SERIKALI YA CHADEMA INGEKUWA MADARAKANI BAJETI YAKE INGEBORESHA MAISHA YA MTANZANIA WA CHINI; ZITTO

  • WAZIRI KIVULI WA FEDHA NA UCHUMI, ZITTO ZUBERI KABWE

    KAMBI HIYO IMEPINGA NYONGEZA YA ASILIMIA MBILI KATIKA MUDA WA MAONGEZI YA SIMU.

  • YATOA MBINU MBADALA KWA SERIKALI YA KUONGEZWA MAPATO YA SERIKALI KWA SH2.885 TRILIONI.

  • TUCHUKUE MIKOPO KUWEKEZA KWENYE MIRADI ITAKAYOKUZA UCHUMI NA KUZALISHA KODI ZAIDI SI KWA AJILI YA MATUMIZI YA KAWAIDA NA POSHO.

  • YASHAURI UWEKEZAJI UFANYIKE KWA WATU WA VIJIJINI ILI WAONGEZE UZALISHAJI, HUO NDIYO MWALABAINI WA MFUMUKO WA BEI.

WAZIRI Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe Jumatatu June 18 2012 aliwasilisha bungeni bajeti mbadala ya Kambi ya Upinzani kwa mwaka wa fedha 2012/2013, huku akibainisha kasoro lukuki katika bajeti ya Serikali.

Pamoja na kupendekeza njia kadhaa za kupanua wigo wa mapato ya Serikali, wapinzani wametaka kufanywa kwa ukaguzi wa deni la taifa, ili kubaini chanzo cha Serikali kukopa na kuweka wazi jinsi fedha hizo zilivyotumika hadi kufikia Sh22 trilioni.

“Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaonyesha kuwa Deni la Taifa linazidi kuongezeka kwa asilimia 38 kutoka Sh10.5 trilioni mwaka 2009/2010 hadi Sh14.4 trilioni 2010/2011. Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Deni la Taifa limefikia Sh20.3 trilioni mpaka ilipofika mwezi Machi mwaka 2012,”alisema Zitto na kuongeza:

“Ukisoma taarifa ya Mwezi wa Mei 2012 ya Benki Kuu ya Tanzania, Deni la Taifa sasa limefikia Sh22 trillion. Suala hapa sio ustahmilivu wa Deni kama inavyodai Serikali, bali ni kwamba tunakopa kufanyia nini?”

Alisema hesabu za bajeti ya Serikali ya 2012/13 inayopendekezwa zinaonyesha kwamba Serikali bado ina mpango wa kukopa kwa ajili ya kugharamia matumizi ya kawaida ambayo hayazalishi wala kutozwa kodi.

“Hatutaki mikopo kwa ajili ya matumizi ya kawaida ya posho, kusafiri, magari n.k. Tuchukue mikopo kuwekeza kwenye miradi itakayokuza uchumi na kuzalisha kodi zaidi,” alisema.

Zitto ambaye pia ni Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni katika hotuba yake alisema mapato ya Serikali yanaweza kuongezwa kwa Sh2.885 trilioni, hivyo kupunguza utegemezi wa mikopo ya kibiashara ambayo imekuwa ikiligharimu taifa kiasi kikubwa cha fedha.

Kuhusu mfumuko wa bei, Zitto alikosoa hatua zinazopendekezwa na Serikali kukabiliana nao, kwamba ni zile zilizoshindwa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, mwaka huu.

Alisema hatua hizo ambazo ni kutoa vibali kwa wafanyabiashara vya kuagiza mchele na sukari bila kutoza kodi, haziwezi kusaidia kwa kuwa hatua kama hizo zilipochukuliwa awali zilisababisha bei ya bidhaa hizo kuongezeka.

“Baada ya hatua hii bei ya sukari ilipanda kutoka Sh1,700 mpaka 2,800 kwenye maeneo mengi nchini… Serikali inachukua hatua zile zile kwa tatizo lile lile ikitegemea matokeo tofauti,” alisema Zitto.

Alirejea pendekezo la mwaka jana kwa Serikali kutoa vivutio kwa wakulima wadogo kuzalisha chakula kwa wingi akisema kuwa hatua hiyo pekee ndiyo itapunguza mfumuko wa bei.

“Hakuna mbadala wa kudhibiti mfumuko wa bei zaidi ya kuongeza uzalishaji wa chakula na kuwekeza kwa wananchi wetu. Serikali inafikiria uzalishaji utaongezeka kwa kusaidia wakulima wakubwa ambao watageuza wananchi wetu kuwa manamba na vibarua ndani ya nchi yao,” alisema na kuongeza:

“Tuwekeze kwa watu wetu vijijini ili waongeze uzalishaji na kwa kufanya hivyo mfumuko wa bei ya chakula utakuwa historia. Hakuna mwarobaini wa kupanda kwa bei za vyakula isipokuwa kilimo”.

