SERIKALI MBONA HAMTUFARIJI; TUNALIA MAISHA MAGUMU, HAKUNA MATIBABU WALA USALAMA WA WATETEZI WETU.

 • HAKUNA TAARIFA RASMI KUTOKA SERIKALINI MPAKA SASA.

 • MGOMO WA MADAKTARI SASA WAPAMBA MOTO

 • CHADEMA WAUNGANA NA WANAHARAKATI  KULAANI TUKIO HILO

 • VYOMBO VYA HABARI VYA SERIKALI   VYAKWEPA KURIPOTI MATUKIO HAYA

Tukiwa bado katika hali ya sintofahamu kutokana na ugumu wa maisha pamoja na kukosa uhakika wa matibabu tumekumbwa na mshituko mkubwa baada ya kupokea taarifa za matumizi ya nguvu kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuzima hoja au udhaifu wa serikali katika kutatua matatizo ya wananchi.

Mambo kama hayo ni mageni kwa watanzania na tumezoea kuyasikia yakitokea kwenye nchi za kidikteta na zile zinazoongozwa  kiimla.

Tukio la hivi karibuni ni lile la watu wasiojulikana, Jumanne Juni 26, 2012 usiku kumteka, kumpiga, kuvunjwa meno kadhaa, mbavu na miguu ikiwamo kuumizwa sehemu za siri na kumjeruhi vibaya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, kisha kumtupa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji Dar es Salaam.

Msitu wa Pande ulioko wilayani Kinondoni ni maarufu kwa matukio haya ya kinyama na inaaminika kutumiwa na serikali katika kuwahoji watuhumiwa, ikumbukwe ni sehemu hiyo hiyo ndiko wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam waliuawa na polisi mwaka 2006.

Daktari huyo ambaye amekuwa akiratibu mgomo wa madaktari unaoendelea, aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono na miguu akiwa katika hali mbaya, huku akiwa ameng’olewa meno na kucha na watu ambao hawajajulikana, huku baadhi wakidai ni watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa, na wengine wakisema ni majambazi.

Baadhi ya madaktari walishindwa kuhimili na kuangua vilio vilivyoongeza simanzi huku wengine wakisema kauli ya ‘liwalo na liwe’ iliyotolewa Bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda imeanza kutekelezwa.

Taarifa za kujeruhiwa kwa Dk. Ulimboka zilisambaa kwa kasi katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii na wengine kutumiana ujumbe mfupi wa simu isipokuwa vile vya serikali tu (TBC na magazeti yanayomilikiwa na serikali).

Kutokana na tukio hilo, wanaharakati wa haki za binadamu wameituhumu Serikali kuhusika na tukio hilo, huku Serikali ikikana tuhuma hizo, na papohapo ikiagiza Jeshi la Polisi kuwasaka waliohusika kwa udi na uvumba.

Akizungumza kwa taabu baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Ulimboka alisema akiwa na rafiki zake alipigiwa simu na mtu anayemfahamu na ambaye walishawahi kukutana akimtaka wakutane.

Ulimboka alisema mara baada ya mtu huyo kufika walipokuwa, walianza mazungumzo, lakini wakiwa katikati yule mtu aliwasiliana kwa njia ya simu na watu asiowafahamu, na baada ya muda mfupi kabla ya kuagana liliwasili gari moja lenye rangi nyeusi likiwa halina namba.

“Wakashuka watu kama watano hivi wakiwa na bunduki wakawaambia wale wenzangu na yule niliyekuwa naongea naye kuwa wako free (huru), wakaniingiza kwenye gari lao kwa nguvu,” alisema Dk. Ulimboka.

Naye Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Godwin Chitage alisema siku ya tukio wakiwa na Dk. Ulimboka walipigiwa simu na mtu wa Usalama wa Taifa (jina limehifadhiwa) akamtaka wakutane usiku huo.

