WATANZANIA wengi wanadai kuchoshwa na vyombo vya sheria, wakidai kuwa vyombo hivyo avifanyi kazi yake na hivyo kuamua kujichukulia sheria mikononi kwa kuwadhibu wausika wenyewe.

Tabia hii ya Watanzania inaonekana kukithiri miongoni mwa jamii. Kutokana na hali hiyo sisi tunaona ipo haja kwa viongozi wa Serikali na wale wote wenye mamlaka katika jamii usika kuikemea.

Mfano mbaya wa tabia hiyo ni kisa cha hivi karibuni kilicho tokea ambapo watu watatu mkoani Arusha waliuawa na wananchi katika Mtaa wa Ngusero, Kata ya Sombetini kwa tuhuma za ujambazi.

Taharifa zinadai wananchi waliwaona watu hao wakizunguka zunguka katika mtaa huo usiku wa manane wakiwa ndani ya gari aina ya Toyota Mark II na kuwatilia shaka.

Inadaiwa baada ya kuwatilia shaka, wananchi hao waliamshana na kuwazingira watuhumiwa na walipofanya upekuzi waliwakuta na silaha za jadi ndani ya gari lao.

Baada ya kuwakuta na silaha hizo, wananchi hao waliamua kuwashambulia watuhumiwa hao watatu kwa kutumia silaha mbalimbali na kuwasababishia vifo vyao.

Pamoja na Polisi kudai kuwa waliouawa walikuwa wakitafutwa kwa tuhuma za ujambazi, lakini hiyo haihalalishi kuuawa kwa watuhumiwa hao.

Kwani pia inawezekana kabisa katika gari hilo alikuwepo mtu mwingine asiyehusika na akaadhibiwa au kuuawa.

Mbali na uwezekano wa kumuadhibu au kumuua asiye na kosa, lakini pia mauaji hayo yameikosesha Polisi ushahidi wa matukio ya ujambazi na kupoteza vielelezo vya kuwanasa wengine kama wapo.

Tunakemea tabia hiyo kwa kuwa si ya jamii iliyostaarabika, inaweza kuwatia hatiani wasio na kosa lakini pia inazuia uwezekano wa kukomesha matukio ya ujambazi, kwani kwa maamuzi hayo ya wananchi Polisi wanapotezewa vyanzo vya taarifa muhimu.

Tunasema hivyo kwa kuwa kama watuhumiwa hao walikuwa na wenzao ambao wamekuwa wakishirikiana katika uhalifu, kuna uwezekano wangewataja wenzao na kuiwezesha Polisi kunasa na kuutokomeza mtandao wa majambazi.

Lakini kwa kuwaua, wananchi hawajasaidia chochote katika kupunguza au kuzuia uhalifu, badala yake wameshiriki kuzuia Sheria isichukue mkondo wake na kuzuia Polisi kukamata mtandao wa wahalifu na kuukomesha.

Wakati umefika kwa Serikali kuchukua hatua kali zaidi dhidi ya watu wanaobainika kujichukulia sheria mkononi ili tabia hiyo iondoke nchini.

Lakini pia viongozi katika jamii kuanzia wa kisiasa, kijamii na hasa wa dini ambao wanaaminiwa zaidi, wanapaswa kusaidia kuhamasisha jamii kuacha kuchukua sheria mkononi dhidi ya watuhumiwa wa uhalifu.

Tena kwa viongozi wa dini itakuwa rahisi zaidi kwa kuwa dini karibu zote zinakataza kuua, watakuwa wanatimiza wajibu wao wa kukemea maovu kwa kuwa katika tabia hii ya kujichukulia sheria mkononi, kuna uwezekano wa watu wasio na hatia kuadhibiwa na hata kuuawa.

Mbaya zaidi tabia hii ya kujichukulia sheria mkononi imekuwa haitendi haki kwa kutoa adhabu kulingana na kosa la mtu badala yake imekuwa ikisababisha watuhumiwa kupewa adhabu ambazo hawastahili.

Advertisements