HOJA YA SERIKALI MBILI KATIKA KATIBA NI YA CHAMA AU WATANZANIA?

Erick Luwongo Mratibu wa Katiba wa Asasi ya HAKI-MADINI

KONGAMANO la ndani lililoandaliwa na Asasi isiyo ya kiserikali ya Community Right Development Organization (HAKI-MADINI) Ijumaa Septemba 21, 2012, kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanahabari kuhusiana na mambo mbalimbali ya Katiba mpya hususan maliasilia limeibua mjadala mzito.

Haki-Madini inayojishugulisha na uchechemuaji pamoja na  uzengezi (ushawishi na utetezi) wa wachimbaji wadogo huku wakiwa wamejikita katika kuwajengea uwezo watanzania hao.

BAADHI YA WASHIRIKI KWENYE KONGAMANO HILO LA KATIBA

Kauli za mchokoza mada iliyotolewa na Erick Luwongo mratibu wa Katiba wa Asasi ya HAKI-MADINI uliainisha mapungufu kadhaa ambayo yasipofanyiwa kazi katika katiba ijayo haitaweza kukidhi haja na kuitwa Katiba ya Watanzania.

Mbali na Erick Luwongo washiriki mbalimbali walioudhuria kongamano hilo wengi wao wakiwa wanahabari pamoja na wanasheria kutoka maeneo yanayoizunguka Arusha waliiasa serikali kuboresha mchakato unaoendelea wa kukusanya maoni ya wananchi ili kuliwezesha taifa kupata katiba yenye hadhi ya kuitwa ya watazania.

BAADHI YA WASHIRIKI KATIKA KONGAMANO HILO LA KATIBA

Miongoni wa hoja zilizojitokeza katika kongamano hilo la katiba lililofanyika kwenye hoteli ya SG Resort katikati ya jiji la Arusha zililenga katika maeneo makuu ya mali asilia, sheria mpya ya marekebisho ya Katiba na muungano.

Luwongo ndiye aliyepata muda mrefu wa kuainisha mapungufu yanayoonekana katika mchakato unaoendelea hususan sheria iliyopitishwa ambayo anasema inaipa mamlaka makubwa tume ya katiba na kuwanyima fursa wananchi ambao ndiyo walengwa wakuu katika mchakato huu.

Tofauti na makongamano mengine, Luwongo aliwasilisha hoja ambayo inahusu mali asilia na kuonyesha namna katiba inavyo waacha watanzania wazawa pembeni bila kuonyesha watafaidika vipi na rasilimali hizo.

“Ibara ya 27 kifungu cha kwanza katika katiba ya  Jamuhuri ya muungano wa Tanzania imebainisha wazi kuwa kila mtu anayo haki na wajibu wa kulinda mali asilia lakini haijaweka wazi walinde vipi na watafaidika na nini kwa ulinzi wao” alibainisha Luwongo.

Hapa ndipo kuna tatizo kubwa, Serikali imejiweka pembeni na kuchukuwa jukumu la kuwa mtumiaji na huku ikimuacha huyu mlindaji (mwananchi) bila faida yoyote kwa kazi yake ya ulinzi, alifafanua Luwongo.

Jovita Mlay mwanaharakati mwenye taaluma ya sheria alipopata nafasi ya kuchangia aliikosoa serikali kwa tabia yake ya kila mara yanapojitokeza matatizo mazito katika suala la muungano, watawala hufikiria njia ya mkato ili kuziba midomo ya watu wanaohoji au wanaokosoa, ndiyo maana mwaka jana chini ya sheria ya marekebisho ya Katiba kuna kifungu kinachozuia uhuru wa kujadili muungano alisema.

Sheria hiyo inataka wananchi wajadili kwa lengo la kuboresha tu muungano. Kwa lugha nyingine, wale wenye maoni tofauti watakuwa wanajisumbua kutoa maoni kwa mtazamo tofauti na muundo wa serikali mbili.

Washiriki walikumbushwa kuwa Rais wa kwanza na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipokuwa anazima madai ya wabunge 55 mwaka 1994 ambao walikuja kujulikana kama G55 baada ya kuanzisha mchakato wa kudai Tanganyika alisema “wote wanaotaka Tanganyika kwanza watoke CCM maana muungano wa serikali mbili ni sera ya chama hicho tawala”.

Wakati sheria inakataza wananchi kuhoji muungano wa serikali mbili au inakataza kujadili kwa mtazamo tofauti, maelfu ya watu wanahudhuria mikutano inayoitishwa na kikundi cha Uamsho chenye msimamo mkali dhidi ya muungano.

Nilipojipa kazi ya uchunguzi wa mikutano ya jumuiya hiyo na hata ninaposoma habari za mihadhara yao, maelfu ya watu wanaohudhuria mikutano wakiulizwa kama wanataka muungano uendelee au uvunjwe, sauti husikika zikisema Uvunjwe.”

Hawa ni Wazanzibari. Hawa hawapaswi kupuuzwa kwa mbinu za sheria, tishio la kufungwa au adhabu nyingine yoyote.

Serikali inataka isikie sauti za watu gani  ili ikubali kuwa umefika wakati wa kutoa fursa watu watoe dukuduku zao? Si tuliambiwa kuwa muundo wa muungano wa serikali mbili ni sera ya CCM, sasa kwa nini sera ya CCM inalindwa kwa sheria? alihoji Amani Mustafha mkurugenzi wa asasi ya Haki-Madini

Kwa majibu hayo, vyama vingine vyote havifungwi na sera hiyo. Sera ya Chama cha Wananchi (CUF) na hata Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ni muungano wa mfumo wa serikali tatu.

Kama muungano ni wa serikali basi waachiwe watawala wafanye wanavyotaka. Ila kama muungano unawahusu watu wapewe fursa ya kuujadili kama tunavyojadili maeneo mengine tunayosema yamepitwa na wakati. kwa wengine muungano huu umepitwa na wakati.

Tume zote zilizoundwa na marais waliopita na hasa ile Tume ya Jaji Robert Kisanga (1999), japo haikupewa hadidu za rejea kujadili muungano, walioulizwa walitaka Zanzibar yao.

“Kwa hiyo, sheria iliyowekwa leo kuzuia watu kuujadili kwa uhuru ni woga wa watawala kuonekana wao wamevunja muungano huo” alisema Mwandishi nguli Abiba Suedi.

Pamoja na Mchakato kupitia hatua nyingi na kusimamiwa na chma tawala lakini lililo wazi ni katiba mpya siyo ajenda ya chama tawala kwa kuwa haiko katika ilani yao. Rais Jakaya Kikwete aliamua kuiweka baada ya kuona huitaji wa watanzania.

Rais alitumia maneno yaliyowapa furaha watu kwamba watapata katiba mpya wakati yeye alikuwa na maana ya kufanyia marekebisho. “Tutahuisha katiba iliyopo,” alinukuliwa akisema. Hii ina maana kuipa uhai, kwa lugha ya kingereza ni Kurenew.

Elimu kwa wananchi, Haki ya kugawana na kutolea maamuzi mali asilia zetu pamoja na  haki kwa wanawake bila kusahau tulipotoka tulipo sasa na tunapokwenda ni baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatiwa katika mchakato wa katiba mpya, ni jukumu letu sote kushiriki katika mchakato huu hili tupate katiba inayostahili kuitwa ya watanzania.

Makala hii pia ilitoka kwenye Gazeti la TAZAMA Tolea Na, 520

Advertisements