“Walitoka Ulimboka na Dk. Deo wakaenda maeneo ya Kinondoni Stereo walipokutana naye akaanza kupiga simu likaja gari jeusi, wakashuka watu wanne wakiwa na silaha, na kumtaka Dk. Deo aondoke, ndipo yakaanza malumbano kabla ya kumzidi nguvu na kumwingiza kwenye gari kisha kuondoka naye.”

“Tulipopata taarifa kutoka kwa Deo tukaanza kupiga simu ya Dk. Ulimboka ikawa haipatikani tena. Tulienda Oysterbay Polisi kutoa taarifa lakini hatukupata ushirikiano wa kutosha, tukaenda ‘Central’ (Kituo Kikuu) tukaambiwa tusubiri hadi kesho, hapo ilikuwa saa saba tangu saa tano walipomteka.

Alisema asubuhi walipata taarifa kutoka kwa msamaria mwema kwamba Ulimboka amepigwa sana na ametelekezwa kwenye msitu wa Pande, na walifuatilia ingawa anadai walikosa ushirikiano kwenye Kituo cha Polisi Bunju.

“Kitendo alichofanyiwa mwenyekiti wetu kimetufanya kuwa imara zaidi katika kupigania haki zetu. Tutasimama kwa pamoja kwa gharama yoyote hata kama ni kutoa uhai wetu.

“Nawaomba Watanzania wote wanaoitakia amani Tanzania walaani kitendo hiki, tunawalaani wote waliofanya juhudi za kumchelewesha Dk. Ulimboka kufika hospitali ili lengo lao la kumtoa uhai litimie,” alisema Dk. Chitage.

Katika tukio lisilo la kawaida mtu mmoja anayedaiwa kuwa mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Daraja la Salenda alipata kipigo kikali kutoka kwa kundi la madaktari, baada ya kuhisiwa kuwa ni mmoja wa watu waliohusika kumteka nyara Dk. Ulimboka.

Inadaiwa polisi huyo alichepuka baada ya kumwona Ulimboka, kisha akasikika akizungumza na wenzake kwa njia ya simu kwamba alikuwa (Ulimboka) hajafa.

Ofisa huyo aliokolewa na askari wanaolinda hospitali hiyo na kupelekwa kwenye chumba kidogo kilichopo jirani na lango la kuingilia hospitalini hapo, ambapo baada ya muda polisi zaidi waliwasili wakiwa katika gari lenye namba za usajili T 226 AMV wakiingia na kutoka katika chumba hicho.

Majira ya saa 05:20 asubuhi gari aina ya Toyota lenye namba za usajili T 716 BKZ ililiwasili na kumchukua ofisa huyo ambaye alidai kupoteza “Radio call” na bastola yake katika shambulio hilo.

Miongoni mwa watu wa kwanza kufika katika Kituo cha Polisi Bunju kumuona Dk Ulimboka ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba ambaye alisema kilichotokea kinaonyesha jinsi gani Serikali ilivyo na woga katika kushughulikia  matatizo ya wananchi.

Dk Bisimba alisema wao wanaamini kuwa tukio hilo lina mkono wa Serikali na kama ni kinyume cha hapo, basi inapaswa kuwaridhisha wananchi kuwa hawana mkono wao katika sakata hilo.

“Kama wao hawana mkono wao basi wanapaswa kuwaridhisha wananchi kuwa hawahusiki kwa kuwatia mbaroni wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria,” alisema Bisimba.

Bisimba alisema baada ya wasamaria kumkuta mnamo saa 12:00 asubuhi, walimpeleka katika kituo kidogo cha Polisi cha Bunju ambako polisi walifungua mashtaka ya wizi wa maungoni na kupatiwa RB yenye namba BJ/RB/1870/2012.

“Mimi nilipata taarifa za kutekwa kwake kutoka kwa mwenziye aliyekuwa naye mnamo saa nane usiku, na baada ya kupata taarifa hizo niliwaeleza wanaharakati wenzangu juu ya hatua za kuchukua,” alisema Bisimba.

Bisimba alisema aliwasili katika Kituo cha Polisi cha Bunju, jana mapema asubuhi na kumkuta Dk Ulimboka akiwa amejeruhiwa vibaya, lakini hakuwa amepatiwa huduma yoyote.

