TGNP WASONONESHWA NA LUGHA ZA MATUSI, KEJELI NA DHARAU ZA BAADHI YA WABUNGE

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP)

DAR ES SALAAM. Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), umesikitishwa na baadhi ya wabunge na kuwataka kuacha mara moja lugha chafu za matusi, kejeli, dharau, na vurugu za kuchana nyaraka za mijadala bungeni kwani hiyo ni kuwatusi wapiga kura wao.

Katika tamko lao, lililosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Usu Mallya, wamemtaka Spika wa Bunge Anna Makinda kutoruhusu ushabiki wa maoni ya mtu binafsi au kikundi, badala yake zijadiliwe hoja za bajeti ya serikali ambayo inawagusa wananchi.

“Waheshimu kwa dhati muda ni gharama za walipa kodi zinazowafanya wawepo Dodoma, mijadala ilenge kuleta tija, mageuzi ya kiuchumi na kubadilisha hali duni ya umaskini wa Mtanzania ambaye amebakia kupata mlo mmoja kwa siku na wengine hawana kabisa,” alisema Usu.

Alifafanua kuwa wananchi wana mategemeo makubwa kwa Bunge katika mjadala huo lakini kinyume chake, wameshtushwa na kusikitishwa jinsi baadhi ya wabunge wanavyoonyesha tabia ya kutumia vibaya dhamana waliyopewa na wananchi.

“Baadhi yao wamekuwa wakitumia vibaya muda kujadili maisha ya watu binafsi, kushambulia vyama vya siasa, kufanya utani badala ya kujadili jinsi ya kusaidia na kuboresha maisha ya Watanzania,” alisema.

Kama wanaharakati na watetezi wa ukombozi wa wanawake, wanawataka wabunge na ofisi ya Spika, kujikita kuchambua, kujadili bajeti na kuishauri serikali namna ya kuboresha na kutekeleza ahadi na mipango yake ya kiuchumi.

Aliongeza kuwa wamekuwa wakifuatilia kwa makini na kwa ukaribu mjadala wa bajeti ya mwaka wa fedha 2012/2013, ambayo imekuja kipindi cha hali ngumu ya maisha kutokana na mfumko wa bei, ukosefu wa ajira, ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, wazee na watoto, na kudorora kwa huduma muhimu.

Advertisements