BURIANI PATRICK MUTESA MAFISANGO, UTAKUMBUKWA DAIMA NA WAPENDA SOKA WOTE WA TANZANIA NA AFRIKA KWA UJUMLA.

PATRICK MUTESA MAFISANGO

FAMILIA ya soka nchini imepatwa na majonzi makubwa kufuatia kifo cha mchezaji nyota wa klabu ya Simba na timu ya taifa ya Rwanda, Patrick Mutesa Mafisango.

Kiungo huyo amefariki usiku wa Jumatano Mei 16, 2012 kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Veta-Keko, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Olilemba Mafisango, katika ajali hiyo Mafisango alikuwa anaendesha huku amewabeba watu wanne, miungoni mwa watu hao kulikuwa na wasichana wawili na wavulana watatu, akiwemo mdogo wake na rafiki yake.

Ajali hiyo ilitokana na nyota huyo kutaka kumpisha mwendesha pikipiki ambaye alikuwa anataka kukatisha kuelekea eneo jingine na ajali hiyo kutokea huku mmoja kati yao akipata majeraha kidogo kichwani.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, mwili wa marehemu Mafisango utaagwa Ijumaa Mei 18 asubuhi katika viwanja vya Klabu ya Sigara, Chang’ombe jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kesho kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa mazishi.

Tunaungana na familia, wana-Simba pamoja na wadau wote wa soka nchini katika kuomboleza kifo cha nyota huyu aliyefariki akiwa na umri wa miaka 32.

Kifo cha Mafisango kimeacha pengo kubwa kwa Simba kutokana na mchango wake kwa timu hiyo aliyojiunga nayo mwaka jana akitokea Azam FC pia ya jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuja nchini, Mafisango, mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyechukua uraia wa Rwanda na kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo, Amavubi kwa takriban miaka mitano, aliwahi pia kuzichezea klabu za TP Mazembe ya DRC na APR ya Rwanda.

Huu ni msiba mkubwa kwa soka ya Tanzania, kwani kwa kipindi chote alichokuwa hapa nchini, akiichezea Azam na baadaye Simba, alitekeleza majukumu yake kwa bidii na ufanisi wa hali ya juu.

Kifo cha Mafisango sio tu kwamba ni pigo kwa klabu yake ya Simba, bali pia kwa familia yake na taifa la Rwanda ambako mchango wake bado ulikuwa ukihitajika sana.

Itakumbukwa kuwa ni hivi majuzi tu nyota huyo aliitwa katika kikosi cha Rwanda kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazopigwa mwaka 2014 nchini Brazil.

WACHEZAJI WANENA

Baadhi ya wachezaji wa klabu mbalimbali na klabu yake walieleza hisia zao mara baada ya kufika katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili wakiwa wamepigwa butwaa na kububujikwa machozi.

Kati ya wachezaji hao ni Emmanuel Okwi, Dereck Walulya, Haruna Moshi ‘Boban’, Uhuru Seleman na Haruna Niyonzima wa Yanga.

Okwi kwa upande wake, alisema kifo cha Mafisango kimekuwa cha ghafla kiasi cha kushindwa kuamini, lakini ndio hivyo, hataonekana tena.

“Ukweli ni kwamba mimi katika maisha yangu sitoweza kumsahau Mafisango kutokana na ukarimu na ukaribu wake kwangu mimi na jana (juzi) mchana nilimpigia simu ili tutoke lakini akawa hapokei simu na hapo ndipo sikumtafuta tena,” anasema Okwi.

Anasema habari za kifo cha Mafisango alizipata alhamisi 17, 2012 majira ya saa 12:30 asubuhi alipopigiwa simu na Haruna Moshi ‘Boban’, aliyemtaka aungane naye kwenda Muhimbili, hivyo wakaambatana kwenda huko na kukuta umati wa watu ukiwa umepigwa butwaa juu ya kifo hicho.

“Niyonzima kwa upande wake, alisema alipata taarifa za kifo hicho akijiandaa kwenda Rwanda tayari kuitumikia timu ya taifa ya huko, Amavuni, na Mafisango alikuwa aondoke leo, lakini akalazimika kuahirisha.

Niyonzima anasema baada ya kuona wameitwa timu ya taifa, aliamua kumpigia simu kocha wao na kumwomba ampe nafasi Mafisango ili apumzike kidogo kwa kuwa alikuwa na uchovu wa safari ya kutoka Sudan akiwa na timu yake ya Simba.

“Kitu kingine, ni kwamba siku ya mechi yetu na Simba ya mwisho wa ligi tulibadilishana jezi na Mafisango na mara baada ya kufika nyumbani, alinipigia simu na kuniambia niivae, na nisije kumpa mwingine katika maisha yangu kuvaa jezi hiyo,” anasema Niyonzima.

Boban alishindwa kuzuia hisia zake ambapo baada ya kufika kwenye chumba cha kutunzia maiti, aliwaomba wafanyakazi kumruhusu walau amuone ndipo aweze kuamini kama kweli Mafisango amefariki.

Baada ya kuona anazuiwa, Boban alishindwa kujizuia na kuangua kilio hadi wafanyakazi hao kumruhusu kuingia na kuuona mwili wa mchezaji mwenzake huku waandishi wakibaki nje, wakimsubiri, lakini haikuwezekana kwani alitokea mlango wa nyuma na kuondoka.