“Tulikwenda kumchukua na kukuta hali yake ni mbaya, lakini cha ajabu pamoja na majeraha yote hakupatiwa msaada wowote wa huduma, jambo ambalo lilitusikitisha sana,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sikika, Irene Kiria alisema kilichotokea ni kitu kibaya na kinaonyesha jinsi gani Serikali inavyoshughulika na watu, badala ya kujali hoja za msingi ambazo zinawasilishwa.

Kiria alisema hoja za madaktari zilipaswa kusikilizwa kwani licha ya madai ya masilahi yao lakini pia wanapigania mazingira bora yenye utu kwa ajili ya wagonjwa.

Madai mengine ni upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wananchi pamoja na upatikanaji wa dawa, mambo ambayo alisema hayahitaji mjadala.

“Suala la masilahi ya madaktari linazungumzika lakini siyo suala la dawa, mazingira bora ya kuwahudumia wagonjwa na upatikanaji wa vifaa tiba na vipimo vingine,” alisema Kiria.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi alisema Serikali imeliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika na utekaji huo.

Dk Nchimbi alisema mjini Dodoma kuwa Serikali haihusiki kwa namna yoyote ile na utekaji nyara huo, na kwamba kitendo hicho kinapaswa kulaaniwa kwani hakikubaliki katika jamii hasa kwa zama hizi.

“Kwanza, madaktari ni watu muhimu ambao wao ndio wanaotuwezesha sisi kuishi, kwa hiyo wapo kwa ajili ya maisha yetu, hata kama asingekuwa daktari, kwa mtu yeyote yule, jambo hili halikubaliki katika nchi yetu,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:

“Tumewaagiza polisi wafanye uchunguzi ili kuwabaini wahusika na wakipatikana wafikishwe katika vyombo vya sheria, maana hatuwezi kwa namna yoyote kuvumilia vitendo vya aina hii.”

Alisema Serikali imeshtushwa sana na tukio hilo na haitavumilia kwa namna yoyote vitendo hivyo pamoja na vile vya unyanyasaji kwani ni kinyume cha sheria.

Kuhusu kupigwa kwa Mkuu wa Upelelezi (OC- CID), ASP Mukiri, Dk Nchimbi alisema lilikuwa ni tukio la bahati mbaya kwamba madaktari waliokuwapo Muhimbili walishindwa kuwa na uvumilivu kwani askari aliyepigwa alikuwa ameagizwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela kwenda kufuatilia matibabu ya Dk Ulimboka.

“Hapa ndipo ninapotofautiana na watu wengi, mnampigaje polisi, maana yule anapaswa kuwa rafiki wa raia, sasa unampigaje mtu ambaye ni mlinzi na umemwajiri, analipwa kwa kodi yako?” alihoji Dk Nchimbi.

Kipigo alichopata kiongozi wa madaktari, Dk. Steven Ulimboka na kauli nzito aliyoitoa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu mgomo wa madaktari, vimelivuruga Bunge.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhoji baada ya kutilia shaka kauli ya Waziri Mkuu Pinda na kipigo cha daktari huyo.

Jumatano June 27, 2012 asubuhi wakati waziri mkuu akijibu mwongozo wa Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), aliyetaka kujua msimamo wa serikali kuhusu mgomo huo, alisema Alhamisi June 28, 2012 serikali itatoa uamuzi mzito kuhusu mgomo wa madaktari na ‘liwalo na liwe.’

Mbunge huyo alisema wakati madaktari walipotoa tishio la mgomo wiki mbili zilizopita, Waziri wa Afya, Dk. Hussein Mwinyi alitoa kauli ya Serikali Juni 22 kwamba Serikali imetekeleza madai ya madaktari na kuongeza posho.

Kwa mujibu wa Zambi, licha ya kauli hiyo, madaktari katika baadhi ya hospitali ikiwamo Muhimbili walianza mgomo.

