KAULI YA SERIKALI BUNGENI KUHUSU MLIPUKO ULIOTOKEA KATIKA KANISA KATOLIKI LA MT. JOSEPH MFANYAKAZI, PAROKIA TEULE YA OLASITI, ARUSHA MJINI, MEI 5, 2013

HAPA NDIPO WABUNGE WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA HUKUTANA

HAPA NDIPO WABUNGE WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA HUKUTANA

Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa Kanuni ya 49 (1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili, 2013, naomba kuwasilisha Taarifa yaawali kuhusu tukio la mlipuko uliotokea katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, Jijini Arusha tarehe 5 Mei, 2013 saa4:30 asubuhi.

Mheshimiwa Spika,
mnamo tarehe 5 Mei, 2013 saa 4:30 asubuhi kulitokea mlipuko katika kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti, jijini Arusha. Mlipuko huo ulitokea muda mfupi baada ya kuanza kwa ibada ya uzinduzi wa Parokia. Mgeni Rasmi katika uzinduzi alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini na Mjumbe wa Baba Mtakatifu, Askofu Fransisco Mantecillo Padilla. Aidha, alikuwapo mwenyeji wake Askofu Josephati Lebulu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha. Katika uzinduzi huo inakadiriwa kuwa kulikuwa na zaidi ya watu 2000. Wakati Mgeni Rasmi akiwa ametoka nje ya Kanisa akijiandaa kukata utepe kama ishara ya uzinduzi mtu alirusha kitu chenye ukubwa wa ngumi kuelekea eneo kulipokuwa na mkusanyiko wa watu ambapo baada ya kutua kulitokea kishindo na mlipuko mkubwa. Mlipuko huo ulisababisha taharuki miongoni mwa waumini na kusababisha watu kukimbia ovyo.

Mheshimiwa Spika,
katika tukio hilo watu wawili wamefariki dunia ambapo REGINA LONGINO KURUSEI, Mwarusha, umri wa miaka 45, mkazi wa Olasiti alifariki dunia siku ya tukio wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount Meru na majeruhi mwingine JAMES GABRIEL umri wamiaka 16 amefariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 6 Mei, 2013. Aidha, watu 59 wamejeruhiwa na watatu kati yao ni mahututi. Majeruhi 38 walikimbizwa hospitali ya Mount Meru kupatiwa matibabu. Majeruhi 16 walikimbizwa hospitali ya St. Elizabeth kwa Father Babu, majeruhi mmoja alipelekwa hospitali ya Selian na majeruhi mwingine alipelekwa katika hospitali ya Dkt. Wanjara, Mianzini. Natumia fursa hii kutoa pole kwa wafiwa, uongozi wa kanisa Katoliki, wakazi wa Arusha na Watanzania wote kwa tukio hili la kinyama. Aidha, nawaombea majeruhi wote wa tukio hilo wapone haraka.

Mheshimiwa Spika,
Viongozi wa dini na Serikali waliohudhuria ibada hiyo hawakupata madhara yeyote kufuatia mlipuko huo. Baada ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kupokea taarifa ya tukio hilo waliimarisha ulinzi kwa kuongeza idadi ya askari katika eneo hilo. Aidha, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mheshimiwa Magesa Mulongo walifika eneo la tukio na kufanya tathimini ya hali ilivyo na kuelekeza hatua za kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika,
kutokana na uzito wa tukio hilo, kitaifa na kimataifa, Makamu wa Rais Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Pereira A. Silima, na Inspekta Jenerali wa Polisi, Said A. Mwema walikwenda Arusha na walitembelea eneo la tukio, waliwatembelea majeruhi na kuelekeza hatua za ziada za kuchukuliwa.

Mheshimiwa Spika,
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mlipuko huo ni bomu. Uchunguzi wa kubaini aina ya bomu lililotumika unaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na Wataalamu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Hadi sasa watuhumiwa sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi. Miongoni mwao ni Victor Calisti Ambrose mwenye umri wa miaka 20, dereva wa bodaboda, mkazi wa KwaMrombo, Arusha ambaye anatuhumiwa kwa kurusha bomu hilo. Watuhumiwa wengine watano waliokamatwa ni raia wanne wa kigeni na Mtanzania mmoja ambao wanashikiliwa kwa mahojiano.

