BAJETI YA SERIKALI 2012/13 KUYAFANYA MAISHA YA MTANZANIA KUZIDI KUWA DUNI.

 • KODI ZA VINYWAJI BARIDI, BIA, SIGARA, SIMU JUU

 • BAJETI BADO NI NGUMU KWA MTANZANIA KUTOKANA NA SERIKALI KUONGEZA GARAMA ZISIZO ZA LAZIMA KAMA KUONGEZA WILAYA NA MIKOA; PROFESA LIPUMBA.

 • MBOWE ASEMA TUSITEGEME CHOCHOTE KWANI HAKUNA MPANGO WOWOTE WA KUPUNGUZA MAKALI YA MAISHA KWA MTANZANIA.

 • FLORIAN MAGOGO, AMESIKITISHWA NA HATUA YA SERIKALI KUONGEZA KODI KATIKA MISHAHARA NA KUDAI HILO LITAONGEZA UGUMU WA MAISHA YA WAFANYAKAZI.

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Dk. William Mgimwa, Alhamisi 14 Juni 2012 alitangaza bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2012/13, ambayo imeongeza kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi pamoja na bidhaa mbalimbali.

Katika hotuba yake iliyochukua saa 2:30; tangu saa 10:00 jioni hadi saa 12:30, Waziri Mgimwa alisema kodi ya mishahara ya wafanyakazi itatozwa kulingana na ongezeko la mshahara wa mfanyakazi. Hata hivyo, hakuweka wazi kiwango cha chini cha kodi kilichoongezwa.

Bajeti hiyo ya sh trilioni 15 imeonesha kuwa kufanikiwa kwa shughuli za maendeleo ya nchi zitategemea zaidi misaada ya wafadhili na marafiki wa nje, ambao sasa watahitaji kuisaidia serikali kwa zaidi ya nusu ya fedha zilizotengwa kwa mwaka ujao wa fedha.

Akiwasilisha hotuba hiyo kwa mara ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo, Waziri Mgimwa alitaja ongezeko la kodi katika bidhaa kadhaa za ndani na nje, muda wa maongezi wa simu za mkononi pamoja na kuongezwa kwa kodi katika mishahara ya wafanyakazi wa serikali na sekta binafsi.

Aidha, bajeti hiyo haikuwaacha nyuma wafanyabiashara wadogowadogo, ambao sasa watalazimika kulipa kodi ya mapato kati ya sh 100,000 hadi sh 575,000.

Pamoja na kuongezwa kwa viwango hivyo vya kodi, serikali imetangaza kutoza kodi katika bidhaa za muziki, filamu na mikanda ya video (DVD, VCD, CD).

Kodi nyingine zimeongezwa katika juisi ya matunda zinazozalishwa hapa nchini kwa sh 8 kwa lita, wakati zile zinazotoka nje ya nchi zitatozwa sh 83 na kwamba mabadiliko haya yamekusudia kuondoa ushindani usio wa haki.

Vinywaji baridi vimeongezeka kodi kutoka sh 69 hadi sh 83, mvinyo wa zabibu kutoka nje ya nchi unaongezeka kodi kutoka sh 1,345 hadi sh 1,614 kwa lita.

Navyo vinywaji vikali kodi yake imepanda kutoka sh 1,993 hadi sh 2,392 kwa lita, wakati bia ya hapa nchini imepanda kutoka sh 248 hadi sh 310 kwa lita huku zile za nje sasa zitatozwa kodi ya sh 525 badala ya sh 420.

Kwa upande wa sigara zisizo na vichungi, kodi yake imepanda kutoka sh 6,820 hadi sh 8,210 kwa sigara 1,000 wakati zile zenye vichungi zilizotengenezwa na tumbaku ya hapa nchini, sasa zitatozwa kodi ya sh 16,114 hadi sh 19,410, sigara zenye sifa mbali na hizo zitatozwa kodi ya sh 35,117.

Vitu vingine vilivyoongezewa kodi ni pamoja na michezo ya kasino na ile ya kubahatisha kutoka asilimia 13 hadi 15, michezo ya utabiri wa matokeo ya michezo kwa asilimia sita na asilimia 43 kwenye michezo ya bahati nasibu kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu.

Aidha, serikali pia imeamua kuanzisha utozaji wa ada kwa wamiliki wa magari ambao watataka kusajili namba zenye utambulisho maalumu kwa ada ya sh milioni tano kwa kila miaka mitatu.

Kodi nyingine zilizoongezeka ni za viwanja vya ndege kutoka kiwango cha sasa cha dola 30 hadi 40 kwa safari za nje ya nchi na sh 5,000 hadi sh 10,000 kwa safari za ndani.