“Mheshimiwa Spika, nimepigiwa simu kutoka Mbeya, Dar es Salaam, Moshi nimeambiwa mgomo unaendelea. Naomba mwongozo wako, hatua gani serikali itachukua kuwaokoa wagonjwa?”

Akijibu mwongozo huo, Waziri Mkuu Pinda alikiri kuwa ni kweli serikali imeenda mahakamani kupinga mgomo huo na mahakama iliwazuia madaktari kugoma na kuwataka watangaze kwenye vyombo kwamba wamesitisha mgomo.

Kwa mujibu wa Pinda, madaktari walikaidi amri hiyo na serikali ilikimbilia tena mahakamani na mahakama ilikazia uamuzi wake wa awali.

“Tunafikiri si vizuri kuingilia kazi ya mahakama lakini pia tulidhani madaktari wataheshimu amri ya mahakama.

“Serikali itatangaza hatua za kuchukua. Maana wakati mwingine Waswahili wanasema ‘liwalo  na liwe,’ alisema Pinda na kushangiliwa na wabunge wa CCM.

Hata hivyo, kauli ya Pinda ilileta tafrani baada ya wabunge wawili wa CHADEMA, Halima Mdee, na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, kutaka maelezo yakinifu kuhusiana na mambo ya kutatanisha katika mgogoro huo.

Mdee alimtaka Waziri Mkuu Pinda kutoa maelezo ya serikali kuhusiana na tukio la kuvamiwa, kutekwa na kisha kupigwa vibaya kwa Ulimboka, ikitiliwa shaka kauli ya kiongozi huyo mkuu wa shughuli za serikali bungeni, aliyedai kuwa sasa ‘liwalo na liwe’.

Mbunge huyo alidai kuwa kauli ya Pinda inaleta mashaka na hisia kuwa serikali inahusika na tukio la kinyama alilofanyiwa Dk. Ulimboka.

Naye Mnyika alisema kukamatwa na kushambuliwa kwa kiongozi wa madaktari, Ulimboka, kutachochea zaidi mgogoro kati ya madaktari na serikali.

“Udhaifu wa serikali kuharakisha kwenda mahakamani kabla ya Bunge kupewa fursa ya kujadili madai ya madaktari na kuisimamia serikali umelifikisha taifa hapa tulipo,” alisema.

Mbunge huyo aliliambia Bunge kuwa serikali inajikanyaga katika sakata hilo kwa sababu imekishitaki Chama cha Madaktari nchini (MAT), lakini iliyotangaza mgomo ni Jumuiya ya Madaktari.

Pia Mnyika aliomba Bunge liruhusiwe haraka kujadili hoja za madai ya madaktari ili kuisimamia serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 (2) ili kupitisha maazimio kupata suluhu ya mgogoro huo.

“Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa maelezo bungeni kuwa tarehe 28 Juni, 2012 serikali itatoa kauli bungeni kuhusu suala la mgomo wa madaktari, hata hivyo kauli hiyo itatolewa kwa mujibu wa kanuni ya 49 (1) hivyo Bunge halitaruhusiwa kujadili kauli husika na hivyo kukoseshwa fursa ya kuisimamia serikali kwa niaba ya wananchi.

Alisema Bunge linakoseshwa fursa ya kusikiliza upande wa pili wa madaktari na wahudumu wengine wa afya ambao walipewa nafasi ya kuwasilisha maelezo na vielelezo vya upande wao kwenye Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii.

Mnyika alidai kumshangaa Naibu Spika, Job Ndugai, kudai kuwa tayari Kamati ya Huduma za Jamii imewasilisha taarifa bungeni wakati wabunge hawajapewa nakala husika na wala haijawasilishwa kwenye Bunge kwa ajili ya kujadiliwa.

“Ikumbukwe kwamba jana tarehe 26 Juni 2012 niliomba muongozo kuhusu kauli za mawaziri kwa mujibu wa kanuni ya 49 (2) na 116, hata hivyo niliruhusiwa kuomba kutoa maelezo kuhusu kauli ya serikali juu ya utekelezaji wa madai ya madaktari na uboreshaji wa masilahi ya madaktari.

