KWA TAKRIBAN MASAA 2:30 MOROGORO MJINI YAGEUKA TOLABORA

BENSON KIGAIYA AKIWA CHINI YA ULINZI WA POLISI WA FFU WATANO HUKU WENGINE WAKIMNYATIA KWA PEMBENI.

  • NGUVU KUBWA ZATUMIWA NA POLISI KUZIMA MAANDAMANO.

  • MUHUZA MAGAZETI APIGWA RISASI YA KICHWA NA KUUAWA NA WENGINE WAWILI WAJERUHIWA

  • TUNDU LISSU ADAI POLISI WALIDHAMIRIA KUUA

  • KAMANDA WA POLISI MOROGORO SHILLOGILE ASEMA HAIJATHIBITISHWA CHANZO CHA KIFO HICHO ATUMA ASKALI KUFANYA UCHUNGUZI.

  • MBUNGE WA MOROGORO MJINI-CCM, AZIZ ABOOD AMEKARIRIWA AKISEMA VITENDO VYA POLISI VINAJENGA CHUKI BAINA YA WANANCHI NA SERIKALI HIVYO KUWEKA JIMBO HILO NA CCM MASHAKANI.

    MKUU WA OPERESHENI SANGARA NA M4C CHADEMA, BENSON KIGAILA AKIWA CHINI YA UANGALIZI WA POLISI NDANI YA GARI LA POLISI MARA BAADA YA KUKAMATWA KATIKA ENEO LA MSAMVU MOROGORO.

JUMATATU Agosti 27 2012 mchana kweye majira ya saa 7:30 jiji la Morogoro lilirindima kwa risasi na sauti ya milipuko na mabomu ya machozi baada ya vurugu kubwa kuzuka baina ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Polisi na kusababisha kifo cha mtu mmoja anayedaiwa kuwa mfuasi wa chama.

Tukio hilo lilisababisha taharuki kubwa katika eneo kubwa la Manispaa ya Morogoro, huku wanachama na baadhi ya viongozi wa chama hicho wakionekana kuzagaa katika maeneo mbalimbali  yakiwamo ya mjini na Hospitali ya Mkoa.

WANAHABARI PAMOJA NA WANANCHI WAKIWA NA MAJONZI WAKATI WAKIUTAZAMA MWILI WA ALLY ZONA ALIYE UWAWA KWA RISASI

Kifo hicho kilitokea katika eneo la Msamvu ambako wafuasi hao walikusanyika, wengine wakitokea Barabara ya Dar es Salaam na wale waliokuwa wakitokea Barabara ya Dodoma, tayari kuwapokea viongozi wa kitaifa wa Chama cha Chadema.

Mfuasi huyo aliyefahamika kwa jina la Ally Zona (38), Mkazi wa Kihonda ni muhuza magazeti kwenye Kituo cha Mabasi Msamvu.

SEHEMU YA UMATI WA WATU WALIOJITOKEZA KWENYE MKUTANO ULIOFANYIKA MOROGORO JUMATATU AGOSTI 27 2012

Watu wengine waliojeruhiwa katika tafrani hiyo wameelezwa kuwa ni mwendesha baiskeli Hashim Seif ambaye amejeruhiwa kwa risasi mguuni akidaiwa alikuwa anapita na baiskeli yake Frank Valimba ambae amejeruhiwa na risasi tumboni inaelezwa kuwa ni muuza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shillogile alithibitisha kutokea kwa kifo hicho lakini akasema haijathibitishwa kwamba aliuawa kwa bomu, risasi au ajali na kwamba jeshi hilo linafanya uchunguzi kujua chanzo cha kifo chake.

MWENYEKITI WA CHADEMA MKOA WA MOROGORO NA MBUNGE WA VITI MAALUM SUZAN KIWANGA AKIMWAGA SERA ZA CHAMA HICHO BAADA YA TAFRANI NA POLISI KWENYE MKUTANO ULIOFANYIKA ALASILI YA JUMATATU AGOSTI 27 2012

“Uchunguzi huo utabaini kama mtu huyo amefariki kutokana na bomu, risasi au ajali kwani wakati wa vurugu hizo watu walikuwa wakikimbia ovyo kwa kutumia magari na pikipiki,” alisema Shillogile na kuongeza:

“Kutoka eneo lililokuwa na vurugu hadi alipookotwa marehemu huyo, pana umbali kidogo kwa hiyo uchunguzi huo ndiyo utakaoeleza ukweli.”

MKURUGENZI WA HABARI NA UENEZI CHADEMA NA MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO JIJINI DAR ES SALAAM JOHN MNYIKA AKIPANDA JUKWAANI WAKATI AKIWASILI KATIKA VIWANJA HIVYO.

Alisema kuwa uchunguzi wa awali, unaonyesha kwamba mwili wa Zona ulikutwa ukiwa unatoka damu kichwani kutokana na jeraha ambalo haijafahamika limetokana na nini.