“Mimi nakumbuka siku ya mechi yetu ya mwisho na Al Ahli Shandi Mafisango alikuwa anaongea uwanjani mpaka mwamuzi akawa anamuita nahodha wa timu na mara baada ya mchezo kumalizika alikuwa akitoa vichekesho tu vya kuchekesha ukweli ni kwamba msiba wake ni pengo kubwa ambalo kuzibika ni kazi kubwa,” anasema Uhuru Selemani na kuongeza:

“Mafisango ndani ya Simba, alikuwa ni zaidi ya mchezaji na hakuna mtu ambaye halijui na kulifahamu hilo na tumepoteza nyota muhimu sana sisi kama wachezaji tunajua na Mungu amlaze mahali pema peponi,” anasisitiza,

WANAMUZIKI WANALONGA

Wanamuziki wa bendi ya Akudo Impact, walifika hospitalini na kuonyesha majonzi makubwa, ambapo Christian Bella, Clary Boteku na Canal Top, walimwelezea Mafisango kama rafiki yao wa karibu, aliyekuwa karibu nao wakati wote.

BONIFACE PAWASA

Kati ya wachezaji wakongwe ambao walikuwa karibu na Mafisango ni Boniface Pawasa ambaye jana alifika katika hospitali ya Muhimbili, kuthibitisha habari za kifo cha ghafla cha Mafisango.

Akimwelezea marehemu, Pawasa anasema Mafisango alikuwa mchezaji mwenye kiu ya mafanikio, kiasi cha kuwa tayari kuomba ushauri wa nini afanye ili aweze kufanikiwa kisoka.

“Mimi na Mafisango tumefahamiana siku nyingi sana wakati nikiwa APR Rwanda, tulikuwa tunaishi nyumba moja mwaka 2008, wakati huo yeye ndiye alikuwa mwenyeji wangu; alinipokea na kunipa ushirikiano wa hali na mali. Kifo chake ni pengo kubwa sana kwangu,” anasema Pawasa.

Pawasa anasema yeye alihusika Mafisango kujiunga Azam na hatimaye Simba, pia alikuwa akimpa ushauri wa mara kwa mara kwani nyota huyo aliamini ulikuwa sahihi kutokana na uzoefu wa Pawasa katika soka la Tanzania ikiwemo Simba.

MBUNGE WA KOROGWE VIJIJINI

Kati ya wadau walioguswa na msiba huo, ni Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stevine Ngonyani ‘Prof Maji Marefu’ ambaye alifika katika vyumba vya kuhifadhi maiti akitokea katika wodi ya Kibasila, alikolazwa kwa siku 25 sasa, akisumbuliwa na vidonda vya tumbo.

“Mimi nimelazwa hapa muda na mimi kama mdau mkubwa wa Simba nimeumia mara baada ya kusikia msiba wa mchezaji wetu Mafisango na ndiyo maana nikaona ni bora nije walau nimuone ila nimeshuhudia maiti yake, Mungu amlaze mahali pema peponi,” alisema Maji Marefu, amen.

Hatuna cha kusema zaidi juu ya msiba huu, zaidi ya kutoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba na Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA).

Wote kwa pamoja tunawataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Mafisango mahali pema peponi. Amina.

Advertisements

KAULI YA MKUU WA MKOA WA ARUSHA DHIDI YA HUKUMU YA LEMA YAZIDISHA HISIA KUWA IMETOKANA NA SHINIKIZO LA KISIASA.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha,
Magesa Mulongo

• Asema sasa mji wa Arusha umetulia

• Amwaga sifa kwa Gabriel Rwakibarila jaji wa hukumu hiyo.

• Waliohudhuria wazua minongo’no, wahoji kauli hiyo.


Katika hali ya Kushangaza mkuu wa mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, ameshindwa kuficha furaha yake dhidi ya maamuzi ya kuenguliwa kwa mbunge wa Arusha Mjini, kulikofanywa na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, akidai kuwa kumesaidia kudumisha amani katika mkoa huo.

Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wakuu wapya wa wilaya sita za mkoa wa Arusha, Alhamisi Mei 17, 2012 katika hafla fupi iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, Mulongo alisema kwa sasa mji wa Arusha umetulia na alimpongeza jaji wa mahakama hiyo, Gabriel Rwakibarila, ambaye alitoa hukumu iliyomnyang’anya ubunge Godbless Lema.

Bila kutaja jina la Lema, Mulongo alizidisha vijembe akidai kuwa hakuna haja kwa aliyeshindwa kesi kulalamika na kuwasakama wengine kwamba wamesababisha ashindwe, badala yake akamtaka akate rufaa mahakama za juu.

“Utawataja wote, kwamba hawa ndiyo wamechangia lakini hukumu tayari imeshatoka, kama hukuridhika ni vema ukaenda mahakama inayofuata,” alisema Mulongo katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Jaji Mfawidhi, Aisha Nyerere.

Kauli ya Mulongo ilipokelewa kwa hisia tofauti kutoka miongoni mwa wageni na viongozi waliohudhuria hafla hiyo kiasi cha kuzua minong’ono ya chinichini.

Matamshi ya sasa ya Mulongo, huenda yakaibua upya msuguano baina ya viongozi hao wawili ambao awali kabla ya kupatanishwa walikuwa katika uhasama mkubwa uliozidisha joto la upinzani katika jiji la Arusha.

Pamoja na kupokwa ubunge wake, Lema bado ana nguvu kubwa ya ushawishi, na anaungwa mkono na kundi kubwa la wakazi wa jiji hili wa ngazi na rika zote.

Hata hivyo, tayari Lema amekata rufaa Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu hiyo, ambayo ilipingwa vikali na wananchi na wanasheria mbalimbali kwa madai kuwa haikuzingatia sheria, na wengine wakidai ilitokana na shikinikizo la kisiasa.

Waliopinga akiwemo Lema mwenyewe walihoji sababu za hukumu hiyo kujulikana kabla haijasomwa, na wengine wakihoji upungufu wa kisheria unaodaiwa kujitokeza likiwemo suala la kuchanganywa kwa vifungu vilivyotumika kufanya uamuzi huo.