GWALIDE LA UTAMBULISHO KUITISHWA KUMSAKA ALIYEPIGA PICHA NA LEMA MELELANI.

Katika  Picha hiyo: Mtu aliyejitambulisha kuwa askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ),kambi ya Monduli,Arusha akiwa na wabunge wa Chadema, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na wabunge hao katika Mji mdogo Mererani,Simanjiro mkoani Manyara.

Mtu aliyejitambulisha kuwa askari wa Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ),kambi ya Monduli,Arusha akiwa na wabunge wa Chadema, Godbless Lema (Arusha Mjini) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na wabunge hao katika Mji mdogo Mererani,Simanjiro mkoani Manyara. PICHA KWA ISANI YA JUKWAA LA MABADILIKO

  • KURUGENZI YA HABARI NA UHUSIANO YA JESHI HILO LATILIA SHAKA KAMA MAVAZI YALIYOVALIWA NI YA JWTZ.

  • KILICHO ICHEFUA JWTZ NI KITENDO CHA ASKARI HUYO KUNYOOSHA VIDOLE VIWILI AMBAYO NI ALAMA YA CHADEMA.

  • AKIPATIKANA KUFUKUZWA KAZI.

  • YEYE ASEMA YUKO TAYARI KWA LOLOTE.

Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limehapa kumtafuta na kumchukulia hata stahiki  aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema akiwa amevaa sare za jeshi hilo.

Kauli hiyo ya JWTZ imekuja baada ya gazeti moja la kila siku la Jumanne 26,12 2012 kuchapisha picha ya mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa JWTZ akiwa amepiga picha na Lema pamoja na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari, huku akiwa amenyoosha vidole viwili alama inayotumiwa na Chadema.

Baada ya taarifa hiyo, JWTZ lilitoa taarifa likieleza kushtushwa na tukio hilo na kusema kwamba linamtafuta mtu huyo kwa udi na uvumba ili kujiridhisha kama kweli ni askari wake.

‘‘Kimsingi Jeshi linafanya uchunguzi wa kumtambua mtu huyo kama kweli ni askari,’’ ilisema sehemu ya taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya jeshi hilo ambayo iliyatilia shaka mavazi aliyokuwa amevaa mtu huyo kama ndiyo yanayotumiwa na jeshi hilo sasa.

Mbali ya taarifa hiyo, Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema endapo itabainika kuwa aliyevaa sare hizo ni mwanajeshi, moja ya hatua dhidi yake ni kufukuzwa kazi mara moja.

Mbali na hatua hiyo, Kanali Mgawe alisema kuanzia sasa, Jeshi limepiga marufuku mtu yeyote kuvaa sare zake katika mikutano yote ya siasa na atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Kwa upande wake, mtu huyo aliyejitambulisha kuwa ni askari wa Kikosi cha Chuo cha Mafunzo Monduli (TMA), mkoani Arusha, alisema ni bora afukuzwe kazi kuliko kunyimwa kujiunga na Chadema.

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina akiwa Mirerani, Simanjiro mtu huyo alisema Chadema ni chama makini chenye uwezo wa kuongoza nchi kwani kinatetea wanyonge na kujali masilahi ya jamii.

Alisema kwa kuwa Katiba ya nchi hairuhusu wanajeshi kujihusisha na vyama vya siasa, yuko tayari kufukuzwa kazi ili aendelee kukishabikia chama hicho.

Askari huyo alipiga picha na Lema baada ya mbunge huyo kuhutubia mkutano uliofanyika huko Mirerani. Katika mkutano huo wa hadhara, Lema alisema: “Ninapoongoza maandamano ya makamanda ninakuwa natetea masilahi yenu mkiwamo polisi ambao mnanipiga mabomu.

Sisi hatuangalii wake zetu wamevaa hereni za dhahabu ila tunaandamana kudai haki, mishahara mizuri kwa madaktari, walimu, askari na maisha bora kwa Watanzania.”

hakimadini 001

Advertisements