NI DHAHIRI BILA MABADILIKO MAKUBWA BAJETI YA 2012 / 2013 KUKWAMA

  • WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA

    • AUNDA KAMATI NYINGINE, SASA KAMATI ZA FIKA TATU.

    • LUKUVI AKIRI KUUNDWA KWA KAMATI HIZO NA KUSEMA NI UTARATIBU WA KAWAIDA.

    • WAJUMBE WANAOUNDA KAMATI HIYO NI DK. MGIMWA, LUKUVI, SITTA, JANUARY MAKAMBA, MALIMA NA AME SILIMA.

    • BAADHI YA KODI KUFUTWA  IKIWEMO ILE YA MAONGEZI YA SIMU NA WAENDESHA PIKIPIKI BODABODA.

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameunda Kamati Maalum ya mawaziri sita kusaidia mchakato wa marekebisho ya Bajeti ya Serikali ambayo mjadala wake utahitimishwa Ijumaa June 22, 2012.

Habari ambazo zimepatikana zinasema kwamba kamati hiyo itafanya kazi ya kubuni vyanzo vingine vya mapato ya Serikali, ili kufidia pengo la baadhi ya kodi ambazo zinatarajiwa kufutwa kutokana na shinikizo la wabunge

Wajumbe wanaounda kamati hiyo ambayo ilifanya kikao chake cha kwanza Jumanne June 19, 2012 ni Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Mgimwa, Lukuvi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Wengine katika kamati hiyo iliyoundwa kwenye kikao cha kazi cha Baraza la Mawaziri, Jumamosi June 16, 2012 chini ya Pinda, ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Naibu Waziri wa Chakula, Kilimo na Ushirika, Adam Malima na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alikiri kuundwa kwa kamati hiyo, lakini akakataa kutoa taarifa za kina kuhusu suala hilo kwa maelezo kwamba huo ni utendaji wa kawaida wa shughuli za Serikali.

Kuundwa kwa kamati hiyo kunazifanya kamati zinazoifanyia kazi Bajeti ya 2012/2013 kufikia tatu.

Ijumaa June 15, 2012 wabunge wa CCM waliunda kamati ndogo kwa ajili ya kusaidi pamoja na mambo mengine kuangalia vyanzo vingine vya mapato na kuona iwapo bajeti ya maendeleo inaweza kuongezwa, kukidhi kiu ya wabunge.

Kamati nyingine ni ile ya Fedha na Uchumi ya Bunge ambayo tayari imetoa maoni yake bungeni kuhusu Bajeti, lakini ikabainisha kuwapo kwa kasoro kadhaa ambazo zinapaswa kurekebishwa.

“Sidhani kama hiyo ni habari kubwa ya kwenda public (kwa umma). Kwanza siyo kamati ya mawaziri, haiwezi kuwa hivyo, na huo ni utendaji wa kawaida wa ndani ya Serikali maana sisi tuna mambo mengi tunafanya,” alisema Lukuvi na Kuongeza:

“Kamati za utekelezaji wa shughuli za Serikali ziko nyingi sana na siyo tu za Bajeti. Kwa hiyo ndio maana nakwambia hilo ni jambo dogo sana ambalo mimi sidhani kama linahitaji kutangazwa, kama lingekuwa hivyo mimi ningekuwa wa kwanza kutaka kulizungumzia,” alisema.

Miongoni mwa kodi hizo ambazo huenda zikafutwa wakati Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa atakapohitimisha Bajeti yake Kesho, ni ile inayopendekezwa kuongezwa kwenye muda wa maongezi ya simu na ile ya waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda.

Kadhalika, kamati hiyo ya mawaziri imepewa jukumu la kuona iwapo itaweza kushauri uwezekano wa kuongezwa Bajeti ya sasa ya maendeleo kutoka asilimia 30 inayopendekezwa na Serikali, jambo ambalo pia limekuwa likipigiwa kelele na wabunge wengi.

“Hatuwezi kufumua Bajeti nzima ila Kusema kweli ni kwamba lazima kutakuwa na mabadiliko mengi, tatizo kubwa ambalo linatuumiza vichwa, tunajiuliza kama tunaweza kupata hiyo nyongeza ya hizo nyongeza ya hizo fedha za maendeleo walau Sh 500 bilioni,” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.