Mheshimiwa Spika,
siku za karibuni kumekuwepo jitihada kubwa sana za watu wachache wasiyoitakia mema nchi yetu kutaka kupandikiza chuki za kidini miongoni mwa watanzania na kuleta mapigano na mauaji miongoni mwa watanzania, sina shaka kuwa shambulio la Arusha ni sehemu ya mikakati hiyo miovu. Nataka niwahakikishie Watanzania kuwa Serikali haitavumilia hata kidogo mbegu za chuki za kidini miongoni mwawatanzania na tutachukua hatua kali bila huruma kuzigandamiza njama hizi mbaya dhidi ya taifa letu. Tutachukua hatua kali kwa mtu yeyote bila kujalihadhi na nafasi yake katika jamii. Amani yetu kwanza na taifa letu kwanza.

Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kukamatwa kwa watuhumiwa hao, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wametoa maelekezo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambapo tayari Inspekta Jenerali wa Polisi kwa kushirikiana na Wakuu wa Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama wameunda Kikosi Kazi maalumu ili kuchunguza tukio hilo.

Mheshimiwa Spika,
kokote duniani, tukio la kushtukiza, linalosikitisha nakuhuzunisha kama hili linapotokea, wananchi wote huungana na kuwa wamoja kama taifa na kulaani wahusika na kuwafariji waathirika wa tukio hilo. Nchini Marekani, Mgombea mmoja wa Urais wakati wa uchaguzi mkuuwa Mwaka 2012 aliishutumu Serikali kutokana na tukio la kulipuliwa kwa Ubalozi wa Marekani nchini Libya. Ni wazi kuwa mgombea huyu alichukua tatizo lile kama ajenda ya kisiasa. Hata hivyo, alishutumiwa vikali na Wamarekani wenzake kwa kuelezwa kuwa ni mtu mwenye kukosa kabisa misingi ya uaminifu na uzalendo kwa taifa lake (Fundamental dishonest).

Serikali inasikitishwa sana wanasiasa wa aina hii ambao wanajitokeza nchini na kutafuta umaarufu wa kisiasa kwa gharama za maisha ya Watanzania. Wanasiasa na viongozi wote wajiepushe na kauli zinazochochea ubaguzi wa kidini, mifarakano ya kijamii na chuki miongoni mwa Watanzania. Serikali isilaumiwe kwa hatua kali za kisheri aitakazochukua dhidi ya viongozi wa aina hii ambao maslahi yao ni muhimu kuliko maisha ya Watanzania, maslahi yao ni muhimu kuliko utulivu waWatanzania na maslahi yao ni muhimu kuliko umoja wa Watanzania.

Mheshimiwa Spika,
kwa niaba ya Serikali naungana na Watanzania wenzangu kulaani wahusika wote wa tukio hilo walioshiriki kwa njia yoyote.

Aidha, Serikali kwa nguvu zake zote itahakikisha kuwa watuhumiwa wote waliohusika na kushiriki kwa namna yoyote katika tukio hili wanasakwa popote walipo na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Tunawataka viongozi wa kisiasa, kidini na wananchi wote kwa ujumla kila mmoja kwanafasi yake kuwajibika ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendelea kuwakisiwa cha amani na utulivu.

Mheshimiwa Spika,
mwisho nawasihi Watanzania wawe watulivu wakati vyombo vya dola vikiwasaka waliohusika na shambulio hilo, kila mwenye taarifa za kuwezesha kukamatwa wahalifu hao atoe taarifa hizo kwa Jeshi la Polisi. Aidha, ninawaomba Watanzania tuendelee kukataa vitendo vyauvunjifu wa amani katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.

Advertisements

2 thoughts on “KAULI YA SERIKALI BUNGENI KUHUSU MLIPUKO ULIOTOKEA KATIKA KANISA KATOLIKI LA MT. JOSEPH MFANYAKAZI, PAROKIA TEULE YA OLASITI, ARUSHA MJINI, MEI 5, 2013

  1. Pingback: News Alert: Kauli ya serikali bungeni kuhusu mlipuko

Comments are closed.