BURIANI PATRICK MUTESA MAFISANGO, UTAKUMBUKWA DAIMA NA WAPENDA SOKA WOTE WA TANZANIA NA AFRIKA KWA UJUMLA.

PATRICK MUTESA MAFISANGO

FAMILIA ya soka nchini imepatwa na majonzi makubwa kufuatia kifo cha mchezaji nyota wa klabu ya Simba na timu ya taifa ya Rwanda, Patrick Mutesa Mafisango.

Kiungo huyo amefariki usiku wa Jumatano Mei 16, 2012 kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Veta-Keko, jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu, Olilemba Mafisango, katika ajali hiyo Mafisango alikuwa anaendesha huku amewabeba watu wanne, miungoni mwa watu hao kulikuwa na wasichana wawili na wavulana watatu, akiwemo mdogo wake na rafiki yake.

Ajali hiyo ilitokana na nyota huyo kutaka kumpisha mwendesha pikipiki ambaye alikuwa anataka kukatisha kuelekea eneo jingine na ajali hiyo kutokea huku mmoja kati yao akipata majeraha kidogo kichwani.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Godfrey Nyange ‘Kaburu’, mwili wa marehemu Mafisango utaagwa Ijumaa Mei 18 asubuhi katika viwanja vya Klabu ya Sigara, Chang’ombe jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kesho kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa mazishi.

Tunaungana na familia, wana-Simba pamoja na wadau wote wa soka nchini katika kuomboleza kifo cha nyota huyu aliyefariki akiwa na umri wa miaka 32.

Kifo cha Mafisango kimeacha pengo kubwa kwa Simba kutokana na mchango wake kwa timu hiyo aliyojiunga nayo mwaka jana akitokea Azam FC pia ya jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuja nchini, Mafisango, mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), aliyechukua uraia wa Rwanda na kuichezea timu ya taifa ya nchi hiyo, Amavubi kwa takriban miaka mitano, aliwahi pia kuzichezea klabu za TP Mazembe ya DRC na APR ya Rwanda.

Huu ni msiba mkubwa kwa soka ya Tanzania, kwani kwa kipindi chote alichokuwa hapa nchini, akiichezea Azam na baadaye Simba, alitekeleza majukumu yake kwa bidii na ufanisi wa hali ya juu.

Kifo cha Mafisango sio tu kwamba ni pigo kwa klabu yake ya Simba, bali pia kwa familia yake na taifa la Rwanda ambako mchango wake bado ulikuwa ukihitajika sana.

Itakumbukwa kuwa ni hivi majuzi tu nyota huyo aliitwa katika kikosi cha Rwanda kwa ajili ya mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia zitakazopigwa mwaka 2014 nchini Brazil.

WACHEZAJI WANENA

Baadhi ya wachezaji wa klabu mbalimbali na klabu yake walieleza hisia zao mara baada ya kufika katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili wakiwa wamepigwa butwaa na kububujikwa machozi.

Kati ya wachezaji hao ni Emmanuel Okwi, Dereck Walulya, Haruna Moshi ‘Boban’, Uhuru Seleman na Haruna Niyonzima wa Yanga.

Okwi kwa upande wake, alisema kifo cha Mafisango kimekuwa cha ghafla kiasi cha kushindwa kuamini, lakini ndio hivyo, hataonekana tena.

“Ukweli ni kwamba mimi katika maisha yangu sitoweza kumsahau Mafisango kutokana na ukarimu na ukaribu wake kwangu mimi na jana (juzi) mchana nilimpigia simu ili tutoke lakini akawa hapokei simu na hapo ndipo sikumtafuta tena,” anasema Okwi.

Anasema habari za kifo cha Mafisango alizipata alhamisi 17, 2012 majira ya saa 12:30 asubuhi alipopigiwa simu na Haruna Moshi ‘Boban’, aliyemtaka aungane naye kwenda Muhimbili, hivyo wakaambatana kwenda huko na kukuta umati wa watu ukiwa umepigwa butwaa juu ya kifo hicho.

“Niyonzima kwa upande wake, alisema alipata taarifa za kifo hicho akijiandaa kwenda Rwanda tayari kuitumikia timu ya taifa ya huko, Amavuni, na Mafisango alikuwa aondoke leo, lakini akalazimika kuahirisha.

Niyonzima anasema baada ya kuona wameitwa timu ya taifa, aliamua kumpigia simu kocha wao na kumwomba ampe nafasi Mafisango ili apumzike kidogo kwa kuwa alikuwa na uchovu wa safari ya kutoka Sudan akiwa na timu yake ya Simba.

