WABUNGE WACHARUKA NA KUAFIKIANA KUICHACHAFYA HOTUBA YA BAJETI BILA KUJALI ITIKADI.

MJADALA mzito wa bajeti ya serikali ya mwaka 2012/2013 iliyowasilishwa Alhamisi Juni 14, 2012 utaanza Jumatatu Juni 18 2012, huku kambi ya upinzania bungeni ikipewa nafasi ya kwanza kujadiri pale itakapowasilisha hotuba ya bajeti mbadala ya fedha.

Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya kambi ya upinzani inayoundwa na wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), zinasema kuwa hotuba hiyo mbadala ya bajeti, itakayosomwa inatarajiwa kuwa chachu ya kuwashawishi hata wabunge wengine ambao wamekuwa wakiitetea ile ya serikali.

Kwa mujibu wa habari hizo, bajeti ya kambi ya upinzani imeandaliwa na jopo la wachumi na wataalamu ambao ni wanachama wa chama hicho, na ripoti sahihi za wasomi waliobobea katika nyanja na sekta zote muhimu zikiwemo za madini, kilimo, miundombinu, elimu, afya katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

Imedaiwa kuwa bajeti hiyo, itajikita katika kuibua udhaifu wa serikali, ikiwemo hoja za matumizi ya fedha ambazo zilitolewa kwa zaidi ya miaka mitano katika miradi ambayo baadhi yake haijakamilika na mingine haipo, lakini kila mwaka inatengewa fedha.

SEMINA YA POLICY FORUM

Wakati hali ikiwa hivyo, semina iliyofanyika Jumapili Juni 17, 2012 iliyoandaliwa na Taasisi ya Policy Forum, hiliibuwa hasira kwa wabunge walio udhulia na kuwafanya kucharuka na kuafikiana kuichachafya hotuba ya bajeti bila kujali tofauti za kiitikadi, baada ya kuelezwa namna serikali inavyopoteza fedha kizembe.

Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) aliweka wazi jinsi makampuni ya madini yanavyoongoza kwa kuliibia taifa, kiasi cha kuifanya sekta hiyo ishindwe kuchangia kikamilifu pato la taifa.

Alisema inashangaza sana kuona kuwa kiwanda cha bia kama Serengeti na kile cha sigara ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa 15 wakati kampuni kama Baricck ikiwa haimo.

Kafulila alinukuliwa akisema, ikiwa CCM italazimisha kupitisha bajeti hii kwa vitisho, itakuwa imejimaliza kwa sababu Watanzania wa sasa si wale wa juzi.

“Sioni pa kukwepa, Na kama kuna mbunge anataka kuendelea na ubunge wake hata akiwa ndani ya CCM, akubali kufia wapiga kura wake. Najua wengi wanaipinga na wengi wameniambia hivyo,” alisema.

Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Kessy Mohamed (CCM) mbali na kuonesha masikitiko yake kwa namna bajeti ilivyo, aliwataka wabunge kuwa makini katika masuala muhimu ya nchi.

Kessy alisema serikali imewaacha watu wakizurura ovyo, na kujiingiza katika biashara zisizozalisha, hivyo kusababisha kupanda kwa bidhaa muhimu nchini.

Katika hatua inayoonesha kuwa serikali itakuwa katika wakati mgumu bungeni, Waziri kivuli wa Fedha, Kabwe Zitto ameeleza wazi msimamo wa CHADEMA, kuwa wanaipinga bajeti hiyo kutokana na ukweli kuwa haimlengi Mtanzania wa kawaida bali imelenga kuwanufaisha wachache.

Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alitoa msimamo huo Jumamosi Juni 16, 2012 wakati akiwahutubia wananchi wa Kata ya Kihesa mjini Iringa.

Alisema kuwa, umasikini wa watu unasababishwa na mfumuko wa bei za vyakula, huku serikali ikishindwa kudhibiti hali hiyo inayoendelea kuwaumiza.

“Mfumuko wa bei umefikia asilimia 18.7 ambacho ni kiwango kikubwa sana kwa maisha ya Mtanzania ambaye anatumia asilimia nane kununua chakula na kipato chake kinazidi kushuka siku hadi siku badala ya kupanda kutokana na rasilimali zilizopo,” alisema Zitto.

Alifafanua kuwa, mfumuko wa bei za vyakula pekee umefikia asilimia 25 na ule wa bei ya nishati ukiwa kwenye asilimi 28 huku deni la taifa likizidi kukua kila siku.

Advertisements