IKULU YAWABEZA VIONGOZI WA DINI, YASEMA MGOMO UMEKWISHA HAKUNA CHA KUJADILI

MKURUGENZI WA MAWASILIANO IKULU SALVA RWEYEMAMU

Kwa mara nyingine tena Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa kauli na kusisitiza kuwa mgomo wa madaktari umekwisha na kuwabeza viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu walio jitolea kujaribu kusuluhisha mgogoro huo wakishauri Rais Jakaya Kikwete akutane na madaktari pamoja na viongozi hao ili kutafuta ufumbuzi wa mgogoro unaoendelea.

Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu, alisema kuwa viongozi hao wa dini mara zote walipoomba kukutana na viongozi wa serikali, akiwemo Rais, hawakupitia kwa mtu yeyote isipokuwa waliomba moja kwa moja na wakakubaliwa.

Akizungumza jioni ya Jumapili Julai 8 2012, Rweyemamu alisema “Hawana sababu ya kupitia kwa watu wengine kuomba kukutana na viongozi wa serikali.”

Aliongeza kuwa mgomo wa madaktari umeisha na walioamua kuendelea na kazi hii muhimu sana ya kutibu binadamu wamerudi kazini, jambo ambalo ni jema sana.

Kuwa sasa si wakati wa kulumbana tena bali ni wakati wa kusonga mbele badala ya kurudi nyuma kwa sababu hakuna mgomo tena wa kujadiliwa aliongeza kwa sauti iliyo onyesha msisitizo.

Awali Jumamosi Julai 7 viongozi hao wa dini walikutana na Jumuiya ya Madaktari na wanaharakati jijini Dar es Salaam katika harakati za kujaribu kuwasihi wasitishe mgomo ili kuwanusuru wananchi na hivyo kupendekeza kuwa iundwe kamati huru mapema iwezekanavyo ili kupata ufumbuzi wa sakata hilo.

Akisoma tamko la viongozi hao, Mkurugenzi wa Baraza la Habari la Kiislamu (Bahakita), Hussein Msopa, kwa niaba ya viongozi hao, alisema kwamba kuundwa kwa kamati huru  na kuchunguza namna ya kutatua mgogoro huo pamoja na kubaini wahusika wa tukio la kupigwa na kuteswa kwa Kiongozi wa madaktari Dk. Ulimboka.


“Tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande Dk. Ulimboka ni la kusikitisha… na tunamuomba Rais Kikwete aunde tume huru itakayo jumuisha madaktari wenyewe, viongozi wa dini, wanaharakati na wanasheria kubaini kiini cha tatizo hilo,” alisema Msopa.

Rweyemamu alifafanua kuwa mara ya mwisho madaktari hao walipoitwa kukutana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, walikataa wakidai kuwa waziri hakuwa na jambo jipya la kuwaambia.

“Tangu madaktari walipoanza kudai maslahi zaidi, serikali ilifanya jitihada kubwa za kukutana nao. Mbali na Kamati ya Majadiliano ya Serikali, madaktari pia wamekutana na Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kamwe serikali haijapata kukataa kukutana na viongozi wa madaktari,” aliongeza Rweyemamu.

Katika tamko lao hilo, pia viongozi hao pamoja na kudai tume huru waliomba serikali kufuta kesi iliyofunguliwa dhidi ya madaktari waliofukuzwa kutokana na mgomo na kuwarejesha kazini ili kumaliza mgomo huo waliodai unaathiri afya za Watanzania.

Advertisements

One thought on “IKULU YAWABEZA VIONGOZI WA DINI, YASEMA MGOMO UMEKWISHA HAKUNA CHA KUJADILI

  1. You can certainly see your enthusiasm within the work you write.

    The sector hopes for more passionate writers like you who aren’t afraid to mention how they believe. All the time go after your heart.

Comments are closed.