MGOMO WA MADAKTARI NAO NI MOJA YA UDHAIFU WA SERIKALI YA CCM

WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII, DK HUSSEIN MWINYI

 • YAWEZEKANA HUU NI UPEPO TU UKAPITA?

 • KWANINI HOSPITALI ZETU ZIWE SEHEMU YA MATESO KWA WAGONJWA BADALA YA KUWA SEHEMU YA FARAJA

 • HATUA YA KUPUNGUZA BAJETI YA WIZARA YA AFYA NI KUWAPUUZA WAUGUZI?

 • TAARIFA ZINAZO TOLEWA KWA UMMA ZISIZO ZA UKWELI NI TIBA YA TATIZO?

 • NI GARAMA YA MAISHA YA WATANZANIA WANGAPI SERIKALI INAITAJI HILI KUJADILIANA NA WATOA HUDUMA HAO WA TIBA NCHINI?

 • SASA NI WAZI WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII, DK HUSSEIN MWINYI KUTOLEWA KAFALA.


ARUSHA. Serikali ya Tanzania imeonyesha kutokuwa na kumbukumbu au kujifunza kutokana na makosa kwa kuchukuwa hatua zile zile zilizo shindwa kuzuia migomo miwili iliyotangulia ya wanaotoa huduma ya tiba hapa nchini.

Baada ya kushuhudia migomo ya madaktari kwa awamu mbili na baadaye kufuatiwa na majadiliano yalioisha havi karibuni sasa kile watanzania wengi walichokuwa wanakihofia kimetokea, baada ya madaktari nchini Jumamosi June 23, 2012 kuanza taratibu mgomo usio na kikomo kwa lengo la kuishinikiza serikali kuwa timizia mahitaji yao ikiwamo kuboresha mazingira ya kufanyia kazi pamoja na nyongeza za mishahara.

Hali hiyo inakuja ikiwa ni miezi mitatu tangu nchi kushuhudia mgomo mkubwa wa wanataaluma hao mapema mwaka huu, ambao ulisababisha kung’olewa kwa vigogo wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Kutokana na mgomo huo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa walisimamishwa kazi; na baadaye aliyekuwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda na naibu wake, Dk Lucy Nkya waling’olewa kwenye nyadhifa hizo, katika mabadiliko ya mawaziri.

Migomo miwili ya kwanza ilipuuzwa hivihivi lakini mwishowe tuliona viongozi wakuu wa nchi wakirudi nyuma na kuomba huruma ya mazungumnzo.

Je mgomo huu wa sasa ni nani alaumiwe kwa kushindwa kutatua mgogoro huu uliodumu kwa kipindi cha nusu mwaka sasa??

Uamuzi huo wa madaktari unapingana na amri ya Mahakama Kuu Tanzania, Kitengo cha Kazi ambayo Ijumaa June 22, 2012 ilizuia mgomo huo baada ya kupokea maombi namba 73 ya 2012 yaliyowasilishwa chini ya hati ya dharura na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).

Mahakama hiyo ilitoa amri ya kusitisha mgomo huo mpaka hapo shauri la pande zote mbili Serikali na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mahakama hiyo iliyotolewa Ijumaa June 22, 2012 jioni na kusambazwa kwenye vyombo vya habari, imewataka MAT na wanachama wake kutoshiriki kwenye mgomo huo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alisema hawajapata taarifa zozote kutoka Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi, ya kuzuia mgomo huo.

Hata hivyo alisema mgomo ulioanza haukihusishi Chama cha Madaktari nchini (MAT).

Alisema wao taarifa hizo wamezisikia katika vyombo vya habari hivyo hawajui kama zinawahusu wao au MAT, na kwamba itakuwa ni vigumu kutolea ufafanuzi jambo lisilowahusu.

Dk. Ulimboka alisema kuwa kimsingi serikali imekuwa ikipotosha dhana nzima ya mgomo huo kwani inaonyesha kuwa suala la posho ndilo linalogomewa na madaktari wakati si kweli.

“Watu wanadhani tunapigania posho zaidi, hapana tunapigania huduma bora kwa wagonjwa, kwa sababu sifa ya kwanza katika hospitali ya rufaa ni kuhakikisha yale yanayoshindikana katika hospitali nyingine yanawezekana katika hospitali za rufaa,” alisema.

Alitolea mfano kifaa cha kupimia cha CT- SCAN ambacho kina zaidi ya miezi saba hakifanyi kazi katika Hospitali ya Muhimbili huku ikiwalazimu baadhi ya wagonjwa wanaofika kutakiwa kufanya kipimo hicho katika hospitali nyingine.