Awali  Shilogile akieleza kuzuia maandamano yaliyopangwa kuanza saa 5 asubuhi, Mkuu wa Operesheni Sangara, Benson Kigaila, alisisitiza kuwa watafanya maandamano kwa kuwa walishakubaliana na Kamanda Shilogile kabla ya kuwageuka.

MBUNGE WA SINGIDA MASHARIKI, TUNDU LISSU AKIZUNGUMZA NA WANANCHI WA MANISPAA YA MOROGORO WALIOJITOKEZA KATIKA MKUTANO PAMOJA NA RISASI NA MABOMU YA MACHOZI YALIYO RUSHWA AWALI


Kwa mujibu wa Gazeti la Nipashe la 27 Agosti 2012, ilielezwa kuwa Kamanda Shilogile alidai kuruhusu baiskeli na watu kutumia barabara kwa sababu ya mikutano ya Chadema ni kuwanyima haki wananchi wengine, na hivyo wataruhusu watu wasiozidi 50 kupita kwa wakati mmoja pasipo kuwa na ishara ya kuonyesha kama wanaelekea katika maandamano.

Hata hivyo, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alidai kwamba kifo hicho kimetokana na risasi aliyopigwa kichwani na siyo bomu… “Kwa kitendo hicho polisi wanaonekana kuwa walifanya kusudi na walidhamiria kuua.”

MAKAMU MWENYEKITI CHADEMA ZANZIBAR SAID ISSA MOHAMED AKIFAFANUA JAMBO KWA WANANCHI WALIO JITOKEZA KWENYE MKUTANO HUO WA CHADEMA

Alisema mwili wa marehemu hautazikwa mpaka uchunguzi wa kidaktari utakapofanyika. Aliwataka walioshuhudia tukio hilo kujitokeza kutoa ushahidi ili askari waliohusika wachukuliwe hatua.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika baadaye jioni ya Jumatatu Agosti 27 2012, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema kifo cha kijana huyo kinaongeza kasi ya mapambano ya chama hicho dhidi ya ukombozi wa kweli.

KATIBU MKUU WA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO CHADEMA, DKT. WILLIBROD SLAA, AKIWAHUTUBIA MAELFU YA WAKAZI WA MOROGORO NA VITONGOJI VYAKE, KWENYE UWANJA WA SHULE YA MSINGI YA UWANJA WA NDEGE.

Alimlaumu Kamanda wa Polisi wa Mkoa na Kamanda wa Polisi Wilaya kwa kuamrisha askari wao kutumia nguvu dhidi ya wananchi wasiokuwa na silaha.

“Tuko tayari kushirikiana na familia ya kijana huyo kwa ajili ya taratibu zote za mazishi. Tutamzika kishujaa kwa kuwa alikufa akikipigania chama,” alisema Dk Slaa.

Aliwataka wananchi kuonyesha uchungu kwa kifo cha mfuasi huyo kwa kutupa kadi za CCM na kuchukua za chama hicho cha upinzani.

Awali, Mwaipaya alisema kifo cha mfuasi huyo kimesababishwa na polisi baada ya kurusha mabomu ya machozi na kusababisha vurugu na taharuki kwa wananchi pamoja na wanachama wa Chadema.

Alisema wakati wananchi wakiwasubiri viongozi wa Chadema; Dk Slaa, John Mnyika, Halima Mdee na Mchungaji Peter Msigwa, walikuwa hawafanyi vurugu zozote.

ALIYEKUWA MGOMEA UBUNGE JIMBO LA IGUNGA KUPITIA CHADEMA, JOSEPH KASHINDE AKIZUNGUMZA NA WANANCHI WALIOHUDHURIA MKUTANO HUO

“Polisi ndio waliosababisha vurugu, baada ya kuanza kurusha mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi. Nilishuhudia wakati marehemu (Zona) akidondoka,” alisema.

Licha ya Kamanda Shillogile kueleza kuwa hakuna kiongozi wa Chadema aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo, taarifa zimeeleza kuwa jeshi hilo linawashikilia viongozi wake kadhaa akiwamo Mkuu wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Benson Kigaila.

Kigaila na viongozi wengine walikamatwa baada ya kufika Msamvu wakati jeshi la polisi likiwa katika harakati za kuzuia mikusanyiko ya watu na kuwalazimisha kushuka katika magari yao na kuwakamata.

Maandalizi ya polisi kudhibiti maandamano ya Chadema yalianza majira ya saa 3:00 asubuhi kwa kutumia Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ambacho kilionekana kikiwa na magari yasiyopungua matano kikirandaranda katika mitaa mbalimbali ya Morogoro.

Polisi hao walikuwa wakitangaza kuzuiwa kwa maandamano hayo na kuwataka wananchi kutojitokeza kushiriki wakionya kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaokaidi.

Advertisements