NCHEMBA AJIPA KAZI YA AFISA HABARI WA BOT NA KUMJIBU ZITTO KATIKA KILE KILICHODAIWA “BENKI KUU HAZINA YA TAIFA IMEKAUKA”.

Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nimesikitishwa na kushangazwa na taarifa iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari hivi leo na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Zuberi Kabwe.

Mimi nilikuwa ni Mchumi Daraja la Kwanza katika Benki Kuu ya Tanzania na nilikuwa nafanya kazi kwenye Kurugenzi ya Utafiti wa Uchumi na Sera. Hivyo, nafahamu jinsi Benki Kuu inavyofanya kazi.

Na nasikitika kwamba wanasiasa sasa, katika kujitafutia umaarufu, tunaingia kwenye kushambulia taasisi muhimu inayoendeshwa kwa weledi na uadilifu mkubwa.

Baada ya Mhe. Zitto Kabwe kukosa taarifa muhimu mtandaoni, ningetegemea Mbunge kama Zitto, ambaye Kamati yake inakagua mahesabu ya BOT, kuwasiliana na Benki na kuuliza kulikoni, badala ya kusambaza taarifa katika vyombo vya habari kulaani Benki Kuu na kusambaza tetesi kuhusu hali ya Hazina ya Taifa.

Lakini vilevile, ningetegemea kwamba, kama ameamua kusambaza taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, basi taarifa hiyo ingejumuisha yale aliyoyabaini baada ya kuzungumza na Benki Kuu.

Yeye kama kiongozi, kama anaamua kuwasiliana na umma kwa kusambaza taarifa kwa vyombo vya habari, basi walau aonyeshe umma jitihada nyingine alizofanya za kupata ripoti hizo zaidi ya kwenda tu mtandaoni, kwasababu sote tunajua kwamba hata namba ya Gavana wa Benki Kuu anayo.

Pili, kutokuwepo kwa ripoti mtandaoni hakumaanishi kwamba ripoti hizo aidha zimefichwa au hazipo.

Ni muhimu sana viongozi wakawa wa kweli na wakaacha mtindo wa kungoja siku ambayo haina habari (Jumapili) na kuamua kutengeneza habari kwa ajili ya vichwa vya habari vya Jumatatu.

Naomba kutoa ufafanuzi wa jinsi ukweli ulivyo, kwasababu hata sisi katika Chama tumekuwa tunafuatilia taarifa hizi za Uchumi kutoka Benki Kuu.

Kwanza, katika taarifa yake Zitto anaomba taarifa za mwezi Januari, Februari, Machi na Aprili zitolewe.

Hili limenishangaza kwasababu nilitegemea kwamba mtu kama Zitto, ambaye ni mchumi na ambaye kamati yake hupitia hesabu za BOT, angefahamu kwamba ripoti ya mwezi husika inaanza kuandaliwa tarehe 15 ya mwezi unaofuatia – kwa maana kwamba report ya mwezi Machi ilianza kuandaliwa tarehe 15 Aprili, report ya mwezi Aprili, itaanza kuandaliwa tarehe 15 Mei, na report ya mwezi Mei itaanza kuandaliwa tarehe 15 Juni.

Huu ni utaratibu wa kimataifa, ambapo inategemewa kwamba katika kipindi hicho cha wiki mbili baada ya mwezi kuisha, takwimu muhimu kutoka sehemu mbalimbali zitakuwa zimekusanywa na kuhakikiwa.

Pili, ningetegemea pia Mhe. Zitto awe anafahamu kwamba kabla ya taarifa hizi za Benki Kuu kuchapishwa ni lazima zipitishwe na Kamati ya Sera za Fedha ya Bodi ya Benki Kuu (Monetary Policy Committee of the Board).

Huko nyuma, Kamati hii ilikuwa inakutana kila mwezi, lakini kutokana na maagizo ya Kamati ya Mashirika ya Umma inayoongozwa na Mhe. Zitto kwamba vikao katika Benki Kuu vipunguzwe.

Hivyo, ikaamuliwa kwamba Kamati hii inayopitisha taarifa hizi muhimu iwe inakaa mara moja kila baada ya miezi miwili. Matokeo yake ni kuchelewa kupitia na kupitisha taarifa hizi muhimu.

Mara ya mwisho kikao kilikaa mwezi Machi kupitia taarifa ya mwezi Januari, ambayo imekwishasambazwa.

Tatu, si kweli kwamba Hazina ya Fedha za Kigeni Taifa imekauka.

Ambacho angeweza kufanya Zitto na ana mamlaka hayo na uwezo anao ni kumpigia simu Gavana au wasaidizi wake na kuwauliza ni kiasi gani cha Hazina kilichopo.

Mimi ndicho nilichofanya, na taarifa rasmi, ni kwamba hazina iliyopo ni kiasi cha dola za kimarekani bilioni 3.6, ambazo zinawezesha kuagiza mahitaji yetu yote ya bidhaa kwa kipindi cha miezi minne, na wala sio mwezi mmoja kama alivyodai Mhe ZITTO.

Na akiba ya watanzania iliyoko kwenye benki zetu nchini ni takribani dola za kimarekani 1.8 bilioni na taarifa hii pia IMF wanayo, (taarifa hii ni kwa kipindi kinachoishia tarehe 11 May 2012).

Binafsi nimesikitika sana kwamba kiongozi anaweza kuwa irresponsible kiasi hiki cha kusambaza taarifa za uvumi wakati anao uwezo wa kupata taarifa sahihi za maandishi na kuujulisha umma ukweli.

