HALIMA MDEE; PROF. TIBAIJUKA ONYESHA UWEZO KWA VITENDO SI MANENO!

TAARIFA KWA UMMA

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (Chadema)

KWA nafasi yangu ya Uwaziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nimefarijika na kauli ya serikali iliyotolewa karibuni na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Prof. Anna Tibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi (Mazingira) Dkt. Terezya Huvisa kwamba nyumba zote zilizojengwa kando kando ya fukwe za bahari na mito zitabomolewa, bila wamiliki kulipwa fidia kutokana na kukiuka Sheria za Ardhi na Mazingira za mwaka 1992, 1995 na 2004.

Pamoja na kufarijika huko, nimelazimika kutoa taarifa hii kwa umma ili kuwakumbusha wahusika na hususan mawaziri husika sasa wathibitishe uwezo wao na dhamira zao kuwatumikia Watanzania kwa kuwajibika kwa vitendo. Si  kwa maneno.

Nasema haya kwa sababu imekuwa ni kawaida sasa kwa viongozi waandamizi serikalini kuwa ’wazuri’ wa kutoa matamko ya kisiasa, lakini wanapatwa na kigugumizi cha hali ya juu unapotakiwa utekelezaji wa vitendo!

Hii pia inachangiwa na ukweli kwamba vyombo vya dola vinavyopaswa kusimamia utekelezaji wa maagizo mbali mbali ya serikali kutawaliwa na rushwa na uzembe uliokithiri!

Ninayarejea haya kutaka tu kuukumbusha umma wa Watanzania ili wawe makini kufuatilia uwajibikaji wa serikali kwa wananchi.

Itakumbukwa kwamba kuwa chanzo cha matamshi hayo ya mawaziri, Prof. Tibaijuka na Dkt. Huvisa ni matokea ya ziara iliyofanywa na Waziri wa Ardhi, Jimbo la Kawe, Kinondoni, Dar es salaam.

Ziara ambayo ilishuhudia pasipo kificho, namna ambavyo watu wenye nguvu ya fedha wanadiriki kuharibu mazingira kwa makusudi pasipo kujali athari ambazo zinaweza kutokea sasa na baadae kwa wakazi wa maeneo jirani na Taifa kwa ujumla!

Ninasema kwa makusudi haya kwa kuwa baadhi ya majumba makubwa yaliyojengwa maeneo yasiyoruhusiwa tuliyoyatembelea, yanamilikiwa na viongozi wakubwa Serikalini.

Lakini pia kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Kawe kwa kushirikiana na NEMC, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Ole Medeye na maofisa wa ngazi za juu wa Wizara ya Ardhi na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa nyakati tofauti tulitembelea maeneo yanayotolewa maagizo sasa hivi yakiwa katika hatua ya awali ya ujenzi wa msingi!

Leo ni mengine ni majengo makubwa tayari!

Ndio maana nadiriki kusema yaliyozungumzwa na mawaziri hao sio mapya! Hata kidogo.

Nasisitiza tena, wawajibike kwa vitendo kwa kuchukua hatua ambazo ziko ndani ya uwezo wa serikali. Si maneno.

Nitatoa mifano michache, ambayo kama ingefanyiwa utekelezaji kama amri za serikali zilivyoelekeza hapo awali, ingetosha kuwa fundisho kwa wengine wote ambao wanadhani nguvu yao ya fedha inaweza kuwafanya wawe juu ya sheria na mstakabali wa Watanzania!

1. Mwaka jana 4/1/2011 Wizara ya Ardhi kupitia barua yenye kumbukumbu namba LD/297571/18 waliandika barua kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kuhusiana na uvamizi wa kiwanja namba 2019 na 2020  kilichoko Mbezi Kawe.

Katika barua hiyo pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba wizara imefanya ukaguzi katika viwanja Vilivyotajwa hapo juu baada ya kupata malalamiko juu ya uharibifu wa mazingira unaoendelea katika eneo hilo.

Barua husika inabainisha kwamba ukaguzi walioufanya umeonesha kuwa ujenzi unaofanyika katika eneo husika, ambalo kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (GN) No. 76 ya mwaka 1992 uendelezaji unaofanyika hauruhusiwi.

Kisha ilimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuchukua hatua za kubomoa/kuondoa uendelezaji batili unaofanyika katika viwanja Na 2019 na 2020 Mbezi Kawe.

Barua husika ilisainiwa na bwana Sadoth K. Kyaruzi, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara.

