JICHO LETU LASHANGAZWA NA MAISHA YA WAPIGA KURA WA EDO

TASWIRA YA AWALI AMBAYO JICHO LETU ILIJIONEA LILIPOKUWA LINAINGIA KATIKA KIJIJI CHA EMAIRETE KATIKA KITONGOJI CHA MORIJO WILAYANI MONDULI MKOANI ARUSHA NA KUJIULIZA MASWALI YASIYO NA MAJIBU.

Wakati mwezi wa Agosti ukiwa umeishajigawa katikati  na uchovu wa sherehe ya wakulima ya nane nane ukiwa umetoweka,  Jicho Letu likapata Simu na kuambiwa kuwa litembelee  maeneo  ya Wilaya ya Monduli hususani katika kijiji cha Emairete.

Jicho letu halikungoja mtu aliyekuwa anaongea upande wa pili wa simu amalize bali lilikubali haraka haraka huku likijitengenezea taswira ya wilaya hiyo ambayo anatoka Waziri Mkuu Msataafu na mbunge al-maarufu Edo!

Katika kujiandaa na safari hiyo Jicho Letu likawa linaweka kumbukumbu za simulizi nyingi kuhusu zile za maendeleo makubwa ya Wilaya hiyo pamoja na  kazi alizofanya Mbunge huyu maarufu kwa kufanya harambee za maendeleo nchini bila mipaka hadi sehemu za ibada

BAADHI YA NYUMBA ZA MAKAZI NA SHULE KATIKA KIJIJI CHA EMAIRETE KATIKA KITONGOJI CHA MORIJO WILAYANI MONDULI MKOANI ARUSHA .

Awali Jicho Letu liliambiwa kuwa pamoja na ukame uliyoleta tatizo kidogo katikati ya mwaka jana wilaya hiyo inaongoza na kuwa na miundombinu ya kisasa ya maji safi ya kunywa pamoja na ya kunyweshea mifugo. Jicho Letu likajipa matumaini kuwa kwavile liliona taswira ya mkuu wa Kaya akifungua mradi wa aina yake wa kugawa ng’ombe ambao Jicho Letu liliufananisha mradi huu sawa na wa nchi za magharibi ambao huwapatia pesa za kujikimu raia wao, Jicho letu likajisemea moyoni mwake kwa kujivunia utaifa wake kuwa  wao wana fedha na sisi tuna mifugo.

Jicho Letu likiwa njiani kuelekea katika wilaya hiyo maarufu hapa nchini lilishtushwa na taswira iliyoanza kuziona. likaanza kujiuliza maswali mengi ambayo hayakupata majibu stahiki. Hapo likakumbuka  kuwa wilaya hii ilikuwa ya 100 kati ya wilaya 119 za hapa nchini kwa kiwango cha umaskini. japo taarifa hii ni ya kitambo kidogo lakini Jicho Letu lilikumbuka kuisoma kwenye Taarifa ya PHDR ya mwaka 2005 iliyokuwa ikionyesha mgawanyo wa viashiria tofauti vya umaskini.

JICHO LETU LIKIANGALIA GARI ILIYO WALETA KIJIJI CHA EMAIRETE KATIKA KITONGOJI CHA MORIJO WILAYANI MONDULI MKOANI ARUSHA IKIONDOKA

Jicho Letu lilijaribu kupata tafsiri sahihi ya Kiwango cha Umaskini, tafsiri iliyokuja haraka haraka kichwani mwa Jicho Letu ilikuwa ni asilimia ya watu waliopo chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi. Kwa Tanzania kiwango cha  mahitaji ya msingi mnamo mwaka 2000/01 kilikuwa  shilingi za Kitanzania 262 kwa kila mtu mzima kwa siku.

Jicho Letu Likiwa katika wimbi kubwa la mawazo, na kufahamu wazi halitapata hasa kile lilichotarajia na ugumu wa kusambaza habari hii kwa vyombo husika lilisikia kelele za shangwe za wananchi wenye asili ya kimasai wakiwashangilia na kuwapokea wageni likiwemo Jicho Letu.

Wanakijji wa kijiji cha Emairete katika kitongoji cha Morijo Wilayani Monduli Mkoani Arusha walionekana ni wenye furaha tofauti na hali ya mazingira duni yaliyokuwa yamewazunguka.

BAADHI YA WAKAZI WA KIJIJI CHA EMAIRETE KATIKA KITONGOJI CHA MORIJO WILAYANI MONDULI MKOANI ARUSHAWAKICHEZA NGOMA ZAO ZA ASILI WAKATI JICHO LETU LILIPO TEMBELEA KIJIJI HICHO.