Mnyika alisema kuzembea ama kupuuza kuchukua hatua dhidi ya udhaifu uliojitokeza kutaleta madhara zaidi kwa kuwa hata serikali ikichukua hatua za kudhibiti mgomo kwa kutumia vyombo vya dola, madaktari na watumishi wa afya wataendelea na mgomo wa chini kwa chini, hivyo afya na maisha ya wananchi yataendelea kuathirika kwa muda mrefu zaidi.

“Ikiwa wabunge tutaelezwa ukweli na kupewa taarifa kamili tutaweza kuisimamia serikali na kuwaeleza ukweli madaktari kipi kinawezekana na kipi hakiwezekani na nichukue fursa hii kuwaomba madaktari kufanya kila kinachowezekana kuokoa uhai wa wagonjwa katika kipindi hiki kigumu,” alisema Mnyika

Advertisements

7 thoughts on “SERIKALI MBONA HAMTUFARIJI; TUNALIA MAISHA MAGUMU, HAKUNA MATIBABU WALA USALAMA WA WATETEZI WETU.

 1. Ni ushauri tu wa kuongeza madai yao yaani baada ya magari pia serikali iwapatie ndugu zetu hawa SILAHA ili waweze kujilinda kutokana na unyeti wa sehemu waliyopo na umuhimu wao, pia kama inawezekana madaktari bingwa wawekewe ulinzi kabisa.(Nasisitiza – wapatiwe na serikali sambamba na mafunzo ya namna ya kujihami na kuzitumia)

 2. Kupigwa kwa Dr. Ulimboka, kumepelekea kutengenezwa kwa “conspiracy theories” mbalimbali kuhusu tukio hilo, na wengi wamesha reach conclusion kuwa hiyo ni “inside job” na imefanywa na vijana wa ‘sehemu’ wajulikanao kama “the oparatives” ndani ya ‘sehemu’!, hivyo ni muhimu sana rais JK kama Amiri Jeshi Mkuu, kwenda kumfariji Dr. Ulimboka, with “genuine heart felt feelings za pole” katika move ya kuuthibitishia umma kuwa uvamizi ule is not “inside” job, bali umefanywa na wahalifu, kama uvamizi mwingine wowote!.

  Nawaombeni wenzangu, “please don’t assume or insinuate any rush conclusions”, tuwe wavumilivu na wastahimilivu kusubiri majibu ya ukweli ambayo its only “time will tell”!.

  Kilichomtokea Dr. Ulimboka sio kitu kigeni, na sio mara ya kwanza kutokea kama alivyodai kamanda Kova, bali Dr. Ulimboka is such lucky guy who will “live to tell”!, wenzake kama kina Bazigiza, wale wafanya biashara wa madini, Wakili fulani, Prof. Jwani Mwaikusa na wengine wengi, they were not so lucy!.Huu pia ndio wakati muafaka wa kujadili, hawa “oparatives” what are they capable of and what they are not, ili tupate “clear conscious” what is “inside job” and what is “isolated events”!.

  Lets, wish Dr. Stephen Ulimboka, a speedy recovery!

  God Bless him!.

 3. ‘Conspiracy theory’ Number 1: ” It is “inside job”!.
  theory hii ambayo ndiyo ya walio wanaamini kabisa ile ni kazi ya serikali, kwa Msingi kuwa yeye ndio chanzo cha mgomo toka mwanzo, kwa hiyo, akishughulikiwa, mgomo ndio utamalizika rasmi, hivyo serikali ikawatumia vijana wake waitwao “the oparatives” wamshughulikie vile wataona inafaa, na kweli vijana wakaingia kazini na kilichotokea ni motokeo ya kazi “nzuri” ya vijana wale ambao wameitekeleza vibaya (incomplete), hivyo sasa kui embarass serikali!.

