DK. STEVEN ULIMBOKA BAADA YA KUTUA JIJINI DAR JUMAPILI AGOSTI 12 2012 AKITOKEA AFRIKA YA KUSINI ALIPOKUWA ANATIBIWA ANAONEKANA AKIWA AMEZUNGUKWA NA WANANCHI WALIOJITOKEZA KUMLAKI HUKU WALINZI WAKE WAKIJARIBU KUMSIDIKIZA KWENYE GARI .
  • AWASHUKURU WATANZANIA WOTE NA KUSEMA AMERUDI KUMALIZIA KAZI ALIYOANZA.

  • WANANCHI WALIHOJI IKITHIBITIKA YALE YALIOANDIKWA NA MWANAHALISI NI YAKWELI GAZETI HILO KULIPWA FIDIA?

Dk. Steven Ulimboka ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Tanzania amerejea Jumapili Agosti 12 2012 akitokea nchini Afrika kusini ambako alipelekwa na Madaktari wenzake tangu Juni 30 2012 baada ya kutekwa na kupata kipigo na kundi la watu wasiojulikana.

Tukio la kurudi nyumbani kwa Dk. Ulimboka awali  h alikutangazwa na utaratibu mzima kufanywa kwa siri kubwa liliwastajabisha wengi, kwa umati mkubwa uliojitokeza uwanjani hapo kumlaki.

Daktari huyu ambaye amejizolea umaarufu hapa nchini kwa harakati zake bila kuchoka kudai haki na maslahi bora pamoja na huduma bora hospitalini aliwasili majira ya saa nane mchana katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam na SA Airways na kusababisha mlipuko wa shangwe nderemo na vifijo kutoka kwa umati mkubwa uliokuwa unamsubiri.

SEHEMU YA UMATI WA WATU WALIOJITOKEZA KUMLAKI DK. STEVEN ULIMBOKA BAADA YA KUFIKA JIJINI DAR AKITOKEA AFRIKA YA KUSINI ALIPOKUWA ANATIBIWA MAJERAHA YALIYOSABABISHWA NA KIPIGO ALICHOKIPATA KUTOKA KWA WATU WASIYO JULIKANA

Akionekana ni mwenye afya nzuri huku akiwa amevalia tisheti na sura yake kupambwa na tabasamu ingawa alionyesha uchovu ambao wengine walisema ni wa safari,  alifanikiwa kusema machache huku wapokeaji wake wakimwekea ulinzi na kufanya iwe ngumu kwa wanahabari kupata picha pamoja na kunasa kauli yake.

“Nimepona ndugu zangu….nawashukuru nyote mlioniombea, watanzania, madaktari, ndugu na jamaa zangu nashukuru pia kunisaidia kupata matibabu bora hadi leo hii narudi nyumbani, niko fiti  nikitembea mwenyewe,” alisema Dk. Ulimboka.

DK. STEVEN ULIMBOKA AKIWA AMEBEBA UWA AKIINGIA KWENYE GARI AMBALO LILIKUJA KUMPOKEA BAADA YA KUWASILI KUTOKA AFRIKA KUSINI ALIPOKUWA ANATIBIWA.

Taarifa za ndani zinadai kuwa hakuweza kuongea mengi kutokana na ushauri aliopewa na wanasheria wake kwa kuwa kesi yake bado ipo mahakamani.

Dk. Ulimboka alitekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye Msitu wa Pande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ambapo Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam lilidai kuwa aliyemteka daktari huyo ni raia wa Kenya ambaye tayari wanamshikilia.

NDUGU JAMA NA MARAFIKI WAKIONYESHA NYUSO ZA KUTOKUAMINI MACHO YAO BAADA YA KUMLAKI DK. STEVEN ULIMBOKA ALIPO REJEA AKITOKEA AFRIKA KUSINI ALIPOKUWA AKITIBIWA.

Taarifa hiyo ya polisi inashindwa kukubalika masikioni mwa wananchi wengi huku kwa upande mmoja jamii ikitaka kujua ukweli wa jambo lililopelekea gazeti la Mwanahalisi kufungiwa, ujio wake safari hii umetoa imani mpya kuwa watanzania wataujua ukweli kupitia kwake.

Naye Katibu wa Jumuiya hiyo Dk. Edwin Chitage amewaahidi wanahabari kuitisha mkutano mapema ili kujuza umma wa watanzania na dunia kwa kina kuhusu kupona kwa Dk. Ulimboka

GARI LILILO MBEBA DK. ULIMBOKA KUTOKEA UWANJA WA NDEGE MARA TU BAADA YA KUWASILI AKITOKEA AFRIKA YA KUSINI ALIPOKUWA AKITIBIWA LIKISUKUMWA NA BAADHI YA WANANCHI WALIOJITOKEZA KUMLAKI.

Advertisements