“Wengine hawana uwezo huo, wale wanaobahatika kufika huku wanakuta kifaa hakifanyi kazi, huyu ni mgonjwa bado unamuongezea gharama nyingine, tukiyasema haya wanasema sisi hatuwajali wagonjwa,” alisema Dk. Uliomboka.

Alisema madai mengine ni pamoja na miundombinu ya hospitali kwa kile alichoeleza haziwiani na idadi ya wagonjwa na kutolea mfano wodi ya watoto katika Hospitali ya Temeke kuwa mazingira ni magumu.

Alibainisha kuwa kitaaluma ni lazima wawahudumie wagonjwa wakiwa vitandani na inapotokea wagonjwa wakiwa chini inawawia vigumu kuwahudumia, na kwamba hayo ndiyo masuala waliyokuwa wanalalamikia.

“Kwanini hospitali zetu ziwe sehemu ya mateso kwa wagonjwa badala ya kuwa sehemu ya faraja? Tunaambiwa tuwaandikie dawa wagonjwa, wakienda dirishani hata Panadol hakuna, haya hawataki kuzungumzia, wameamua kupandisha posho ya maiti wakati hata katika madai yetu hatukuwa na dai hilo,” alisema.

 

MGOMO WAANZA

Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam huduma za dharura zinatarajiwa kusitishwa wakati wowote kuanzia sasa.

Mwana habari wetu aliyetembelea hospitali za Jiji la Dar es Salaam ikiwemo Muhimbili na zile za mkoa ambazo ni Temeke, Amana na Mwananyamala na kushuhudia kusuasua kwa huduma.

Vitengo vya dharura katika hospitali hizo viliendelea kupokea wagonjwa huku baadhi ya madaktari wakiweka wazi kuwa kuna uwezekano wa huduma hizo kusimama katika muda wa saa 24 kuanzia Jumamosi June 23, 2012.

MUHIMBILI

Katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wagonjwa walilamikia huduma zilizokuwa zikitolewa huku wengine wakisema wametelekezwa na wauguzi waliokuwa zamu.

Eneo la mapokezi baadhi ya askari walionekana wakiwaeleza wagonjwa waliofika kuwa huduma zimesimama na kuwasihi waondoke eneo hilo.

Mgonjwa mmoja ambaye alionekana kuchanganyikiwa alisikika akisema kuwa alimkabidhi nchi Rais Jakaya Kikwete lakini haieleweki kiongozi huyo anakoipeleka.

“Rais Kikwete nilikukabidhi nchi hii sasa unaipeleka wapi?” alisikika akisema.

John Kobelo, alisema kuwa tangu juzi kijana wake alitakiwa kufanyiwa upasuaji lakini ilipofika Jumamosi June 23,2012 aliambiwa ampatie mgonjwa wake chakula kutokana na huduma hiyo kutokuwepo.

“Kwa kweli hali inasikitisha na kukatisha tamaa, sijui nchi hii tunaelekea wapi maana viongozi wanaamua kwa makusudi kuchezea uhai wa Watanzania,” alisikika baba mmoja akilalamika.

Mwanahabari wetu alipofika katika wodi ya Sewa Haji na kukutana na mgonjwa ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake lakini alilalamikia kitendo cha madaktari kushindwa kupita zamu kwa siku ya Jumamosi June 23, 2012 huku huduma zikiwa zimezorota.

Katika wodi ya Kibasila mwakilishi wetu alikutana na baadhi ya wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao walikuwa wakiangaika kumhamisha mgonjwa wao aliyekuwa akilalamika kwa maumivu makali.

Mwanahabari wetu alilazimika kufika katika Kitengo cha Mifupa (Moi) ambapo ilikutana na Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Jumaa Almasi, ambaye alisema kuwa kwa Jumamosi June 23, 2012 ilikuwa ni vigumu kuzungumzia mgomo huo kutokana na kuwa siku ya mapumziko.

“Unajua kwa (leo) yaani Jumamosi June 23, 2012 siwezi kuzungumzia mgomo kwa kuwa tuna kliniki mbili za binafsi, labda picha kamili ya kuwepo kwa mgomo tunaweza kuipata kuanzia Jumatatu, kwa vile kuna kliniki zote,” alisema.

Aidha, Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha, alijikuta akishindwa kutokea katika kikao cha waandishi wa habari alichokiita ofisini kwake.

MWANANYAMALA NA TEMEKE

Hali ilikuwa si shwari kwani baadhi ya wagonjwa walisikika wakisema kuwa hawajapata huduma na baadhi ya wauguzi wanajifanya kutoa huduma baada ya kuona wanahabari.

