MASIKINI MIZENGO PINDA, BAADA YA KUNUSURIKA KWA WABUNGE UPEPO WA KUMG’OA BADO WAMWANDAMA.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda

• Khamis Mgeja, ataka naye ang’atuke kama mawaziri wenzake.

• Yusuf Makamba, alimlipua kwamba hana mawasiliano mazuri na serikali.

• Kingunge asema kwa kutokujiamini kwake ndiyo sababu ya wananchi kupoteza imani kwa CCM na serikali yake.


Waziri Mkuu Mizengo Pinda, anaendelea kuandamwa na jinamizi la kutaka kumng’oa ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), mjini Dodoma ikiwa ni ndani ya wiki 3 tu toka kunusurika kung’olewa na Bungeni.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilicho malizika Jumanne Mei 15, 2012 mjini Dodoma zilidai kuwa baadhi ya wajumbe wa NEC waliibua hoja ya kumtaka Pinda apime uzito wa tuhuma zinazo mwandama Bungeni na achukue hatua za kuwajibika.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, ndiye aliyekuwa mwiba mkali kwa Pinda kwa kuibua hoja ya kumtaka naye ang’atuke.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mgeja akichangia ajenda ya hali ya kisiasa ndani ya chama hicho, alisema haoni sababu ya Waziri Mkuu kutowajibika wakati mawaziri wake wamewajibika, tena wengine si kwa makosa yao bali ya uzembe uliosababishwa na watendaji wao.

Mgeja alisema Pinda anapaswa kuwajibika kutokana na ubadhirifu mkubwa wa fedha za serikali ulioainishwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Huku akiungwa mkono na baadhi ya wajumbe wa NEC kwa kupiga makofi, mwenyekiti huyo alisema CCM inapakwa matope kwa makosa ya viongozi wa serikali kutowajibika na kusisitiza kuwa Pinda anapaswa kupima uzito wa hoja kwani ndiye kiranja wa mawaziri waliong’olewa kwa tuhuma za ufisadi.

Alihoji kuwa kama mawaziri wanane wameng’olewa kutokana na ripoti ya CAG na shinikizo la wabunge wakiwemo wa CCM kutishia kupiga kura ya kutokuwa na imani na Pinda, Waziri Mkuu huyo hana uhalali wa kubaki madarakani akaendelea kuaminika.

Mtoa taarifa wetu kutoka ndani ya kikao hicho, alisema Mgeja alitoa mfano wa ufisadi wa mamilioni ya fedha unaofanywa na watendaji katika wilaya za mkoa wake kupitia vocha ya pembejeo kwamba ni wa kutisha, na alishatoa taarifa kwa waziri mkuu ambaye hakuzifanyia kazi hadi sasa.

Hoja hiyo iliungwa mkono Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM, Yusufu Makamba, ambaye alimlipua Waziri Mkuu Pinda kwamba hana mawasiliano mazuri na serikali.

Alisema haridhishwi na utendaji wa kiongozi huyo kwani ni rahisi kumpata Raisi kuliko waziri mkuu, jambo ambalo alisema halileti tija kwa serikali.

Mjumbe mwingine aliyekosoa utendaji wa Pinda ni mkongwe Kingunge ngombale Mwiru ambaye alimtaka mtendaji huyo kufanya kazi kwa kujiamini ili kurejesha imani ya wananchi kwa CCM iliyoanza kupoteza Mwelekeo

Habari zinasema kuwa wakati Pinda akishambuliwa na kutakiwa kujiuzulu, Mwenyekiti wa CCM Taifa, RaisiKikwete, na Pinda mwenyewe, hawakujibu chochote.
Advertisements

JOPO LA MAWAKILI WA UTETEZI WA KESI YA LULU WATUPA KETE NYINGINE MAHAKAMA KUU KUSHINIKIZA UCHUNGUZI WA UMRI WA MTEJA WAO.

• Wadai Hakimu Mmbando alijielekeza vibaya kwa kusema kuwa mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza ombi lao.

• Pia wanaiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa Mahakama ya Kisutu haina uwezo huo, basi yenyewe ifanye uchunguzi huo.

• Lengo la uchunguzi huo ni  kuifanya Mahakama ijiridhishe kama mshtakiwa ni mtoto au ni mtu mzima kwa lengo la kuangalia maslahi ya mtoto.


Katika hatua mpya jopo la mawakili 3 linalo mtetea msanii wa filamu nchini, Eizabeth Michael ‘Lulu’, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya msanii mwenzake, Jumanne Mei 15, 2012 wamewasilisha ombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakiomba maakama hiyo ielekeze Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ishughulikie ombi lao linalo omba  kesi hiyo isikilizwe katika mahakama ya watoto kwa kuwa mshtakiwa huyo ana miaka chini ya 18.