Watumiaji wa simu za mkononi sasa watalazimika kulipa kodi ya asilimia 12 badala ya asilimia 10.

Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF, Ibrahim Lipumba, wameielezea bajeti hii kuwa ni mzigo mkubwa na haikulenga kumkomboa Mtanzania.

Profesa Lipumba alisema kuwa inasikitisha kuona serikali inaweka kiwango kikubwa cha bajeti katika matumizi ya kawaida badala ya kutenga fedha nyingi katika mambo ya kimaendeleo.

Alisema bajeti bado ni ngumu kwa maisha ya Mtanzania kutokana na serikali kuongeza majukumu lukuki kwa kuongeza wilaya na mikoa.

Mbowe kwa upande wake alisema bajeti hii itaendelea kumuumiza Mtanzania kwani serikali haijaweka mikakati yoyote ya kuonyesha ni jinsi gani itapunguza makali ya maisha kwa Mtanzania.

Mbali na hilo alisema kuwa shida iliyopo ni kuwa serikali imategemea fedha nyingi kutoka kwa wahisani badala ya kutumia vyanzo vyake vya ndani jambo ambalo alisema limetokana na kukosekana kwa mipango bora.

Alisema serikali imekuwa kila mwaka inaongeza ushuru katika tumbaku na vinywaji kana kwamba hakuna vyanzo vingine vya mapato kama vile madini pamoja na rasilimali mbalimbali zilizopo nchini.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Uchumi, alisema bajeti hiyo itamkomboa tu Mtanzania anayeishi mjini wakati wale wa vijijini hawawezi kunufaika kwa jambo lolote.

Hata hivyo Zitto alisema amefurahishwa na jinsi serikali ilivyoweza kuthibiti kazi za wasanii ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele kwa muda mrefu na wabunge wa upinzani.

Naye Florian Magogo ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), alisema amesikitishwa na hatua ya serikali kuongeza kodi katika mishahara ya wafanyakazi na kudai kuwa huko ni kuwakandamiza na kuwaongezea ugumu wa maisha wafanyakazi.

“Hali ya maisha ni ngumu sana hivi sasa, mimi binafsi nilitegemea serikali itatusaidia wafanyakazi na kutupunguzia kodi na badala yake inaongeza kodi huko ni kutunyanyasa, ukizingatia mishahara yenyewe ni midogo,” alisema Magogo.

Pia alionyesha kutoridhishwa na hatua ya serikali kuweka bajeti ndogo katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji ambayo asilimia 90 ya Watanzania inazitegemea katika kuingiza kipato kupitia sekta hizo.

Alisema katika eneo hilo bajeti haijawa sawa kwani  ilipaswa kuongeza zaidi bajeti ili kuboresha sekta hizo.

Kwa upande wake, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Benno Ndullu, alisema mwelekeo wa bajeti hiyo utatoa nafasi kwa serikali kupunguza utegemezi wa bajeti kutoka kwa wahisani.

“Wapo watu watakaosema lakini kwa mwelekeo huu naamini tutapunguza utegemezi badala ya kutegemea wafadhili kwa asilimia 50 sasa tutawategemea kwa asilimia 30 kwenye bajeti nzima,” alisema Gavana Ndullu.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema kutoza kodi katika pombe kila mwaka ni uduni wa kufikiri kwa watendaji wa serikali.

“Serikali ni bingwa wa kuwakamua wafanyakazi, yaani kodi kubwa katika mishahara… kama hali ikienda hivi ilivyo mwaka 2015 bajeti itafikia sh trilioni 50 jambo ambalo ni hatari kwa uchumi,” alisema Kibamba na kuhoji sababu za serikali kushindwa kubuni vyanzo vipya vya mapato.

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratian Mkoba, alisema bajeti hiyo haikidhi mahitaji ya walimu na kuongeza kwamba serikali inadharau sekta ya elimu kwa kuitengea fedha kidogo kulingana na umuhimu wake.

“Bajeti kupangwa na kusomwa ni kitu kimoja utekelezaji ni kitu kingine, kila mwaka wanatupa makaratasi kwamba hela fulani itakwenda kwenye eneo fulani lakini pesa inayopatikana ni kidogo ambazo huliwa na wajanja wachache.

“Tusubiri japo imejaribu kuja na vyanzo vipya lakini siamini sana… serikali inafanya mzaha na sekta ya elimu nchini, nashauri fedha kidogo zilizotengwa zisiwekwe mikononi,” Mukoba.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Ukimwi nchini (AJAAT), Simon Kivamwo, alieleza kufurahishwa na hatua ya serikali kurejesha mafunzo ya kijeshi.

Alisema amefurahishwa na hatua hiyo hasa baada ya kusikia kwamba vijana wapatao 5,000 wataingia jeshini katika awamu ya kwanza ya mpango huo.

