NAPE ACHANA NA PROPAGANDA CHAFU; MNYIKA

JOHN MNYIKA

  • AMTAKA AZITAJE NCHI NA WAFADHILI WANAO KISAIDIA CHAMA CHA CHADEMA NA WAMETOA KIASI GANI?
  • ASEMA KWANZA ALIANZA WASSIRA NA SASA NAPE AHOJI KAMA MIKAKATI HII MICHAFU INA BARAKA ZA KIKWETE.

MBUNGE WA UBUNGO, JOHN MNYIKA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA akizungumza kutokea Dodoma amesema siku ya Jumapili Agosti 12 2012 Katika mitandao ya kijamii kumesambazwa habari zikimnukuu msemaji wa CCM kutoa madai mbalimbali ya uzushi katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu CHADEMA na utekelezaji wake wa mikakati na mipango ya kuwaunganisha watanzania kupitia falsafa ya ‘nguvu ya umma’ katika kuchangia vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika maeneo mbalimbali nchini.

Mnyika ameahidi kutoa tamko kamili na kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa iliyotolewa kwa ukamilifu, hata hivyo kuhusu madai yaliyokwisha sambazwa kwenye mitandao ya kijamii na CCM Mnyika aliyatolea kauli ya awali kama ifuatavyo:

WanaCCM mtanisamehe, lakini imenibidi kutoa kauli hii ya awali kufuatia madai ya uzushi na ya kijinga yaliyotolewa na Msemaji wa CCM dhidi ya CHADEMA.

Madai kama haya yanaendelea kudhihirisha kuwa taifa letu limefika hapa lilipo kwa pamoja na sababu zingine ‘upuuzi wa CCM’. CHADEMA haijawahi kufadhiliwa mabilioni kutoka nje, michango kwenye M4C iwe ni kwenye kumbi za hoteli au vijijini tunapochangiwa na wananchi wenye kutaka mabadiliko ya kweli ni ishara ya imani ambayo watanzania wanayo kwa CHADEMA.

Badala ya CCM kuisingizia CHADEMA kuwa inafadhaliwa na mataifa ya nje kupora rasilimali za nchi ikiwemo mafuta na gesi yanapaswa kupuuzwa kwa kuwa CCM ndio inao wajibu wa kuwatajia watanzania viongozi wa Serikali na CCM waliongiziwa mabilioni Uswisi kuingia mikataba mibovu ya rasilimali za nchi yetu.

Aidha, CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kuwataja kwa majina wanaoingia mikataba mibovu ikiwemo kwenye madini, CCM kwa kuwa ilikubali kuwa ina magamba ya ufisadi irejee kwenye orodha ya mafisadi na kuchukua hatua ya kujivua gamba badala ya kufanya siasa chafu dhidi ya CHADEMA.

Majibu zaidi mnaweza kuyasoma kwenye mnyika.blogspot.com na kuendelea kuunganisha nguvu ya umma kupitia CHADEMA katika kuwezesha Tanzania kupata uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya taifa letu na watu wake wote bila kujali itikadi. Hakuna Kulala, Mpaka Kieleweke

Kuibuka huku kwa CCM na kufanya propaganda chafu ni ishara ya kwamba CCM inaumizwa na namna ambavyo watanzania wanajitokeza kuunga mkono CHADEMA kwa hali na mali hivyo CCM sasa inatapatapa kujaribu kudhibiti wimbi la mabadiliko kwa kutumia siasa chafu.

Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete anapaswa kueleza watanzania iwapo mikakati hiyo michafu ina baraka zake na za serikali anayoiongoza kwa kurejea pia madai yaliyotolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) Steven Wassira kuwa CHADEMA itasambaratishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kwa mbinu mbalimbali.

CCM kwa kuwa imekuwa na kawaida ya kufanya usanii kuhalalisha fedha haramu kama ilivyofanya kwenye chaguzi zilizopita baada ya viongozi waandamizi wa CCM na makada wake kuchota fedha chafu za kifisadi kama zile za kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) na vyanzo vingine vichafu na kuzisafisha kupitia harambee za hadaa zilizofanywa na CCM kwa nyakati mbalimbali; inataka kuichafua CHADEMA inayopata fedha kutoka vyanzo halali kwa njia za wazi ili kukatisha tamaa umma wa watanzania unaochangia vuguvugu la mabadiliko.

Viongozi wa CCM wameamua kujidanganya, kuidanganya Serikali yao na kujaribu kuwapotosha watanzania lakini CHADEMA inatambua kwamba watu wachache wanaweza kudanganyika kwa muda mchache lakini si watu wote wakati wote; na kwamba watanzania wa leo kwa uwingi wao hawawezi kudanganyika na uzushi wa kijinga wa CCM.

Ni ukweli ulio wazi kwamba CHADEMA imekuwa ikifanya harambee kwa uwazi kwa nyakati mbalimbali katika kumbi na katika mikutano ya hadhara ikiwemo ya vijijini ambapo michango hutolewa kwa uwazi, aidha michango kwa njia ya simu inaweza kufuatiliwa na kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba watanzania wameamua kuchangia mabadiliko ya kweli.

Madai ya CCM kuwa CHADEMA imepokea au itapokea mabilioni ya shilingi kutoka mataifa ya nje ni ya uzushi na narudia kwa mara nyingine tena kuitaka CCM itaje majina ya serikali, taasisi ama makampuni ya nje ambayo CCM inadai kwamba CHADEMA imepokea mabilioni ya shilingi katika siku za karibuni au inatarajia kupokea.

Badala ya CCM kuisingizia CHADEMA ilipaswa CCM ieleze watanzania orodha ya vigogo wa Serikali inayoongozwa na wanachama waandamizi wa CCM ambao wanaelezwa kuwa na akaunti nchini Uswisi na nchi zingine wakituhumiwa kupewa fedha za kifisadi kutoka kwa makampuni ya utafutaji wa mafuta, gesi asili pamoja na uchimbaji wa madini.

CCM ilipaswa ieleze watanzania sababu za kuendelea kusuasua kujivua magamba ya ufisadi kinyume na maazimio ya CCM yaliyofikiwa baada ya msukumo wa CHADEMA kutaja orodha ya mafisadi kwa kuwa kati ya mafisadi hao ni pamoja na viongozi wa CCM walioiingiza nchi katika mikataba mibovu.

Advertisements