili limeleta madhara makubwa. Mara kadhaa serikali imelazimika kukopa benki za biashara ili kukidhi mahitaji yake ya kuendesha shughuli zake.

Mtindo huu unajenga taswira mbaya kwa wananchi na hata kwa wafadhili au washirika wa maendeleo; ambao wamekuwa wakiishutumu serikali kwa matatizo hayahaya tunayoyaelezea.

Mwezi mmoja uliobaki wa maandalizi ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2012/13 hautawasaidia. Baasi, wajiandae kukabili vishindo vya wabunge walioamua kutumikia umma badala ya nafsi zao kwanza utakapoanza mkutano wa bunge la bajeti katikati ya mwezi ujao.
Advertisements

3 thoughts on “MWEZI ULIOBAKI KABLA YA BAJETI YA MWAKA 2012/13 UNATOSHA KULINUSURU BARAZA JIPYA LA MAWAZIRI?

  1. Mawaziri wapya wasipo jingalia bujeti ijayo zitakwamishwa. Wabunge wa safari hii wanajuwa wanacho fanya. kwamaneno machache tutegeme uteuzi mpya hivi karibuni

  2. Tatizo ni mfumo wetu wa uongozi. Kikawaida viongozi hawa ni viongozi wa kisiasa tu siyo watendaji. hilo ni tatizo tusipo angalia tutakuwa tunafukuza mawaziri kila mwaka.

Comments are closed.