PPRA YA ZICHUKULIA HATUA KAMPUNI 34 ZILIZOBAINIKA NA MAKOSA MWAKA WA FEDHA 2011/12

Kaimu Mwenyekiti body ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Jaji Thomas Mihayo (Katikati) akizindua utaratibu wa kutangaza zabuni kwa njia ya ujumbe wa simu ya mkononi katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya PPRA jana. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Push Media Mobile, Fredd Manento na kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa PPRA, Dk Ramadhani Mlinga.

MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imezifungia kwa kipindi cha mwaka mmoja kampuni 34 kutopewa zabuni zozote Serikalini baada ya kubainika kuwa na makosa mbalimbali yakiweno ya ufisadi kwa kushirikiana na watendaji wa Serikali kuiba mamilioni ya fedha kupitia mikataba hewa.

Hatua hiyo imeandamana na mkakati wa kuikabidhi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) halmashauri 4 zilizohusika katika upotevu wa mamilioni hayo ili kufanya uchunguzi na kuchukua hatua wahusika.

Akitangaza uamuzi huo, Jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Jaji Thomas Mihayo alisema hatua hiyo ilichukuliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo baada ya kupitia kwa kina ripoti ya uchunguzi ya PPRA.

“Kufungia kampuni hizo ni kwa mujibu wa kanuni 102 (2) ya Tangazo la Serikali namba 97 la mwaka 2005,” alisema Jaji Mihayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Jaji Mihayo alisema licha ya kuchukua hatua hiyo alionya kuwa kuna kila dalili Taasisi 29 kufanya ubadhirifu wa mabilioni ya fedha kupitia manunuzi katika mwaka wa fedha 2011/12.

Mkurugenzi wa PPRA, Dk Ramadhan Mlinga alizitaja kampuni nane zilizofungiwa na bodi kutokana na madai ya kuingia mikataba hewa na halmashauri kuwa ni Muson Engineers Ltd, Man-Ncheye Pa Ltd, F.I.C Ltd Nyegezi JJ Construction Ltd, Jossam and Company Ltd, Satelite Construction Ltd, Icon Engineers na Tengo Construction.

Alizitaja halmashauri zinazotuhumiwa kuinga mikataba hewa na kampuni hizo ni Bahi, Magu, Sengerema, Geita na Mvomero.

Kampuni nyingine 26, alisema zimefungiwa kwa madai kwamba zimeshindwa kutekeleza mikataba na taasisi za serikali zilizozipa zabuni ya ununuzi wa vitu mbalimbali.

Kuhusu taasisi ambazo zina kila dalili ya kusababisha upotevu wa mabilioni ya fedha za umma katika mwaka ujao wa fedha, Dk Mlinga alisema ni kutokana na watendaji wake kushindwa kutekeleza maagizo ya bodi.

“Taasisi zao (watendaji) hazikufanya vizuri katika ukaguzi wa mwaka 2010/11 kwa kukiuka taratibu za ununuzi… Moja ya maagizo ya bodi kwa taasisi hizo ilikuwa ni kuandaa mafunzo yatakayotolewa na wataalamu wa PPRA ili wajisahihishe,” alisema Dk Mlinga.

Kilichoifanya bodi kutoa tahadhari kwa umma alisema; “Taasisi hizo (29) zimeamua kutotekeleza agizo hilo.”

Dk Mlinga alizitaja taasisi hizo za umma kuwa ni Mahakama Kuu ya Tanzania, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bodi ya Kahawa Tanzania, Bodi ya Pamba Tanzania, Baraza la Kiswahili Tanzania na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Taasisi nyingine ni Bodi ya Makandarasi Tanzania (CRB), Mamlaka ya Maji Mijini na Vijijini Lindi, Mamlaka ya Maji Mjini na Vijijini Mtwara, Mamlaka ya Maji Morogoro (Uwasa), Idara ya Magereza na Chuo cha Mahakama na Utawala.

Nyingine ni halmashauri za Urambo, Mkinga, Igunga, Sengerema, Masasi, Kilolo, Kilombero, Nachingwea, Magu, Mvomero na Tunduru. Nyingine ni manispaa za Temeke, Kinondoni, Ilala, na Singida.

Kampuni 26 zilizofungiwa kwa kushindwa kutekeleza mikataba ni Lemungo Construction Co Ltd, Majujulu Investiment Ltd, Ostrich Maintenance Works Ltd, Nzori General Enteprises Ltd, Niako Supplies Co Ltd, Shedol Construction Ltd na Maktech& Tel Co Ltd.

Dk Mlinga alizitaja kampuni nyingine kuwa ni Jimmy Money Enterprises, Mahende Garage and Construction Co Ltd, Nyanda & Company, Kipusi Traders, Jawabu Construction Co Ltd, Rana Decoration Building and Civil Constractors na Grace Mbilinyi.

Kampuni nyingine alizitaja kuwa ni Computech ICT (T) Ltd, Girland Developers Ltd, Camsa Construction Co Ltd, Twabaha Construction Co Ltd, Malaika Building Constructors and Civil Works, Mussa S. Mbweso, Ligero Constructors Company Ltd, Ligero Constractors Co. Ltd na Julius Mwamlima Constractors.

Advertisements