Wasiwasi ulikuwa ni iwapo ushauri wa kamati hiyo utaweza kuzingatiwa katika majumuisho ya Waziri wa Fedha na Uchumi wakati atakapohitimisha Bajeti yake, lakini Jumatano June 20, 2012 Spika wa Bunge, Anne Makinda alifungua milango inayowezesha Serikali kuongeza vyanzo vipya vya mapato hata baada ya Bajeti Kuu kupitishwa.

Hatua hiyo ni dalili kwamba Serikali sasa iko tayari kufanya marekebisho makubwa ya Bajeti yake na hata zile za kisekta, hasa katika maeneo ya kuongeza vyanzo vipya vya mapato kadri Kamati za Bunge, wabunge na Kambi ya Upinzani watakavyopendekeza.

Kusogezwa huko pia kumewezesha kuongezwa siku moja ya majadiliano ya hotuba ya Bajeti kutoka siku nne hadi tano, pia unatoa fursa ya Serikali kuongeza vyanzo vyake vya mapato kwa kuzingatia maoni, mawazo na ushauri wa wabunge.

Muswada wa Sheria ya Fedha ulikuwa umepangwa kuwasilishwa Ijumaa June 22, 2012 kama hitimisho la mjadala wa Bajeti ya Serikali, lakini sasa umepelekwa mbele kutokana na kile Makinda alichosema kuwa ni kutoa fursa kwa wabunge kuishauri Serikali kuhusu vyanzo vipya vya mapato.

Makinda alisema uamuzi huo ulifanywa katika kikao cha Kamati ya Uongozi cha Juni 18, mwaka huu baada ya kuzingatia maoni ya wabunge, Serikali na Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi ambao walitaka kuahirishwa kwake, ili kuruhusu Serikali kuongeza vyanzo vya mapato kadri itakavyoshauriwa na wabunge.

Aliongeza kuwa Bunge limeridhika kwamba licha ya kutopitishwa kwa muswada huo mapema kama inavyotakiwa, bado Serikali itaweza kukusanya kodi kwa kutumia sheria nyingine za nchi zilizopo.

Mabadiliko hayo ni mwanzo wa mchakato wa mabadiliko ya Kanuni za Bunge ili kuwezesha vikao vya Bunge la Bajeti kufanyika mapema na kuhitimishwa Juni 30, ili kuruhusu Serikali kuanza mwaka wa fedha baada ya Bajeti nzima na Sheria ya Fedha kuwa vimepitishwa.

“Mabunge mengi ya Jumuiya ya Madola yana utaratibu wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Fedha na Muswada wa Mutumizi mwishoni kabisa mwa mjadala wa Bajeti. Lakini tumefuatilia na kubaini kuwa mchakato wa kupitia Bajeti ya Serikali huanza mapema na kumalizika kabla ya mwaka mpya wa fedha kuanza,”alisema Makinda na kuongeza:

“Bunge letu lingepaswa liwe linakutana na kuanza mchakato wa kupitia Bajeti ya Serikali mapema, ili inapofika Juni 30, mkutano wa Bajeti uwe umemalizika na Muswada wa Sheria ya Fedha kuanza kutumika ifikapo Julai Mosi ambapo mwaka mpya wa fedha unaanza”.

Alisema kutokana na hali hiyo Kanuni za Bunge zitaendelea kufanyiwa marekebisho ili mikutano ya Bunge la Bajeti iweze kuanza mapema kama ilivyo katika nchi nyingine za Jumuiya ya Madola.

Lukuvi, alisema uamuzi wa Serikali kukubali hoja ya kusogezwa mbele muswada huo, ni kutoa fursa ya kuzingatiwa kwa maoni ya wabunge na kuendelea kuibuliwa kwa vyanzo vipya vya mapato.

“Kama Serikali isingekubali, basi ujue hilo la kuahirisha muswada lisingewezekana kabisa, maana ukishapitisha Muswada wa Sheria ya Fedha hata maoni yatakayoendelea kutolewa kwenye bajeti nyingine yangekuwa hayana maana,” alisema Lukuvi.

Advertisements

One thought on “NI DHAHIRI BILA MABADILIKO MAKUBWA BAJETI YA 2012 / 2013 KUKWAMA

  1. JAMANI NA SISI SERIKALI KIVULI YAANI WANANCHI HATUPEWI CHANCE YAKUUNDA KAMATI????YAANI KAMATI TATU ZOOOOTE MMEUNDA WENYEWE SIO SAWA JAMANI MNATUTENGA HIVYO

Comments are closed.