  Hakuna ubishi, “the oparatives wapo”, na hizo ndizo kazi zao, lakini naomba kutofautiana na wanaoamini its an ‘inside job’, kwa sababu ili “oparatives” waingie kwenye any ‘covert’ oparation, lazima kwanza waweke malengo, “what do they want to achieve”, ili kujaustify “the motive behind”, na kabla ya utekelezaji, lazima wapime, “impact” na “consequences” ndipo huamua “the best way” ya utekelezaji, na kwa vile “they are proffessionals”, siku zote hutekeleza with very high degree za ‘precise’ na leaving no trace behind!.

  Kilichomtokea Dr. Ulimboka ni kazi ya “amateures” kwa kuacha loop holes kibao, uta doubt kama ile ni kazi ya “professionals”, hivyo inawezekana kabisa sio “inside job”, unless kilichofanyika kiwe ni tactics za vijana wa “inside job” to carry out kihovyo hovyo ili ionekana ni amateures na huko kumuacha aishi pia ndio lengo na sio aliachwa kuishi kwa bahati mbaya!.

  Normal comon sense inanishawishi nijiulize, kama Dr. Ulimboka ndie adui wa serikali, kama serikali hiyo hiyo imeamua kumshughulikia kwa njia hiyo ili iachieve nini?. Ule msemo wa mchawi, mpe mwanao akulelee kwa imani kuwa hawezi kumdhuru!, hivi inawezekana kweli serikali yetu ndio iliyomshughulikia Dr. Ulimboka na kwa nanma ile?!. Kama ni kweli, hii ni kazi ya “inside job”, then for sure, “hii itakuwa ni serikali ya vichaa!”.

  Conspiracy Theory No. 2. Could it be just a “Smear Caipaign”?!.
  Adui wa adui yako ni rafiki yako, kwa vile Dr. Ulimboka ndiye kiongozi wa hii migomo, na hii migomo imeishaipasua sana kichwa serikali, hadi rais Jakaya Kikwete, akautangazia umma kuwa mgomo ule ni wa mwisho, na kwa vile sasa mgomo umeibuka tena na kuwafanya wote waliojifanya kuuepusha tangu mwanzo kuonekana wajinga, akiwemo rais JK, its obvious Dr. Ulimboka ndie alishaonekana ni adui wa serikali na kila mtu anajua, hivyo jambo lolote litakalomtokea Dr. Ulimboka, automatically, fingers zitakuwa pointed kwa serikali kuwa sio mshukiwa bali ni mhusika mkuu!.

  Kwa msingi kuwa, Dr. Ulimboka ni adui wa serikali, automatically atakuwa ni rafiki wa maadui wa serikali, hivyo sasa amegeuka target nzuri kwa maadui wa serikali waliomo within, ambao hawaitakii mema serikali yao, wakaamua kumshughulikia Dr. Ulimboka ili kuiembarass serikali kunyooshewa vidole vya lawama kwa utaratibu unaojulikana kama “smear Campagn”!.

  Could it be?.

  Pole Dr. Ulimboka.

  Get well soon!.

 4. Nathibitisha kua kupigwa kwa Dkt Ulimboka serikali ilihusika au kufahamu na kuruhusu itokee kwa sababu hizi:
  Mgomo wa madaktari ni kitu kikubwa, kinahatarisha usalama wa nchi. Kiutaratibu vyombo vyote vya ulinzi vilipaswa kufanya uchunguzi

  Katika uchunguzi wao viongozi wote wa madaktari walitakiwa kuchunguzwa masaa 24 haya yafuatayo:
  1. Wanajadiliana na kupanga nini
  2. Wanawasiliana na nani na kuongea nini
  3. Wako wapi na wanafanya nini

  Narudia, ni ktk masaa yote 24 na hii inahusisha vinasa sauti, eavesdropping, suprise meetings(kama huyo abeid wa ikulu), top classified field agents ktk taxi, wapiga debe, barmaid etc.
  Pia kungekua na physical suspect tracking, kuwafatilia wako wapi na wanafanya nini muda wote.