Katika Hospitali ya Amana, Tulishuhudia shughuli za matibabu zikiwa zinaendelea ingawa baadhi ya wagonjwa walikuwa wakilalamika kukaa muda mrefu pasipo kupatiwa huduma.

Mmoja wa watu waliokuwa hospitalini hapo aliyempeleka ndugu yake kupatiwa huduma baada ya kupata ajali aliwaambia wanahabari kuwa wamekaa katika eneo hilo zaidi ya saa tatu bila mgonjwa wake kupatiwa matibabu.

“Nipo hapa na huyu afande tumemleta mtu aliyepata ajali maeneo ya Sitakishari lakini hatujahudumiwa mpaka saa hizi sasa sijui ndiyo wanagoma kisirisiri?” alisema mtu huyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe.

Katibu wa utawala wa hospitali hiyo, Tunu Mwachale, alisema madaktari waliotakiwa kufika zamu kwa siku ya Jumamosi June 23, 2012 wote walifika na kwamba walikuwa wakiendelea na kazi kama kawaida.

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA MOROGORO

Katika kikao cha madaktari na wahudumu wa afya Ifakara kilichofanyika tarehe 16 June 2012, Kwa pamoja kilikataa taarifa iliyotolewa na serikali kuhusu madai ya Madaktari na Wahudumu wa Afya.

Kikao kilitoa maazimio yafuatayo

 1. Tunasikitishwa na msimamo wa serikali kutokuonyesha lengo la kutatua madai ya madaktari na wahudumu wa afya.
 2. Tunatangaza mgogoro rasmi dhidi ya serikali kuhusiana na madai yetu kudharauliwa na kutofanyiwa kazi.
 3. Tutaungana na madaktari na wahudumu wengine wa afya Tanzania katika mgomo utakaoanza tarehe 23 Juni 2012. Kama Serikali haitafanyia kazi madai yetu.
 4. Tunaukumbusha umma kuwa serikali ilikuwa na muda wa kutosha kufanyia kazi na kutatua madai ya madaktari na wahudumu wa afya

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA BUGANDO MWANZA.

Kutokana na kikao cha tarehe 15/06/2012 hapa Bugando na kanda ya Ziwa kwa ujumla tunatamka kwamba:-

 1. Hatukubaliani na namna serikali ilivyo- na inavyoshughulikia suala la madaktari na wahudumu wengine wa afya hapa nchini.
 2. Ni vema serikali itoe tamko lenye tija juu ya mgogoro unaondelea kati yake na wafanyakazi wa sekta ya afya nchini
 3. Tutaungana na madakrai wote pamoja na wahudumu wengine wa afya katika mgomo utakaonza tarehe 23/06/2012 ikiwa hatua madhubuti na zenye tija hazitachukuliwa

Mungu Ibariki Tanzania Mungu Ibariki Afrika

TAARIFA KWA UMMA KUTOKA WAHUDUMU WA AFYA DODOMA

Baada ya kupata muda wa kupitia na kuchambua kwa kina ufafanuzi wa serikali kuhusu madai ya madaktari. Madaktari na wahudumu wa afya Dodoma tunapenda kutoa tamko kama ifuatavyo.

 1. Tunaunga mkono maamuzi ya kikao cha madaktari na wahudumu wa afya cha tarehe 9/06/2012 kwa kuukataa ufafanuzi wa madai ya msingi kwani hauna nia ya dhati wa kuleta suluhisho la kudumu katika sekta ya afya. Hivyo tupo katika mgogoro na serikali na tutaungana na wenzetu katika mgomo utakaoanza tarehe 23/06/2012.
 2. Tunaitaka serikali iache mara moja jitahada zake za kutugawa wahudumu wa sekta ya afya kwani kwa kufanya hivyo kutadhorotesha ufanisi wa utoaji wa huduma za afya katika hospitali mbalimbali nchini. Hivyo tunaitaka serikali ianze mara moja kuwalipa wahudumu wote wa afya posho mpya za kuitwa kazini.
 3. Tunawaomba wahudumu wa afya wote na popote walipo kuendelea kuwa pamoja katika kutetea huduma bora na maslahi mazuri katika sekta ya afya.

MUNGU IBARIKI TANZANIA.

Advertisements

2 thoughts on “MGOMO WA MADAKTARI NAO NI MOJA YA UDHAIFU WA SERIKALI YA CCM

 1. Kwa ufupi serikali ya CCM imeshindwa kuongoza nchi hii.. Tunamuomba raisi wetu mpendwa wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ajiuzulu wadhifa wake ndani ya siku 90…

Comments are closed.