Katika hatua nyingine, kambi hiyo imepinga pendekezo la nyongeza ya asilimia mbili katika muda wa maongezi ya simu kwa maelezo kwamba hatua hiyo itamkadamiza mwananchi wa kawaida, kwa kuwa itaongeza gharama za simu.

“Hoja ya wananchi hapa ni kwamba Kampuni za Simu za mkononi hazilipi kodi ya kutosha na hasa Kodi ya Makampuni (corporate tax). Kampuni za simu zinapaswa kulipa kodi ya mapato na sio kukandamiza wateja kwa ushuru wa bidhaa, ilihali huduma zenyewe za simu hazina ubora,” alisema.

“Waziri Mkuu alipokuwa anafunga Bunge la Bajeti mwaka 2011 alitangaza kampuni ambazo ni walipa kodi wakubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Katika orodha hiyo kulikuwa na kampuni moja tu ya simu za mkononi, AirTel.”

Bajeti ya Zitto ilitanguliwa na hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Rais – Mipango, Christina Mughwai ambaye pia aliweka wazi kile alichokiita udhaifu wa Serikali katika kuitekeleza mipango yake ya kiuchumi, hali ambayo inasababisha umaskini kwa wananchi.

Hotuba zote mbili, ya Zitto na Mughwai, zilisema licha ya Serikali kutangaza kwamba bajeti ya 2011/12 ilikuwa ya kupunguza makali ya maisha, hakukuwa na nafuu yoyote kwa wananchi kwani maisha yameendelea kupanda.

Kwa upande wake Christina Mughwai alibainisha kuwapo kwa mkanganyiko katika hotuba ya Serikali ya hali ya uchumi na mipango ya maendeleo, jambo ambalo alisema ni aibu kwa Serikali.

Alisema wakati Serikali inasema kwamba ukuaji usioridhisha wa Pato la Taifa unatokana na ukame ulioathiri Sekta ya Kilimo, kwa upande mwingine katika kitabu hicho hicho inasema kwamba uzalishaji wa mazao ya chakula hususani ngano, mihogo, maharage, ndizi na viazi uliongezeka ikilinganishwa na mwaka 2010 kutokana na hali nzuri ya hewa na mtawanyiko mzuri wa mvua kwa ustawi wa mazao.

“Mkanganyiko huu ni dalili ya ukosefu wa umakini katika kuandaa taarifa muhimu za Serikali na unaitia Serikali hii aibu,” alisema mbunge huyo wa Viti Maalum (Chadema).

Alisema kuongezeka kwa mfumuko wa bei hadi kufikia asilimia 19.2 Novemba mwaka jana kulipunguza uwezo wa Serikali kununua bidhaa na huduma kwa takribani asilimia 6.

“Hii ni sawa na Sh780 bilioni kuyeyuka katika Bajeti katika kipindi cha miezi minne tu ya utekelezaji wa wake,” alisema. 

Alisema kasi ya ukuaji wa mfumuko wa bei ni dhahiri kwamba, sehemu kubwa ya bajeti hasa ya maendeleo ilishindwa kutekelezeka.

Msemaji huyo alibainisha kuwa hali ni mbaya zaidi kwa wananchi kutokana na mfumuko wa bei za vyakula ambao kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ulifikia asilimia 24.7 Novemba mwaka jana.

“Ukilinganisha na bei za vyakula mwaka 2010, mwananchi amepoteza uwezo wa kununua chakula kwa zaidi ya robo kati ya Novemba 2010 na Novemba 2011. Jumla ya vyakula ambavyo mwananchi alinunua kwa Sh10,000 mwaka 2010, sasa atanunua kiwango kile kile kwa Sh12,500,” alisema.

Kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, alisema imeendelea kushuka ukilinganisha na fedha za kigeni kutokana na kutokuwapo kwa mikakati thabiti ya kuihimarisha.

“kushuka kwa thamani ya shilingi licha ya kupanga kwa mauzo yetu nje kwa sekta zote mbili tunazotegemea sana (madini na utalii) kuanaacha maswali mengi kuhususiana na chaguo letu kuhusu hifadhi ya fedha za Kigeni,” alisema Mughwai.

Zitto alisema kama wapinzani wangekuwa madarakani wangekusanya kiasi cha Sh15 bilioni sawa na ile ya Serikali, lakini tofauti ni hatua ya kutenga asilimia 35 ya mapato ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi wa bajeti kutoka asilimia 42.37 za Serikali hadi asilimia 21.3.

Advertisements