“Kitu kingine, ni kwamba siku ya mechi yetu na Simba ya mwisho wa ligi tulibadilishana jezi na Mafisango na mara baada ya kufika nyumbani, alinipigia simu na kuniambia niivae, na nisije kumpa mwingine katika maisha yangu kuvaa jezi hiyo,” anasema Niyonzima.

Boban alishindwa kuzuia hisia zake ambapo baada ya kufika kwenye chumba cha kutunzia maiti, aliwaomba wafanyakazi kumruhusu walau amuone ndipo aweze kuamini kama kweli Mafisango amefariki.

Baada ya kuona anazuiwa, Boban alishindwa kujizuia na kuangua kilio hadi wafanyakazi hao kumruhusu kuingia na kuuona mwili wa mchezaji mwenzake huku waandishi wakibaki nje, wakimsubiri, lakini haikuwezekana kwani alitokea mlango wa nyuma na kuondoka.

“Mimi nakumbuka siku ya mechi yetu ya mwisho na Al Ahli Shandi Mafisango alikuwa anaongea uwanjani mpaka mwamuzi akawa anamuita nahodha wa timu na mara baada ya mchezo kumalizika alikuwa akitoa vichekesho tu vya kuchekesha ukweli ni kwamba msiba wake ni pengo kubwa ambalo kuzibika ni kazi kubwa,” anasema Uhuru Selemani na kuongeza:

“Mafisango ndani ya Simba, alikuwa ni zaidi ya mchezaji na hakuna mtu ambaye halijui na kulifahamu hilo na tumepoteza nyota muhimu sana sisi kama wachezaji tunajua na Mungu amlaze mahali pema peponi,” anasisitiza,

WANAMUZIKI WANALONGA

Wanamuziki wa bendi ya Akudo Impact, walifika hospitalini na kuonyesha majonzi makubwa, ambapo Christian Bella, Clary Boteku na Canal Top, walimwelezea Mafisango kama rafiki yao wa karibu, aliyekuwa karibu nao wakati wote.

BONIFACE PAWASA

Kati ya wachezaji wakongwe ambao walikuwa karibu na Mafisango ni Boniface Pawasa ambaye jana alifika katika hospitali ya Muhimbili, kuthibitisha habari za kifo cha ghafla cha Mafisango.

Akimwelezea marehemu, Pawasa anasema Mafisango alikuwa mchezaji mwenye kiu ya mafanikio, kiasi cha kuwa tayari kuomba ushauri wa nini afanye ili aweze kufanikiwa kisoka.

“Mimi na Mafisango tumefahamiana siku nyingi sana wakati nikiwa APR Rwanda, tulikuwa tunaishi nyumba moja mwaka 2008, wakati huo yeye ndiye alikuwa mwenyeji wangu; alinipokea na kunipa ushirikiano wa hali na mali. Kifo chake ni pengo kubwa sana kwangu,” anasema Pawasa.

Pawasa anasema yeye alihusika Mafisango kujiunga Azam na hatimaye Simba, pia alikuwa akimpa ushauri wa mara kwa mara kwani nyota huyo aliamini ulikuwa sahihi kutokana na uzoefu wa Pawasa katika soka la Tanzania ikiwemo Simba.

MBUNGE WA KOROGWE VIJIJINI

Kati ya wadau walioguswa na msiba huo, ni Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stevine Ngonyani ‘Prof Maji Marefu’ ambaye alifika katika vyumba vya kuhifadhi maiti akitokea katika wodi ya Kibasila, alikolazwa kwa siku 25 sasa, akisumbuliwa na vidonda vya tumbo.

“Mimi nimelazwa hapa muda na mimi kama mdau mkubwa wa Simba nimeumia mara baada ya kusikia msiba wa mchezaji wetu Mafisango na ndiyo maana nikaona ni bora nije walau nimuone ila nimeshuhudia maiti yake, Mungu amlaze mahali pema peponi,” alisema Maji Marefu, amen.

Hatuna cha kusema zaidi juu ya msiba huu, zaidi ya kutoa pole kwa familia ya Mafisango, klabu ya Simba na Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA).

Wote kwa pamoja tunawataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Mafisango mahali pema peponi. Amina.

Advertisements

One thought on “BURIANI PATRICK MUTESA MAFISANGO, UTAKUMBUKWA DAIMA NA WAPENDA SOKA WOTE WA TANZANIA NA AFRIKA KWA UJUMLA.

Comments are closed.