Jopo hilo linaloongozwa na Wakili Kennedy Fungamtama lina wajumuisha Wakili Peter Kibatala ambaye ni Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), mawakili wengine katika jopo hilo ni Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG) Joaquine De- Melo, pamoja na Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Ombi hilo Na.46/2012, liliwasilishwa Jumanne Mei 15, 2012 mchana, chini ya hati ya dharura iliyosainiwa na kiongozi wa mawakili wanaomtetea Lulu, Fungamtama.

Kwa mujibu wa hati ya madai ya ombi hilo, mawakili hao wanadai kuwa Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Augustina Mmbando, Mei 7, 2012 alikataa kulitolea uamuzi ombi la mawakili wa Lulu, lililokuwa likitaka kesi hiyo ihamishiwe katika mahakama ya watoto, kwa sababu mshtakiwa huyo ana miaka chini ya 18 na badala yake hakimu huyo akasema mahakama hiyo haina mamlaka ya kutolea uamuzi ombi hilo na kuwashauri mawakili hao kuliwasilisha Mahakama Kuu.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya madai, wakili Fungamtama alidai kuwa Hakimu Mmbando alijielekeza vibaya kwa kusema kuwa mahakama ile ilikuwa haina mamlaka ya kusikiliza ombi lao, kwa hiyo wanaiomba Mahakama Kuu, imwelekeze asilikize ombi lao na alitolee maamuzi na kuwa endapo Mahakama Kuu itabaini vinginevyo, basi mahakama hiyo ya juu itoe tafsiri ya umri wake kuhusu ombi hilo.

Awali mawakili hao waliwasilisha maombi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakiiomba iamuru kesi ya msanii huyo isikilizwe katika mahakama za watoto, wakidai kuwa bado ni mtoto.

Katika uamuzi wake, Hakimu Mkazi, Augustina Mmbando, anayesikiliza kesi hiyo alisema kesi hiyo bado iko kwenye upelelezi na kwamba kulingana na jinsi ilivyo isingekuwa busara kuamua hoja yoyote.

Hata hivyo, upande wa jamhuri kupitia wakili wa serikali mwandamizi, Elizabeth Kaganda, ulipinga maombi hayo na kudai kuwa bado wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo na hivyo kuomba wapewe muda zaidi.

Wakili Kaganda pia alidai kuwa hata jina linaloonekana katika cheti cha kuzaliwa cha mshtakiwa huyo linasomeka kama Diana Elizabeth, wakati mshtakiwa huyo ametajwa mahakamani hapo kama Elizabeth Michael.

Akijibu hoja hiyo, wakili Fungamtama alikiri jina hilo kusomeka Diana Elizabeth na kudai kuwa ni jambo la kawaida hasa kwa Wakristo kuwa na majina mawili.

Katika maombi hayo namba 46 ya mwaka 2012, yaliyosilishwa na Wakili Peter Kibatala kwa niaba ya jopo la mawakili hao, pia wanaiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa Mahakama ya Kisutu haina uwezo huo, basi yenyewe ifanye uchunguzi huo.

Akifafanua juu ya maombi hayo, Kibatala alisema Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, Kifungu cha 113 inaruhusu Mahakama kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa.

Wakili Kibatala alisema lengo la uchunguzi huo ni  kuifanya ijiridhishe kama mshtakiwa ni mtoto au ni mtu mzima kwa lengo la kuangalia maslahi ya mtoto.

“Baada ya uchunguzi huo, mahakama ikijiridhisha kuwa ni mtoto, basi mwenendo wa kesi hiyo utaendeshwa kwa maslahi ya mtoto kwa mujibu wa Kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Mtoto,” alisema.

Kifungu hicho huelezea ulinzi na maslahi ya mtoto katika uendeshaji wa kesi kwa watoto wanaokinzana na sheria.

Kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Mei 21 mwaka huu na msanii huyo bado anaendelea kusota rumande kutokana na kesi inayomkabili kutokuwa na dhamana.

MAELEZO YA MH. EZEKIEL MAIGE KWENYE FB STATUS YAKE

Ndugu zangu na rafiki zangu.

Kwanza niwape pole kwa mshituko mlioupata kwa haya yaliyojitokeza.

Naomba msisikitike sana.

Kila jambo alilopanga Mola hutokea kadiri ya mapenzi yake. Route ya maisha ya mwanadamu hupangwa na Mola mara tu anapompulizia pumzi ya uhai.

Hili lilipangwa hata kabla sijatokea duniani miaka 42 iliyopita! Mungu hakushindwa kumwokoa mwanawe Yesu asisulubiwe, tena kwa kuonewa! Hasha, tungeupataje ukombozi bila hilo kutokea?

Wakati mwingine Mungu hutoa nafasi kwa mambomagumu kuwafika waja wake, si kwamba hawapendi,bali ili unabii utimie.

