MILYA ATANGAZA KUWANIA KITI CHA SENDEKA 2015

JAMES Ole Millya, kada wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi na Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama hicho (UVCCM), mkoa wa Arusha aliyetimkia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),  ametangaza rasmi kuwania ubunge jimbo la Simanjiro katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2015.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Mirerani wilayani Simanjiro , Ole Millya alitangaza elimu, ajira kwa vijana na mazingra bora ya ufugaji kuwa baadhi ya vipaumbele atakavyovisimamia akifanikiwa kushinda ubunge.

Katika kipengele cha ajira, alisema atahakikisha madini ya Tanzanite yanayopatikana Simanjiro, Tanzania pekee duniani yanawanufaisha kwanza vijana wa wilaya hiyo kwa wenye sifa za kitaaluma kwa kuajiriwa kwenye mgodi wa wawekezaji wa Kampuni ya Tanzanite One.

“Tanzanite kuwanufaisha kwanza vijana na wananchi wa Simanjiro siyo ubaguzi bali ni kutumia rasilimali tulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu kujiendeleza na kuboresha maisha yetu, hili nitalisimamia kikamilifu bila kulionea aibu,” alisema Ole Millya

Katika kufanikisha ajenda hiyo, Ole Millya aliyewania uteuzi wa kuwania ubunge Simanjiro kupitia CCM na kuangushwa na mbunge wa sasa, Christopher Ole Sendeka alisema atahakikisha ajira zisizohitaji utaalamu zinatolewa kwanza kwa vijana wa Simanjiro.

Alidai hivi sasa ajira hizo licha ya kutozingatia wana Simanjiro kwanza, pia zinatolewa kwa upendeleo unaozingatia wahusika kujuana au kufahamiana na wakubwa kama wabunge, mawaziri na viongozi wa serikali.

Alitaja vipaumbele vingine kuwa ni uwezeshaji kiuchumi kwa kuboresha mazngira ya ufugaji na elimu kwa watoto wa jamii ya wafugaji wa Kimaasai ambao ndio wakazi wengi wa jimbo hilo kwa kujenga shule na kuboresha mazingira ya kusomea ikiwemo babweni kwa watoto wa kike ambao wengi wao huozeshwa wakiwa na umri mdogo.

Akitumia usafiri wa Chopa kuzunguka katika vijiji vya Narakauwo, Naberera, Orkesmet, Mirerani na Loibosiret akiwa ameongozana na Mjumbe wa Kamati Kuu wa Chadema (CC), Godbless Lema, Ole Millya alitamba kushinda kiti cha ubunge kutokana na uungwaji mkono anaopata tangu ahamie upinzani tofauti na alivyokuwa CCM.

Kwa upande wake, Lema alisema eneo la Mirerani lilipaswa kuwa moja ya maeneo tajiri nchini kutoka na Tanzanite lakini hali ni tofauti kwani wakazi wake wanaishi kwenye umaskini wa kutupwa kiasi kwamba wapo wasiomudu milo miwili kwa siku huku wakazi wa Jaipur nchini India yanakosafirishwa madini hayo kwa wingi wakiishi maisha bora.

“Tanzania yenye utajiri wa madini kama Tanzanite, mlima wa pili kwa urefu duniani, mbuga za wanyama, gesi na rasilimali kadhaa haipaswi kuendelea kuwa omba omba duniani na wananchi wake kuishi kwenye lindi la umaskini kama ilivyo sasa, Simanjiro ikiwemo,” alisema Lema

Lema anayetumia muda mwingi kuzunguka sehemu mbalimbali nchini katika kampeni ya Chadema ya ‘Vuguvugu la mabadiliko’ (Movement for change, M4C), tanguubunge wa jimbo la Arusha mjini upotenguliwa na Mahakama Kuu Aprili 5, mwaka huu aliwataka wananchi kuinyima kura CCM 2015 akidai imedidimiza uchumi wa taifa licha ya utajiri na rasilimali zilizopo.

Alphonce Mawazo, diwani wa Kata ya Sombetini, Manispaa ya Arusha aliyetimkia Chadema aliwaasa Watanzania kuondoa uoga na kuwakosoa viongozi wa ngazi zote wanapokwenda kinyume na matakwa na matarajio umma badala ya kulalamika kichinichini.

Advertisements