  upelelezi wote huu kitaaluma ungesimamiwa na vyombo vitatu tofauti, kila kimoja kikijiendesha kivyake kwa ajili ya kua na fair analysis wakati wa kumshauri mkuu wa nchi
  1. Usalama wa Taifa
  2. Idara ya ujasusi jeshini
  3. police

  kama taratibu hizi hazikufanyika, Tanzania haiko salama!

  ushahidi wa kuhusika serikali
  1. Abeid kutoka ikulu
  2. Kuvamiwa Leaders (kumbe walikua wanamfatilia)
  3. Watekaji kudai kawasumbua(ni kweli walikua na hasira kwa kuwalaza nje kumfatilia masaa 24)
  4. Gari halikua na Plate no kusafiri umbali mkubwa(sio ishu sana), ila hizo bunduki na mazingira ya nyumba walizompeleka ni safe house
  5. Kipigo alichopewa ni very pro, walipiga kama wanampiga jasusi mwenzao. (sina uhakika ilikuaje hawakutumia umeme)
  6. Mabishano namna ya kumuua, kama ni kwa sumu au ajali(Kwa mfumo wetu wa ulinzi kama nilivyosema awali unahusisha vyombo vitatu tofauti. Napata hisia waliungana kumtesa ila kumuua wakatofautiana, kila chombo kina kiongozi wake na anafanya kazi kivyake bila kushirikisha upande mwingine)
  7. Hakukua na maandalizi(kawaida ya serikali hii haipangilii mambo na viongozi kuamua kwa pamoja kama wanamuua ulimboka au hapana)

  kama nimechemka, wanausalama wenzangu mtanisaidia

 5. Plan ilikuwa:
  Ulimboka anapigwa na kuuawa,
  mwili unaokotwa mabwepande,
  Polisi wanaingilia kati investigation,
  wanatafutwa waliokuwa nae for the past 24hrs,
  Wajumbe wote wa kamati ya jumuiya ya madaktari wanakamatwa,
  Key people wa MAT wanakamatwa,
  wote wanawekwa ndani kusaidia polisi upelelezi,
  Madaktari waliogoma wanachanganyikiwa,
  Pinda anatoa mkwara mzito na madaktari wanakosa mwelekeo,
  mgomo unafika mwisho,
  Pinda na serikali yake wanaibuka kidedea.
  Kamati ya mgomo inasahaulika mahabusu!
  Just trying to decode the plan the government had.

 6. Kwani huyo Uli ni nani nchi hii, mnaacha kujadili watanzania wenzetu wanaokufa pale Muhimbili na kwengine kwa kukosa huduma za madaktari mnazungumzia mtu ambaye hakutaka kutekeleza wajibu wake kutibu wengine hadi yeye anaumia, Mungu hamfichi mnafiki, vizuri hajafa ili ajue uchungu wa kuugua halafu anayekuuguza anahangaika na vikao visivyokwisha kudai kitu kisichowezekana, mnaujua mshahara wa mwalimu anayeanza kazi leo huku akiwa na degree yake. Hizi ni siasa ndani ya kazi za kitaaluma, adui wa adui yako ni rafiki kwako na unaweza kumtumia vyovyote vile ili kubadilisha hali ya hewa. Serikali imuue au imteke Ulimboka wa kazi gani na ana nguvu gani, pongezi kwa madaktari wote ambao wanaendelea kuhudumia watanzania huku wakisubiri kutekelezewa madai yao pasipo kuwaumiza watanzania wasio na hatia, wangapi wamekufa mgomo wa february halafu tunasubiri daktari aumie tuisingizie serikali, wanaotafuta umaarufu wa kisiasa tunawaona hata bungeni wakitumia mgomo huu kujipatia mtaji zaidi, wananchi wanajua nani mkorofi kati ya serikali na madaktari wanaogoma kwa sasa. Hata pole Ulimboka kwa kilichotokea inaweza kuwa ni majambazi tu , kwa kudra zake utapona na ukweli utajulikana.

 7. Asante Mh. Mnyika kwa kuomba bunge liruhusu mjadala wa madaktari na kuwasihi madaktari kufanya kila linalowezekana kunusuru maisha ya wagonjwa. Well done

Comments are closed.