Ilifika wakati hata Yesu akaona kama Mungu kamuacha! Hasa sisi kwa hili tunaweza kudhani Mungu katuacha! Hasha, ni njia ya kuufikia ukombozi wa kweli.

Pili, kwa kifupi sana, niwafahamishe kuwa, yaliyotokea ni ushahidi kwamba maliasili ni ngumu.

Kukabiliala na wabaya ni kazi ngumu. Wapo waliojipanga ukiwavamia ovyoovyo unaondoka wewe. Ndivyo ilivyotokea.

Niwahakikishie, wazalendo wamepoteza mpambanaji. Nimepambana na wahalifu angani, majini, porini, mijini na vijijini ndani na nje ya nchi.

Nilitumia kila aina ya uwezo wangu kulizawadia taifa langu utumishi uliotukuka. Sikubakisha chembe ya energy. Waziri gani aliyesimamia sheria na kuwapa vitalu watanzania maskini wenye sifa na kuwaacha wazungu kama sheria ilivyoelekeza?

Waziri gani aliyewafikisha mahakamni watorosha twiga akina Kamrani na wenzake? Watu wametumia records za matukio ya 2009/10 kuficha matendo na maamuzi ya kishujaa ya maige ya 2011.

Yawezekana hawakutaka nipate sifa, lakini ipo siku nitaipata. Tena si siku nyingi. Niliwaomba wenzangu wamwogope Mungu. Bado nasisisitza hivyo, si Mungu wangu kama ilivyodhaniwa, bali Mungu wetu wa haki.

Waziri gani aliyefunga biashara ya wanyamahai? Waziri gani aliyeonyesha mfano wa kuchukua hatua kwa watumishi pale alipoona hawatendi sawa? Maige hakusita kuchukua hatua. Maamuzi haya ni magumu na yamegusa watu wenye nguvu na ushawishi mkubwa.

Nilitegemea vita hii, na ninaamini tutashinda. Nilisema Bungeni, watanzania wapenda haki wanisikilize kwa makini. Muda haukuruhusu, ila nitarudi Bungeni na nitasema. Imesemwa issue ya nyumba. Nimefafanua na kutoa vielelezo. Kila mbunge aliyetaka amekopeshwa shs 290m, wengine wameanzisha biashara na wengine wamenununua magari na wengine majumba.

Wapo walioficha, na tupo tuliojiweka wazi! Mkopo wangu huo umekuwa my contribution na balance kulipwa na benki na nyumba kuimortgage. Nimetoa nyaraka zote kwa wanahabari na vyombo vyote husika. Nimesema mwenye mashaka aende kwa Msajili wa hati wizara ya ardhi, au kwa kamishna wa maadili, au CRDB Azikiwe na Dodoma nilikokopa au amtafute muuzaji.

Kote huko utapata rekodi ya bei na mode of payment. Wapo wahuni, kwa maslahi ya kisiasa na chuki binafsi wametangaza bei tofauti na niliyonunulia. Manasheria wangu anashughulikia hilo.

Niwahakikishie, vita nimepigana, imani na dhamana nimeilinda, muda wa kutuzwa na mwenye kumbukumbu sahihi, Mungu utafika. Naamini nimejiwekea akiba isyooza Mbiguni. Yapo mengi yasiyo sahihi yaliyosemwa.

Nitakuwa nafafanua kila nipatapo fursa na muda utazidi kutufunua. Kwa kifupi, kwa suala la vitalu, hakuna kampuni hata moja iliyopewa kitalu cha uwindaji bila kuomba, kukaguliwa na kamati ya ushauri na hatimaye kupewa alama. Kampuni zisizokuwa na sifa ni zile zilizopata chini ya alama 50.

Na kwa kampuni zilizokuwa kwenye biashara, passmark ni alama 40 kwa mujibu wa kanuni ya 16(5) ya kanuni za uwindaji wa kitalii za mwaka 2010. Hakuna kampuni iliyopata chini ya alama 50 iliyopata kitalu. Hakuna kampuni ya kizalendo iliyopendekezwa na kamati ya ushauri ambayo haikupewa kitalu.

Kwa upande wa report ya CAG, haikunigusa binafsi kwani ilikuwa inaishia juni 2010 wakati mimi ilishika dhamana Novemba 2010. Ka upande wa biasharaya wanyamahai, hakuna wanyama waliosafirishwa kinyume cha sheria wakati wangu (2011), na matukio ya utoroshaji tulipoyabaini, tulifungua mashitaka kwa watuhumiwa nakufnug biashara hiyo. Naanza kazi ya kuwawakilisha wananchi wa Msalala.

Nitawawakilisha kwa mujibu wa katiba na ahadi zangu kwao hadi 2015 watakapopata fursa ya kuamua vinginevyo.

Mara nyingi watenda mema hufanyiwa hiyana.

Ka wakristo, naomba msome Mwanzo 4:1-15. Wasalaam