UHAMASISHAJI WA UMMA KUHUSU SENSA NI JUKUMU LETU SOTE; MAKUNGA.

MKUU WA WILAYA YA HAI NOVATUS MAKUNGA WA PILI KUSHOTO

Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga amewataka viongozi wote wa vyama vya siasa na serikali katika ngazi zote wilayani humo kutoa ushirikiano katika kuhamasisha na kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa wananchi kushirikiana na makarani wa sensa kwa kutoa taarifa sahihi wakati wa zoezi la kuhesabu watu.

Bw Makunga ametoa wito huo wakati anafungua mafunzo ya wasimamizi na makarani wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kwa wilaya ya Hai inayowashirikisha makarani wapatao 644

Ameeleza kuwa utaratibu umeshaandaliwa wa kufanyika zoezi la uhamasishaji katika maeneo yote litakalofanywa na wenyeviti wa vijiji na vitongoji pamoja na waheshimiwa madiwani pamoja na kamati ya sensa ya wilaya katika juma la mwisho kabla ya kufanyika kwa sensa

Amewataka makarani wote waheshimu dhamana kubwa waliyopewa na serikali kwa kuwa miongoni mwa wananchi wapatao 2,700 walioomba kufanyakazi ya sensa kwa kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa na kwa kasi lakini yenye uhakika

Makunga ameeleza kuwa baada ya mafunzo hayo kutakuwa na mitihani ya kuwapima makarani hao katika kile walichofundishwa kwa nadharia na vitendo

Aidha Makunga ametumia nafasi hiyo pia kufafanua madai yanayoenezwa na baadhi ya watu wilayani humo kuwa uongozi wa serikali wilayani humo unawachukia walimu na ndiyo maana hawakuteuliwa katika sensa

Makunga ameeleza katika kundi hilo la makarani sehemu kubwa ni walimu ambao ni 340 huku wengine wakiwa wahitimu wa kidato cha nne, sita na vyuo vikuu na wachache ni watumishi wa umma.

“Tungependa kuchukua watu wote 2,700 walioomba lakini kwa bahati mbaya nafasi zilikuwa ni 644 hivyo katika hizo chache tumehakikisha tunachanganya makundi yote yakiwemo ya wazoefu na wasiokuwa na uzoefu,”alifafanua.

Ametaka propaganda mbalimbali zinazoenezwa mitaani zipuuzwe kwani hata siku moja serikali haiwezi kuwachukia watu wake ambao inajukumu la kuwahudumia na kuwatendea haki.

Advertisements