TAKUKURU YAMPANDISHA KIZIMBANI MKURUGENZI WA ZAMANI WA HALMASHAURI YA MANISPAA YA ARUSHA.

ARUSHA

  • SHITAKA LA KWANZA NI MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA.
  • SHITAKA LA PILI NI KUTOA ZABUNI YA UJENZI WA BUSTANI YA KIJENGE KWA KAMPUNI YA LUNECO BILA KUISHIRIKISHA BODI YA ZABUNI YA HALMASHAURI HIYO.
  • SHITAKA LA TATU NI KUMLIPA MZABUNI ASIYE STAHILI
  • SHITAKA LA NNE NI KUSHINDWA KUSIMAMIA UJENZI WA BUSTANI YA KIJENGE

ARUSHA. Aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Arusha, Rafael Mbunda (51), Mwanasheria wa halmashauri hiyo, Paul Mugasha, kaimu mweka hazina, Christopher Mbarakai na mkurugenzi wa kampuni ya ujenzi ya Luneco Nestory Ng’hoboko, wamefikishwa mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi ikiwemo kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh milioni 25.5.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Gwantwa Mwanguga, washitakiwa hao walisomewa makosa manne tofauti na waendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU), Hangi Chang’a na Rehema Mteta.

Shitaka la kwanza la matumizi mabaya ya madaraka linawakabili Mbunda, Mbarakai na Mugasha ambao wanadaiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa kumwezesha mkurugenzi wa kampuni ya Luneco Investment, Ng’hoboko, kuwasilisha nyaraka za zabuni bila kufuata sheria ya manunuzi ya umma nchini.

Mteta alidai mahakamani hapo kuwa shitaka la pili linalowakabili washitakiwa hao watatu wanaodaiwa kuwa Agosti 23, 2010, washitakiwa hao waliokuwa watumishi wa halmashauri hiyo walitoa zabuni ya ujenzi wa bustani ya Kijenge kwa kampuni ya Luneco bila kuishirikisha bodi ya zabuni ya halmashauri hiyo.

Katika shitaka la tatu, wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya ambapo Agosti 23 mwaka huu walitoa fedha za serikali sh milioni 45.7 kwa kampuni ya Luneco ambayo haikustahili kwa mujibu wa sheria.

Shitaka la nne, linawakabili washtakiwa wote wanne ambapo inadaiwa kuwa kati ya Septemba 23 na Oktoba 20, 2010 walishindwa kusimamia ujenzi wa bustani ya Kijenge na hivyo kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya sh milioni 25.5.

Washitakiwa wote walikana mashitaka na wako nje kwa dhamana ambapo shauri hilo litasomwa mahakamani hapo kwa kutajwa Julai 19, mwaka huu, baada ya upande wa mashitaka kudai kuwa upelelezi haujakamilika.

Alisomewa mashitaka hayo na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU, Jakopio Richard mbele ya Hakimu Mkazi, Judith Kamara, ambapo shauri hilo limeahirishwa mpaka Julai 17 litakaporudi kwa ajili ya kutajwa.

Advertisements