PAMOJA NA KUOKOA ZAIDI YA SHILINGI 3BILIONI HATUA ZA KINIDHAMU KUMKABILI WAZIRI WA NISHATI, KATIBU MKUU PAMOJA NA MKURUGENZI WA TANESCO.

KATIBU MKUU WA WIZARA YA NISHATI NA MADINI ELIAKIM MASWI

  • NI KWA KUKIUKWA KWA SHERIA YA MANUNUZI YA UMMA
  • WENYEWE WAWATAKA WATANZANIA WAZALENDO KUWAUNGA MKONO KATIKA MAPAMBANO YAO DHIDI YA UFISADI.

Sintofaham baina ya wabunge pamoja na wananchi imejitokeza kutokana na kuibuka kwa maoni tofauti dhidi ya hatua gani zichukuliwe dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Pofesa Sospeter Muhongo, Katibu wake Mkuu Eliakimu Maswi  pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando katika sakata la ukiukwaji wa sheria ya Manunuzi ya Umma.

Ukiukwaji huo wa sheria ya ununuzi wa umma ulifanyika kwa kuipa zabuni Kampuni ya Puma Energy ya kununua mafuta  ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na kuziweka kando kampuni zilizokuwa zimechaguliwa kupitia mchakato halali wa zabuni ya Tanesco.

Sakata hilo liliibuka baada ya kusimamishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando ikiwa ni hatua baada ya kukataa kutii maelekezo ya Wizara.

Chanzo cha mgawanyiko huo ni sababu zilizotolewa na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini kwamba waliwapa Tanesco fedha za kununua mafuta mazito ili kuiepusha nchi na mgawo wa umeme, lakini wakaelekeza mafuta hayo yanunuliwe Kampuni ya Purma ambako bei ya lita moja ni Sh1,460.

Kwa kufanya hivyo uongozi wa Wizara unadaiwa kuokoa kiasi cha Sh3 bilioni ambazo zingetumika kama mafuta yangenunuliwa katika kampuni zilizokuwa zimeshinda zabuni kupitia mchakato wa Tanesco.

Ndani ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, baadhi ya wajumbe walinukuliwa wakisema kuwa hata kama Muhongo na Maswi walikuwa na nia njema ya kuokoa fedha za umma, lakini waondoke kwa kukiuka sheria.

Hoja hiyo inapingwa na baadhi ya wajumbe wanaosema uamuzi waliofanya (Muhongo na Maswi) unapaswa kupongezwa, kwani ni mwanzo wa kumaliza ufisadi ulioota mizizi ndani ya Tanesco na Wizarani kwa ujumla.

Maswi katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam Jumanne Julai 24 2012, aliwashutumu baadhi ya wamiliki wa kampuni za mafuta akisema wamekuwa wakifanya vitendo vya ufisadi na kutaka Watanzania wazalendo kuunga mkono juhudi za wizara yake za kupambana na hali hiyo.

Maswi alifafanua kwamba, baadhi ya kampuni (majina tunayo) zimekuwa zikinunua mafuta kwa bei rahisi kutoka Puma Energy na kisha kuiuzia  IPTL kwa bei ya juu na kupata mabilioni ya shilingi.

Mtendaji mkuu huyo wa wizara alisema haiwezekani kwa akili ya kawaida Serikali iache kusimamia fedha za umma kwa kuhakikisha mafuta yananunuliwa kwa bei nafuu moja kwa moja toka Puma Energy badala ya kununua kwa mtu wa kati ambaye anaongeza bei ya mafuta hayo.

Akitoa mfano wa ufisadi unaofanywa na baadhi ya kampuni, Maswi alisema kuwa, Januari mwaka huu kampuni moja kati ya zilizopata zabuni ya kupeleka mafuta Tanesco, ilinunua mafuta kutoka kwa Puma  Energy kwa bei ya Sh 1,068 kwa lita moja ya ujazo, kisha ikaenda kuuzia IPTL kwa Sh1,860.

“Kwa hiyo, haya mambo Watanzania wanapaswa kuyafahamu. Na ninyi waandishi msaidie kuandika mambo yenye maslahi kwa taifa. Mimi nitasimamia maslahi ya taifa, hatuwezi kuacha kununua mafuta kwa bei rahisi halafu tununue kwa bei ya juu. Shilingi moja tu kwa mfano, katika maisha ya Mtanzania ni kubwa. Si mnaona mkipandishiwa bei ya dizeli na petroli mnavyolalamika!” alisema.

Akizungumzia tuhuma za kukiuka sheria kwa kuipa zabuni PUMA Energy, Maswi alisema mchakato wote ulifanyika na kukamilika kabla hajateuliwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

“Ikumbukwe kuwa niliteuliwa kuja Wizara ya Nishati na Madini, tarehe 22 Julai, 2011 siku ya Ijumaa na nilianza kazi kama Kaimu Katibu Mkuu Julai 25, 2011 siku ya Jumatatu. Kabla ya kuanza kazi niliwaeleza wenzangu utendaji wangu na ninavyopenda twende kwa kufuata utaratibu,” alifafanua Maswi.

Mwishoni mwa mwaka 2010/11 kulikuwa na mgawo mkubwa umeme nchini, na Serikali kulazimika kuingilia kati kuhakikisha mgawo huo unaondolewa na kuitaka IPTL kuwasha mitambo yake katika kiwango cha megawati 100.

“Aliyefanya  hivyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco na siyo Wizara. Ikumbukwe pia kipindi hicho IPTL ilikuwa inasimamiwa na Wakala wa Vizazi na Vifo (Rita) kwa kuwa kulikuwa na amri ya kufilisi (under liquidation process).” alisema Maswi

Aliongeza kwamba,  Tanesco ilifanya hivyo kwa barua Kumb. Na. SMSC/MSC/IPTL ya Juni 10, 2011 ambapo kampuni hiyo ilitakiwa kuanza kufua umeme hadi Desemba 2011 na kuondoa mgawo wa umeme.

“Aidha, Tanesco walipeleka barua RITA wakitaka mafuta ya kuendesha mitambo yapatikane. Ieleweke kuwa ili kuendesha  IPTL kwa siku moja tunahitaji MT500,” alifahamisha Maswi.

Advertisements