KAULI YA RAIS JAKAYA KIKWETE YA CHOCHEA MGOMO WA MADAKTARI

RAIS JAKAYA KIKWETE


  • SERIKALI HAINA NIA YA DHATI YA KUMALIZA MGOGORO HUO.

  • RAIS HAJAPATA TAARIFA SAHIHI AU YEYE MWENYEWE AMEAMUA KUPOTOSHA …. TUNASIKITIKA KUONA WATANZANIA WANADANGAYWA; MADAKTARI.

  • MUDA WA KUBADILI HALI HIYO UMEFIKA, NI MGOMO TU UNAOWEZA KUWASAIDIA WATANZANIA MASKINI WANAOTIBIWA KWENYE HOSPITALI HIZO; MADAKTARI BINGWA

  • HATUPENDI KUBISHANA NA MAMLAKA YA RAIS, ILA JK AKIAMUA ANAWEZA KULIMALIZA BADALA YA KUTOA VITISHO.


AGIZO la Rais Jakaya Kikwete kuwataka madaktari wanaoendelea na mgomo kuacha kazi limechochea mgomo na ukubwa wa sakata hilo baada ya madaktari bingwa ambao awali hawakuhusika kabisa na mgomo huo, kutoa tamko wakimtaka kiongozi huyo wa nchi kuwatimua wao kwanza kabla ya wale wa ngazi ya chini.

Madaktari bingwa ambao walitangaza kujiunga na wenzao Jumapili July 3, 2012 baada ya kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dk. Steven Ulimboka, walisema wataendelea na mgomo wao hadi hapo serikali itakapo warejesha kazini madaktari na madaktari wanafunzi wote waliofukuzwa.

“Madaktari bingwa hatuwezi kufanya kazi bila madaktari wa chini yetu… kama serikali imedhamiria kuwafukuza kazi hawa na interns (waliopo kwenye mafunzo ya vitendo) ianze na sisi.”  Alisema kiongozi wa madaktari Dk. Catherine Mng’ong’o

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la watoto kwenye hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Katibu wa Jumuiya hiyo Dk. Edwin Chitage alisema wako tayari kukutana na rais kama anaitaji kuujuwa ukweli.

“Rais hajapata taarifa sahihi au yeye mwenyewe ameamua kupotosha … tuko tayari kumweleza ukweli kama wasaidizi wake wanamdanganya, tunasikitika kuona watanzania wakidanganywa.

Katibu huyo alisema moja ya madai yao yalikuwa kuomba kila hospitali ya wilaya ipate mashine moja ya X-ray kwa vile, haiwezekani nchi nzima kukosa mashine ya CT-Scan wakati bei yake ni sawa na gari aina ya shangingi moja la kiongozi wa serikali,” alisema Dk. Chitage.

“Wanaelezwa hoja dhaifu za kuonyesha kwamba madaktari hatuna uzalendo wakati madai yetu pia ni kwa maslahi ya wagonjwa wote hasa pale tunapodai mazingira bora ya kazi.

Katibu huyo alikiri kwamba posho ni sehemu ya madai yao huku akisisitiza kwamba hawang’ang’anii nyongeza hiyo badala yake kuwepo kwanza na mazingira bora ya kazi ili kutoa tiba sahihi kwa mgonjwa.

Dk. Chitage alisema hawapendi kubishana na mamlaka ya rais huku akisisitiza uwezo wa kumaliza hili ni Kikwete kukaa nao meza moja kwa ajili ya kuzungumza badala ya kutoa vitisho.

Akitoa tamko la madaktari bingwa waliokutana kwa dharura Jumatatu July 2, 2012 na kamati ya jumuiya ya madaktari kujadili hotuba ya rais Kikwete, kiongozi wa madaktari hao mabingwa Dk. Mng’ong’o alisema huo ni msimamo wa madaktari wenzake, huku akitaka kufunguliwa kwa meza ya majadiliano ya dhati yenye nia ya kumaliza mgogoro wao.

“Tuko tayari kufukuzwa iwapo madai yetu ya msingi hayatatekelezwa na kama kuondoka waanze kutufukuza sisi kwanza,” alisema Dk. Mng’ong’o baada ya kumalizika kwa kikao cha madaktari bingwa kilichoketi kwa zaidi ya saa tano kwenye viunga vya hospitali hiyo.

Alisema hata wao hawana sababu ya kuendelea kufanya kazi katika mazingira magumu na kuwaona Watanzania wakifa kwa kukosa vifaa, tiba na dawa.

Dk. Mng’ong’o alisema madaktari hapa nchini wamefanya kazi katika mazingira magumu kwa muda mrefu hivyo wakati wa kubadili hali hiyo umefika na kuwasaidia Watanzania maskini wanaotibiwa kwenye hospitali hizo.

“Tuna mheshimu rais na mamlaka zote ila tunachoamini ni kuwepo kwa meza huru ya majadiliano kati yetu na yeye kwa sababu nafasi ya kumaliza kero hii anayo,” alisema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Dk. Godbless Charles alihoji sababu za kuwepo kwa taarifa tofauti kuhusu ongezeko la mishahara wakati waliishauri serikali kuwa wazi kuhusu nyongeza hiyo.

“Kumekua na majibu tofauti mfano Waziri wa Afya na UStawi wa Jamii aliliambia Bunge kwamba nyongeza ya mishahara ni asilimia 15. Hotuba ya rais Kikwete inasema nyongeza hiyo ni asilimia 20 wakati ripoti ya wataalam iliyokutana na kamati ya Waziri Mkuu ilipendekeza asilimia 25 je, nia ya serikali iko wapi?

“Wakati viongozi wa serikali wakitoa taarifa zinazotofautiana ripoti ya ufafanuzi wa madai na hoja za madaktari iliyotokana na majadiliano ambapo tulikuwa wajumbe hatukutoa pendekezo lolote juu ya ongezeko la mshahara,” alisema Dk. Godbless.

Alisema tangu kuanza kwa mgogoro kati ya madaktari na serikali jumla ya vikao sita viliketi kati ya hivyo vikao vinne vilijadili juu ya uboreshaji wa huduma za afya kwa watanzania.

“Ni masikitiko yetu kuwa ripoti ya ufafanuzi wa hoja na madai yetu iliyotolewa Juni 31 mwaka huu, taarifa ya waziri wa afya, taarifa ya waziri mkuu ndani ya Bunge na hotuba ya rais haikuzungumzia kwa jinsi gani serikali itaboresha huduma za afya kwa watanzania,” alisisitiza Dk. Godbless.

Advertisements

One thought on “KAULI YA RAIS JAKAYA KIKWETE YA CHOCHEA MGOMO WA MADAKTARI

  1. THE tanzania is dying why should us watch it is better to die like MTEMI MIRAMBO rather than watching this death

Comments are closed.