YALIYOJIRI KWA UFUPI BUNGENI KATIKA MJADALA WA BAJETI YA 2012 / 13 ALHAMIS JUNE 21, 2012. IKIWEMO KAULI TATA YA NGELEJA

WILLIAM NGEREJA

Katika mjadala uliyo endelea siku ya Alhamis June 21, 2012 safari hii aliyekuwa kivutio kikubwa alikuwa waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja Mbunge wa Sengerema (CCM), alisababisha mvutano mkubwa ndani ya Bunge na kuondoa utulivu kwa muda.

Kutokuelewana huko kulitokana na mchango wake wa kuiponda Bajeti ya Upinzani uku akitupiana maneno na wabunge watatu wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Tundu Lissu na Halima Mdee.

Ngeleja aliyekuwa akichangia hotuba ya bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013 muda mfupi baada ya Mbowe, alitumia muda mwingi kuishambulia hotuba ya maoni ya bajeti ya Kambi ya Upinzani akidai ni mbovu na haitekelezeki.

Huku akishangiliwa na wabunge wenzake wa CCM, Ngeleja alikwenda mbali zaidi akinuku hotuba hiyo iliyowasilishwa na Waziri kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe, na kusema kuwa wana vyanzo vya ukusanyaji mapato ambavyo vinaonesha shilingi sifuri.

Ngeleja aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini hadi Mei 4, mwaka huu alipong’olewa na Rais Jakaya Kikwete, aliwabeza wapinzani kuwa Bajeti yao ilikuwa imeandaliwa na watu ambao wana maono ya kuandaa bajeti za harusi na maandamano, lakini si katika hali ya kuandaa Bajeti ya nchi kama Tanzania.

“Mheshimiwa Spika, hawa wenzetu walio mbele yangu hawana jipya, na ningependekeza wasimame na kuwaomba radhi Watanzania maana wameandaa bajeti ya maandamano na harusi,” alisema Ngeleja.

Alisema Bajeti ya Upinzani ni ya ovyo na haikuainisha vyanzo mbadala vya mapato na hivyo kuwataka Watanzania kuipuuza.

Huku akishangiliwa na mawaziri na wabunge na CCM, alisema kama viongozi wa upinzani wanaitakia mema Tanzania, ni vyema wakatumia nafasi zao ndani ya Bunge kusimama na kuwaomba radhi wananchi kwa kuwa wamesababisha baadhi kutoijali mipango mizuri ya Serikali.

Hali hiyo ilisababisha wabunge wengi wa Chadema kusimama na kuomba Mwongozo wa Spika kuhusu jambo hilo.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee walipewa nafasi ya kuzungumza, huku Ngeleja akipinga kila kitu walichosema.

Mdee alimweleza Spika kuwa tatizo la Ngeleja siyo kupingana na maoni ya Kambi ya Upinzani bali ni hasira za kuondolewa katika nafasi ya uwaziri wa Nishati na Madini, jambo ambalo bado linamuuma.

“Mheshimiwa Spika, hakuna kitu kama hicho, tatizo la Ngeleja ni kuondolewa katika nafasi ya uwaziri na siyo kitu kingine, maana kama ni maneno ambayo yalikuwa yamekosewa tayari tulishaleta mabadiliko yake humu ndani,” alisema Mdee, kisha akakubaliana na Spika, kuondoa maneno kuwa tatizo la Ngeleja ni uwaziri.

Kwa upande wake Mbowe, alisema kuwa Ngeleja hakusoma bajeti yao vizuri na kumwomba Spika kutoa tamko la namna ya kuwashughulikia wote wanaodanganya umma katika michango yao.

Lissu alitoa ufafanuzi ulioafikiwa na Spika, kuwa Bajeti inayojadiliwa bungeni ni moja ambayo ni ya Serikali, na kwamba Kambi ya Upinzani haina ya kwake, bali inatoa maoni kwa ile ya Serikali.

“Sisi wapinzani tunawasilisha maoni yetu kuhusu bajeti ya serikali ili yafanyiwe kazi na si bajeti kivuli wala mbadala kama baadhi ya wabunge wanavyojaribu kupotosha,” alisema Lissu na kuungwa mkono na Spika.

Spika Anne Makinda alifafanua kuwa hakuna bajeti kivuli wala mbadala na badala yake kambi hiyo hutoa hoja ya kuhusu bajeti ya serikali inayokuwa imesomwa ikionesha kama wao wangekuwa madarakani wangeipanga hivyo.

Hata hivyo Ngeleja aliikataa taarifa hiyo na hivyo kuzidi kushikilia msimamo wake, jambo lililomlazimu Mbowe, kuomba mwongozo wa Spika akiuliza kiti chake kinawachukulia hatua gani wabunge kama hao wanaopoteza muda kwa jambo lililokwisha kufafanuliwa.

