NINI TUMEJIFUNZA KUTOKANA NA AJALI YA MV BUKOBA?

PICHA HALISI YA MV BUKOBA IKIZAMA

Mei 21, ya kila mwaka Watanzania Tunakumbuka kwa majonzi na simanzi kubwa ajali mbaya ya kuzama kwa meli ya Mv Bukoba iliyoangamiza maisha ya mamia ya wananchi Wengi

Mwaka 2012 imetimia miaka 16 tangu ajali hii mbaya kabisa kuwahi kutokea katika ziwa Viktoria huku ikikadiriwa watu zaidi ya 1000 walifariki dunia.

Tukio hili baya lililotokea kama sinema, kwa saa kadhaa huku likishuhudiwa na baadhi ya wakazi wanaoishi kandokando ya Ziwa Viktoria nje kidogo ya jiji la Mwanza.

Hakuna lugha nyepesi inayoweza kuelezwa kwa jinsi wengi wa Watanzania walivyoachwa midomo wazi kwa huzuni isiyomithilika, wengine wakibaki yatima kwa kupoteza wazazi wao wote.

Chanzo cha ajali ile iliyoangamiza maisha ya kundi zima la kaya, idadi kubwa ya wanafunzi wasichana wa Shule ya Sekondari ya Rugambwa waliokuwa wakirejea majumbani  kwao baada ya kuhitimu kidato cha sita, wanandoa wapya waliokuwa wakijiandaa kuanza maisha mapya, inaelezwa kuwa ni uzembe unaotokana na kujazwa kupita kiasi abiria na mizigo.

Inadaiwa kuwa meli hiyo ilikuwa na abiria mara mbili ya uwezo wake, kiasi kikubwa cha mizigo, lakini pia kukiwa na madai kuwa ilikuwa na hitilafu kubwa na iliishawahi kushauriwa kusimamisha kutoa huduma mpaka ifanyiwe marekebisho makubwa.

Wakati wa msiba huo wa kitaifa, viongozi karibu wote wa serikali, walisikika wakitoa hotuba nyingi za kuapiza kuwa wangelifanya hili ama lile na kwamba wale wote waliohusika na uzembe huo wangelichukuliwa hatua za kisheria.

Watanzania wakayapokea maneno hayo kwa faraja, lakini  Chonde Chonde mpaka leo hii hakuna lolote la maana lililofanyika, Likiwemo la kununua meli mpya, ahadi ambayo mwaka juzi ilirudiwa tena na mgombea wa CCM nafasi ya uraisi.

Inaumiza kwamba kwa uzembe wa hali ya juu, hakuna mkuu wa mkoa, wilaya, mkurugenzi wa shirika la reli, meneja, waziri wa uchukuzi na mawasiliano aliyeguswa na msiba huo kiasi cha kulazimika kujiuzulu.

Tulichoshuhudia ni kufikishwa mahakamani kwa aliyekuwa nahodha wa meli hiyo tu. Wengine wote wakabaki katika nafasi zao wakila mema ya nchi na familia zao.

Tunayo kila sababu ya kuamini kuwa huu ni uzembe mwingine wa serikali, kwa sababu licha ya kutochukuliwa kwa hatua zozote dhidi ya watendaji wa serikali, leo hii uzembe umeendelea kutokea na kusababisha vifo vya ajali chungu mzima. Tunajiuliza, tutavumilia hadi lini?Jipu limepasuka siwezi kuwa adui ya Mtu,Mungu awalaze Mahali pema peponi marehemu wote wa Mv Bukoba,Ameni 

    Imehaririwa na Chocks Chokala

Advertisements