Tangu barua hiyo iandikwe na kuelekeza hatua zichukuliwe, leo mwaka 1 na miezi 5, hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa. 

Taarifa za uhakika na ukweli zilizopo, ni kwamba ubomoaji ulikwama mara kadhaa kwa sababu National Environment Management Council (NEMC) pamoja na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni walikosa ushirikiano kutoka Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni! 


Wasingeweza bomoa pasi na ulinzi! Kuna harufu ya Rushwa.

2. Nyaraka nyingine ni barua ya tarehe 30/9/2011 toka NEMC kwenda kwa Bwana Frank Mushi. 

Barua husika, ilitoa maelekezo kwa Bwana Mushi kuvirudisha katika hali yake ya kawaida, viwanja namba 2019-2020 kwa mujibu wa vifungu 55(2) (a) (e), (3) na 151 (1) ,(2) (a), (b), (3) ,(4) (b) na (f) vya Sheria ya Mazingira, sura 191 ya mwaka 2004. 

Barua husika inabainisha kwamba timu ya wataalam toka Baraza la Mazingira (NEMC), Wizara ya Maji, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam na Manispaa ya Kinondoni ilitembelea eneo husika kufuatia malalamiko kutoka kwa viongozi na wakazi wa Kawe Beach.

Timu hiyo ilibaini kwamba mto Ndumbwi, pamoja na bahari ilikuwa inajazwa mawe na vifusi hali iliyosababisha kupatikana kwa viwanja na 2019 na 2020.

Ambapo ndani ya viwanja hivyo lilikuwa linajengwa jumba kubwa kinyume kabisa na vifungu 55(2)(a) , 55(2) (b) , 55(2)(d) na 55(2)(e) vya Sheria ya Mazingira.

Pia ilibainika kwamba mikoko ilikatwa kinyume na s.63(1) ya Sheria ya Mazingira.

Kwa mujibu wa nyaraka nilizonazo, yafuatayo yalijitokeza

 i) Timu ya wataalam ilibaini kwamba, tayari Wizara ya Maliasili na Utalii ilishatoa zuio la ujenzi katika kiwanja husika.

 ii) Manispaa ya Kinondoni, mara kadhaa iliweka zuio la uendelezaji na kutoa amri kwa ’mmiliki’ wa eneo husika kubomoa, lakini mmiliki huyo alipuuza amri hiyo na kuendelea na ujenzi! Taarifa zilizopo Bwana Mushi yupo kama chambo. Nyuma yake kuna kiongozi mkubwa Serikalini. Ukifika wakati mwafaka tutamtaja. 


Hasa iwapo viongozi husika wataendelea ’kuwauzia’ wananchi maneno badala ya vitendo.

 iii) Ilitolewa amri ya Mahakama, tarehe 5/4/2011 kumtaka Bwana Mushi asiendelee na ujenzi. Bwana Mushi aliipuuza amri husika na kuendelea na ujenzi.

Baraza la Mazingira lilimwagiza tena, Bwana Mushi:-

  • Kuacha ujenzi mara moja
  • Kuvunja majengo yote yaliyoko kwenye viwanja vyenye mgogoro
  • Ndani ya siku saba, tokea amri husika kutolewa (amri ilitolewa 30/9/2011) awe ametoa mawe na vifusi vyote vilivyoharibu mkondo wa maji na bahari na kuurudisha mto na bahari katika hali yake ya kawaida.
  • Ndani ya siku 30 chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kwamba mikoko yote iliyokatwa imerudishwa katika hali iliyokuwa awali. Kwa gharama za Bwana Mushi.

Hakuna kitu chochote kilichofanyika! Ujenzi umeendelea, nyumba imekwisha, mto, bahari na mazingira kwa ujumla vimeharibiwa vibaya! Juu ya sheria. Juu ya maslahi ya wananchi wa eneo husika na Watanzania.

3. Nyaraka nyingine ni Taarifa ya Uchunguzi wa Mgogoro wa Ardhi na Mazingira katika eneo la Kawe Beach.

Taarifa hii ilitolewa na Ofisi ya Makamu wa Raisi, Agosti 2010 kufuatia kuundwa kwa kikosi kazi kuchunguza uhalali wa viwanja namba 1040, 1041, 2000, 2002 na 1071.

Chanzo cha mgogoro husika ni kubuniwa kwa viwanja vya nyongeza kando kando ya Mto Mbezi katika eneo linaloelekea baharini, hali inayopelekea maji ya mto kutuama na kuharibu mazingira na makazi ya wananchi walio jirani na eneo hilo!