“…Naona kijamii itarejesha moyo wa kujituma miongoni mwa vijana wetu ambao siku hizi wanakuwa wabishi, wasiojua kujituma au kujitolea/kwa ajili ya kulitumikia taifa,” alisema Kivamwo ambaye alipitia mafunzo hayo.

Naye Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy, aliisifu bajeti hiyo akisema ni ya matumaini kwa Watanzania.

“Bajeti ni ya matumaini kwa Watanzania. Changamoto ni kukusanya mapato. Kuondolewa ushuru kwenye ving’amuzi kutasaidia uendaji wa digitali ufanikiwe,” alisema Mungy.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Hebron Mwakagenda, alisema kuwa, katika bajeti iliyosomwa hakuna kitu kipya, bali waliyoyaeleza ni yale yale yaliyozoeleka.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino, Profesa Mwesiga Baregu, alisema amefuatilia bajeti kwa umakini lakini ameona kuwa kuna matatizo makubwa katika kuzikabili changamoto zilizopo.

Baregu alisema bajeti imesomwa bila kulenga na kuweka vipaumbele vya changamoto vinavyolikabili taifa huku akitaja kuwa ni pamoja na ajira na mfumuko wa bei uliosababisha ukuaji wa uchumi kuzorota.

Naye Mratibu wa Habari sera na Utetezi wa Chama cha Uzalishaji na Maendeleo nchini (TAMADA), Godfrey Dhahabu, alisema bajeti si mbaya, mwelekeo wake ni mzuri hasa kwenye kilimo lakini tatizo litakuwa kwenye utekelezaji.

Advertisements

7 thoughts on “BAJETI YA SERIKALI 2012/13 KUYAFANYA MAISHA YA MTANZANIA KUZIDI KUWA DUNI.

 1. Huu ulimbukeni unaelekea kuua Taifa kwa mtindo huu.
  Ya mwaka ujao tusishangae, ikija na style ya vyangu doa na mashoga kupewa lesini na kulipia kodi.
  Eeh! Mungu ni chukue mapema kabla maandiko hayajatimia..

 2. Yaani serikali inaintroduce plate no zenye majina ya watu lengo ni kukusanya 50mil!
  Mgimwa give me a break ivi hawa watu wa migodini mnawaogopa ni miungu watu?

 3. hii budget itawaletea matatizo CCM. Watakuza uchumi toka 6.4% to 6.8%! (0.4% increament!). Put that into practice, kama sasa hivi watu wanabaingaiza na uchumi ni 6.4% ukiongoza 0.4% watapata nafuu kiasi gani?

  Now, angalia kwenye misamaha ya kodi, sioni jambo tofauti sana, but I’m smelling blood.

 4. Nimuombe Mzee Edwin Mtei, Salaam sana mzee wetu, Hii budget ni Pro-rich. Tafadhali saidia vijana upande wa pili (CDM) ili waje na Pro-Poor budget.

  Kilimo/food security
  1. Kuwepo na target kwamba tunataka kupata kiasi gani cha chakula, then split that kwenye maeneo/mikoa ambayo ni more attractive kufikicha malengo (multipliying effect kwanza). Sasa ukishakuwa na target, area,then weka mabwana shamba sawa na uwape challenge/task ya kusimamia na kila mmoja kwenye eneo lake ili by the end of the day ijulikane tunataka kupata how much, na nani anasimamia nini na wapi.

  2. Mikopo ya Kilimo inayotolewa na TIB ni utani maana TIB iko Dar. Kuna wakulima gani Dar. Kama kuna ulazima sana kwamba lazima TIB wapate chunk ya fungo hilo la kilimo basi waandae utaratibu mwingine kwa kushirikiana na bank nyingine hasa NMB na CRDB. Na pia ikiwezekana wawashirikishe vyama vya ushirika.

 5. WAFANYAKAZI BAJETI HII NI TATIZO KWETU. JE, TUKITAFUTA KAZI NJE YA NCHI KWANI KUNA NINI? KWA NINI KUKAA TUKIGOMBANA NA HAWA WATU AMBAO HAWATUJALI? TUCHUKUE PASSPORT ZETU TUANJE SAFARI.

 6. Madini, utalii, uvuvi, kilimo kwa bajeti hii si vyanzo vya kutuwezesha kuendesha nchi. Pombe, sigara, kumnyang’anya mfanyakazi pesa zake(yaaani udanganye kuwa umempa halafu uzichukue), ndizo pekee zaweza kuiongoza nchi hii. MAWAZIRI NA WABUNGE MNALIPA KODI KWENYE MISHAHARA YENU? MMESHACHANGIA KWA KIASI GANI?

Comments are closed.