Jicho Letu likiwa limetaharuki liliamua kuongea na wapiga kura hao wa Edo na kutaka kujua maoni yao na jinsi walivyojipanga kujikwamua na hali hii ngumu ya maisha.

Jicho Letu liliwanukuu wananchi hao wakiilalamikia serikali kwa kitendo cha kuwasahau hasa katika mahitaji muhimu kama chakula pamoja na maji jambo ambalo hupelekea maisha yao kuwa duni na ya kukatisha tamaa.

Jicho Letu lilishindwa kujizuia kushangaa pale wanakijiji hao waliposema kuwa wengi wao ni wa jamii ya wafugaji (Maasai) lakini halikuweza kuona mifugo yoyote likajiwazia je mradi wa mheshimiwa wa Kaya bado haujafika huku Emairete?

HILI NDILO BWAWA LA MAJI AMBALO UTUMIWA NA JAMII YA WAFUGAJI PAMOJA NA MATUMIZI YA NYUMBANI. MAJI KATIKA BWAWA HILI NI MACHAFU SANA NAHIVYO KULIFANYA JICHO LETU KUGOMA KUYATUMIA HATA KUNAWIA MIKONO.

katika hali ya kuchanganyikiwa Jicho Letu liliomba kuonyeshwa mitandao ya Maji ambayo lilisikia sifa zake kwa muda mrefu. Vijana wa kimasai waliliongoza Jicho Letu mpaka kwenye Bwawa la maji ambayo Jicho Letu lilishindwa kujua rangi halisi ya maji hayo?

Vijana hao pamoja na kina mama walilieleza jicho letu kuwa hayo ndiyo maji peke ambayo wanakijiji hicho hutegemea kwa matumizi ya mifugo yao pamoja na nyumbani, Chanzo cha maji mengine kinapatikana katika kijiji cha Eluwawi ambao ni umbali wa kutembea siku nzima. kiukweli pamoja na vumbi ambayo ilikuwa imelijaa Jicho Letu lilishindwa kutumia maji hayo hata kunawia mikono kutokana na uchafu wake.

Jicho Letu liliambiwa kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ni wakulima na hujishughulisha na ulimaji wa mahindi, ngano na maharage lakini hata hivyo kutokana na hali ya ukame ukuaji wa mazao mwaka huu hauridhishi.

BAADHI YA WANAKIJIJI WAKIWA WANARUDI MAKWAO BAADA YA KUHUDHURI UGENI KIJIJINI MWAO LIKIWEMO JICHO LETU.

Jicho Letu likiongea na mmoja wa wakazi wa kijiji hicho Bi, Nemuto Mungaya ambaye ni mkazi wa kijiji hicho alisema kuwa hali hiyo imekuwa ngumu sana kwao kuendesha familia zao kwa kuwa hutembea siku nzima kutafuta maji huku wakilazimika kutumia mlo mmoja kwa siku jambo ambalo hupelekea afya zao kudhoofika.

“Sasa tunalazimika kuishi kwa mlo mmoja kwa siku, asubuhi  uji hadi jioni na usiku ni ugali kama upo  kama hakuna utapika tena uji ili familia yako iweze kunywa na kulala” alisema Bi.Mungaya

jambo jingine ambalo jicho letu halitalisahau ni pale lillipoambiwa kuwa kwasasa debe moja la mahindi linanunuliwa kwa bei ya shilingi 10,000/= hapo kijijini.  Jicho Letu likabakia na maswali je kama wananchi hao wanaishi chini ya kiwago cha umaskini ambacho ni shilingi 262 kwa kila mtu mzima kwa siku ikiwa ni kiwango cha Tanzania mnamo mwaka 2000/01 wataweza vipi kumudu gharama hizi?

Jicho Letu likajiondoa taratibu na kwenda kupanda gari ya kurudi Arusha huku likiapa kuwa safari hii litahitaji simu ya mwaliko wa kwenda kuonana na Mheshimiwa Edo ili lijue tatizo ni nini? hata hivyo lilishindwa kupata jibu la ni namna gani taarifa za ubora na maendeleo ya Monduli zinasambazwa wakati siyo kweli! na wanao sambaza wana malengo gani…

Advertisements

One thought on “JICHO LETU LASHANGAZWA NA MAISHA YA WAPIGA KURA WA EDO

  1. Pingback: Hali ya monduli kwa edo yalistajabisha jicho letu.

Comments are closed.