Kamati ilifanya kazi yake na kutoa mapendekezo mazuri yenye lengo la kuokoa mazingira! Tangu mwaka 2010 hadi leo hakuna kilichofanyika!

Kitu kinachoshangaza na kusikitisha ni UJASIRI na WEPESI wa kutoa matamko, kuunda kamati au vikosi kazi, lakini vikosi kazi baada ya kufanya kazi yake, linapokuja suala la utekelezaji wahusika, wakiwemo mawaziri wanapatwa na vigugumizi.

Haijulikani wanakopata pia ujasiri wa kutoa visingizio wakati sheria ziko wazi.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mazingira, Sura 191 ya mwaka 2004, Fungu 57(1) hairuhusiwi kufanya shughuli zozote za kudumu za kibinadamu ndani ya mita 60 ambazo kwa asili yake zinaweza kuhatarisha au kuathiri vibaya ulinzi wa mazingira na utunzaji wa bahari au kingo za mto, bwawa au mwambao wa asili wa ziwa.

Halikadhalika, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 (Sura 113) Fungu 7 (1) (d) inabainisha kwamba eneo lolote lililo ndani ya mita 60 kutoka kingo ya mto na bahari linatakiwa kutangazwa kama ardhi hatari au kuhifadhiwa.

Pale inapotokea kuwa masharti ya Sheria moja yanapingana na Masharti ya Sheria ya Mazingira, kuhusu mambo yanayohusu usimamizi wa Mazingira, Sheria ya Mazingira ndiyo hutumika, kwa mujibu wa Fungu 232 la sheria ya mazingira sura 191 ya mwaka 2004.

Ndio maana nasisitiza! Hatuna haja ya kutoa matamko! Walio na mamlaka, waliokabidhiwa dhamana, sasa tufanye kazi kwa vitendo!

Haitoshi tu kutamka maneno makali ya kisiasa, wananchi wanataka kuona uwezo wenu dhahiri kwenye kuchukua hatua, tena zilizoko ndani ya uwezo wenu kisheria.

Si vinginevyo.

Nadhani ni wakati muafaka sasa kwa Waziri wa Ardhi , wakati akijiandaa kuvunja majumba yote yaliyojengwa ufukweni kufanya tathmini yale aliyokwisha yatolea matamko huko nyuma, yamefanikiwa kwa kiwango kipi!

Namkumbusha hili sambamba na ahadi zake kwa Watanzania za kurudisha viwanja vya wazi vyote vilivyovamiwa.

Zoezi ambalo limekuwa likienda kwa kusuasua sana!

Awaambie amefikia wapi au anakwamishwa na nini kilicho juu ya sheria na maslahi ya umma wa Watanzania.

Tunataka viongozi wa serikali waelewe kuwa Watanzania wamechoka na maneno na ahadi za kila siku ambazo hawaoni utekelezaji.

Wanataka ’kuuziwa’ matendo si maneno!


Halima Mdee (MB)

Waziri Kivuli, Wizara ya Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Advertisements

3 thoughts on “HALIMA MDEE; PROF. TIBAIJUKA ONYESHA UWEZO KWA VITENDO SI MANENO!

  1. Huku mbezi beach kwa Sykes kuna viwanja vinabuniwa kwa kukata mikoko na kujaza vifusi na kuziba bahari na mto Ndumbwi na hivi sasa nyumba zinajengwa kama uyoga; moja ya nyumba hizo inasemekana ni ya mbunge mama Lwakatare!!Sasa tuone kama serikali itakuwa na ubavu wa kulivunja hilo hekalu lililojengwa na kupandwa minazi inayotegemewa kuzaa baada ya kupandikizwa muda wa miezi mitatu!! Hiyo ndio jeuri ya pesa!!

  2. Sijui huyu mama Prof atasema nini, maana Dar imeharibika kwelikweli. Ukitoka mikoani, ukifika mbezi unasikia harufu mbaya kweli. Watu wamekaa katika hifadhi za serikali, bara bara hamna, zilizopo zinazibwa. waziri yupo tu. wajifunze kwa Magufuli. Yaani mimi sitaki kukaa Dar. Kutoka kona moja hadi nyingine masaa matatu. Uzalishaji mali utafanyikaje. Mvua zikinyesha, vifusi vichafu vinaelea barabarani. Hii wizara ngumu jamani.

    Halima Kaza buti, labda huyu mama prof ataamka, kutoka usingizi wa maneno matupu. Hayavunji mfupa.

Comments are closed.