Wakati Spika akijaribu kumaliza ubishi huo, Mbunge wa Kawe, Mdee, aliinuka na kuomba kumpa taarifa Ngeleja na kusema kuwa kipengele anachokisemea mbunge mwenzake kilishatolewa ufafanuzi kwamba kulikuwa na kasoro za uchapaji.

Awali wakati wa mchango wake, Ngeleja alisema kuwa hali ya uchumi wa nchi yetu kwa sasa inachangiwa na upungufu wa chakula ambapo bei ya bidhaa hiyo imepaa na kuongeza makali ya maisha kwa wananchi.

Ngeleja alisema pia tatizo la nishati limekuwa chanzo cha kuongeza makali ya maisha kwani bei ya nishati imekuwa ikipaa mara kwa mara.

Naye Mbowe katika mchango wake, mbali na kulalamikia deni la taifa na kuitaka serikali ifanye juhudi za makusudi kuwaondoa wananchi kwenye umaskini walionao sasa, pia alikemea lugha za matusi kwa baadhi ya wabunge, hivyo kumtaka spika na wasaidizi wake kutenda haki kwa pande zote.

Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo, (CCM), alianza kwa kuipongeza kambi ya upinzani bungeni akisema kuwa inafanya kazi yake vizuri kwa kuishauri na kuikosoa serikali.

Shellukindo aliwataka wabunge wenzake wa chama tawala kuweka mambo ya vyama pembeni na kuangalia masilahi ya taifa, kwani kazi ya wabunge wote bila kujali itikadi za vyama ni kuishauri serikali katika masuala ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema hakuna Bunge katika nchi yoyote ambalo ni la chama tawala wala cha upinzani, huku akiwapongeza wapinzani kuwa wanakitakia mema CCM kwa kuwakosoa ili warekebishe.

Aidha, mbunge huyo alikosoa sera ya Kilimo Kwanza huku akibainisha kuwa haimlengi mkulima wa kawaida bali ni wakulima wakubwa.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Selukamba (CCM), alisema mfumuko wa bei unachangiwa na ubovu wa miundombinu jambo ambalo husababisha mazao yanayotoka shambani ambako ni vijijini kufika mjini na kuwa katika bei ya juu kuliko yalivyozalishwa.

Selukamba alibainisha kuwa mazao au bidhaa ikitoka kijijini inapofika mjini huuzwa kwa bei ya juu zaidi kutokana na gharama kubwa kutumika katika usafirishaji wake.

Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), naye amekuwa kama mwenzake wa Kisesa, Luhaga Mpina, kwa kugoma kuiunga mkono bajeti ya serikali akitaka maelezo ya serikali kuhusu fedha za miradi ya maendeleo zilizotengwa katika Wizara ya Uchukuzi.

“Katika bajeti iliyopita tulisema na serikali kupitia waziri mkuu, ikatangaza kuongeza sh bilioni 90 kwa Wizara ya Uchukuzi na kati ya hizo sh bilioni sita, zilipelekwa katika sekta ya meli Ziwa Nyasa na fedha zilizoletwa ni sh milioni 200 pekee,” alisema.

“Nawaomba wabunge wenzangu tuwe wakweli, kwa hili  lazima tuihoji, na kwa serikali hii ya CCM ni yetu, kama hatutafanya hivyo tutakuwa hatuna maana ya kuwapo kwetu hapa bungeni,” alisema Filikunjombe.

Kwa upande wake Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, ameibua ufisadi unaodaiwa kufanywa katika mgodi wa Kiwira na kulitaka Bunge kuunda kamati maalumu ya uchunguzi.

Mkono alidai kuwa sehemu moja ya mgodi huo yenye utajiri mkubwa imeuzwa kwa bei ya kutupwa kwa kampuni moja ya Australia.

Alisema uuzaji huo ni kinyume cha makubaliano yaliyofikiwa na Bunge  mwaka 2007 ambapo liliagiza kuwa mgodi wa Kiwira uliokuwa umeuzwa kwa Kampuni ya Tan Power urudishwe serikalini baada ya kuwa umeuzwa kwa dola laki saba tu.

Hata hivyo, Mkono alisema kuwa katika hali ya kushangaza Kampuni ya Tan Power ambayo ilikuwa imeingia ubia na serikali iliuzwa kwa Waustralia  kiasi cha mabilioni ya dola.

“Mheshimiwa Spika, Kiwira kulikoni? Lini Bunge litaunda kamati ya kwenda kuangalia Kiwira?” alihoji na kusema kuwa pamoja na yote hayo, sasa serikali imetenga sh bilioni 40 kwa ajili ya mradi wa Kiwira na kuhoji nani aliteketeza fedha za awali zilizotolewa kwa ajili hiyo.

Advertisements

2 thoughts on “YALIYOJIRI KWA UFUPI BUNGENI KATIKA MJADALA WA BAJETI YA 2012 / 13 ALHAMIS JUNE 21, 2012. IKIWEMO KAULI TATA YA NGELEJA

Comments are closed.