Mwisho, napenda kumsihi Mbunge mwenzangu kwamba ni muhimu kuwa makini na kutokurupuka katika mambo muhimu kama haya na ni muhimu kufanya utafiti kidogo kabla ya kuwasiliana na umma kwani sisi viongozi tunasikilizwa na kuaminiwa na watu na tunategemewa kuwa sahihi na wakweli wakati wote.

Imetolewa na:

Mwigulu Lameck Nchemba (MB)

Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM Taifa

Dodoma 13 Mei 2012

Advertisements

8 thoughts on “NCHEMBA AJIPA KAZI YA AFISA HABARI WA BOT NA KUMJIBU ZITTO KATIKA KILE KILICHODAIWA “BENKI KUU HAZINA YA TAIFA IMEKAUKA”.

 1. Mambo ya ajabu sana.

  CCM!? Naona habari za BOT badala ya kuitafuta BOT ili watoe majibu anamkimbilia mfanyakazi wa zamani wa BOT!

  Huku kama sio kuhamaki ni nini?

  Karibu websites za wizara zote za serikali hazina kitu cha maana Mwigulu na Nape wanasemaje maaana sasa wamejigeuza kuwa wasemaji wasio na idara maalum?

 2. Sasa kama bodi ya bank inakaa kila baada ya miezi miwili…

  toka November mpaka leo MEI hiyo ni miezi 6, mbona hawaeleweki.

  Waziri wa fedha aliyepita(mkulo) na Gavana wa benk ndio wanajua sababu ya hizi report kutokua available for the public…

  Na according to CAG report wizara ya fedha imekua ikifuja pesa ndio maana tunataka kujua hizo report zitawekwa lini..

 3. Nyie CCM hata mijisafishe vipi mbele ya umma na chama lenu hilo kamwe hamuwezi kusafishika, kwani jamii nzima imeshawaona kuwa ninyi ni wezi wa fedha zetu na twiga wetu, dhambi zenu haziungamiki hata kidogo, pia jua kwamba zitto ni mtu makini na huwa anafanya mambo yake kwa umakini mkubwa so hakuna alichokosea but nyie majambazi Nape na Mwigulu mme-note vibaya maneno ya zitto kwa kihoro chenu na kuropoka kwenu kwani nyie mmezoea kukanusha kila kitu hata kama ni cha kweli.

  ZITO HAJASEMA KWAMBA HAZINA BOT IMEKAUKA BALI ZITTO KASEMA KWA KUULIZA SWALI HIVI ” HAZINA YA BENKI KUU IMEKAUKA?” s

  sasa nashangaa magamba mnaanza kujihami.

 4. Sasa wewe Nchemba sijui Nape ndio umekuwa Vick Joan Msina PRO wa BOT.

  Na kwa mamlaka gani uliyonayo yanayokufanya uwe na uwezo wa kukanusha taarifa kama hyo ya taasisi nyeti nchini.

 5. Mi nataka kufahamu nani anawajibika kuisea BOT / Serikali??

  Ni Nape, Nchemba, Dr Mgimwa, Ndullu au??

  Zitto ni waziri kivuli wa Fedha na uchumi ametimiza wajibu wake!!

  So who are these morons talking shity??

 6. Hii taarifa imetolewa na chama (CCM) kwa sababu gani?

  Mwigulu Nchemba ni msemaji wa BOT?

  Kufanya kazi BOT ndiko kimempa mamlaka ya kuwa msemaji wake?

  Mwigulu anasema kwamba “hazina iliyopo ni kiasi cha dola za kimarekani bilioni 3.6, ambazo zinawezesha kuagiza mahitaji yetu yote ya bidhaa kwa kipindi cha miezi minne”!

  Kapata wapi hizi habari huyu Mwigulu?

  Mbona sizioni kwenye website ya BOT?

  Kama taarifa zilikuwepo kwa nini hawakuweka kwenye website?

  Na kama Zitto hakuwatoa huko pangoni wanakojificha ni lini wangeanza kuongea?

  Bado tatizo liko pale pale, BOT wanatakiwa waweke taarifa hadharani na sio wanasiasa uchwara wanaojiunga vitambaa shingoni! Kuna watu wanalipwa hela za walipa kodi kufanya hivyo kazi, we want results/accountability.

 7. Mpaka hapo sijajua wewe Mwigulu unalalamika nini? na kilichokuboa sana hapo ni kipi? maana kama taarifa alizotoa Mh ZITTO ni kwa ajili yetu wananchi wenye mali! na alikuwa anatimiza wajibu wake tuliompatia serikalini! unalalamika na kujitahidi kukanusha kwa lugha ya kushawishi, kama taarifa alizotoa Zitto si za kweli basi tuwekee wazi taarifa za kweli unazozijua wewe ili tukusadiki, pili, wewe umejibu hili kwa niaba ya nani? na ukiwa kama nani BOT kwa sasa? tatu! hizo bilion 3.6 mbona hatuzioni katika mtandao? mnataka kufungia maandazi au? all in all we need transparent, accountability and open minded

 8. Ndg mwigulu, wewe na wana ccm wenzio inabidi mtambue mipaka yenu, juzi nape anatangaza nia ya kikwete kuvunja baraza ilhali anatambua kuwa ikulu ina msemaji wake ndg rweyemamu, leo wewe nawe unakurupuka ujui unamjibu nani unaropoka tu, zitto hakuzungumza kama kiongozi wa chama alizungumza kama mchumi na waziri kivuli wa fedha kwa hiyo ulikuwa mtu mdogo sana kumjibu aliepaswa kumjibu kama sio waziri wa fedha bac gavana wa bot,ni heri mwenda wazimu akae kimya ili tumhisi kuwa mwenda wazimu kuliko kutamka vitu visivyo na mashiko anajibainisha yeye ninani, VIONGOZI WA C.C.M TAMBUENI MIPAKA YA KAZI ZENU.

Comments are closed.