IKULU YA NENA KUFWATIA YALE YALIYOTOKEA MTWARA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amelaani vikali fujo na ghasia zilizofanyika mjini Mtwara jana, Jumatano, Mei 22, 2013, akisisitiza kuwa raslimali yoyote inayopatikana katika sehemu yoyote ya nchi yetu ni mali ya Watanzania wote na lazima itumike kuwanufaisha wote.

Rais anaamini kuwa ni jambo lisilokubalika kuwa raslimali ya nchi inaweza kuzuiliwa isitoke katika eneo ambako inapatikana kwa vile hakuna nchi yoyote duniani inayoruhusu jambo la namna hiyo. Nchi hiyo haipo na wala sera za namna hiyo haziwezi kuanzia Mtwara.

Aidha, Rais anasisitiza kuwa Sera ya Serikali ni kwamba kila mtu, kila Mtanzania anayo haki ya kunufaika na raslimali ya nchi yetu yakiwemo maeneo ambako inatoka raslimali.

Rais Kikwete haoni sababu yoyote ya msingi ya kufanyika kwa fujo na ghasia za Mtwara. Fujo hizo hazina kichwa wala miguu, hazina mshiko na wala waliofanya fujo hizo hawaelezi wanataka nini isipokuwa kuhitimisha nia na dhamira yao ya kufanya fujo na kuharibu bila sababu mali za wananchi na zile za taasisi za Serikali.

Itakumbukwa kuwa wakati zilipotokea fujo na ghasia kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa mwaka huu, Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda alikwenda Mtwara akakutana na akazungumza na makundi mbali mbali na wananchi wa Mtwara. Ilionekana kama ulikuwa umepatikana mwafaka wa kuhakikisha kuwa jambo hilo halitokei tena.

Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Pinda aliwaelezea kwa undani kabisa fursa nyingi zinazowasubiri wananchi wa Mtwara kwa sababu ya ugunduzi wa gesi asilia na mipango ya Serikali kuhakikisha kuwa Mtwara na maeneo jirani yananufaika. Miongoni mwa mambo mengine, Mheshimiwa Pinda aliwaeleza yafuatayo:

(a)           Kwamba kiasi cha viwanda 57 vya shughuli mbali mbali vitajengwa Mtwara ili kuhudumia shughuli za uzalishaji wa gesi asilia na maendeleo ya uchumi wa Tanzania kutokana na gesi asilia hiyo. Idadi hii ya viwanda haijapata kujengwa katika eneo lolote la nchi hii katika historia.

(b)          Kwamba kiasi cha gesi asilia ambacho kitatoka Mtwara kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa shughuli nyingine za kitaifa ikiwamo kufua umeme ni asilimia 14 tu, na kuwa kiasi kinachobakia cha asilimia 86 kitabakia Mtwara kwa ajili ya kuzalisha huduma mbali mbali na kuhudumia idadi hiyo kubwa ya viwanda.

Isitoshe, Rais anajiuliza kuwa kama gesi asilia isipotoka Mtwara itabakia huko inafanya nini kwa sababu bidhaa yoyote ni lazima ifikishwe sokoni ili iweze kuuzika. Gesi asilia hiyo ikibakia katika eneo la bahari la Mtwara itawafaisha vipi wananchi wa Mtwara hata kama wakifanya fujo kila siku?

Rais Kikwete anawakumbusha wafanya fujo wa Mtwara na vinara wa fujo hizo kuwa Serikali inao wajibu wa kulinda usalama wa wananchi pamoja na usalama wa mali zao. Hivyo, Rais Kikwete hakubali fujo na ghasia zilizofanyika Mtwara leo. Anazilaani vikali na wala hatakubali wafanya fujo wachache kuvuruga amani na usalama wa nchi yetu popote walipo na kwa kisingizio chochote kile iwe ni kutafuta umarufu wa kisiasa ama kulinda maslahi binafsi ya kibiashara.

Serikali itawasaka na kuwakamata wote walioshiriki katika fujo za leo na kuwafikisha mahakamani. Aidha, Serikali itawasaka na kuwakamata viongozi na vinara wa fujo na ghasia hizo na kuwafikisha mbele ya sheria hata kama wana mapembe makubwa kiasi gani.

Rais Kikwete anawapa pole sana wananchi wa Mtwara ambao wameathirika binafsi kwa kuumizwa ama mali zao kuharibiwa katika fujo na ghasia za leo. Anapenda kuwahakikishia kuwa Serikali yake itachukua hatua za kukomesha vitendo hivyo vya fujo na ghasia katika eneo hilo.

Imetolewa na :
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu .
Dar es Salaam .
21 Mei, 2013
Advertisements